Watoto wanaangalia televisheni |
MAJUZI jirani yangu mmoja (ambaye amenunua kisimbuzi hivi
karibuni) aliniita nyumbani kwake na kuniomba nimsaidie kuweka namba za siri
(password) kwenye baadhi ya chaneli za televisheni yake ili kuwadhibiti watoto
wake wasiweze kuangalia sinema na vipindi visivyo na maadili. Aliamua kufanya
hivyo baada ya kugundua uwepo wa chaneli zinazoonesha mambo yenye ukakasi.
Kwa sasa ni jambo la kawaida sana kwa watoto wengi
kutazama filamu, televisheni, video, kucheza michezo (games) ya kompyuta, na
kutumia Intaneti. Kulingana na makadirio fulani, watoto na vijana hutazama na
kuvitumia vyombo vya habari kati ya mara 20 au 30 zaidi ya wakati
wanaotumia kufanya mambo na familia zao. Jambo
hilo huwafanya watoto wapate habari nyingi zenye kudhuru.
Televisheni huwa kama “mhadithiaji mkuu, mlezi wa watoto
na kifaa kinachoathiri maoni ya umma,” inabainisha ripoti ya Not in the Public Interest—Local
TV News in America, iliyokusanywa na
shirika moja linalochunguza habari huko Marekani.
Televisheni iko kila mahali. Imeenea sana kama moshi wa
sigara hewani. Kutazama vipindi vya televisheni kwa muda mrefu bila kuwa mteuzi
husababisha madhara kama vile kuvuta moshi wa sigara ulio hewani — hasa watoto.
Kuhusu uhalifu na jeuri kwenye televisheni, ripoti
hiyohiyo yasema kwamba “uchunguzi chungu nzima umeonesha kwamba kutazama picha za
jeuri huathiri sana kusoma, makuzi na hisia za watoto.”
Katika miaka ya hivi karibuni, watu wamekuwa na maoni
mbalimbali kuhusu kuongezeka kwa ngono, jeuri, na lugha chafu katika sinema au
televisheni. Mambo hayo ni muhimu kwa wazazi na wote wanaothamini sana viwango
vya maadili kuwa na tahadhari nayo.
Mwanadada mmoja aliwahi kulalamika: “Ninapopuuza dhamiri
yangu na kurudi kutazama sinema fulani, huwa nahisi vibaya sana. Mimi huona
aibu kwa ajili ya wale waliotengeneza sinema hiyo mbovu na kwa ajili yangu
mwenyewe kwa kuitazama. Ni kana kwamba kutazama sinema hiyo kumenishushia
heshima.”
Ninachowashauri wazazi, hawapaswi kulalamika tu bali kuwapa
watoto wao mwanzo mzuri maishani. Tukumbuke pia televisheni
inaweza kuwa kifaa kizuri sana cha kujifunzia. Hata
hivyo, akili na miili ya watoto inaathiriwa kwa kutumia muda mwingi kutazama
televisheni, na hivyo kuwanyima nafasi ya kushiriki utendaji unaowasaidia kuwa
wabunifu, kujifunza, na kuchangamana na watu.
Kuna ripoti moja ya uchunguzi baada ya kuchunguza mazoea
ya kutazama televisheni ya watoto 2,500, watafiti katika Hospitali moja ya
Watoto nchini Marekani walitambua kwamba kadiri watoto walio na umri wa kati ya
mwaka mmoja hadi miaka mitatu walivyotazama televisheni sana, ndivyo hatari yao
ya kukosa kuwa makini ilivyoongezeka walipofikia umri wa miaka saba.
Watoto hao walikuwa wajeuri kupita kiasi na hawakuwa
watulivu na waliweza kukaza fikira kwa muda mfupi tu. Wazazi wengi ambao watoto
wao walikuwa na matatizo ya kukaza fikira walitambua kwamba hali hiyo
ilibadilika na kuwa nzuri baada ya kuwazuia watoto wao kutazama televisheni.
Kama wazazi tunapaswa kutafuta namna ya kufanya ili
kupunguza muda ambao watoto wanatumia kutazama televisheni. Ripoti ya watafiti
katika Hospitali ya Watoto inatoa mapendekezo yafuatayo:
Weka mipaka kuhusu ni wakati gani na kwa muda gani watoto
wako wanaweza kutazama televisheni kila siku. Epuka kutumia televisheni kuwa
mlezi. Badala yake, mhusishe mtoto wako katika kazi nyingi iwezekanavyo za
nyumbani. Chagua vipindi ambavyo mtoto wako anaweza kutazama, na uizime
televisheni baada ya vipindi hivyo kwisha. Inapowezekana, tazama vipindi
ulivyochagua pamoja na mtoto wako na mzungumzie kuhusu mambo mnayotazama.
Mwishowe, weka mipaka kuhusu muda ambao wewe mwenyewe unatumia kutazama
televisheni.
Hata hivyo, ieleweke kuwa kulalamikia mambo yanayooneshwa
katika sinema si jambo jipya. Wakati sinema zilipoanza kutengenezwa, watu
walikasirika sana walipoona sinema zilizokazia zaidi mambo ya ngono na uhalifu.
Hatimaye, katika miaka ya 1930, sheria ambazo ziliweka mipaka kuhusu mambo
ambayo yangeweza kuoneshwa katika sinema zilitungwa nchini Marekani.
Kulingana na machapisho ya
The New Encyclopædia Britannica, sheria
hizo mpya “zilikandamiza sana, na kuzuia kuoneshwa kwa jambo lolote ambalo
linahusiana na mambo ambayo hufanywa na watu wazima. Zilikataza kuoneshwa kwa
‘mambo yoyote ya kimahaba’ na uzinzi, ngono haramu, utongozaji, na ubakaji wala
mambo hayo hayakupaswa kutajwa isipokuwa tu iwe ni lazima kabisa kwa sababu
yalihusiana na hadithi inayosimuliwa, na waliofanya mambo hayo waadhibiwe
kufikia mwisho wa sinema hiyo.”
Kuhusiana na jeuri, filamu “hazikupaswa kuonesha au kuzungumzia
silaha zilizokuwa zikitumika wakati huo, kuonesha uhalifu ukitendeka, polisi wakiuawa na wahalifu, ukatili
au uchinjaji mwingi, au kuonesha uuaji kimakusudi au kujiua, isipokuwa mambo
hayo yawe ya lazima kwa hadithi hiyo. Haikuruhusiwa kuonesha kwamba uhalifu
ulifaa chini ya hali zozote zile.” Kwa ufupi, sheria hizo zilisema kwamba
“hakuna picha itakayooneshwa ambayo itashusha viwango vya maadili vya wale
wanaoitazama.”
Kufikia miaka ya 1950, watayarishaji wengi wa filamu huko
Hollywood walikuwa wakipuuza sheria hizo wakihisi kwamba zilikuwa zimepitwa na
wakati. Hivyo, mnamo 1968, sheria hizo ziliondolewa na badala yake viwango vya
sinema vikawekwa. Hata hapa kwetu tunayo
Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza, inayoshughulikia viwango na kupanga
madaraja ya sinema.
Kwa sababu ya viwango na madaraja hayo, sinema inaweza
kuonesha wazi mambo yasiyofaa, lakini inatiwa alama kuwaonya watu kwamba
inapaswa kutazamwa tu na “watu wazima.” Lengo kubwa likiwa ni “kuwaonya wazazi
ili waweze kuamua sinema ambazo watoto wao wanaweza kutazama na zile ambazo
hawapaswi kutazama.”
Nchi nyingi ulimwenguni zina mfumo kama huo ambao alama
fulani hutiwa kuonesha sinema fulani inapaswa kutazamwa na watu wa umri fulani.
Kwa kuongezea, huenda viwango vya sinema vikatofautiana katika nchi mbalimbali.
Huenda sinema inayoonwa kuwa haiwafai vijana katika nchi moja ikaonekana kuwa
inafaa katika nchi nyingine.
Katika nchi nyingi, wenye mamlaka hujaribu kuweka sheria
na viwango kuhusu umri ambao mtu anaruhusiwa kuona filamu fulani. Hata hivyo,
kulingana na ripoti mbalimbali, si nyakati zote ambazo watoto na wazazi huelewa
viwango hivyo, au wao huzipuuza. Pia, inajulikana kwamba majumba mengi ya
kuoneshea filamu na maktaba za kukodi mikanda ya video hupuuza sheria zilizowekwa
kuhusu umri. Isitoshe, programu fulani na filamu hazina viwango vya umri.
Michezo mingi ya video, ya kompyuta, na hata vibonzo
vilivyotayarishwa hasa kwa ajili ya watoto, huwa na mambo ambayo yanaweza
kudhuru.
Ripoti moja inasema kwamba kila familia “ina wajibu wa
kuamua filamu na programu ambazo watoto watatazama.” Lakini swali muhimu la
kujiuliza: “Je, sisi watu wazima tuna nia, uwezo, na njia ya kuwalinda watoto
kutokana na madhara ya vyombo vya habari?”
Nikiwa mzazi huwa nawajibika kusoma maoni ya wachambuzi
au kutazama sehemu ndogo ya sinema ambazo zitaoneshwa kwenye televisheni kabla
ya kuwaruhusu watoto wangu kuangalia. Pia hutafuta habari kuhusu sinema hiyo
kwenye Intaneti. Na kama nikihisi kwamba sinema hiyo haifai, hutoa sababu kwa
watoto kwanini sitaki waangalie sinema hiyo.
Haya yanapaswa kufanywa kwa uwazi na kueleza sababu zitakazowasaidia
watoto kuelewa, ieleweke kuwa kama wazazi wakiwakataza watoto wao vitumbuizo
fulani na kukosa kuwapa vitumbuizo vinavyofaa, huenda watoto hao wakajaribu
kutosheleza tamaa zao kwa siri.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment