Wasanii Hemed Suleiman na Yusuf Embe wakipozi wakati wa upigaji picha ya Blackmail eneo la Sunrise Hotel, Kigamboni.
Waafrika katika filamu za Wazungu mara nyingi walikuwa wakifanywa waonekane (na bado wanaendelea kuonekana) ni washenzi, watu wa chini, wafungwa, nk. Wakati mwingine huwa wanafanywa waonekane wakatili sana na wanaoamini mambo ya kishirikina.
Mugeta Mwendwa yupo kikazi zaidi, hapa ni wakati akipiga picha katika moja ya kazi za filamu za Kitanzania
Miaka ya nyuma kidogo enzi za Ukoloni, Colonial Film Unit (CFU) katika bara la Afrika ilianzisha shule ya filamu mjini Accra, Gold Coast (sasa Ghana) hasa baada ya waraka wa Grierson kwa UNESCO.
Grierson aliandika waraka huo maalaum akiwapasha habari kuhusu CFU kuwa sinema zilizokuwa zikitengenezwa na “Bantu Film Experiment” na hata zilizotengenezwa na “Colonial Film Unit” hazikuwa zikiwavutia tena watazamaji walengwa (Target Audience) ambao ni Waafrika kwa sababu hawakuzielewa kabisa.
Na hivi ndivyo Grierson alivyoandika (hii ni tafsiri yangu):
“Natumai kuwa tutaweza kutatua tatizo hili lililopo kwenye hizi sinema katika makoloni yetu ya Afrika, si kwa kuwaonesha sinema zitokazo Magharibi, bali kwa watu wetu kujitengenezea sinema wenyewe ndani ya makoloni yetu” (Van Beaver, uk. 16-17).
Hivyo shule hiyo ya filamu iliyoanzishwa Accra ilikuwa ikitoa mafunzo kwa muda wa miezi sita tu, baada ya hapo wanafunzi walitakiwa kugawanyika kwenye makundi madogo madogo kwa ajili ya kutengeneza sinema za majaribio. Lakini baada ya miezi sita tu ya mwanzo, shule hiyo ilihamishwa na kupelekwa Jamaica, na baadaye London!
Kwa mujibu wa Van Beaver; matokeo ya shule hiyo hayakuwa mabaya, yalikuwa ni ya kuridhisha sana kwenye sekta ya filamu. “Wanafunzi wa Kiafrika walikuwa wakipatiwa mafunzo hayo ili waje kuwa wasaidizi wazuri kwenye timu ya uzalishaji wa sinema iliyopelekwa Afrika Magharibi na makao makuu ya kitengo cha filamu (CFU) yaliyokuwa London” (Van Beaver, uk. 23).
“Bantu Film Experiment” na “Colonial Film Unit” kwa namna fulani walikuwa wamejitwika “U-baba” kwa kugharamia masuala yote yaliyohusu sekta ya filamu, ingawa walikuwa na kasoro kubwa, walitawaliwa na ubaguzi wa rangi (racism).
Walikusudia kubadili kabisa historia ya filamu kwa kuanzisha aina tofauti ya sinema kwa ajili ya Waafrika badala ya ile iliyokuwa ikitumika barani Ulaya na Marekani, sababu kubwa ni kwamba waliwachukulia Waafrika kama watu wenye ufinyu wa akili kiasi cha kushindwa kuendana na sinema za Magharibi zilizoendelea.
Kwa maana nyingine ni kwamba walikusudia kuturudisha nyuma, yaani mwanzo wa historia ya filamu – kwa kutumia na kutufundisha mfumo wa kizamani (uncut scene), kupunguza urefu na mwenendo wa hadithi, na kutumia waigizaji wachache kadri iwezekanavyo.
Mtazamo wao haukuendana kabisa na ukweli halisi kuwa Waafrika walikuwa binadamu waliokamilika kiakili kama wao (Wazungu).
Mtazamo huo finyu uliwazuia hata watengeneza filamu wa Kikoloni kuuona ukweli huu: sinema zao zikaanza kuchosha (boring) na kutovutia tena watazamaji wa Kiafrika.
Mkosoaji mmoja maarufu J. Koyinde Vaughan aliandika maneno haya katika kipindi cha mwaka 1957 (tafsiri yangu):
“Ingawa watazamaji (audience) wa sinema wa Kiafrika walikuwa wakiongezeka kila kukicha, lakini walijikuta wakiwa hawana namna nyingine bali kutazama ‘sinema zinazochosha’ zilizoandaliwa na ‘CFU’ na kitengo cha mambo ya nje (foreign commercial entertainment film) ambazo zilionekana kushindwa kabisa kukidhi matakwa, licha ya ujuzi katika kazi za sanaa. Katika miji ya Kiafrika kama Freetown, Accra, Kumasi, Lagos, au Nairobi, charles Chaplin na waigizaji wengine maarufu wa Hollywood ndio walioendelea kutawala kwenye fikra na midomo ya watazamaji.”
Uingereza pia ilijikuta ikishindwa kuyatambua maisha na tamaduni za Kiafrika.
Kitengo cha sinema cha kikoloni “CFU” walikuwa wakikichukulia kila kitu cha Kiafrika kama ushirikina na kubaki nyuma ya wakati. Walikuwa wakilinganisha kila kitu cha Ulaya katika mazingira ya Kiafrika, kana kwamba walitaka kuua kabisa na kuzipoteza mila na desturi za Kiafrika katika dunia hii ili kuanzisha tamaduni za Ulaya (kwa mujibu wa Rouch, uk. 392).
Kutokana na ubabe, ubaguzi na kutoyaona hayo, vitengo vya filamu havikuweza kabisa kutoa mafunzo fasaha kwa Waafrika ili kuwafanya waweze kutengeneza kazi zao katika kiwango kilichokubalika. Kama wangeweza kujitengenezea kazi zao kwa usahihi, ‘CFU’ isingehitajika tena kwa kazi hizo.
Lakini haikuchukua muda mrefu hatimaye Uingereza ililitambua hilo na ndiyo maana waliamua kuachia ngazi katika miaka ya mwanzo ya hamsini, hasa hii ilitokana na mwanzo wa vuguvugu la nchi nyingi za Kiafrika kuanza kudai uhuru.
No comments:
Post a Comment