Feb 4, 2015

Dunia na historia ya filamu

D. W. Griffith

Muongozaji wa filamu Tanzania, John Lister Manyara
SINEMA za mwanzo zilijielekeza kama vile sehemu ya jukwaa mbele ya pazia. Kamera iliwekwa katika sehemu moja na matendo yote katika tukio zima yalifanyika ndani ya fremu moja ya kamera na kwa pigo moja (one shot). Mtazamo wa watazamaji kipindi hicho haukutofautiana na watazamaji ambao leo wanakaa mbele ya jukwaa wakiangalia maigizo ya jukwaani. Ni D. W. Griffith, aliyekuwa wa kwanza kuwahamishia watazamaji katika ulingo wa sinema kwa kazi zake za “For Love of Gold (1908)”; “The Lonely Villa (1909)”; “The Lonedale Operator (1911)”; na iliyovutia zaidi, “Birth of a Nation (1915)”.

Grifftith alikuja na mbinu ya kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi zake. Sababu ya kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi ni kuifanya hadithi yako ivutie zaidi – isisimue zaidi. Lakini hii hufanywa kwa kuwaingiza watazamaji katika matukio, na kulenga zaidi kwenye usikivu wao hapa, na pale.

Muongozaji anaweza kuwachanganya na kuwakanganya watazamaji kiurahisi. Jiografia ya eneo au mwili wote wa mhusika hugawanyika. Hivyo, yasiwepo maswali, ule mkono wa nani? Mhusika A anahusiana vipi na Mhusika B? Mara nyingi muongozaji mzuri hapendi kusababisha mtanziko. Hupenda kuwafanya watazamaji wake wajisikie furaha katika ulimwengu wa filamu – kuwa sehemu ya hadithi – ili kwamba hadithi yake iweze kueleweka vizuri.

Siku zote, muongozaji hutaka watazamaji wake wajue kuwa, “Huo wanaouona ni mkono wa Daud, na Daud ameketi kushoto kwa Jesca” (hata kama hawajamuona Jesca kwa kipindi kirefu). Kuna wakati, hata hivyo, tunapaswa kutumia mbinu ya kuwachanganya watazamaji kama njia bora ya kutengeneza mazingira yenye kuleta msisimko au taharuki.

Sinema nyingi zilizofanikiwa huwa zina mhusika mkuu (protagonist) aliye wazi, na swali la kwanza katika kazi yetu ya ufuatiliaji kwenye mwongo za filamu ni: Nani ni mhusika mkuu kwenye filamu yetu? Njia nyingine ya kuuliza swali hilohilo, ni: Ni filamu ya nani (mhusika)? Ni mhusika gani tunayemfuatilia kwenye filamu? Ni mhusika gani tunayemtumainia au kumhofia – tukitumaini kuwa atapata anachohitaji, au tuna hofu kuwa hatafanikiwa?

Kwa muongozaji, ili afanikiwe kuwateka watazamaji wake anatakiwa kwanza kuijua “genre”. Genre ni aina ya hadithi inayosimuliwa, mfano, hadithi ya upelelezi; uchawi; ucheshi; kutisha; mapenzi nk. Tunapoangalia filamu, tunakumbuka na kuwa na matarajio fulani kuhusu mhusika, mandhali na matukio: ni vitu hivi ambavyo hutusaidia kufurahia na kubashiri kile kitakachotokea baadaye na kufanyia kazi matukio yanakoelekea.

Genre humruhusu muongozaji kubuni kitu kitakachobeba uhalisia kwa sababu tunashindwa kuona kuwa tunachokiangalia si kitu halisi. Kwa hiyo… kwenye aina ya hadithi ya kijambazi, kwa mfano, hatutajali kuona mmiliki wa casino anauawa kwa sababu tunamuona ndani ya genre, akiwa upande wa adui ‘villain’.

Makampuni ya filamu hupenda kutumia genre kwenye mambo yote kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mauzo na kusaidia kupata filamu nzuri: genre maarufu huleta nafasi nzuri kwenye mauzo, hivyo, genre ni njia nzuri ya kupanga filamu, hurahisisha sana katika uandikaji wa hadithi mpya.

Filamu zimekuwepo kwa zaidi ya miaka mia moja, kuanzia mwishoni mwa karne ya 19. Filamu zimepitia hatua kwa hatua zikianzia kwenye mawazo yaliyoonekana mapya hadi kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano na burudani, na hata kuwa mwasilisha taarifa muhimu wa karne ya 20 na 21. Filamu pia zina athari kubwa (substantial impact) kwenye sanaa, teknolojia, na siasa.

Machapisho mbalimbali yamekuwa yakiwataja ndugu wawili kutoka Ufaransa, Auguste na Louis Lumière kama waasisi wa filamu duniani ingawa ni William Kennedy Laurie Dickson (WKL Dickson), aliyekuwa injinia mkuu katika kampuni ya Edison Laboratories ya Marekani ndiye anayesadikiwa hasa kuwa “baba wa filamu duniani,” na ndiye aliyevumbua mfumo wa picha unaojulikana kitaalamu kama “Celluloid Strip”, mkanda maalum wenye picha mbalimbali za matukio yanayofuatana (sequence of images) yaliyochukuliwa kwa kamera maalumu na baadaye kuzionesha kwa njia ya sinema.

WKL Dickson alizaliwa mwaka 1860 huko Minihic-Sur-Rance, Ufaransa kwa wazazi wenye asili ya Uingereza na Uskochi (English-Scottish parents), na baadaye alihamia Marekani ambako alijiunga na kampuni ya Thomas Edison. Mwaka 1879 akiwa London, yatima Dickson, aliyekuwa na miaka 19 wakati huo na alikuwa amefiwa na baba yake, alisoma habari kwenye gazeti moja la London iliyomhusu Tomas Edison na maabara yake (Menlo Park Laboratory). Dickson alivutiwa sana, miaka miwili baadaye alituma 'telegram' kwenye kampuni ya Edison akiomba kazi.

Edison alimjibu Dickson kwa kifupi kuwa “hakuna kazi”. Miaka minne baadaye, mwaka 1883, Dickson akiwa amefanikiwa kukusanya pesa kidogo alielekea Marekani akiwa na ujuzi kidogo wa upigaji picha, huko Marekani alijibanza chini ya paa la kampuni ya Edison na kupafanya sehemu ya kazi zake huku akisubiri huenda ikatokea siku akabahatika kupata nafasi muhimu ya kuajiriwa kwenye kampuni hiyo.

Ilikuwa ni mwaka 1888 ambapo Dikson alipata kazi ya kufanya utafiti kuhusu maendeleo ya mpigapicha maarufu wa enzi hizo, Eadweard Muybridge, na wavumbuzi wenzake ambao kwa wakati huo walikuwa wakirekodi picha. Muybridge alikuwa katengeneza picha kadhaa za matukio (sequential photographs) kuhusu mwendo wa farasi. Mwaka 1877, chini ya udhamini wa Leland Stanford, Muybridge alifanikiwa kumpiga picha farasi aitwaye “Sallie Gardner” akiwa katika mwendo kasi kwa kutumia kamera 24 za Stereoscopic.

Majaribio hayo yalifanyika tarehe 11 Juni, kwenye shamba la Palo Alto jimboni California. Sababu ya zoezi hilo ilikuwa kufanya utafiti kama farasi anapokimbia huinua miguu yote minne kwa mara moja. Kamera zilipangwa sambamba na eneo alilokuwa akikimbilia farasi, na kila kamera ilidhibitiwa kwa waya. Miaka miwili baadaye, 1879, Muybridge alivumbua kifaa kilichoitwa “zoöpraxiscope”, kilichotumika kuoneshea na kuzihuisha (animating) picha za wanyama alizopiga.

Hivyo, Dickson alifuatilia nyendo za Muybridge katika kila jambo aliloona ni jipya kuhusu ugunduzi huo. Alijikuta akipata wazo la kutengeneza kamera na vifaa vingine vitakavyomsaidia kuona picha mbalimbali. Pamoja na changamoto alizokutana nazo Dickson hakuwa mwepesi wa kukata tamaa, alijifunza kwa bidii akitumia mbinu na nyendo za John Carbut, mpigapicha wa Kiingereza aliyehamia Amerika kutokana na ushindani uliokuwa huko na kufanya tafiti mbalimbali juu ya mkanda maalum wa filamu wa kurekodia picha “Celluloid Photographic Film”.

Kwa kuwa Dickson alikuwa na wazo la muda mrefu la kutengeneza sinema, huo ulikuwa wakati wa kutimiza ndoto yake na alimweleza bosi wake, Edison, kuhusu majaribio yake, lakini Edison hakutilia maanani majaribio hayo. Alipoona anapuuzwa, Dickson aliachana na Thomas Edison na kujiunga na kampuni ya George Eastman Company ili aweze kukidhi haja yake ya uvumbuzi.

Baada ya muda, Dickson alimtafuta mchungaji Hannibal Goodwin, wa kanisa la Episcopal, aliyekuwa ametafiti na kuvumbua mafuta maalum mazito ya kulainishia mkanda wa picha (photographic emulsion) na kuufanya uzunguke kwa urahisi. Dickson alimlazimisha Goodwin akubali kuidhinisha utafiti wake utumike kwenye kampuni ya George Eastman kwa ajili ya uzalishaji.

Hatimaye Dickson “king’ang’anizi” alifanikiwa kuvumbua kamera mnamo Novemba 1890, na kuifanyia majaribio ya picha za sinema (filming), jaribio lake la kwanza aliliita “MONKEY SHINES”.

Kamera hiyo aliipa jina la “Kinetograph”, na kuionesha kwa Thomas Edison, ambaye aliunda timu maalum ya kuuendeleza ugunduzi wa Dickson, na hatimaye kutengeneza kifaa kingine kilichopewa jina la “Kinetoscope”, kilichokuwa na tundu dogo (peep-hole) kwa ajili ya kuonea picha.

Uvumbuzi huo wa Dickson ulihusisha mkanda wenye picha kadhaa za matukio yaliyofuatana uliokuwa ukipitishwa mbele ya lenzi yenye kutoa mwanga kwa msaada wa balbu, na nyuma yake kulikuwa na gurudumu lenye kuzunguka. Gurudumu hilo lilipozunguka, muonekano wake ulimfanya mtazamaji aone jumla ya picha 46 za matukio yanayofuatana ndani ya sekunde moja tu, hivyo, kumfanya anayetazama aone matendo halisi (lifelike motion).

Kutambulishwa kwa kifaa cha “Kinetograph” mnamo Oktoba 1892 ikawa chachu na mwanzo wa sekta ya filamu kukua na kufikia ilipo sasa.  Mnamo 1897, Dickson alirudi England, na miaka miwili baadaye, alitambuliwa na kupewa heshima na wanahistoria kama “Baba halisi wa sinema” na mtu aliyechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo na uvumbuzi wa sinema.

Dickson alifariki kwa ugonjwa wa kansa tarehe 28 Septemba 1935, Twickenham, Middlesex, Uingereza. Katika kipindi cha uhai wake, Dickson alioa mara mbili na alipokufa aliacha mtoto mmoja wa kiume aliyemuasili (adopted son).


No comments: