Mzee Rashid Mfaume Kawawa, mmoja wa Watanzania wa mwanzo kucheza na kuongoza filamu kwenye miaka ya 1950.
Serikali ya Kikoloni katika koloni la Tanganyika ilianzisha rasmi Kitengo cha Filamu cha Tanganyika mapema mwaka 1948. Ilipofika mwanzoni mwa miaka ya 1950, tayari kulikuwa na vitengo vya filamu vya kudumu katika Afrika Mashariki.
Tanganyika (sasa Tanzania) kitengo hicho kiliweza kutengeneza sinema kumi na sita (zote za miaka ya 1950) za ukulima wa pamba. Ni katika kipindi hicho ndipo mzee wetu, mzee Rashid Mfaume Kawawa alipopata kuwa mmoja kati ya waigizaji wa filamu wa mwanzo kabisa wa Kitanzania na kufungua njia kwa Watanzania wengine.
Kadri uhuru kwa nchi za Afrika Mashariki ulivyokuwa ukikaribia, ndivyo pesa za Serikali za Kikoloni katika Afrika Mashariki zilivyokuwa zikihitajika zaidi kwa mahitaji mengine na hivyo kujikuta vitengo vya sinema vya nchi hizi vikitelekezwa bila msaada, ingawa baadhi yake vilikuja kufufuka tena baada ya nchi hizi kupata uhuru. Mwaka 1955 “CFU” ilitoa tamko kwamba imejipatia mafanikio makubwa na kufikia lengo kwa kile walichokikusudia: yaani kutoa elimu ya utengenezaji wa sinema kwa Waafrika.
Makoloni yote katika nchi hizi yaliombwa kugharamia kazi za sinema zao badala ya kuendelea kutegemea pesa kutoka Uingereza. Ndipo “CFU” ilipoamua kubadili jina lake na kuwa “Overseas Film and Television Centre”. Hivyo CFU haikutaka tena kujihusisha na uandaaji wa sinema kwenye makoloni hayo, bali ilibaki kutumika kama makao makuu ya uratibu wa vitengo huru vya utengenezaji sinema kwenye makoloni yote na kusimamia utoaji wa mafunzo kwa waandaaji wa sinema na televisheni.
Pia ilitumika kama kituo maalum cha mauzo ya vifaa vya kutengenezea sinema (film equipments) kwa Waafrika, na mahala pa kufanyia uhariri (post-production) wa kazi za Waafrika. Kwa maneno mengine, Uingereza ilijivua kabisa mzigo wa kugharamia sekta ya sinema kwenye makoloni yake. Sera hii pia ilikuwa ni ishara ya matayarisho kwa makoloni yake kupatiwa uhuru ili yaweze kuendeleza kazi zao. Mabadiliko haya ya kisera yalikuja kwa sababu Uingereza ilijua fika kuwa wakati wowote makoloni hayo yangekuwa huru (Rouch, uk. 390).
Kwa upande wa Serikali ya Kenya, kitengo cha filamu kilikuwa kimeanzishwa rasmi mwaka 1950, madhumuni yakiwa yale yale: kueneza propaganda kwa njia ya sinema, hasa ikizingatiwa kuwa Uingereza ilikuwa ikikabiliwa na vita mbaya sana ya Mau Mau ambayo waliipa jina la “Mau Mau emergency”. Kabla kitengo cha filamu cha Kenya hakijatelekezwa mwaka 1961 kutokana na matatizo ya kiuchumi, tayari kilikuwa kimeshatengeneza sinema iliyokuwa ikihimiza kuhusu kilimo cha pamba, kama sehemu yake ya tamasha kubwa la kampeni maalum za Kiserikali ikiwa ni pamoja na kutumia “posters”, radio, maonesho, nk.
Pia kitengo hicho kilitengeneza sinema zingine kama ile yenye ujumbe kuhusu kifua kikuu (tuberculosis), uvuvi, umuhimu wa kulipa kodi, kazi za Kiserikali, na sinema zilizohusu mambo ya utalii.
Kitengo cha filamu katika Tanganyika kilikuja kurithiwa na Serikali ya Tanganyika baada ya uhuru na kupewa jukumu la kuhifadhi matukio muhimu ya Serikali. Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC) ilianzishwa rasmi mwaka 1968. Ilitoa filamu za matukio kwa ajili ya mashirika ya umma na kumiliki studio ya kurekodi kwa ajili ya kuhifadhi kazi za muziki wa bendi na kwaya.
Filamu ndefu za wananchi zilizotengenezwa ni pamoja na: “FIMBO YA MNYONGE (1974)”, “ARUSI YA MARIAM (1984)” zilizoongozwa na Ron Mulvihill na Marehemu Nganyoma Ng’oge, na “YOMBA YOMBA (1985)” ya Martin Mhando. Pia kuliibuka studio binafsi zilizojitokeza baadaye kutoa kazi, ikiwemo Masai Studios iliyoandaa vipindi vya televisheni na Video Tumaini.
Sinema zingine zilizotengenezwa ni kama “MAMA TUMAINI (1986)” iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa Watanzania na Marekani, na ilipata tuzo katika tamasha la filamu (FESPACO) mjini Ouagadougou mwaka 1987. kazi nyingine, “MAANGAMIZI (1996)” iliyoongozwa na Ron Mulvihill akishirikiana na Martin Mhando pia ilioneshwa kwenye tamasha hilo (FESPACO) mwaka 1997, na baadaye ikaja kushinda tuzo ya sinema bora “Golden Dhow Award” na kuzawadiwa dola za Kimarekani 5000 kwenye tamasha la kwanza la Filamu la Kimataifa la Nchi za Jahazi, Zanzibar (ZIFF) mwaka 1998.
Mafanikio ya sinema za Kitanzania hayakuishia hapo, pia sinema hiyo ya “Maangamizi” ilifanikiwa kutoa muigizaji bora wa kike, Prof. Amandina Lihamba, ambapo sinema ya “GUBU LA WIFI” ilimtoa Abeid Swaa kama mwigizaji bora wa kiume
Mary-Beatrix Mugishagwe, mmoja wa Maproducer wa Kitanzania wenye sifa kubwa nje ya nchi.
Sinema nyingine ya “NEEMA” ya Geoffrey Mhagama ilishinda na kupata tuzo kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa la Nchi za Jahazi, Zanzibar (ZIFF) mwaka 2000. Miaka michache baadaye, mwaka 2004/05 sinema ya “TUMAINI (2004)” iliyoandaliwa na kuongozwa na Beatrix Mugishagwe (Abantu Vision) iliyopigwa maeneo ya Muleba, Bukoba mjini na Mwanza pia ilipata tuzo za UNICEF kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa la Nchi za Jahazi, Zanzibar (ZIFF). Hizo ndizo baadhi ya kazi za Kitanzania zilizopata mafanikio makubwa katika sekta ya filamu.
Ukiachilia kazi hizo chache za Watanzania zilizopata mafanikio, siku hizi soko la ndani limedorola sana kutokana na mambo kadha wa kadha ambayo nitayaeleza siku nyingine panapo maajaliwa.
No comments:
Post a Comment