Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akizungumza Bungeni
KATIKA
jitihada za kuhakikisha kuwa wasanii hapa nchini Tanzania
wanatengenezewa mazingira mazuri zaidi ya kufaidika na kazi
wanazotengeneza, Serikali imetoa
maagizo kwa Chama Cha Hatimiliki Tanzania,
COSOTA
na Mamlaka ya Mapato nchini, TRA, kukutana ndani ya siku tano za kazi
kuanzia sasa. Mpango huu ni kwa ajili ya kutengeneza makubaliano juu
ya mfumo utakaofaa kwa ajili ya kukusanya na kudhibiti mapato ili
kuboresha faida kwa wasanii na serikali.
Naibu
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, alitoa kauli hiyo bungeni
ambapo alitaka waangalie namna ya kuboresha stempu/stika
zinazobandikwa katika kazi za wasanii ili badala ya kutumika
kukusanya ushuru peke yake zitumike pia kulinda kazi za wasanii hao.
Kwa
hili naipa tano Serikali kwani itasaidia kuondoa sintofahamu
kuhusiana na stempu za TRA, ambapo serikali kwa kupitisha sheria ya
stempu za TRA imekuwa ikijigamba kuwa imezirasimisha sekta za filamu
na muziki. Nimekuwa nikisisitiza kuwa hakuna 'excuse' yoyote kwa
wasanii katika kukuza pato lao, kuondokana na umaskini na hata
kushindana kimataifa kama hawataingizwa kwenye mfumo rasmi ambao
utawafanya watambulike ndani na nje ya nchi ili kujenga mazingira ya
wao kuweza kukopesheka, kupata fursa za kikazi na kukuza kazi
wanazozifanya. Katika mataifa mengine wasanii wako rasmi na wameweza
kuvuma na kupaa kiuchumi.
Lakini
urasmishaji ninaoukusudia si huu ambao tumekuwa tukiushuhudia wa
kutubandikia stempu za TRA zitakazotumika kabla kazi hazijaingia
sokoni. Inawezekana kabisa serikali ilikuwa na nia nzuri lakini bila
kujua ikataka kutumia mfumo ambao si mzuri na imegundulika kuwa
serikali kwa mfumo huu “ilishaingia mkenge” na kukosa nia ya
dhati ya kumkomboa msanii, hii imethibitishwa na kauli ya Naibu
Waziri, Mwigulu Nchemba, alipokiri
kuwa ni kweli kuweka stempu za TRA kwenye kazi za wasanii hakulengi
kulinda kazi za wasanii zaidi ya kukusanya mapato ya serikali.
Mpango
huu unaodaiwa ni wa kurasimisha sekta hii ili kuiboresha umekuwa na
maswali mengi mno bila majibu, hasa kutokana na kile kinachoonekana
kuwa upande wa serikali (kupitia taasisi zake) hauelewi upande wa
pili unatendaje kazi zake, unataka kuchukua haki ya upande wa pili na
kutokana na upya wa dhana yenyewe pande zote hazielewi nini
kinatakiwa.
Pamoja
na TRA kujidai kuwa wamefanya utafiti wa kutosha kabla ya zoezi zima
za urasimishaji lakini ukweli hakuna utafiti wowote wa kitaalam
uliofanyika, hii inathibitishwa na majibu ya viongozi wa maamlaka
wenye dhamana pale wanapobanwa kwa maswali, na mara nyingine
walifikia hatua ya kutaka kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kutoa
majibu mepesi lakini wakisisitiza kuwa wao wanachotaka ni kukusanya
kodi tu na hawatarekebisha chochote bali kukazia, masuala mengine
hayawahusu!
Kuna
wakati katika mkutano mmoja kati ya mamlaka za serikali zenye dhamana
kuhusiana na sekta ya filamu na muziki ikiwemo TRA na wasanii
kulitokea mtafaruku baada ya maofisa wa TRA walipoulizwa kwanini
wanadai TRA inawalinda wasanii wakati ni wazi katika hili kazi yake
ni kukusanya kodi kutoka kwa wasambazaji, jambo ambalo halina tija
yoyote kwa wasanii binafsi? Majibu yaliyotolewa yalileta mvurugano
mkubwa kati ya mamlaka za serikalai na wasanii.
Sielewi
ni kwanini serikali imekuwa ikidharau tafiti zinazofanywa na wadau
mbalimbali zinazoegemea kwenye hali halisi, tafiti ambazo zimekuwa
zinakuja na muarobaini wa kutatua mambo. Mimi pia nimewahi kufanya
utafiti kuhusiana na filamu ikiwemo urasimishaji, nikagusia mfumo
unaotumika Afrika Kusini ambao ungetufaa sana.
Kama
serikali wameliona hili itakuwa vyema maana wengine tulishafikia
hatua ya kutaka “kuingia msituni” ili kupigania uwepo wa mfumo
sahihi badala ya hiki tulichokiona cha serikali kupitia TRA kuhitaji
kodi tu kutoka kwa wasanii lakini ikiwa haina mpango wa dhati kuhusu
wasanii, tulitaka tupiganie haki hadi kieleweke, hasa baada ya mfumo
uliopo kuonesha kushindwa hata kabla haujaanza.
Kama
nilivyowahi kushauri mwaka juzi kuwa ili kuleta ufanisi katika sekta
hii serikali inapaswa kuziagiza mamlaka husika kuandaa takwimu za
kina kuhusu soko la filamu na kuzitazama fursa zilizopo kabla ya
kuamua chochote. Na yote haya yatategemea sera nzuri ya filamu
itakayokuwa imeanzishwa. Sera ya filamu ndiyo hati pekee yenye
kueleza kwa ufasaha uwezekano mbalimbali katika kuandaa mazingira
mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu.
Sera
hii inapaswa iende mbali zaidi ikizingatia mchakato wa utoaji wa
filamu na uanzishwaji wa haki za usambazaji wa miliki. Katika
mchakato huu, wasambazaji wenye leseni watatarajiwa kuwasilisha
ripoti ya kila wiki ya kisheria katika shughuli zao za usambazaji
ambayo inaweza kutumiwa katika kutathmini utendaji wa kifedha wa
filamu.
Kwa
mfumo uliopo sasa, nimekuwa nikijiuliza maswali mengi yasiyo na
majibu. Hivi ni kweli stampu za TRA pekee zinatosha kuleta ufanisi
katika soko la filamu bila hata kuijua nguvu ya soko? Mbali na stampu
hizi je, kuna mikakati gani katika kudhibiti kazi zisizo na stempu?
Je, mlaji atatofautisha vipi stempu halali na batili? Hivi zoezi hili
litafanikiwa kweli pasipo elimu kwa walaji?
Sikuishia
hapo bado niliendelea kujiuliza maswali lukuki: ni 'mechanisim' gani
itakayotumika kuweza kutekeleza hilo na je, msanii atahakikisha wapi
kipato chake? Kwenye stampu au wapi? Je, kuna mpango gani katika
kuandaa miundombinu ya soko la filamu ili wasanii na watengeneza
filamu pia wafaidi jasho la kazi zao tofauti na ilivyo sasa? Je,
Serikali ikisharasimisha sekta hii, itawekeza au ndiyo itaingia
kwenye mpango wa kuvuna pasipo kupanda? Maswali haya yalikuwa
yakinijia kichwani kwa kuzingatia kuwa mfumo wa biashara ya filamu
nchini umekaa kienyeji sana. Sidhani kama ni busara kwa serikali
(kupitia Mamlaka ya Mapato) kukusanya mapato wakati haijengi
miundombinu ya soko, haijengi shule zitakazowasaidia wadau wa filamu,
wala haisaidii katika kutafuta soko!
Hapa hata mkikusanya kiasi gani, bado haitatusaidia kama elimu kwa wasanii na wadau wengine haitatolewa. Hivi kuna vyuo vingapi vinavyofundisha filamu? Kwa sheria iliyopo inambana msambazaji/muuzaji kuhakikisha analipa kodi lakini haimsaidii mtayarishaji/msanii ambaye anaendelea kunyonywa kama kawaida.
Kwa
mfumo huu serikali bila kujua ilikuwa inatengeneza bomu kwa tasnia ya
burudani, bomu ambalo limeleta mgogoro mkubwa katika nchi ya Ghana
sababu ya msingi ikiwa ni ndogo tu, kazi ya Mamlaka ya Mapato si
kulinda haki za wasanii bali ni kukusanya kodi. Kazi ya kulinda haki
hizi iboreshwe katika vyombo vya wasanii husika na Chama Cha
Hakimiliki ili TRA iweze kupata takwimu sahihi za kukusanya kodi.
Naomba
katika kikao watakachokaa Cosota na TRA wajaribu kuangaalia ni namna
gani wataweza kuwa na mfumo wenye kuleta tija, ikiwa ni pamoja na
kuangalia kama tunaweza kuwa na chombo chenye mfumo ambao utaweza
kudhibiti aina na aina ya wasambazaji, kutoa miongozo kwa ajili ya
usajili na leseni ya wasambazaji (ambayo ada fulani wanatarajiwa
kulipwa), na kubainisha aina ya haki za usambazaji ambayo wasambazaji
katika ngazi mbalimbali wataendelea kumiliki pamoja na udhibiti ili
kuhakikisha kuwa haki hizi zinalindwa.
Chombo
hiki kiambatane na kuwepo kwa sera mpya itakayoonesha pia sifa
zinazopaswa kuchukuliwa katika mkataba halali wa usambazaji ambao
pamoja na mambo mengine, utalazimisha wahusika kuandikisha filamu zao
kama miliki bunifu (intellectual property). Moja ya masuala ya
ubunifu wa sera ya uzalishaji wa fedha na ulinzi ambayo nadhani sera
inayopaswa kuwepo ni ya kutoa ufadhili kwa wamiliki wa haki za
filamu.
Alamsiki…
No comments:
Post a Comment