Dec 28, 2016

Wasanii mmejipangaje kwa mwaka 2017?

· Ni wakati sasa mfikirie kuwa na dira

Wafanyuakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) walipotembelea wauzaji wa filamu za Tanzania kuhakiki kazi zenye stempu za TRA

Mmoja wa wasanii wa filamu Tanzania, Vicent Kigosi, maarufu kama Ray

KWA Tanzania hakuna msanii yeyote anayeweza kusimama na kujisifu kwamba anakula halali kulingana na wingi wa jasho lake. Kila mmoja anatambua kuwa kuna mfumo kandamizi unaonyonya jasho la wasanii. Na ili kuendelea kuwanyonya, sasa wameaminishwa (na wale waliolishika soko) kuwa soko la kazi zao limekufa.

Wameaminishwa hivyo kwa kuwa soko la kazi zao linadhibitiwa na wafanyabiashara wachache, wasiozingatia taaluma na wasioongozwa na weledi. Ki ukweli kwa sasa soko halieleweki kabisa! Hali hii imesababisha watu kushindwa kutofautisha iwapo wanachokiona ni filamu, maigizo au mkanda wa harusi wenye “taito” za majina ya wasanii na wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia!


Kisingizio kikubwa cha soko kufa ni kuwepo kwa filamu za nje ambazo zinasemwa kuwa zinaharibu soko la filamu za wasanii wa ndani. Ukiachana na kisingizio hiki (ambacho binafsi sikiamini sana), hali ya soko kwa sasa inakatisha tamaa kabisa, kiasi kwamba kuna wakati nahisi kama wasanii (na hata viongozi wao) wengi wamefikia ukomo wa kufikiri, wameridhika au pengine wamekata tamaa, ingawa bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi!

Haiwezekani ulilie kuthaminiwa wakati umesahau kuwa mambo yote haya ni lazima yaanze ndani yako, kisha yaende kwenye jamii. Wasanii wengi wamekosa kujipa thamani na kujipenda, na hivyo imekuwa vigumu kutoa kwa wengine. Wengine wengi wanahisi hawana stahili ya mambo yote hayo. Wanajitazama wenyewe kama dhaifu kuliko wengine ama bora kuliko wengine.

Kwa hali ilivyo, wasanii wanapaswa wajue kwamba watu wanaoshabikia ujinga ni wachache sana siku hizi; na watu wa maana wanaoelewa nini wanafanya ni wengi zaidi na hawana muda na upumbavu. hivyo imefika mahali watu wanaendelea na mambo yao ya maana, na kuupa kisogo kabisa upande wa sanaa, hasa filamu za ndani, sekta inayoongoza kwa umbumbumbu, majungu na mambo yanayotia kichefuchefu katika jamii.

Kielelezo cha maendeleo ya nchi yoyote huchagizwa na ubora wa sanaa zake, hasa filamu na muziki. Wasanii wanapokuwa na maisha mazuri na wakawa wanaishi maisha ya msanii (kuishi kisanii), ni dalili kuwa nchi husika ina mwamko mzuri wa kiuchumi (angalia nchi zilizopiga hatua). Utajiri wa wasanii ni utajiri wa jamii, ni utajiri wa nchi.

Wengi tunatamani sana kuona uwepo wa mazingira bora ya soko huria, ili wasanii wafanye biashara bila longolongo, watengeneze fedha, wafikie daraja la kuitwa matajiri ili tuone raha yake. Wasanii wanapofanya biashara na sanaa ikapita kwenye mkondo wake barabara, husisimua uchumi wa sekta ya Viwanda na Biashara.

Pia huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii. Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu.

Katika nchi yenye mfumo bora au yenye kuwajali wasanii, wasanii huvuna stahili ya jasho lao na kutengeneza fedha za kutosha, jambo linaloweza kupunguza msongamano wa wananchi wanaojibana kutibu njaa katika sekta isiyo rasmi, kwani wengi wa waliopo huko, wana vipaji sana lakini hawavitumii kikamilifu kwa kuona na kuamini kwamba maisha kwenye sanaa ni magumu na hayalipi.

Biashara ya sanaa inaposhika nafasi stahiki na kujaa kwenye mifereji yake, inaweza kuchangamsha ubunifu kwa watu na kufanikisha kutengeneza ajira, badala ya kufikiria kuajiriwa tu. Mafanikio hasi ya wasanii wa Tanzania, ni sababu ya vipaji vingi kupotea.

Ni ukweli usiopingika kuwa kwa kiasi fulani kuna mafanikio katika sekta za filamu na muziki. Ni kweli filamu na muziki vimevuka mipaka ya Tanzania (japokuwa ni kwa nguvu binafsi za wasanii wachache). Ni kweli, filamu na muziki zinaitangaza sanaa ya Tanzania, lugha ya Kiswahili pamoja na nchi yetu. Lakini, mafanikio haya yanaweza yasionekane kwa sababu yanawabeba wasanii wachache sana, ukilinganisha na idadi ya wasanii wote nchini.

Hali iliyopo sasa, wapo wasanii wachache mno (wa filamu na muziki) wanaopata ‘promo mbuzi’ kwa sababu maalum. Wanapewa promo ili watumike kuuhalalisha mfumo dhalimu uliopo, hao ndiyo huwaponda wenzao wanaolalamika kuwa hawauzi, kwamba muziki wao au filamu zao hazikubaliki ndiyo maana wanaponda mfumo.

Pamoja na ripoti ya Shirika la Hakimiliki Duniani (WIPO) ya mwaka 2012 kuonesha mchango wa mapato uliotokana na shughuli za Hakimiliki (sanaa) kuwa zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini, au mchango wa ajira katika kazi zilizotokana na Hakimiliki kuwa zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii; inasikitisha kuona bado sekta hii inaendelea kuwa duni siku hadi siku.

Naamini kuna uchumi mkubwa sana ndani ya sanaa ila imekuwa vigumu sana kuuona au hata kuufikia kama soko lake linakuwa limebanwa. Lazima kwanza soko liwe jepesi na huria, wasanii watengeneze fedha na hapo ndipo itakuwa rahisi kuona manufaa mapana ya kiuchumi ndani ya jamii na taifa kwa jumla.

Ni wakati mwafaka sasa, unapotembelea shuleni na kumuuliza mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, matarajio yake nini kwa maisha yake ya baadaye, naye ajibu kuwa yeye ana kipaji, kwa hiyo anatamani kuwa msanii maarufu wa kimataifa, mwenye mafanikio na kutengeneza fedha nyingi. Msanii kwa kawaida mkondo wake ni maisha ya burudani. Starehe kwa sana!

Ni vigumu leo hii, umuulize mtoto anataka kuwa nani baadaye, naye akujibu kwamba anaota kuwa msanii mkubwa kwa sababu anapozungumza na wazazi wake, wanamwambia kazi nzuri ni Uinjinia, Udaktari, Urubani, Ubunge na ajira nyingine ambazo ni rasmi kwa sasa.

Mzazi mwenyewe anajua kwamba wasanii wanahangaika na njaa (wanaishi maisha ya kuigiza yasiyo na uhalisia). Hii ndiyo sababu mpaka leo, kila unapomuuliza swali msanii anayetambulika, alipotoka mpaka kufika alipo, atakwambia kwamba wazazi wake hawakutaka kabisa awe msanii. Si kwa sababu ni fani mbaya la hasha! Wanaona sanaa ni kupoteza muda, ni uhuni tu! Laiti wangeona mafanikio ya wasanii, wasingewakataza watoto wao hata kidogo.

Ifike wakati sanaa iwe ndiyo kimbilio la vijana wenye vipaji, na wazazi waone fahari kuwaunga mkono watoto wao pale wanapoona wanaonesha vipaji wakiwa wadogo kwa sababu ya kuamini kwamba watakuwa watu mashuhuri na wenye utajiri mkubwa.

Angalia Marekani: Mama yake Justin Bieber, alipoona mwanaye ana kipaji cha muziki, alimnunulia gita kwa sababu ya kuamini mwanaye anapita njia ya mafanikio. Leo hii anafaidi matunda ya kipaji cha mtoto wake. Ifike wakati, wazazi wote wawe na imani hiyo na wawekeze kwenye vipaji vya watoto wao.

Watu wanashindwa kufikiria na kubuni njia ya kutengeneza fedha kupitia sanaa kwa sababu ya kuona jinsi wasanii wanavyoishi kwa taabu. Inahitaji mtu mwenye akili ya uthubutu kama mwendawazimu, ndiye anaweza kuona kitu fulani hakilipi na kimewapotezea dira wengi, kisha naye akifanye kwa kuamini kitampa mafanikio.

Ni wazi kwamba hapa Tanzania inawezekana kabisa kufikia hatua nzuri na kuona matokeo ya faida ya sekta ya filamu, na sanaa zingine, katika ukuaji wa pato la taifa na la wasanii wenyewe kama wasanii watafanikiwa. Kujitangaza inahitaji fedha, msanii wa Kitanzania hawezi kujulikana kila kona ya Afrika, Ulaya, Asia, Marekani, Australia na kwingineko kama hajitangazi. Na bila dira, malengo na mikakati mizuri atajitangaza vipi?

Huu ni wakati sasa wasanii waandae dira itakayowaongoza kwenye mafanikio ya kisekta, ikifuatiwa na malengo yatakayofikiwa na mikakati mizuri. Katika kuboresha kazi na kujitangaza kimataifa wafikirie kuwasilisha proposals zao kwenye mamlaka za Utalii kama Tanapa, Bodi ya Utalii n.k., ili wawezeshwe, wadhaminiwe na kisha wasaidiwe kujitangaza nje ya nchi. Baada ya hapo kutakuwa na matokeo yanayoonekana.


Alamsiki.

1 comment:

Unknown said...

naomba unijibu hili swali.

hivi tatizo kubwa liko wapi? kwenye usambazaji au utengenezaji?