Kikosi Kazi cha wasanii 12 kilichokwenda Bungeni Dodoma kuonana na Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa katika picha ya pamoja na Mh. Samwel Sitta
IMEKUWA ni kawaida kila
wakati wa uchaguzi kuona wasanii wakitumika kuvuta watu wakati wa mikutano ya
kampeni za wagombea urais, ubunge na hata udiwani. Hutumiwa kuwavuta watu ili
wafike kwenye mikutano hiyo kabla ya wanasiasa kuanza kampeni zao za kutaka
kuungwa mkono.
Pindi wanasiasa wanapopata
madaraka wamekuwa hawawakumbuki tena wasanii hadi pale uchaguzi mwingine
unapokaribia. Hili ni jambo linalokatisha tamaa, na limeendelea kujitokeza hata
sasa wakati tukiwa kwenye mchakato wa kutafuta Katiba mpya itakayotuongoza kwa
miaka mingine hamsini baada ya uhuru, ambapo vikao vya Bunge Maalum la Katiba
vimeanza mjini Dodoma tangu Februari 18, mwaka huu.
Wanasiana wameonekana
kupeleka nguvu zao kwenye masuala ya kisiasa kama muundo wa serikali na masuala yenye maslahi ya kisiasa na kusahau
mambo mengine muhimu ya kijamii, ikiwemo suala la wasanii ambao hutumika kama kivutio cha kuwavuta wapigakura kuja kwenye mikutano kusikiliza sera
za vyama.
Hivi karibuni timu ya
wasanii kumi na mbili ilikwenda Dodoma kuongea na Wajumbe wa Bunge la Katiba ili
kuwashawishi kuingiza vipengele viwili muhimu kwenye katiba ya nchi baada ya
Tume ya Katiba kuyapuuza maoni yao . Wasanii kupitia Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa
waliunda Baraza la Katiba ambapo Mashirikisho yalitoa mapendekezo kadhaa
yaliyofikishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pamoja na mapendekezo hayo
kupokewa lakini hakukuwepo na jambo lolote lililotokana na mawazo hayo (pamoja
na uzuri wake) lililochukuliwa na kuingizwa kwenye rasimu ya Katiba.
Kumekuwepo na kasumba ya
kuendelea kuitambua sekta ya sanaa kama ni sehemu
ya utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na
chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential).
Kwa mujibu wa utafiti wa
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wa mwaka 2006 unaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na wasanii milioni 6. Sasa ni miaka saba
imeshapita na kwa vyovyote idadi hii itakuwa imeongezeka mara dufu hasa
ikizingatiwa kuwa teknolojia imekuwa sana na asilimia 60 ya Watanzania ni vijana.
Ninapozungumzia wasanii
namaanisha watu wote wanaofanya kazi za sanaa na ubunifu, na si kama wengi wanavyodhani kuwa ni wale wanaoigiza au kuimba tu. Sanaa kwa
sasa ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika la Hakimiliki la Kidunia (WIPO)
ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato uliotokana na shughuli za Hakimiliki
ulikuwa ni zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini. Pia mchango wa ajira katika
kazi zilizotokana na Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji,
usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii. Pia wasanii ndiyo
wamekuwa wakilipa jina na utambulisho Taifa hili.
Hivyo, inashangaza kuona
kuwa Rasimu ya Katiba imetambua uwepo wa makundi mbalimbali kama wakulima, wavuvi, wafanyakazi, wafugaji nk. lakini ikashindwa
kutambua uwepo wa kundi kubwa la wasanii!
Kwa takwimu hizi utagundua
kuwa wasanii ni kundi kubwa sana
linaloyazidi makundi mengine huku likizidiwa na kundi moja tu la wakulima, pia
ni kundi linalochangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi, hivyo kutolitambua ni
makosa. Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Hakimiliki la Dunia (WIPO) wa Septemba 2012, sekta
ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 4.275.
Kwa
kutambua jambo hilo , Shirikisho la Filamu
Tanzania (TAFF) likishirikiana na Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (TAMUNET) waliunda
Kikosi Kazi cha watu 12 na kwenda Dodoma kupigania mambo makuu
mawili.
Kwanza
wasanii kutajwa na kutambuliwa katika Katiba mpya kuwa ni kundi rasmi kutokana
na ukubwa wa kundi hili nchini, kama yalivyotajwa makundi ya wakulima,
wafugaji, wavuvi na kadhalika, pia mchango wake katika ajira ya vijana na
ukubwa wa pato linalotokana na kundi hili, ambalo kutokana na kutokutambuliwa
linapotelea katika mifuko ya watu na kukosesha wasanii na Taifa pato
kubwa.
Kikosi Kazi hiki pia kilitaka ubunifu ulindwe kwanza kwa ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) kutajwa rasmi katika katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi zao uwekokama ilivyo katika mali nyingine za wananchi
wengine. Kwenye Rasimu ya Katiba imetajwa ulinzi wa kazi zinazohamishika na
zisizohamishika lakini mali zisizoshikika (za
ubunifu) hazikutajwa.
Kikosi Kazi hiki pia kilitaka ubunifu ulindwe kwanza kwa ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) kutajwa rasmi katika katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi zao uweko
Milikibunifu
ni mkusanyiko wa haki mbalimbali anazopewa mbunifu. Wasanii hulindwa na
Hakimiliki ambayo ni sehemu tu ya Miliki Bunifu. Kampeni ya wasanii kuhusu hili
la Intellectual Property (IP) kutajwa katika katiba ni kuwa katika Katiba
kumetajwa ulinzi wa mali zinazohamishika na zisizohamishika, lakini mali zisizoshikika
zinazotokana na ubunifu hazikutajwa na ndiyo maana pamoja na sheria kuweko,
serikali huzilinda hizo kama fadhila.
Nchi
kadhaa hutajwa kuwa zilikuwa na uchumi sawa na Tanzania wakati nchi yetu ikipata
uhuru wake mwaka 1961, zikiwamo Singapore, Korea Kusini, Thailand, Malaysia na
kadhalika, na kilichowafanya kutuacha kimaendeleo na kupata maendeleo ya haraka
ni ulinzi na uendelezaji wa Miliki Bunifu na ndiyo maana leo kuna Samsung, Hyundai,
LG, Daewoo nk. Suala hili la Miliki Bunifu ni pana zaidi ya sheria ya copyright
ambayo nayo kutokana na spidi ya teknolojia hujikuta ikipitwa na wakati kila baada
ya muda mfupi, ni muhimu kuwa katika sheria mama (Katiba) ambayo itaangalia
hali leo na miaka 50 baadaye.
Kwa
sasa Tanzania imepiga hatua kubwa ya
ubunifu katika maeneo nyeti ya kiuchumi kama vile kilimo, kwa hiyo
ipo haja ya kuhakikisha uvumbuzi huo unalindwa ipasavyo. Ni muhimu pia kulinda mali asili zetu kama vile utamaduni, na
maeneo ya kijiografia. Maeneo mengine yanayohitaji kulindwa ni pamoja na
muziki, na sanaa.
Kuwepo
kwa kwa sheria ya Miliki Bunifu kwenye Katiba ya nchi kutaleta uhakika wa
ulinzi wa haki hizi na kutawezesha kutungwa kwa sheria bora zaidi za ulinzi wa
haki ambao matokeo yake katika nchi zilizofuata mfumo huu ni maendeleo makubwa
sana katika sanaa na teknolojia.
Wizara
ya Viwanda na Biashara umeshaandaa sera ya Taifa ya Miliki Bunifu itakayokidhi
mahitaji ya nchi kwa kujenga msingi wa matumizi ya Miliki Bunifu ili kuchangia
kikamilifu katika kufikia lengo la Taifa la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka
2025. Lakini sera hii bila kukaziwa kwenye sheria mama inaweza isipewe uzito
unaostahili.
Ieleweke kuwa Ubunifu ni nyenzo muhimusana ya kuongeza ubora wa
bidhaa na huduma zinazozalishwa kwa gharama nafuu. Kutajwa kwenye Katiba ya
nchi, Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu itasaidia kufikiwa kwa malengo ya 2025
ikiwemo kupunguza umasikini nchini. Kufanikishwa kwa lengo hili la kitaifa kutasababisha
ukuaji wa uchumi wetu kwa kiwango kati ya asilimia 8 hadi 10 katika sekta ya
kilimo sambamba na sekta ya viwanda inayotegemewa na karibu asilimia 70 ya
Watanzania.
Ieleweke kuwa Ubunifu ni nyenzo muhimu
Kwa
hiyo, hili si jambo linalohusu sanaa peke yake bali ni suala mtambuka kwa
maslahi ya Taifa zima. Hii itawezekana tu iwapo itatambuliwa na kusababisha
kuwepo maendeleo ya kibiashara na uhamasishaji wa matumizi ya bidhaa
zinazozalishwa na viwanda vyetu vya ndani katika masoko ya maeneo EAC na SADC
pamoja na masoko mengine ya kimataifa ambako kuna ushindani mkubwa.
Tanzania ni mjumbe wa WTO
katika kundi la nchi masikini (LDCs) ambapo inayo fursa ya kufaidika na
makubaliano mbalimbali ya kimataifa ambayo hupatikana tu pale ambapo nchi
husika itazingatia utekelezaji makini na wa kimkakati wa Sera ya Taifa ya
Miliki Bunifu. Ni wakati sasa wa kutambua uhalali wa sanaa na Miliki
Bunifu kwa kuviweka kwenye Katiba mpya kwa maendeleo ya nchi.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment