Msanii wa Afrika Kusini, Bibi Esther Mahlangu |
NI ukweli usiopingika kuwa sekta ya sanaa nchini
ipo chumba cha wagonjwa mahututi, na hatua za makusudi zinahitajika kuchukuliwa
(na wasanii wenyewe) kunusuru hali hii.
Nakumbuka miaka ya 1990 hadi 2000, wasanii wa
sanaa ya uchoraji walitingisha sana kutokana na kazi zao za michoro. Enzi hizo
wachoraji ndio wasanii waliokuwa maarufu (kwa majina yao), ingawa watu
hawakuwafahamu kwa sura, kwa kuwa michoro yao ilitamba sana kwenye magazeti na
majarida. Na waliweza hata kumiliki magari, japo hayakuwa ya kifahari.
Wachoraji kama James Gayo, John Kaduma, Ali Masoud
(Kipanya), Adam Luta, Abdul King.O, Nathan Mpangala, Noah Yongolo, Cloud
Chatanda, Paul Ndunguru, Chris Shola na wengine wengi (hata mimi nilikuwemo)
walimfanya hata mtoto mdogo kutamani kuwa kama wao.
Baada ya teknolojia ya computer kuingia nchini,
wengi wakaacha uchoraji na kujikita kwenye graphic designing, hivyo sanaa ya
uchoraji kubaki kwa wachache, hasa wachoraji wa picha za rangi kama tingatinga
n.k.
Zikaja zama za wanamuziki wa kizazi kipya (Bongo
Fleva) kutingisha, hata hivyo haikuchukua muda wasanii wa filamu nao wakaibuka
na kushika chati. Miziki na Filamu za Tanzania zikazipiga kumbo kazi za nje,
kama Nigeria, India, DR Congo n.k. hivyo, kumfanya kila kijana kutamani kuwa
mwigizaji au mwanamuziki.
Lakini leo hii, hakuna msanii yeyote (wa sanaa
yoyote nchini) anayeweza kusimama na kujisifu kwamba anakula halali kulingana
na wingi wa jasho lake. Wote wanalalamikia mfumo kandamizi unaonyonya jasho
lao.
Hata wazazi leo
hii hawapendi watoto wao wajishughulishe na sanaa maana wanajua kwamba
wasanii wanahangaika na njaa. Hii ndiyo sababu mpaka leo, kila unapomuuliza
msanii maarufu, alipotoka mpaka kufika alipo, atakwambia kwamba wazazi wake
hawakutaka kabisa awe msanii.
Si kwa sababu ni fani mbaya la hasha! Wanaona
sanaa ni kupoteza muda, ni uhuni tu! Laiti wangeona mafanikio ya wasanii,
wasingewakataza watoto wao hata kidogo.
Pamoja na kuwepo fursa
nyingi lakini tatizo kubwa hivi sasa linalowasumbua wasanii wetu ni dhana
dhalili (inferiority complex), kwani hawajiamini tena (hasa ukiwalinganisha na
wasanii kutoka Kenya, Uganda na kwingineko) eti kwa kuwa hawajui/ hawawezi
kuongea Kiingereza kwa ufasaha, hivyo, kujikuta wakipoteza fursa nyingi.
Mfano ni hivi karibuni, gazeti la HabariLeo lilimkariri
mwigizaji wa filamu nchini, Jackline Wolper akisema lugha ya Kiingereza imekuwa
kikwazo cha yeye kuigiza na waigizaji wa nje ya nchi, na inamfanya ashindwe
kufanya kazi na waigizaji wa nje ingawa wamekuwa wakija hapa nchini.
Hali hii imeufanya hata uchumi wa nchi hii kuwa
tegemezi mno kwa kuwa hatuna tena wabunifu au wenye maono. Nadhani utakubaliana
nami kuwa ubora wa sanaa ni kielelezo cha maendeleo ya nchi.
Wasanii wanapokuwa na maisha mazuri na wakawa
wanaishi maisha ya msanii yasiyo ya kuigiza, ni dalili kuwa nchi husika ina
mwamko mzuri wa kiuchumi (angalia nchi zilizopiga hatua). Utajiri wa wasanii ni
utajiri wa jamii, ni utajiri wa nchi.
Sanaa ni kilainishi (grisi) cha uchumi wa sekta
nyingine nyingi. Kwa maana nyingine, mafanikio ya sanaa ndiyo msisimko wa
uchumi kwa taifa. Pia huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea
kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii.
Hata Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka
kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu. Ni ukweli
usiopingika kuwa uchumi wa sanaa unaweza kuibeba jamii kwa upana wake. Pia
Sanaa inapotumika vizuri hufanya kazi kama mhimili huru unaosimamia dola.
Katika nchi ambayo Bunge linatawaliwa na ushabiki
wa kivyama, vyombo vya habari navyo vikawa kimya, sanaa inaweza kuwa nyenzo
imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na kuieleza jinsi mambo yasivyo sawa.
Sanaa kwa kushirikiana na vyombo vya habari na
Bunge, inaweza kuwa daraja rahisi la jamii kujua kinachoendeleaa kwenye nchi
yao na hata kujua udhaifu au uimara wa serikali. Hapa ni suala la namna ya
kuitumia sanaa.
Mwananchi anaweza asiwe mfuatiliaji wa Bunge,
hasomi magazeti na hataki kusikiliza taarifa za habari lakini akasikiliza
nyimbo, akaangalia filamu au kusoma katuni na michoro mingine na kupata ujumbe.
Na ukitaka uiue jamii yoyote ile, basi haribu
mfumo wake wa sanaa na wasanii wajikite kwenye mambo mengine bila kumulika
matatizo ya jamii wanayoishi. Inaweza kuchukua miaka 50 kubadili fikra za
wananchi lakini tungo na msimamo wa wasanii kwa mwezi mmoja, zinatosha kufanya
mabadiliko makubwa kwenye jamii.
Nimalize makala yangu kwa kumtazama Bibi Esther Mahlangu, ambaye kwa sasa ana miaka
81. Bibi huyu alizaliwa mnamo 11 Novemba 1935, huko Middleburg,
Mpumalanga-Afrika Kusini. Anaongea vyema lugha yake ya Ndebele, hajui lugha ya
Kiingereza hata kidogo.
Gari iliyochorwa kwa ustadi mkubwa na Bibi Esther Mahlangu |
Bibi Esther Mahlangu
kupitia karama yake ya uchoraji, mnamo mwaka 1991 aliweza kubuni na kuchora
michoro [patterns] kwenye gari aina ya BMW 525i na kuwa gari ya kwanza kutoka
katika company ya BMW (Bavarian Motor Works) kuchorwa na mbunifu toka Afrika
kuipitia kitengo chao cha BMW Art Car.
Ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza inayoonesha ubunifu wa Bibi Esther Mahlangu |
Mwaka 1997, kazi ya
Esther Mahlangu ilitumiwa na shirika la British Airways kuchora mkia wa ndege
zao, katika namna ileile ya mbinu na ubunifu alioutumia kuchora BMW 525i,
ubunifu wake uliwafanya kampuni ya Fiat, kumpa nafasi ya kuchora gari yao aina
ya Fiat 500 katika mji wa Turin mwaka 2007.
Bibi Esther Mahlangu
amethubutu na hatimaye ameweza kuishi vizuri kwa kipaji chake ingawa hajaenda
shule, na wala hajui kuongea Kiingereza kama ambavyo wengi wetu
tunavyojidanganya.
Ujumbe wangu kwa
Wasanii wa Tanzania: Usiogope kuchangamkia fursa kwa kuogopa kutofahamu kwa
ufasaha lugha ya Kiingereza, wala usihuzunike kwa kukosa cheti. Badala yake jivunie
hazina yako ya maarifa na kipaji chako, sababu kipaji kilichopakwa mafuta
kinafuatwa na lugha zote ili kuleta flava na ubora.
No comments:
Post a Comment