SEKTA YA FILAMU nchini imekuwa inakua kwa kasi na kuwa
kimbilio la vijana wengi, hata wale walioshindwa (failures) katika sekta
zingine. Ukuaji wake umeambatana na changamoto nyingi katika kufikia ubora
unaokubalika kimataifa kwenye filamu zetu.
Filamu ni nguzo muhimu sana ya Utamaduni wa nchi. Filamu
zimeibuka kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na
mawasiliano ghali katika karne ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya
sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni
katika mataifa mengi kama hii.
Lakini kwa miaka ya karibuni filamu zetu – zilizoanza
kututangaza nje ya mipaka yetu – zimeanza kukosa mwelekeo, na zinatupeleka
kusikojulikana. Filamu zetu nyingi kwa muda mrefu zimekuwa ni za kulipuwa tu huku
hadithi zikiwa si za asili yetu bali tunanakili kwa wenzetu zenye vitendo na
maudhui ya jamii za nje!
Watayarishaji wetu wa sinema wanalipua kazi; waigizaji
hawalipwi vizuri; utengenezaji sinema unafanywa haraka haraka. Sinema zinatengenezwa
kwa wiki moja hadi mbili na zinatolewa ndani ya mwezi mmoja tu. Haraka haraka… Halafu
tunataka kujilinganisha na tasnia za filamu zilizoendelea, kama Hollywood, Bollywood
nk.
Katika miongo kadhaa iliyopita sinema nyingi zenye
mafanikio zimetolewa huko Hollywood. Hilo limekuwa na uvutano mkubwa
ulimwenguni pote kwani sinema nyingi za Marekani hutazamwa katika nchi nyingine
majuma machache au hata siku chache tu baada ya kuoneshwa kwa mara ya kwanza
nchini Marekani.
Sinema fulani hata zimeoneshwa kwa mara ya kwanza tarehe
ileile duniani kote. Rais wa usambazaji wa filamu nchini Marekani wa shirika la
Warner Brothers, Dan Fellman, anasema: “Soko la ulimwenguni kote la uuzaji wa
sinema linazidi kukua nalo linasisimua sana, kwa hiyo tunapotengeneza sinema,
huwa tunaitengeneza kwa ajili ya soko la ulimwenguni kote.” Sasa kuliko wakati
mwingine wowote, kile kinachotendeka huko Hollywood huathiri biashara ya sinema
ulimwenguni.
Lakini kupata faida kutokana na sinema si rahisi kama tunavyodhani.
Sinema nyingi zinahitaji kiasi kikubwa mno cha pesa ili kulipia gharama ya
kuzitengeneza na kuziuza. Na kufanikiwa kwake kunategemea watazamaji ambao mtu
hawezi kutabiri watapendezwa na nini. Huwezi kujua ni lini jambo fulani
litawavutia au kuwasisimua watazamaji.
Kwa hiyo watengenezaji wa sinema huongezaje uwezekano wa
sinema yao kufanikiwa? Ili kupata jibu, tunahitaji kuelewa mambo machache ya
msingi yanayohusika katika utengenezaji wa sinema.
Mara nyingi, matayarisho yanayofanywa kabla ya upigaji
picha ndiyo sehemu muhimu zaidi ambayo huchukua muda mrefu katika utengenezaji
wa sinema. Kama tu ilivyo na mradi wowote mkubwa, mafanikio yake hutegemea sana
matayarisho. Inatumainiwa kwamba pesa zozote zinazotumiwa wakati wa matayarisho
zitapunguza sana gharama za kutengeneza sinema yenyewe.
Kutengenezwa kwa sinema huanza na hadithi fulani ambayo huenda ikabuniwa
au ikategemea matukio halisi. Mwandishi huandika hadithi hiyo kwenye hati
(script). Hati hiyo inaweza kufanyiwa marekebisho mengi kabla ya rasimu ya
mwisho kupatikana.
Rasimu hiyo ya mwisho huwa na wahusika pamoja na maelezo
mafupi kuhusu kitendo kitakachofanywa. Pia hutoa maagizo mengine kama vile
mahali ambapo kamera zitakuwa na mabadiliko yatakayofanywa katika kila onesho.
Hata hivyo, ili sinema iweze kukidhi mahitaji hati hiyo hutegemea
inatolewa msimu gani na imekusudiwa kuwalenga watu gani zaidi. Ila watayarishaji
wengi hupendezwa hasa na sinema ambayo itawavutia zaidi vijana. Hati inayofaa
hata zaidi ni ile itakayowavutia watu wa umri mbalimbali.
Mtayarishaji akiona kwamba hati inaweza kuwa sinema
nzuri, huenda akainunua na kumpa muongozaji na mwigizaji maarufu. Kuwa na mwongozaji
na mwigizaji maarufu kutafanya sinema hiyo ivutie sana wakati itakapotolewa.
Hata katika hatua hii ya kwanza, waongozaji na waigizaji maarufu wanaweza
kuwavutia wawekezaji wanaohitajika ili kugharimia utayarishaji wa sinema hiyo.
Hatua nyingine ya matayarisho ni kutengeneza michoro mbalimbali
ya filamu hiyo hasa ile inayohusisha mapigano. Michoro hiyo humwongoza
mpiga-picha za sinema nayo husaidia kupunguza wakati unaotumiwa kupiga picha. Hakuna
jambo baya zaidi kama kupoteza wakati wa kupiga picha kwa sababu tu ya kutojua
mahali ambapo kamera inapaswa kuwa.
Kuna mambo mengine mengi muhimu yanayopaswa
kushughulikiwa wakati wa matayarisho. Kwa mfano, picha zitapigiwa wapi? Je,
itakuwa lazima kusafiri? Je, kuna picha zitakazopigwa ndani ya nyumba, nayo
itapambwaje? Je, mavazi maalum yatahitajika? Ni nani atakayeshughulikia
mwangaza, kupamba na kutengeneza nywele za waigizaji? Na vipi kuhusu sauti,
madoido, na yule atakayeigiza sehemu hatari badala ya mwigizaji mkuu?
Hayo ni baadhi ya mambo yanayohitaji kufikiriwa hata
kabla ya kupiga picha za filamu. Ukitazama majina yanayooneshwa mwishoni mwa
sinema inayotazamiwa kuleta faida kubwa, huenda ukaona kwamba mamia ya watu
walihusika kuitayarisha! Hii inamaanisha kua ni watu wengi sana huhusika katika
kutengeneza filamu nzuri.
Kupiga picha za sinema kunaweza kuchukua wakati mwingi,
kunaweza kuchosha, na pia kunaweza kugharimu pesa nyingi. Kwa kweli, kupoteza
dakika moja tu kunaweza kugharimu maelfu ya dola. Nyakati nyingine inabidi waigizaji,
wafanyakazi, na vifaa visafirishwe hadi sehemu ya mbali. Hata hivyo, haidhuru
picha hizo zitapigiwa wapi, lazima pesa nyingi sana zitatumika kila siku.
Watu wanaoshughulikia mwangaza, wale watakaowapamba na
kuwatengeneza nywele waigizaji huwa kati ya watu wa kwanza kufika mahali ambapo
picha zitapigiwa. Kila siku ya kupiga picha, waigizaji wakuu hupambwa kwa saa
kadhaa. Kisha picha hupigwa kwa siku nzima.
Mwongozaji husimamia kwa uangalifu kupigwa picha kwa kila
onesho. Inaweza kuchukua siku nzima kupiga picha za onesho fupi sana. Picha za
maonesho mengi katika sinema hupigwa kwa kutumia kamera moja, kwa hiyo, onesho
moja linaweza kupigwa picha kadhaa kutoka pembe tofauti-tofauti.
Isitoshe, huenda onesho lilelile likapigwa picha mara
kadhaa ili kupata picha bora zaidi au kurekebisha tatizo la kiufundi. Ikiwa onesho
ni refu, huenda picha 50 au zaidi zikapigwa! Kwa kawaida, mwishoni mwa
kila siku, mwongozaji huchunguza picha zote na kuamua ni zipi zitakazotumiwa.
Kazi ya kupiga picha inaweza kuchukua majuma au hata miezi kadhaa.
Baada ya upigaji picha ndipo hatua ya kuunganisha sinema iliyotengenezwa
huanza. Katika hatua hii, picha zilizopigwa huboreshwa na
kupangwa zinavyopaswa kufuatana. Kwanza, muziki utakaotumiwa huambatanishwa na sinema hiyo. Kisha, mhariri
huunganisha sehemu za sinema hiyo na kufanyiza nakala ya kwanza isiyo kamili.
Madoido ya sauti na picha pia huongezwa katika hatua
hiyo. Nyakati nyingine kompyuta hutumiwa kutia madoido hayo katika hatua hii
ambayo ni mojawapo ya sehemu ngumu zaidi za utengenezaji wa filamu. Kazi
inayofanywa katika hatua hii inaweza kuifanya sinema ivutie na ionekane kuwa
halisi.
Muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema hiyo huongezwa
katika hatua hiyo, na jambo hilo ni muhimu katika filamu za leo. Kwa watengenezaji
wa sinema makini hutaka muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema, nao
hawataki muziki wa dakika ishirini tu au vipindi vifupi vya muziki, bali wao
hutaka muziki utakaochezwa kwa muda unaozidi saa nzima.
Nyakati nyingine filamu iliyoboreshwa huoneshwa watu
wachache ambao wanaweza kuwa rafiki wa mwongozaji au wafanyakazi wengine ambao
hawakuhusika katika kutengeneza filamu hiyo. Ikitegemea jinsi watakavyoitikia,
mwongozaji anaweza kupiga picha upya maonesho fulani au kuyaondoa kabisa.
Katika visa fulani, umalizio wote wa filamu ulibadilishwa kwa sababu watu
walioitazama kwanza hawakuupenda.
Hatimaye, filamu iliyokamilika huoneshwa kwenye majumba
ya sinema na kabla kuuzwa kama bidhaa kwa ajili ya kutazama nyumbani (DVD). Ni
wakati huo tu ndipo inaweza kujulikana ikiwa sinema hiyo itafanikiwa au
haitafanikiwa, au itakuwa ya wastani.
Lakini mambo mengi yanahusika kuliko kupata faida. Sinema
kadhaa zikikosa kufanikiwa zinaweza kuharibu sifa ya mwongozaji na matarajio ya
mwigizaji kupata kazi.
Kwa watengenezaji wetu wa filamu wanapaswa kujua kuwa
watu wanaotafuta sinema, kwa ujumla hawafikirii ikiwa watengenezaji wa sinema
hiyo watapoteza kazi zao au la. Wao hujiuliza yafuatayo: Je, nitafurahia sinema
hii? Je, inafaa nitumie pesa zangu ili kuitazama? Je, sinema hii itanivutia au
itanichukiza? Je, inawafaa watoto wangu? Hivyo, watengenezaji sinema wanapaswa
kuwafikiria zaidi wateja wao kuliko kujifikiria wao.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment