Nov 27, 2012

Ni wiki ya majonzi kwa wasanii na wadau wa filamu nchini


 Mlopelo enzi za uhai wake

Wiki iliyopita ilishuhudia msanii aliyepata umaarufu mkubwa enzi za Kaole ya ITV, maaruf kwa jina la Mlopelo aliyefariki dunia mchana wa Alhamisi kwenye hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia aliyejitambulisha kwa jina moja la Azizi aliyesema kwamba katika maisha yake yote, Mlopelo alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya mwili yaliyokuwa yakitulia na kuibuka tena hadi umauti ulipomfika.



Mazishi ya Mlopelo yalifanyika Temeke siku ya Ijumaa na msiba ulikuwa eneo la Temeke Wailes mtaa wa Boko. Kabla wasanii wa filamu hawajatulia, msanii mwingine wa filamu nchini Tanzania, John Stephano Maganga, akafariki dunia katika hospitali ya Muhimbili kutokana na Ugonjwa wa kongosho ambao ulikuwa ukimsumbua kwa muda mrefu. 

 Marehemu John Maganga enzi za uhai wake

Hali ya marehemu John ilibadilika na kuvimba tumbo ghafla, hali iliyosababisha kufanyiwa upasuaji ili kuokoa maisha yake lakini ilishindikana na hatimaye kupoteza uhai wake.

Msiba wa marehemu John Stephano Maganga ulikuwa nyumbani kwao Mwananyamala na mazishi yamefanyika leo kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Enzi za uhai wake marehemu aliwahi kuigiza filamu kama Mrembo Kikojozi, Chanzo ni Mama, Barmaid na nyinginezo.

Marehemu Sharo Milionea enzi zake

Na habari nyingine mbaya zikatufikia jana usiku kwamba muigizaji na mwanamuziki, Hussein Ramadhan Mkieti almaarufu kama Sharo Milionea, alikuwa amefariki dunia kutokana na ajali ya gari iliyotokea mida ya saa mbili usiku katika eneo la Maguzoni Songa katikati ya Segera na  Muheza mkoani Tanga.

Habari za ajali hii na tukio hili la kusikitisha zilithibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Constantine Masawe. Kwa mujibu wa Kamanda huyo, gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T478 BBR alilokuwa akiendesha marehemu kutokea Dar es Salaaam kwenda Muheza lilipofika katika eneo hilo liliacha barabara na kupinduka na hivyo kusababisha mauti yake.

Mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali Teule ya Muheza ukisubiri kuzikwa hapo kesho kijijini kwao.

No comments: