Afisa Utafiti Mwandamizi wa TRA, Ephraim Mdee, akielezea
kuhusu stempu maalum zitakazoanza kutumia mwakani
BADO naikumbuka hotuba ya
Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, aliyoitoa katika kikao cha bunge la bajeti
kwa mwaka 2012/13, pale aliposema: “Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA
147 kama ifuatavyo:-
“Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu
cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi
wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato
itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya
kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya
kudurufu kazi za sanaa hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa
nchini.
“Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu kwenye
bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii kupata
kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia serikali
mapato. Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na
kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii utaanza rasmi
tarehe 1 Januari, 2013…”
Kauli hii ilinifanya kuona kuwa angalau
sasa serikali imeanza kuonesha kuutambua mchango wa sekta ya burudani (filamu
na miziki) hapa nchini. Ikumbukwe kwa miaka mingi sasa, wasanii na
watengenezaji wa sinema miongoni mwa wadau wengine wa sekta ya burudani wamekuwa
wakitoa sinema ili kujipatia riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio.
Mwanzoni
niliamini kabisa kuwa kauli ya waziri iliashiria kuwa Serikali imekusudia kusaidia
sekta ya burudani ikue na kuleta tija kwa nchi yetu, na nilidhani imechelewa
kutolewa lakini baada ya kufuatilia kwa makini zoezi zima la matayarisho kuelekea
kwenye uwekaji stampu maalum kwenye kazi za sanaa litakaloanza Januari Mosi,
2013, nimekuwa na wasiwasi kama kweli serikali kupitia taasisi zake wanaifahamu
nguvu ya soko la filamu na muziki.
Nilihudhuria
semina moja iliyofanyika siku za karibuni katika ukumbi wa mikutano wa hoteli
ya Peacock, ambapo mwakilishi wa TRA alikuwepo na kuelezea jinsi ambavyo mamlaka
hiyo ilivyojiandaa kushughulikia suala la stempu maalum katika kuhakikisha
wasanii wanafaidi jasho lao.
Taarifa
za mamlaka zimetawanywa wiki hii kwenye vyombo vya habari kupitia kwa Afisa
Utafiti Mwandamizi wa TRA, Ephraim Mdee, kuwa mamlaka itaanza kuzishughulikia
kazi ambazo hazina stempu maalum kuanzia Januari Mosi mwakani, na kwamba
uzalishwaji, usambazwaji, uingizwaji kutoka nje, uuzaji, utumiaji au ununuaji
wa bidhaa za tasnia za filamu na muziki nchini kama vile CD, DVD au kanda
zisizo na stempu maalum za kodi litakuwa ni kosa la jinai na hivyo wahusika
watachukuliwa hatua kali! Eti lengo likiwa kukomesha wizi kupitia udurufishaji
wa nakala bandia na hii itasaidia kuinua pato la nchi na kuwanufaisha wasanii
kutokana na jasho lao!
Hivi,
ni nani aliyewaambia kuwa piracy (uharamia) ndiyo tatizo pekee lililopo katika
soko la filamu na muziki nchini? Hivi stempu hizi katika mazingira ya soko la
sasa zitasaidia nini kutibu matatizo kwa maendeleo ya sekta ya burudani? Hivi TRA
wanajua kuwa sekta ya filamu imefukarishwa kwa makusudi na watu wachache kwa
maslahi binafsi, tena hata baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi zake
wakiwemo?
Je,
wanaelewa kuwa utengenezaji wa filamu kwa soko la Tanzania unatafsiriwa kuwa sawa na
biashara ya barafu inayoweza kumyeyukia aliyenayo mikononi wakati wowote? Hali hii
huwafanya watengeneza filamu wa Kitanzania wajikute wakiingia mikataba haraka
ya kupata pesa japo kiduchu kabla barafu haijawayeyukia na kugeuka maji? Wakati
mwingine bila hata kurudisha gharama walizoingia!
Sijaelewa
kama TRA wana lengo la kuisaidia sekta ya filamu na muziki na wakati huohuo
kuongeza pato la nchi au lengo lao ni kujipatia pato litakalowafanya wafikie
lengo walilowekewa na rais na mwisho wa siku wasifie kuvukaa lengo! Maana
nawaona wanawekeza nguvu kubwa kuhakikisha stempu zinatengenezwa na kuanza
kutumika badala ya kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wasanii na
wanunuzi wa kazi za sanaa.
Niliongea
na wasanii kadhaa, tena kati yao wakiwa ni wasomi walioonesha kufurahishwa sana
na mpango huu wa TRA wa kuweka stempu, wakielekeza matumaini yao kwa TRA kuwa
itafanya kazi ya kulinda haki za
wasanii, wakisahau kuwa TRA kazi yake ni kukusanya kodi tu. Sasa kama elimu
haijatolewa tutakuja kuingia kwenye mgogoro mkubwa sana kwa wasanii kudhani kuwa kazi zao
zinalindwa na TRA.
Tusidanganyane,
hakuna mnunuzi wa kazi za sanaa Tanzania
anayenunua kwa kutazama stempu. Kwanza kazi
hizi zinanunuliwa na watu wa tabaka la chini, na wala si wale wa tabaka la kati
na la juu ambao wala hawana habari nazo. Hivyo elimu ni muhimu sana kutolewa kwa wanunuzi
katika kuzitambua hizi stempu maalum, na kujua umuhimu wa kununua kazi halisi.
Ki
ukweli, Mpango huu wa TRA umebeba maswali
mengi kuliko majibu. Hivi wanadhani stampu za TRA pekee zinatosha kuleta
ufanisi katika soko la filamu bila hata kuijua nguvu ya soko? Mbali na stampu
hizi je, kuna mikakati gani katika kudhibiti kazi zisizo na mhuri? Je,
mlaji atatofautisha vipi mhuri halali na batili? Hivi hawadhani kuwa ili zoezi
hili lifanikiwe inahitajika elimu kwa walaji?
Ni mechanisim gani
itakayotumika kuweza kutekeleza hilo
na je, msanii atahakikisha wapi kipato chake? Kwenye stampu au wapi? Nasema
hivi kwa kuwa hata kazi feki nayo inaweza kuwekewa stampu na atakayenufaika ni
msambazaji na TRA wala si msanii!
Hapa
TRA wanataka kuvuna pasipo kupanda kwa kutotaka kuwekeza kwanza, sijui ni
kwanini wanakimbilia kutaka kukusanya wakati hawajaweka miundombinu mizuri ya
soko la kazi za sanaa. Unatozaje kodi kwa soko la ovyo lisilo na uhakika ambalo
hujaliweka na wala huijui nguvu yake? Nina uhakika kwa kile ninachokisema na
ninachokiona hapa ni sawa na kutaka kumkamua ng’ombe maziwa pasipo kumlisha.
Matokeo yake ng’ombe atakufa na hata hayo maziwa kidogo hayataonekana.
Mfumo wa biashara ya filamu
nchini umekaa kienyeji sana .
Sijui Mamlaka ina mpango gani katika kuandaa miundombinu ya soko la filamu/muziki
ili wasanii na watengeneza filamu pia wafaidi jasho la kazi zao tofauti na
ilivyo sasa? Hivi wakisharasimisha sekta hii, serikali itawekeza au ndiyo
itaingia kwenye mpango ninaousema wa kuvuna pasipo kupanda? Sidhani kama
itakuwa busara kwa serikali (kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ) kukusanya mapato wakati
haijengi miundombinu ya soko, haijengi shule zitakazowasaidia wadau wa filamu
kujiendeleza, na wala haisaidii katika kutafuta soko!
Hapa hata wakikusanya kiasi gani, bado haitawasaidia wasanii
Ukiiangalia kijuujuu utadhani
ni jambo zuri, lakini ukweli serikali kupitia TRA inatengeneza bomu kwa tasnia
ya burudani, bomu ambalo limeleta mgogoro mkubwa katika nchi ya Ghana
sababu ya msingi ikiwa ni ndogo tu, kazi ya Mamlaka ya Mapato si kulinda haki
za wasanii bali ni kukusanya kodi. Kazi ya kulinda haki hizi iboreshwe katika
vyombo vya wasanii husika ili TRA iweze kupata takwimu sahihi za kukusanya
kodi.
Mi
nadhani ili kuleta ufanisi katika sekta hii walipaswa kwanza kuandaa takwimu za
kina kuhusu soko la filamu/muziki na kuzitazama fursa zilizopo kabla ya kuamua
chochote. Walipaswa pia kushirikiana na taasisi zingine za serikali kuandaa sera nzuri ya filamu itakayosimamia mambo haya kwa
kivtendo. Kwa kufanya haya, pia walipaswa kushirikiana na wadau na jopo la
wataalam watakaoangalia kanuni zilizopo kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini
cha sera mpya ya filamu. Sera ya filamu ndiyo hati pekee yenye kueleza kwa
ufasaha uwezekano mbalimbali katika kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya
uzalishaji wa filamu.
Sera hii inapaswa iende
mbali zaidi ikizingatia mchakato wa utoaji wa filamu na uanzishwaji wa haki za
usambazaji wa miliki. Katika mchakato huu, wasambazaji wanapaswa kuwasilisha
ripoti ya kila wiki ya kisheria katika shughuli zao za usambazaji ambayo
inaweza kutumiwa katika kutathmini utendaji wa kifedha wa filamu. Lakini pia
wawekewe mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao.
Nitashangaa kama TRA
watakana kuwa hata hizo DVD zinazoitwa za wizi huwa hazilipiwi kodi TRA. Zinalipiwa
kwa kisingizio cha wao hawajui kipi halali na kipi si halali, kwa msingi huu
TRA wamekuwa wanakusanya kodi ya kazi za wizi za wasanii siku zote.
Wanatuhakikishiaje kuwa mchezo huu hautakuwepo tena?
Kurasimisha sekta ya
filamu/muziki ni sawa, lakini tujipe muda kwanza kwenye hili suala la stempu na
kuelekeze nguvu kwenye kutoa elimu kwanza na kuandaa sera nzuri ya filamu,
vinginevyo tujiandae kuizika rasmi tasnia ya filamu/muziki.
Alamsiki…
No comments:
Post a Comment