Mar 16, 2011

Wasanii kuisusa Cosota ni kujimaliza wenyewe

*Cosota ni ya wanachama, si taasisi ya Serikali kama wanavyodhani
*Wanachama wa Cosota wana nguvu ya kisheria kuwashughulikia wezi

Katibu Mtendaji wa Cosota, Yustus Mkinga

NI jambo la kufurahisha sana kuona tasnia ya filamu Tanzania (Bongo movies), inazidi kushamiri na kukubalika ndani na nje ya mipaka yetu.

Licha ya mafanikio hayo, bado zipo changamoto nyingi zinazowakabili wasanii wa filamu pamoja na filamu zao kupendwa na kusambaa sehemu nyingi duniani. Mambo yanayowakwaza watayarishaji na wasanii wengi wa filamu ni kutokuzijua haki zao na wala hakuna jitihada zozote zinazofanywa kutaka kuzijua.


Kumekuwepo dhana iliyojengeka miongoni mwa wasanii, si wa filamu tu bali hata wale wa fani nyingine kuwa Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), hakina faida kwao kwa sababu ya kuendelea kuibiwa kazi zao zinazowanufaisha wachache ikiwa ni pamoja na kutolipwa pesa za kutosha zinazokusanywa kupitia kazi zao na hivyo wangependa chama hicho kivunjwe.

Licha ya kufahamika wazi kuwepo kwa chama kinachosimamia na kulinda kazi za wasanii (Cosota), kilichoanzishwa kwa kujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge mwaka 1999, bado tatizo la kuibiwa kazi lingalipo. Kila siku wasanii wamekuwa wakilalamikia kuibiwa kazi zao, zinazonakiliwa isivyo halali kisha kuuzwa kwa wingi bila wenyewe kufaidi jasho lao.

Hivi karibuni nilifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Chama cha Waongozaji wa Filamu (Tafida), Christian Kauzeni maaruf kwa jina la John, aliyeniambia kuwa wanachama wa chama anachokiongoza na shirikisho la filamu kwa ujumla wanaona moja kati ya sababu inayowafanya waibiwe na kupoteza haki zao ni Cosota kushindwa kufanya kazi zake ipasavyo. Hivyo wasanii na wadau walio wengi wameamua kuisusa Cosota kwa kudhani kuwa haina umuhimu tena kwao.

Kauzeni alisema pamoja na kuanzishwa kwa Cosota, sheria haijatumika kikamilifu kudhibiti vitendo vya kuvunja haki za watunzi, wasanii, wafasiri, watangazaji, wachapaji na hasa katika kuhakikisha wanapata maslahi yanayolingana na kazi zao baada ya kuuzwa au kusambazwa kazi hizo.

Wakati wasanii na wadau wakipinga uwepo wa Cosota, chama hicho kimekuwa kikitoa wito kwa wasanii wote nchini kuwa na ushirikiano ili kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa kazi bandia ili kuongeza kipato chao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Cosota, Yustus Mkinga, amekuwa akikaririwa mara kwa mara kuwa ushirikiano mdogo wa wasanii ndiyo kikwazo.

Naamini kama wasanii wenyewe wataamua kwa dhati kukaa chini, kujifunza na kurekebisha baadhi ya mambo, hakuna shaka watapiga hatua kubwa zaidi ya waliyoifikia na kutimiza malengo waliyojiwekea.

Pamoja na hayo Cosota inatakiwa kutekeleza majukumu yake kuwasaidia wasanii ikiwemo kuhamasisha na kuelimisha kuhusu hakimiliki na ikiwezekana kutafsiri sheria hiyo au maeneo muhimu ya sheria hiyo katika lugha ya Kiswahili.
Elimu hiyo inapaswa itolewe sambamba na kuwaelimisha wanachama au wadau wake kuhusu hatua za kuchukua pale mgogoro wa hakimiliki ukitokea. Wanachama wa Cosota na wadau wengine wa sheria ya hakimiliki waelimishwe au kupewa mwamko wa kufahamu haki zao kisheria, yaani jinsi zinavyolindwa, zinavyohifadhiwa na namna ya kuzidai na kuzitetea.

Lakini pamoja na kuwa Cosota kimeonekana kushindwa kutekeleza mambo hayo ipasavyo, bado sioni mantiki ya wasanii kuisusa bali wanapaswa kutambua kuwa ili Cosota iweze kufanya kazi yake ipasavyo ni wao kujiunga kwa wingi katika chama hicho, watakapokuwa wanachama wa Cosota watapata nguvu ya kisheria kuwashughulikia wezi wanaonakili na kutumia kazi zao kinyemela. Kwa mujibu wa sheria, Cosota ni mali ya wanachama na wala si taasisi ya Serikali kama ambavyo wengi wanadhani.

Wanapaswa waelewe kuwa Mtendaji wa Cosota ni mwajiriwa wa mkataba maalum na alipewa kipindi cha miezi sita tu ili kuthibitishwa, hivyo tangu aingie madarakani katikati ya 2007 alipaswa kupewa uthibitisho na bodi ya Cosota lakini kwa kutokuwepo bodi amekuwa akitumia nafasi hii kukwepa kuhojiwa na kutathminiwa na Bodi iliyomweka.

Ili kuifanya Cosota iwajibike na kumaliza tatizo la wizi wa kazi za sanaa wasanii wanapaswa watambue ukweli uliopo kuhusu Cosota, kwani tatizo la wizi wa kazi za sanaa lina sura nyingi na lilishafanyiwa kazi kuanzia mwaka 2001 na National Anti Piracy Committee, taratibu (regulations) za kutekeleza hili zilishapitishwa tangu mwaka 2006 na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo, Nazir Karamagi.

Lakini tangu Karamagi aidhinishe taratibu hizo, kumekuwepo tatizo la serikali kutotoa fungu la fedha la kuwezesha utekelezaji wa kazi hiyo, na jambo hilo halijatekelezwa hadi leo. Waziri aliyefuatia katika wizara hiyo baada ya Karamagi akakalia uamuzi wa kuchagua Mwenyekiti wa Bodi ya Cosota kwa sababu fulanifulani.

Waziri huyo ndiye amekuwa chanzo cha yote kwani aliamua kutoikubali bodi iliyochaguliwa na wadau katika mkutano wa mwisho uliofanyika mwanzoni mwa 2007, na wala hakuiruhusu bodi iliyopita kuendelea mpaka utatuzi upatikane na aliamua kukaa kimya (kuna uvumi unaosema) ili achomeke watu wake katika bodi nzima ingawa ana uwezo kisheria kuteua wajumbe watatu anaowataka kuwepo kwenye bodi yenye jumla ya wajumbe 15.

Siku chache kabla ya Bunge la Bajeti la mwaka huo, waziri akapeleka majina ili yachapishwe kwenye gazeti la Serikali. Cha kushangaza majina hayo yalikuwa tofauti na yale ambayo wanachama wa Cosota walichagua katika Mkutano wao Mkuu, aliingiza chaguo lake ambalo haliwakilishi wadau kamili wa Cosota kwa kufuata uchangiaji wao katika Cosota.

Tangu wakati huo Bodi ya Cosota haijawahi kukukutana na haijulikani hatima yake ni nini, ambapo pamoja na kazi nyingine uhakiki wa bajeti na mahesabu ya taasisi hupitishwa na bodi kwanza ndipo huenda serikalini kwa hatua nyinginezo, kutokana na kutokuwepo bodi ambayo ndiyo muajiri wa 'staff' wa cosota kwa mujibu wa sheria inayoiunda ikiwa ni pamoja na Mtendaji, imepelekea mtendaji aliyepo kufanya usaili na uajiri kwa matakwa yake binafsi.

Siku zote nimekuwa nikiwaeleza jamaa zangu ambao ni wasanii na watayarishaji wa filamu kuwa haki ya mtu hainunuliwi, hakimiliki na hakishiriki ya Mtunzi kwa Tanzania hainunuliwi hata baada ya kifo chake huendelea kuwepo kwa zaidi ya miaka 50, kwa nchi kama Marekani imepanda na kuwa miaka 75 baada ya kifo, kwa mantiki hiyo kuuza haki (kama ambavyo wasanii wamekuwa wakifanya) ni kosa kubwa, labda wasanii wakielimishwa hili na kujua hasara zake inaweza kuwasaidia.

Kila kukicha wasanii wanatengeneza filamu, lakini ukweli uliopo ni filamu hizi kutokuwa mali yao kwani wanauza haki zao kwa wasambazaji, tena kwa muda wote, wala hakuna muda wa kumilikiwa kazi zao wakati iwapo mtunzi atakubaliana na Msambazaji au Mtayarishaji lazima kuwe na muda maalum wa umiliki wa kazi hiyo na si kama ilivyo sasa.

Nawashauri viongozi wa Shirikisho la Filamu (TAFF) kuwaelimisha wanachama wao kuwa kuisusa Cosota hakuwasaidii, wanatakiwa kujiunga kwa wingi ili kukomesha tabia hii kwani kila mtayarishaji au msanii anaonekana (ashakum) mjinga kwa kushindwa kujua haki zake za msingi. Huu ni ujinga usiopaswa kuvumiliwa hata kama sababu iliyomfanya aibiwe ni kutokana na umbumbumbu wa kutojua sheria za Hakimiliki na hakishiriki.

Nimewahi kusoma mahali fulani kuwa zipo haki tisa za kazi lakini sina uhakika kama kuna msanii yeyote anayejua ni haki zipi zinamhusu yeye na kuzitumia kwa ajili ya kulinda maslahi yake. Kuna mdau mmoja alinidokeza kuwa wasanii sasa watarajie “maumivu makubwa” kwani dunia inabadilika kuelekea mfumo wa Digitali, wasingeuza haki zao huu ungekuwa wakati mzuri sana kuvuna fedha iwapo wangekuwa ni wamiliki wa filamu hizo.

Nawashauri viongozi wa shirikisho na vyama vya sanaa kuwaelimisha wasanii wote wajiunge Cosota ili kupata nguvu ya kisheria badala ya kususia jambo ambalo haliwezi kuleta ufanisi wowote katika kazi zao, badala yake watajikuta siku moja wakilia na kusaga meno.

Naomba kuwasilisha.

No comments: