Wasanii wakifuatilia semina ya TRA kwenye ukumbi wa maonesho wa Makumbusho ya Taifa, Jumanne wiki hii
Pia nilikuwepo kwenye semina hiyo, hapa nipo na mdau
NIMEKUWA nikisisitiza kuwa
hakuna 'excuse' yoyote kwa wasanii katika kukuza pato lao, kuondokana na
umaskini na hata kushindana kimataifa kama
hawataingizwa kwenye mfumo rasmi ambao utawafanya watambulike ndani na nje ya
nchi ili kujenga mazingira ya wao kuweza kukopesheka, kupata fursa za kikazi na
kukuza kazi wanazozifanya. Katika mataifa mengine wasanii wako rasmi na
wameweza kuvuma na kupaa kiuchumi.
Lakini pia nimekuwa nikitoa
wito kwa serikali kutumia fursa ya kuirasimisha tasnia ya burudani hususani
filamu kwa kutuanzishia chombo cha kusaidia maendeleo ya miradi kama sehemu muhimu ya kuifanya sekta hii ifikie
tunapopataka, na ni msingi muhimu ambapo mkakati wowote wa utengenezaji wa
filamu unapaswa kujengwa.
Badala yake wiki hii
tumeshuhudia kioja ninachoweza kukiita cha karne kilichotokea kwenye Semina ya
TRA ya urasimishaji wa tasnia ya muziki na filamu, ambayo iliisha kwa
kusambaratika bila hata kuagana rasmi kutokana na wasanii kuja juu baada ya maswali
waliyouliza kupata majibu ya kisiasa na ya kukatishana tamaa.
Semina hiyo iliyofanyika
katika ukumbi wa maonesho wa Jumba la Makumbusho ya Taifa katikati ya Jiji, kwanza
ilichelewa kuanza, badala ya kuanza muda uliotajwa wa saa tatu ilianza saa tano
huku wasanii mbalimbali wa filamu na muziki wakiitikia mwito huo.
Upande wa serikali
kulikuweko na Maafisa kutoka Kurugenzi ya Utamaduni ya Wizara ya Habari,
Utamaduni na Michezo, Basata, Cosota, Bodi ya Filamu na TRA, ambao ndio
walikuwa wasemaji wakuu. Semina ilianza kwa maelekezo kuhusu nini kitakachofanyika
ili kuanza kuhakikisha stempu za TRA zimebandikwa kwenye kila kazi ya sanaa.
Cosota ndiyo itakayokuwa
ikihakikisha uhalali wa kazi, Basata na Bodi ya filamu zitahakiki maadili ya
kazi husika na ndipo stempu maalum zitakapotumika kabla hazijaingia sokoni. Kwa
kweli ni mfumo mzuri ingawa imegundulika kuwa serikali haina nia njema kwa
tasnia ya burudani kama nitakavyoeleza
baadaye.
Mpango huu unaodaiwa ni wa
kurasimisha sekta hii ili kuiboresha umekuwa na maswali mengi mno bila majibu,
hasa kutokana na kile kinachoonekana kuwa upande wa serikali (kupitia taasisi
zake) hauelewi upande wa pili unatendaje kazi zake, unataka kuchukua haki ya
upande wa pili na kutokana na upya wa dhana yenyewe pande zote hazielewi nini
kinatakiwa.
Pamoja na TRA kujidai kuwa
wamefanya utafiti wa kutosha kabla ya zoezi zima za urasimishaji lakini ukweli
hakuna utafiti wowote wa kitaalam uliofanyika, hasa kutokana na maelezo
yaliyowasilishwa na hata majibu ya kukanganya yaliyotolewa na viongozi wa
mamlaka hiyo.
Inashangaza sana pale
viongozi wa TRA pamoja na kuelezwa ukweli wa matatizo yaliyopo na ambayo hayajapatiwa
ufumbuzi kwa miaka mingi sasa kati ya wasanii kwa upande mmoja na taasisi za
serikali (Cosota na Bodi ya filamu), lakini waliamua kufunika kombe mwanaharamu
apite kwa kutoa majibu mepesi lakini wakisisitiza kuwa wao wanachotaka ni
kukusanya kodi tu na hawatarekebisha chochote bali kukazia, masuala mengine
hayawahusu!
Ki ukweli wasanii hawana
imani kabisa na Cosota na Bodi ya filamu ambayo hata hivyo imebainika kuwa
haipo kwa sasa. Sijui inawezekanaje kuwaambia wasanii wapitie kwanza kwenye
taasisi ambazo hawaziamini kabla hawajapatiwa stempu?
Wasanii waliiuliza TRA
kwanini inadai inawalinda wasanii wakati ni wazi katika hili kazi yake itakuwa
ni kukusanya kodi kutoka kwa wasambazaji, jambo ambalo halina tija yoyote kwa
wasanii binafsi? Majibu yaliyotolewa yalileta mvurugano kiasi cha kusababisha
viongozi wote kuondoka kimyakimya kwa kupitia mlango wa nyuma na kuwaacha
wasanii wakiendelea na kikao kisicho rasmi ambacho kilihamia nje na kufikia
kutengeneza kamati ambayo itatayarisha mkutano mkubwa wa wasanii wote wa muziki
na filamu kutoa tamko la pamoja.
Sielewi ni kwanini serikali
imekuwa ikidharau tafiti zinazofanywa na wadau mbalimbali zinazoegemea kwenye
hali halisi, tafiti ambazo zimekuwa zinakuja na muarobaini wa kutatua mambo.
Mimi pia nimewahi kufanya utafiti kuhusiana na filamu ikiwemo urasimishaji,
nikagusia mfumo unaotumika Afrika Kusini ambao ungetufaa sana .
Tatizo la serikali yetu limekuja
pale wanapotaka kutumia utaratibu mpya kabisa ambao haujawahi kufanyika nchi
nyingine yoyote, utaratibu usioeleweka na usiofanyiwa utafiti, sijui kwanini
serikali inataka kugundua njia hiyo mpya ambayo mchambuzi mmoja anaiita ya ‘kibongobongo’
ili kulinda kazi za wasanii, wakati duniani kote taratibu zinafahamika? Hii
maana yake nini? Kwamba serikali inahitaji kodi tu kutoka kwa wasanii lakini
haina mpango wa dhati kuhusu wasanii. Kwangu hili halina ubishi.
Bila hata haya kiongozi wa
TRA anasimama mbele ya wasanii na kusema kuwa wamefanya utafiti na kugundua
kuwa wasanii wa Nigeria ni matajiri na sekta yao ni tajiri kwa kupitia njia hii
wanayotaka kuifanya! Hivi ni utafiti upi alioufanya na kwa Nigeria ipi? Labda nyingine lakini
si hii ninayoijua ambayo tasnia yake ya filamu inajulikaana kama
Nollywood.
Nollywood imekufa! Imekufa
kwa sababu ya viongozi waliopewa dhamana ya kuilinda na kulinda maadili kujiingiza
katika kukusanya mapato kibao bila hata kujali itaathiri vipi soko la filamu la
nchi hiyo. Fikiria, kwa sekta ya filamu iliyokuwa inatengeneza sinema mia moja
kila mwezi katika siku za nyuma, hivi sasa haiwezi hata kutengeneza sinema saba
katika mwezi! Hapa lazima kuna tatizo kubwa; 7/100! Hakika huko ni kushindwa!
Nollywood kumebakia watu wachache
kama Desmond Elliot, Uche Jumbo, Monalisa Chinda, Stephanie Okereke, Emem Isong
na wengine wachache wanaojaribu kutoa sinema. Wao wanajaribu kupambana kama mtu mmoja mmoja. Pia ieleweke kuwa wao ni sehemu ya
wasanii tu ambao wanapenda kufanya wakipendacho. Lakini unaweza kuona, wao si
watayarishaji wa filamu, ni waigizaji tu.
Hivyo mwisho wa siku,
watayarishaji halisi wa Nollywood hawatoi tena sinema. Kwa yeyote anayefuatilia
tasnia ya filamu ya Nigeria atakuwa anajiuliza wako wapi kina Chico Ejiro, Zeb
Ejiro, Fred Amata, Paul Obasele, Jetta Amata, Teco Benson, Fidelis Duker na
wengine? Tujiulize, kwa nini Nollywood imesimama? Kwa nini haifanyi tena sinema
katika Lagos ? Hata
Idumota au Ebinpejo Lane
hazisikiki tena katika ulimwengu wa filamu? Kwa asiyejua, haya ndiyo maeneo
maarufu ya Nollywood.
Kiongozi huyu wa TRA utafiti
huo kaufanyia wapi? Pia kwa kiongozi mwandamizi wa TRA kusema kuwa mamlaka
haitajali hata kama kazi za sanaa zitatumiwa
ovyo bila makubaliano ili mradi tu ziwe na stempu ya TRA inaashiria nini? Hebu
jaribu kutembelea mitaa ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam , nyakati za mchana utakuta
vijana wengi wameketi na kompyuta zao juu ya meza wakirudufu kazi za wasanii
mbalimbali, wa sasa na wa enzi hizo, bila hofu yoyote. Hili TRA inasema ruksa
ili mradi tu wawe na kazi zenye stempu ya TRA! Hivi hapa kuna urasimishaji kweli
au wanataka kodi tu ili wafikie lengo walilowekewa na Rais linaloanzia 2013?
Mbali na Kariakoo, shughuli
hizi zimekuwa zinafanyika karibu kila mahali jijini Dar es
Salaam na katika miji mingine ya Tanzania . Wala huhitaji kutumia
nguvu nyingi kuwatafuta na kuwakamata watu hawa. Wanaonekana kabisa tena mchana
kweupe! Lakini inasikitisha pale TRA wanapodai haliwahusu! Hata taasisi
inayohusika (Cosota) hawasemi chochote. Tukihoji tunaonekana tunalalamika.
Nathubutu kusema kuwa
sijawahi kuona mpango mbovu kama huu, halafu
bila aibu wanajisifu eti wamekuja na mkakati wa kuisaidia sekta ya burudani.
Hapa wanamuongopea nani? Wanashindwa hata kubainisha ni vipi msanii atafaidika
na hizi stempu za TRA huku vijana wanaorudufu kazi za msanii wakifanya wizi huu
kwa uhuru kabisa na bila bugudha yoyote hadi huo uharamia wao wanaoufanya kuonekana
kama ni jambo la kawaida!
Siku zote wasanii wa
muziki, maigizo, filamu na tamthilia wamekuwa wakilia ‘njaa’ wakati kazi zao
zikiibiwa kirahisi namna hii, Cosota ipo, Basata ipo, TRA wapo na taasisi
zingine zipo na hazifanyi chochote kuwanusuru na kadhia hii.
Sitaki kuamini wala
kukubaliana na kauli kutoka kwa mdau mmoja aliyeniambia kuwa katika hizi kazi
za kiharamia (piracy) kwa kazi za sanaa baadhi ya vigogo na viongozi ndani ya
Cosota wanahusika kwa kumiliki mitambo ya kurudufu kazi.
Nauliza tena, kwanini
tusijifunze kutoka sekta ya burudani ya Afrika Kusini?
Nawasilisha…
No comments:
Post a Comment