* Wapo waliohusisha vifo hivi na kafara
Marehemu George Otieno Okumu "Tyson" |
Marehemu Adam Phillip Kuambiana |
TUMEINGIA mwaka mpya 2015 tukitaraji mafanikio makubwa
zaidi na tukiuaga mwaka 2014 uliokuwa wa simanzi kwa tasnia ya filamu tulipokumbwa
na taharuki kufuatia vifo vilivyotokea mfululizo vya wasanii wa filamu
vilivyotokea katika muda mfupi mfupi. Kufuatia vifo hivyo tetesi zilienea mitaani
kwamba vifo hivyo vilitokana na kutoana kafara!
Tetesi
hizi zilinilazimu kufanya utafiti ili kujua nini maana ya Kafara, na kama kweli
kuna kafara katika vifo hivi. Inasemwa kuwa kafara ni kitendo cha
kutoa damu ya mnyama, ndege au mtu kama sadaka kwa mzimu ili kupata
upendeleo maalumu kutoka kwa mzimu huo. Upendeleo huo unaweza kuwa ni
utajiri, mali, mafanikio katika biashara, uongozi, kazi, mapenzi, ulinzi wa kishirikina,
nguvu za kishirikina na kadhalika.
Kwa lugha
nyingine kafara ni mabadilishano ya vitu kati ya mtoa kafara na mzimu au
muungu ambao unapokea kafara hiyo.
Wataalamu
wanatueleza kuwa zipo aina mbalimbali za kafara, lakini zilizo kuu ni
mbili: Kafara ya Damu; ambapo mtu hutakiwa kutoa kafara ya mnyama aliye hai,
ndege au hata mtu. Na kafara ya kutoa kiungo cha mwili; hii
ikimaanisha kuwa mtu hutakiwa kutoa kiungo chake cha mwili ili aweze kukidhi
matakwa ya kafara. Hii inawahusu zaidi wanaume, na mara nyingi huambiwa watoe
uanaume wao (kuhasiwa) au kuondolewa uwezo wa kumzalisha mwanamke.
Vitu vyote hivi hufanyika kichawi.
Hebu
tuziangalie aina hizi mbili kwa kina zaidi ili kulinganisha na vifo
vilivyotokea mfululizo vya wasanii wetu kama mazingira yanafanana. Je, kwanini
mizimu hutaka kafara ya damu?
Kwa
mujibu wa mtaalam mmoja Mungwa Kabili, aliyejitambulisha kama mtaalam wa kafara
anasema kuwa zipo sababu mbalimbali kwanini mizimu huomba kafara ya damu,
lakini kubwa kuliko zote ni hii kwamba mizimu huwa hailipwi kwa pesa,
bali kwa damu. Kwa lugha nyingine, damu ya wanyama katika kafara hutumika
kama fedha ya kununua upendeleo (privilege) kwa mzimu.
Mtaalam
huyu anabainisha kuwa kafara za damu nazo zimegawanyika katika
makundi makuu mawili: damu ya mnyama asiye mwanadamu na damu ya mtu. Kafara
ya damu ya mtu hutolewa kwa njia za kishirikina. Mtu aliyetolewa
kafara anaweza kufa kifo cha kawaida kabisa kama vifo vingine, lakini kiukweli anakuwa
ametolewa kafara kishirikina. Kwa mfano mtu anaweza kuugua ghafla, au kupata ajali
nk. Wakati mwingine kafara aina hii inaweza kuhusisha kundi kubwa la watu. Mara
nyingi hutokea katika ajali nk.
Lakini
bado tuna swali la kujiuliza, je, vifo mfululizo vya wasanii wa filamu
vilivyotokea mwaka 2014 vimetokana na kafara? Mtaalamu huyu anasema si kweli
kuhusu dhana potofu iliyosambaa miongoni mwa jamii kwamba, eti vifo mfululizo vya
wasanii wa filamu vilitokana na kafara inayofanywa na watu waliomo ndani ya
Tasnia ya Filamu kwa lengo wanalolijua.
Hata
wataalam wengine waliobobea katika masuala ya “ulimwengu usioonekana”, wamebainisha
kuwa vifo mfululizo vya wasanii waliofariki mwaka 2014 havikutokana na kafara kwa
sababu haviendani na “sifa ya kafara inayolenga watu waliopo katika jamii moja
kama vile wanafunzi katika shule ama chuo fulani, wanafamilia fulani ama wana
ukoo fulani!”
Kafara
inayowalenga watu waliopo katika jamii moja, huwa na sifa zifuatazo: kwanza
aina za vifo hufanana. Kama ni wanafunzi ama wanafamilia ama wanaukoo ama
wafanyakazi wa kampuni au taasisi fulani, basi wote watakuwa wanakufa vifo
vya aina moja. Vifo hivyo vinaweza kuwa kufa kwa ajali ya aina moja tena katika
mazingira yanayofanana, au kuanguka chooni, au kufa kwa kuugua kichwa nk.
Hivyo,
ukiangalia vifo vya wasanii vimetofautiana, Adam Kuambiana alikuwa anasumbuliwa
na kisukari na vidonda vya tumbo kwa muda mrefu, Recho Haule alifariki wakati
akijifungua, George Otieno “Tyson” alifariki kwa ajali ya gari, na Mzee
Small alikuwa akisumbuliwa na kiharusi. Hivyo, kwa mujibu wa wataalam wa
masuala ya kafara wanabainisha kuwa vifo hivi haviwezi kuwa vimetokana na kafara!
Pili;
aina ya watu wanaofariki kwa sababu ya kafara hufanana, hii
inamaanisha kuwa vifo huwalenga waliopo kwenye kundi moja na huwa na sifa zinazofanana
na kushabihiana Inaweza ikawa ni wanawake tu au ikawa ni wanaume tu. Kwa mfano
kama kafara imewalenga wanafunzi wa shule fulani, basi watakaokufa lazima watakuwa
wa jinsia moja na vifo vyao vitafanana sana.
Ikitokea wamekufa
wanafunzi, basi huwa ni wanafunzi tu, haiwezi kuwalenga na walimu kwa wakati mmoja.
Kama ni kwenye shule ya watu wa jinsia moja, basi wahanga watakuwa ni watu wenye
sifa zinazofanana, kwa mfano wanaweza kuwa viranja tu, au mamonita wa
madarasa tu.
Hivyo,
kwa sababu hiyo, vifo vya wasanii haviwezi kuwa vimetokana na kafara, kwa sababu
walio fariki hawana sifa zinazofanana na kushabihiana hata kidogo. Licha ya
kwamba wanatoka katika jinsia tofauti lakini pia walikuwa na majukumu tofauti katika
tasnia ya filamu. Kama ingekuwa ni kafara lazima ingelenga watu ambao roles zao
katika filamu zinaendana, kwa mfano waongozaji wa filamu, watayarishaji, waigizaji
nk!
Tatu;
mazingira ya vifo vya kafara hufanana. Hii maana yake kuwa vifo vya kafara iliyolenga
watu walio katika tasnia moja au jamii moja hufanana na kushabihiana kwa
asilimia mia moja. Sasa hapa ukitazama mazingira ya vifo vya mfululizo vya wasanii
waliofariki mwaka 2014 hawa hayafanani wala kushabihiana kwa lolote lile. Kwa
kuwa tarehe za vifo huwa na alama au utata wa kinyota unaofanana na
kushabihiana kwa kiasi kikubwa sana: Hebu tazama tarehe za vifo vya wasanii
hawa wanne wa filamu.
Katika
uchambuzi na hesabu za kinyota, ukitaka kujua kama vifo vya wasanii hawa
vimetokana na kafara unaweza kuangalia mifano hii inayobainishwa na wataalam wa
masuala ya kafara. Marehemu Adam Kuambiana ambaye alifariki alfajiri ya tarehe 17/05/2014,
hivyo kwa kubainisha hesabu za kinyota, chukua 17 ambayo ndiyo tarehe
aliyofariki Adam kisha jumlisha 05 ambao ndiyo mwezi aliofariki. Hesabu itakuwa
kama ifuatavyo: 1+7+0+5=13. Kwa kuwa jibu linatakiwa liwe kati ya 1 hadi 9,
jumlisha 1 na 3 ambapo jibu lake litakuwa ni 4.
Rachel Haule
alifariki usiku wa kuamkia tarehe 27-05-2014. Kwa hesabu za kinyota, tarehe 26
mwezi wa 05: 2+7+0+5=14. Hivyo, 14 =1+4 = 5. George Tyson alifariki
tarehe 31-05-2014. Kwa hesabu za kinyota, tarehe 31 mwezi wa 05: 3+1+0+5 = 9.
Na Mzee Small alifariki usiku wa tarehe 7 mwezi wa 06: Kwa hesabu za kinyota
7+0+6=13. Hivyo 1+3=4.
Ukiangalia
namba hizi utagundua kuwa kama wangekuwa wametolewa kafara basi kungekuwa na
utata wa kinyota unaofanana sana. Namba za mwisho lazima zote zingefanana.
Kwanini
lazima kuwe na ufanano? Jibu ni moja tu, nalo ni kwa sababu mauaji ya kishirikina
hufanywa na kitu kimoja kwa sababu moja. Kila mzimu, pepo au muungu huwa una njia
zake na namna zake za kufanya mambo yake. Kila roho itendayo kazi kishirikina huwa
na mipaka yake ya utendaji kazi. Kwa mfano, mzimu fulani unaweza kuwa na uwezo wa
kuwasaidia watu matatizo ya uzazi lakini watu hao lazima wawe wanawake au wanaume
tu.
Mzimu
au pepo fulani linaweza kuwa na uwezo wa kuua watu lakini ili watu hao wauawe ni
lazima wawe ndani ya maji kama mtoni, baharini au ziwani, au ni lazima wawe
chooni, nje na maeneo hayo mzimu huo unakuwa hauna nguvu. Mzimu fulani unaweza kuwa
na uwezo wa kuua biashara fulani, lakini ni lazima ufilisi biashara hiyo kwa njia
ya ajali ya moto au chumaulete nk.
Hivyo,
mzimu huo unapokuwa katika kutimiza lengo la kutoa kafara za watu walio katika
jamii moja ni lazima watu hao watakuwa wenye sifa zinazofanana, na vifo vyao vitakuwa
vya aina moja.
No comments:
Post a Comment