Desmond Eliot, msanii wa Nollywood
HIVI karibuni Nigeria imetangazwa kuwa ndilo Taifa lenye uchumi mkubwa barani
Africa na kuipita Afrika Kusini. Pato Ghafi la Ndani (Gross
Domestic Product ‘GDP’) la Nigeria limefikia Dola Billion 509 huku lile la Afrika ya
Kusini likifikia Dola Bilioni 322.
Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu yaNigeria , Nigeria imekuwa Taifa lenye uchumi mkubwa Afrika baada ya
wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za Mawasiliano na Filamu (Nollywood)
kwenye takwimu. Ni dhahiri kuwa soko la Filamu la Nigeria linatoa mchango mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi
wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Nigeria ilionekana kama taifa linalotegemea zaidi uuzaji wa mafuta na ilikadiriwa kuwa pato la
mafuta lilichangia asilimia 32 kwenye GDP lakini ripoti ya wanauchumi hivi
karibuni imeonesha sasa pato la mafuta huchangia Asilimia 15 tu ya pato ghafi
la ndani.
Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya
Haikuishia hapo, ripoti
imeonesha pia utegemezi wa kilimo katika kuchangia pato la Taifa nchini Nigeria umepungua. Kwa wanataaluma wa uchumi wanaelewa kuwa
kupungua kwa utegemezi wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi maana yake uchumi
unapiga hatua. Ili mjitoe katika nchi tegemezi na kuingia kwenye nchi
za daraja la kati ni lazima mtegemee zaidi sekta ya viwanda kwa ukuaji badala
ya kilimo, wakati nchi zilizoendelea hutegemea sana huduma.
Kwa hali hiyo, kuna nafasi
kubwa ya masoko ya Nigeria kuvutia mitaji ya uwekezaji kutoka ndani na nje ya
nchi na kupunguza nakisi kubwa ya bajeti (budget deficit) jambo litakaloongeza
pia tija, uchumi kupaa na ushawishi wa nchi hiyo katika diplomasia na siasa za
kimataifa utaongezeka.
Wakati Nigeria wakijitoa kwenye kutegemea kilimo na kuigeukia sekta
ya filamu kama chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic
potential), sisi Tanzania tunafanya mzaha. Bado tunang’ang’ana kwenye kilimo cha
jembe la mkono huku tukibadili misamiati kila mwaka: Kilimo cha kufa na kupona,
Siasa ni kilimo, Kilimo ni uti wa Mgongo, Kilimo Kwanza n.k. na kuzipuuza sekta
ambazo zingeweza kuwa mchango mkubwa katika kuliletea Taifa pato. Au basi
tungeboreshaa kilimo chetu.
Nollywood ndiyo sekta ya
pili kwa kutoa ajira katika nchi ya Nigeria baada ya sekta ya kilimo, na mchango wake kwa Taifa
ni mkubwa sana kwani ina thamani ya Naira bilioni 853.9 (Dola za
Marekani bilioni 5.1). Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya filamu inavyoweza kukuza
na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo ya kukubalika kwa sinema pia
huwafanya watayarishaji wa sinema, waigizaji na watendaji wengine kuwa na
heshima kwenye jamii na hata kisiasa.
Mfano, wakati wa kuondolewa
kwa ruzuku ya mafuta Nigeria miaka kadhaa iliyopita, Rais Goodluck Jonathan
alimtuma mwakilishi wake kujadili suala hilo na wadau wa Nollywood kuhusu kupunguza
udhibiti wa kibiashara, mkutano ulioandaliwa na kikundi cha Segun Arinze wa
Chama Waigizaji wa Nigeria (AGN). Hapa najaribu kuonesha umuhimu wa sekta ya
filamu katika kubadilisha sera za kiuchumi katika uhusiano na siasa nchini Nigeria . Si hivyo tu, mwaka jana Rais Goodluck Jonathan alitangaza
kutoa Naira bilioni 3 kwenye kuiendeleza Nollywood, jambo linaloonesha
kuutambua mchango muhimu wa sekta hii.
Serikali ya Nigeria inaichukulia sekta ya filamu kwa umakini mkubwa.
Vipi kuhusu serikali yetu? Na moja ya maendeleo ya kutia moyo sana Nigeria
ni uwepo wa sera ya filamu iliyopatikana mwaka 1991 wakati Shirika la Filamu la
Nigeria (NFC) lilipoandaa jopo kuangalia kanuni zilizokuwepo kwa lengo la
kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera ya filamu.
Pia sanaa zetu zimekuwa
hazilindwi, hazikuzwi, hazitangazwi, hazitambuliki na wala hazipewi umuhimu
unaostahili kama ambavyo sekta iliyo rasmi inavyopaswa kuwa. Serikali
imeshindwa kuitilia maanani, kuchukua hatua stahiki, kutoa takwimu halisi za
mchango wa sekta hii kwa uchumi wa taifa pamoja na ukuaji wa kasi wa sekta hii hali
inayosababisha ishindwe kupata pato halisi linalotokana na sekta hii.
Shughuli nyingi zinafanyika
kiholela bila wahusika kuwa na hakimiliki na sehemu kubwa ya mchango wake kwa
pato la taifa haijarekodiwa katika vitabu vya mapato vya taifa. Hii inaonesha
kuwa mchango wa sekta hii katika pato la taifa ni mkubwa zaidi kuliko takwimu zinavyoonesha.
Sera bora zitachochea
maendeleo ya kisekta, mazingira ya ubunifu yenye ushindani na salama ambayo
serikali itayatumia kuendeleza sekta hii na kutambua thamani ya kazi za
ubunifu.
Pamoja na hayo, bado sekta
ya hakimiliki nchini mwaka 2009 kwa mara ya kwanza katika pato la taifa,
iliingiza Sh676 bilioni ikiwa ni asilimia 4.6 ya Pato la Taifa (GDP), likiwa ni
zaidi katika uchumi wa taifa kuliko sekta ya hoteli, migahawa na madini.
Taarifa hiyo ambayo
imetolewa hivi karibuni kwa lugha ya Kiingereza ikiwa na jina: ‘The Economic
Contribution of Copyright-Based Industries’ kwa mwaka 2012, imebainisha kwamba
sekta ya madini imechangia asilimia 2.6 ya GDP wakati hoteli na migahawa imechangia
asilimia 4.5, sekta ya hakimiliki imefanya vyema.
Pia sekta hii imeajiri watu
wengi zaidi ya wale walioajiriwa na sekta ya afya na ustawi wa jamii, fedha,
majumba ya kukodisha, huduma za biashara, ujenzi, usafirishaji, mawasiliano,
madini, umeme, gesi na sekta ya maji. Mchango wa sekta ya hakimiliki kwa malipo
ya wafanyakazi, ulikuwa Sh 80.474 bilioni sawa na asilimia 5.
Tusiishie kusema tu,
tutafute suluhisho kwa kuhakikisha kuwa tunao mfumo wa kutathmini na kuangalia
ukuaji wa sekta kwa kuzingatia ukuaji wake ambao kwa sasa unakwenda kasi, kama ambavyo tafiti za WIPO zimebainisha. Ni vyema sasa tukatafuta utaratibu
wa kukusanya takwimu na kuzifanyia uwiano kwa kuziunganisha na takwimu za
Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Imekuwa ikisemwa kuwa nchi
kadhaa ambazo sasa zimeendelea zilikuwa na uchumi sawa na Tanganyika (sasa Tanzania)
wakati tukipata uhuru mwaka 1961, nchi hizo ni pamoja na Singapore, Korea
Kusini, Thailand, Malaysia na kadhalika, ila kilichowafanya kutuacha
kimaendeleo na kupata maendeleo ya haraka ni ulinzi na uendelezaji wa Miliki
Bunifu.
Kwa mfano Korea Kusini imekuwa
ni Taifa kubwa na tishio Barani Asia kwa sababu tu
ya kulitambua kundi la wasanii na kuweka mazingira mazuri ya ulinzi wa Miliki
Bunifu kiasi cha kubatizwa jina la Marekani ya Asia .
Mwaka 2005 serikali ya Korea iliweka lengo la kuhifanya nchi hiyo miongoni mwa
nchi tano bora katika uuzaji wa sanaa na utamaduni. Baadhi ya maeneo ambayo
serikali iliwekeza ni pamoja na kusaidia usambazaji na masoko ya nje na
kusaidia uzalishaji kupitia vifaa na mitaji. Serikali pia ilihakikisha vyombo
vya habari vya ndani vinarusha kwa kiasi kikubwa vipindi vinavyozalishwa ndani.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment