Viongozi wa Mashirikisho la Sanaa wakiwa pamoja na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Paul Mtendah (wa pili kushoto) na Maria Sarungi (wa tatu kushoto), kwenye hoteli ya Dodoma, kabla ya vikao vya Bunge kuanza
WIKI iliyopita kwenye
gazeti moja litolewalo kila siku (ambalo limetoka kifungoni hivi karibuni)
kulikuwa na makala ya mwandishi mmoja ambaye pia ni msanii aliyesomea taaluma
ya sanaa katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, iliyobeza juhudi zinazofanywa na
wasanii hivi sasa kupigania kutajwa kama mojawapo wa
kundi muhimu kwenye Katiba ya nchi. Makala hayo yaliyojikita katika kile ambacho
mwandishi huyu (nitamtaja zaidi kama msanii)
alidai kuwa wasanii wenzake wamekumbuka shuka wakati kumekucha, kiasi cha kuzua
mjadala mkubwa kwenye mtandao wa kijamii wa facebook.
Ukisoma kwa umakini makala
ya msanii huyu utagundua kuwepo kwa mambo makuu matatu: ukosefu wa taarifa,
umimi na kukurupuka kuongelea jambo bila utafiti, ili mradi aonekane anajua
kusema!
Msanii huyu ambaye hupenda
kuponda (yeye huita kukosoa) kazi za wenzake pasipo kuonesha jinsi ya kuboresha
ameona kuwa juhudi zinazofanywa hivi sasa na Shirikisho la Filamu Tanzania na Mtandao wa Wanamuziki Tanzania kupigania mambo mawili yaingie kwenye katiba ya
nchi ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Eti hawajafuata ushauri wake!
Mambo ambayo wasanii
wanataka yaingizwe kwenye Katiba ni kulitambua kundi la wasanii kama mojawapo ya makundi muhimu, kama ambavyo imetambua
uwepo wa makundi ya wakulima, wavuvi, wafanyakazi, wafugaji nk.
Wasanii ni kundi kubwa sana linaloyazidi makundi mengine huku likizidiwa na
wakulima, pia ni kundi linalochangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi,
kutolitambua ni kosa. Kwa mujibu wa utafiti wa WIPO wa Septemba 2012, sekta ya
sanaa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 4.275. Kutokutambuliwa kwa
kundi hili kunafanya pato litokanalo na sanaa kupotelea katika mifuko ya watu
na kuwakosesha wasanii na Taifa pato kubwa.
Jambo la pili ni kuwa kutajwe ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) katika Katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazikama ilivyo katika mali nyingine za wananchi wengine. Kwenye Rasimu ya
Katiba imetajwa ulinzi wa kazi zinazohamishika na zisizohamishika lakini mali zisizoshikika (za ubunifu) hazikutajwa. Kwa
msanii huyu haya yanayopiganiwa ni upuuzi (sijui kwa kuwa hajashirikishwa kama anavyodai?) na kwamba hayatafanikiwa.
Jambo la pili ni kuwa kutajwe ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) katika Katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi
Sanaa zetu zimekuwa
hazilindwi, hazikuzwi, hazitangazwi, hazitambuliki na wala hazipewi umuhimu
unaostahili. Jambo muhimu na la msingi ni kuzingatia, kuzikuza, kuzitambua na
kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko
ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Ieleweke wazi
kwamba sanaa ni kazi ya ubunifu tena yenye ufundi na mvuto kama sumaku, kazi
nzuri ya sanaa ni ile iliyo na ubunifu, uasili na inayotumia mbinu bora ya
uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.
Kwa kuwa mawazo haya
yametoka kwa wasanii ambao hawajaenda shule ni ndoto kufanikiwa! Ila kama yangetoka kwa wasomi isingekuwa shida kwa msanii huyu. Anaposema
‘wasanii wamekumbuka shuka kumekucha’ maana yake, hawapaswi kupigania haki yao kikatiba ila waendelee kulalamika tu?
Msanii huyu badala ya
kuungana na wenzake ili kuhakikisha mambo haya yanapitishwa yeye anaendeleza
mambo yaleyale kama ilivyo kwa viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza
kwenye masuala ya sanaa na utamaduni kushindwa kusimamia, kutudharau (eti
hatujasoma) na kutukatisha tamaa kiasi kwamba hadi leo tumeshindwa kuthamini
tamaduni zetu.
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi
kutamka kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa
utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa
sifa ya kuitwa taifa kamili. Hii ilikuwa wakati wa kuunda Wizara ya Utamaduni wa
Taifa na Vijana, mwaka 1962.
Kupuuzwa kwa tamaduni
kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya
mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na
desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na
kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.
Hii imesababisha hata sera
ya utamaduni kutokupewa nafasi katika serikali hii tangu ilipoanzishwa wizara
inayoshughulikia masuala ya sanaa. Naamini kuwa hali ya mtu kujitenga na
tamaduni asilia kunaweza kuwa tishio katika kupokea hata imani ya kidini. Hii
inatokana na ukweli kwamba imani ambayo mtu aipokeayo kama zawadi toka kwa Mungu ina msingi wake katika mila na desturi
tuziishizo. Hakuna uwezekano wa kuwa na imani ya kidini iwapo mtu hakujengeka
katika utamaduni wa kweli. Ni katika tamaduni zetu ndipo tunapata maana ya utu,
upendo na kadhalika.
Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inatukumbasana vijana ambao bila kujua huwa tunajikuta katika
utamaduni hasi unaotusukuma kudharau tamaduni zetu na kujiingiza katika
mienendo ambayo kwa kiasi kikubwa si tamaduni ila vurugu zinazotokana na
kukosekana kwa tamaduni.
Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inatukumba
Hii inajionesha katika
sanaa zetu tunazoziandaa ambazo nyingi zinajengwa katika misingi isiyo na maana
katika jamii. Uigaji usio na uchambuzi umetupelekea kukosa kabisa vipaumbele
katika maisha yetu, na kubaki kuwa bendera kufuata upepo.
Sijui kama msanii huyu
anajua kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe,
kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, na jambo hili linaonesha umuhimu wa
utamaduni si kitu kilichoibuka tu. Hivyo inapaswa kupiganiwa kwa gharama yoyote
iingizwe kwenye katiba mpya.
Hakuna heshima kubwa
Kama Taifa tumepotea na
tumechanganyikiwa. Tumekumbatia baadhi ya tamaduni za wengine na kuzigeuza kuwa
zetu bila kujali kama zinaakisi jamii husika. Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza
kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida,
hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.
Labda nimuelimishe msanii
huyu kuwa Korea Kusini imekuwa Taifa kubwa na tishio Barani Asia kwa sababu tu
ya kulitambua kundi la wasanii na ulinzi wa Miliki Bunifu kwenye Katiba yake.
Nchi zingine za Asia (China , Japan , Philippines , Indonesia , nk) zimeipa jina la Marekani ya Asia .
Mwaka 2005 serikali ya Korea iliweka lengo la kuhifanya nchi hiyo miongoni mwa
nchi tano bora katika uuzaji wa sanaa na utamaduni. Baadhi ya maeneo ambayo
serikali iliwekeza ni pamoja na kusaidia usambazaji na masoko ya nje na
kusaidia uzalishaji kupitia vifaa na mitaji. Serikali pia ilihakikisha vyombo
vya habari vya ndani vinarusha kwa kiasi kikubwa vipindi vinavyozalishwa ndani.
Kutokana na kutambuliwa kwa
sanaa katika Katiba, kuwa na sera sahihi na uwekezaji mkubwa, nguvu ya
serikali, ubora wa kazi za sanaa na utamaduni ukapanda, uzalishaji ukawa rahisi
huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika ubunifu lakini juu ya msingi wa utamaduni
wa Korea na hivyo kufanya kazi ya kuakisi uhalisia wa maisha ya watu.
Ndiyo maana Marekani
imeendelea kuwa Taifa kubwa na lenye nguvu kubwa, nguvu ambazo hazitokani tu na
uchumi imara na mabavu ya kijeshi bali nguvu za kiutamaduni. Hebu angalia nchi kama China japo ina idadi kubwa ya watu (bilioni 1.5), bado
kiutamaduni hawana ushawishi kama walionao Wamarekani hata katika eneo lao la Asia
Mashariki. Ni Wakorea peke yao
wanaoshindana na Marekani katika soko la sanaa na utamaduni katika nchi za Asia . Kwanini? Kwa sababu wamelitambua kundi la Wasanii na ulinzi wa Miliki
Bunifu katika Katiba yao .
Inashangaza pale msanii wa
Kitanzania, kwa kuwa tu kapata jukwaa (gazeti) anapotumia nafasi hiyo kuwaponda
na kuwakejeli wasanii wenzake badala ya kuwatia moyo na kuisuta serikali kwa
kuwa imeitelekeza sanaa na utamaduni wa nchi na hivyo kushindwa kuenzi asili
yetu.
Tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment