Sep 30, 2015

KAMPENI 2015: U wapi uchumi na utajiri wa wasanii?

Wasanii waliopo katika kampeni ya Mama Ongea na Mwanao mpigie kura Dk. Magufuli
KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zimepambwa zaidi na wasanii mbalimbali. Kumekuwepo na mhemuko wa ajabu wa wasanii kujitokeza kwenye majukwaa ya siasa, wengi wao wakijipambanua kuwa wafuasi au mashabiki wa vyama na wanasiasa fulani. Zikiwa zimesalia siku 22 tu kabla ya kupiga kura kuichagua serikali ijayo (Rais, Wabunge na Madiwani), hali bado ni ya mashaka kwa sekta ya sanaa.

Wasanii wanatumika kwa kiasi kikubwa kwenye majukwaa ya siasa, kiasi cha mikutano kugeuka kuwa matamasha ya burudani, huku wakiwa hawajui majaliwa yao kuhusu ustawi wa sekta ya sanaa, zaidi ya kupigwa porojo na ahadi zisizotekelezeka.


Nimewahi kutahadharisha kuhusu wasanii kutumika kwenye majukwaa ya siasa huku wakiwa hawana ajenda yoyote. Wasanii wanapaswa kuwa macho sana na kuacha kuendekeza njaa. Wanapaswa kung’amua mwenendo mbaya unaowapeleka kwenye shimo la mauti (kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa).

Ni ukweli usiopingika kuwa sekta ya filamu (na sanaa kwa ujumla) ipo chumba cha wagonjwa mahututi, na hatua za makusudi zinahitajika kuchukuliwa kunusuru hali hii. Hali hii ni tofauti na kile ambacho Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za wanyonge nchini (Mkurabita) inataka kutuaminisha kuwa imeirasimisha sekta hii ili kuwafanya wasanii wafanye kazi kwenye mazingira yaliyo rasmi.

Hadi sasa, serikali inafanya maigizo tu, kwani hakuna urasimishaji wowote uliofanyika wenye tija zaidi ya kuwaingiza wasanii na kazi zao kwenye mfumo wa stempu za TRA. Pia katika nchi hii tumekuwa tukiishi katika nadharia zaidi, kwani matamko yoyote yanayotolewa na viongozi huwa hayafanyiwi kazi, hata kama kinachoongelewa kina tija.

Inasikitisha sana pale maisha ya wasanii yanapokuwa maisha ya kuigiza, wanaonekana kama ni wenye neema, kumbe wanaongoza kwa maisha mabaya. Na pale inapotokea neema basi huwa ni kwa muda fulani tu, hasa kipindi kama hiki wanapotumiwa na wanasiasa kwa maslahi ya wanasiasa katika kufanikisha jambo lisilowahakikishia (wao) uhakika wa soko la kazi zao.

Kwa Tanzania hakuna msanii yeyote anayeweza kusimama na kujisifu kwamba anakula halali kulingana na wingi wa jasho lake. Kila mmoja anatambua kuna mfumo kandamizi, mfumo unaonyonya jasho la wasanii.

Ubora wa filamu (na sanaa kwa ujumla) ni kielelezo cha maendeleo ya nchi. Wasanii wanapokuwa na maisha mazuri na wakawa wanaishi maisha ya msanii (kuishi kisanii), ni dalili kuwa nchi husika ina mwamko mzuri wa kiuchumi (angalia nchi zilizopiga hatua). Utajiri wa wasanii ni utajiri wa jamii, ni utajiri wa nchi.

Ni ukweli usiopingika kuwa uchumi wa sanaa unaweza kuibeba jamii kwa upana wake. Nadhani utakubaliana nami kuwa kuna umuhimu mkubwa sana jamii ikiwa na wasanii wenye uwezo mkubwa wa kifedha na nguvu ya kumiliki mali.

Nimewahi kusoma machapisho fulani yenye kuelezea jinsi ambavyo sanaa inapotumika vizuri hufanya kazi kama mhimili huru unaosimamia dola. Katika nchi ambayo Bunge linakosa meno dhidi ya udhaifu wa serikali (kama Tanzania), vyombo vya habari navyo vikawa kimya, sanaa inaweza kuwa nyenzo imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na kuieleza jinsi mambo yasivyo sawa.

Sanaa kwa kushirikiana na vyombo vya habari na Bunge, inaweza kuwa daraja rahisi la jamii kujua udhaifu wote wa serikali au hata uimara wake. Hapa ni suala la namna ya kuitumia sanaa. Mwananchi anaweza asiwe mfuatiliaji wa Bunge, hasomi magazeti na hataki kusikiliza taarifa za habari lakini akasikiliza nyimbo au kuangalia filamu.

Ndiyo maana inaelezwa kuwa ukitaka uiue jamii yoyote ile, basi haribu mfumo wake wa sanaa na wasanii wajikite kwenye mambo mengine bila kumulika matatizo ya jamii wanayoishi. Inaweza kuchukua miaka 50 kubadili fikra za wananchi lakini tungo na msimamo wa wasanii kwa mwezi mmoja, zinatosha kufanya mabadiliko makubwa kwenye jamii.

Bahati mbaya sana tuna mfumo kandamizi dhidi ya sanaa na wasanii, na hata wasanii wenyewe kutojua nguvu waliyonayo. Wanashindwa kuelewa kuwa wakiwa pamoja na kutoa msimamo wa pamoja, tamko lao linaweza kutikisa nchi kuliko wabunge kususia vikao vya Bunge. Ndiyo maana wajanja (wanyonyaji) wenye kuelewa hili wameamua kwa makusudi kuwagawa wasanii ili wasiwe na maono yenye kushabihiana. Kilichobaki kwa sasa ni wasanii wao kwa wao hawaelewani.

Tusidanganyane, wanasiasa wa nchi hii hawana nia njema na sekta hii, japo wanazunguka na wasanii kwenye kampeni zao wakiwatumia katika kuwafikia wananchi, baada ya uchaguzi kupita wasanii watarudi tena kwenye msoto. Sijamuona mgombea mwenye nia ya dhati ya kumkomboa msanii, na simuoni anayehubiri kuhusu uchumi mkubwa uliopo ndani ya sekta ya sanaa. Nina hakika hawana maono hayo, japo baadhi yao wanajidai kuzifahamu shida za wasanii.

Wanasiasa wanaishia kupiga porojo tu, lakini hakuna anayejua thamani ya sanaa. Binafsi natamani sana kuona kila msanii mwenye kipaji na aliye na jitihada za kufanikiwa anafanikiwa na kutengeneza fedha ili kurahisisha mirija mingi ya uchumi kupata mtiririko wenye afya. Imesemwa kuwa sanaa ni kilainishi (grisi) cha uchumi wa sekta nyingine nyingi. Au kwa maana nyingine, mafanikio ya sanaa ndiyo msisimko wa uchumi kwa taifa.

Nimekuwa natamani sana kuona uwepo wa mazingira bora ya soko huria, ili wasanii wa Watanzania wafanye biashara bila longolongo, watengeneze fedha, wafikie daraja la kuitwa matajiri ili tuone raha yake. Wasanii wanapofanya biashara na sanaa ikapita kwenye mkondo wake barabara, husisimua uchumi wa sekta ya Viwanda na Biashara.

Pia huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii. Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu.

Hivi, ni chama gani au mwanasiasa yupi anayeweza kusimama akatuonesha ilani ya chama chake inayoeleza kuhusu jambo hili, japo kwa ufupi?

Katika nchi yenye mfumo bora au yenye kuwajali wasanii, wasanii huvuna stahili ya jasho lao na kutengeneza fedha za kutosha, jambo linaloweza kupunguza msongamano wa wananchi wanaojibana kutibu njaa katika sekta isiyo rasmi, kwani wengi wa waliopo huko, wana vipaji sana lakini hawavitumii kikamilifu kwa kuona na kuamini kwamba maisha kwenye sanaa ni magumu na hayalipi. Sekta hii imekuwa ni ya kuganga njaa tu!

Biashara ya sanaa inaposhika nafasi stahiki na kujaa kwenye mifereji yake, inaweza kuchangamsha ubunifu kwa watu na kufanikisha kutengeneza ajira, badala ya kufikiria kuajiriwa tu. Mafanikio hasi ya wasanii wa Tanzania, ni sababu ya vipaji vingi kupotea.

Hakuna ilani ya chama chochote ambayo imejaribu kugusia au kutueleza namna watakavyobuni njia ya kutengeneza fedha kupitia sanaa kwa sababu ya kuona jinsi wasanii wanavyoishi kwa tabu.

Hivi, hawa wanasiasa (wanaohubiri maisha bora) wanadhani hali hii itaendelea hivi hadi lini bila kuwepo dira? Ikumbukwe kuwa hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kuthubutu kuona kitu fulani hakilipi na kimewapotezea dira wengi, kisha awekeze au akifanye kwa kuamini kitampa mafanikio.

Naamini ni ndoto ya kila mtu (hata mimi) kuwa na maisha mazuri, kwa hiyo watu huangalia maeneo ambayo yanalipa. Hivi tutakuwa ni taifa la aina gani ambalo kila kijana anatamani kuwa ofisa wa TRA au kufanya kazi Idara ya Uhamiaji?

Sababu ni kwamba wanaona jinsi maofisa hao wanavyofanikiwa ndani ya muda mfupi. Wanaiba kwa kutengeneza mirija ya rushwa kwa wafanyabiashara na wahamiaji, kwa hiyo ndani ya kipindi kifupi, watu wanapiga hatua kubwa. Umiliki wa majumba, magari ya kifahari na uwekezaji mwingine.

Binafsi sikushangaa siku niliposhuhudia umati wa watu zaidi ya 70,000, kwenda kufanyiwa usaili Idara ya Uhamiaji. Hiyo ni kuonesha namna gani ajira zilivyo ngumu. Ukweli ni kwamba katika idadi hiyo ya watu, wapo wengi wenye vipaji lakini ni ngumu kuvionesha wala kuvitumia kwa mfumo uliopo.

Hata wazazi huwa hawapendi watoto wao wajishughulishe na sanaa maana wanajua kwamba wasanii wanahangaika na njaa. Hii ndiyo sababu mpaka leo, kila unapomuuliza msanii anayetambulika, alipotoka mpaka kufika alipo, atakwambia kwamba wazazi wake hawakutaka kabisa awe msanii. Si kwa sababu ni fani mbaya la hasha! Wanaona sanaa ni kupoteza muda, ni uhuni tu! Laiti wangeona mafanikio ya wasanii, wasingewakataza watoto wao hata kidogo.


Alamsiki.

No comments: