Kupata mafunzo ni jambo muhimu, picha hii inaonesha
baadhi ya washiriki wa mafunzo ya utengenezaji filamu
katika Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut)
yaliyofanyika mwaka jana
IJUMAA iliyopita nilikutana na muongozaji na mwandishi wa miongozo ya filamu (script), James Gayo, ambaye pia ni msomaji wa makala zangu na tulipata nafasi ya kubadilishana mawazo kuhusu yanayojiri katika tasnia ya filamu hapa nchini.
Gayo hakusita kunieleza wasiwasi wake kuwa pamoja na ujuzi alionao kuhusu filamu lakini amekuwa akisita sana kuingia katika utengenezaji wa filamu za kibiashara kwa soko la filamu nchini kwa sababu ya matatizo yanayoathiri sekta ya filamu ambayo hadi sasa hakuna juhudi zozote zinazochukuliwa kuyatatua. Matatizo hayo ni kutokuwepo malengo, mipango mibovu na uchoyo usiokuwa wa lazima.
Gayo, ambaye pia ni mchoraji wa katuni maarufu ya Kingo na mkurugenzi wa Kampuni ya Gaba Africa inayomiliki shule ya kutoa mafunzo ya sanaa na filamu (Gaba Art Centre) yenye maskani yake Kinondoni (karibu ya viwanja vya Leaders Club) jijini Dar es Salaam, aliongeza kuwa ukosefu wa elimu na kutokuwepo utafiti pia unasababisha kuwa na uzalishaji mbovu wa sinema nchini Tanzania.
Alisema kuwa watayalishaji wa filamu nchini, wamekosa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachokubalika. Kwa mujibu wa Gayo, watayalishaji wengi wa filamu nchini ni wabinafsi na wanaowekeza kidogo na kutarajia wavune mara dufu kwa mara moja.
Ubinafsi huo umesababisha filamu zetu kuwa ni kitu kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Watu wanalipua kazi na wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam. Wanafanya mambo ili mradi wanajua watauza na kupata pesa, basi.
Ubinafsi huu umekuwa ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu na kadhalika.
Ubinafsi huu umekuwa ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu na kadhalika.
“Ni mpaka pale wataalam watakapoachwa wafanye kazi yao kitaalam, msambazaji naye afanye kazi yake ipasavyo, ndipo mambo yatakapoanza kwenda vizuri,” alisema Gayo, na kuongeza kwamba kama kila mtu atacheza upande wake, mambo yatakuwa bora.
Gayo ambaye anaweza asifahamike sana katika ulimwengu wa filamu hapa nchini lakini ni maarufu nje ya mipaka ya Tanzania, amewahi kutengeneza filamu ya 'A Trip', ambayo picha zake zilipigwa jijini Kampala, Uganda na imempatia mafanikio kimataifa ikiwa ni pamoja na kupewa mialiko mbalimbali kuhudhuria mafunzo na utengenezwaji sinema za Hollywood, Bollywood na kwingineko. Gayo pia alinieleza kuwa hadhani kama uharamia katika filamu (film piracy) linaweza kuwa tatizo kubwa sana hapa nchini kama wengine wanavyolichukulia bali uwepo wa mikakati mibovu katika masoko ndiyo tatizo kubwa linaloikabili sekta yetu.
Suala hili la masoko likanifanya nikumbuke kauli ya mmoja wa watayalishaji maarufu wa filamu hapa nchini, Hamisi Kibari, ambaye pia ndiye mhariri wa gazeti hili ambaye huwa hafichi anavyokerwa na kutokuwepo uwazi kwenye usambazaji wa filamu, hasa ile dhana ya filamu kusemwa kuwa hazifanyi vizuri sokoni kinyume na ukweli ulivyo, amekuwa akisisitiza kuwa tatizo ni kutokuwepo uwazi katika biashara kati ya mtayalishaji na msambazaji. “Wanadurufu nakala nyingi zinazofurika sokoni na kisha kukuambia kuwa filamu yako haiuziki,” alinieleza.
Kibari ambaye anatarajia kuingiza sokoni filamu ya “Naomi” iliyotengenezwa takriban miaka minne iliyopita, alilaumu kuwepo hali hiyo ambapo sinema hufurika sokoni bila mpangilio kitendo kinachosababisha kutopata mapato stahiki yanayotokana na uzalishaji. Alishindwa kuingiza sokoni filamu ya Naomi kutokana na kutofautiana na matakwa ya wasambazaji katika mambo fulanifulani ambayo ni kinyume na misingi ya haki.
Suala la masoko ndiyo hoja yangu kubwa inapojikita katika makala ya leo kwa kuwa inakwenda sambamba na mambo aliyoyataja Gayo: elimu, ubinafsi na kukosa malengo. Ieleweke kuwa hii vurugumechi ya soko letu inachangiwa na watu walioko sokoni kujaribu tu kupata faida iliyo kubwa zaidi bila kuangalia upande wa pili unafaidikaje. Kwa maana hiyo, wanachochewa zaidi na uchoyo na ubinafsi, na siyo kuwajali wengine.
Masoko hutegemea sana taarifa iliyo sahihi, ndiyo maana nimekuwa nikiishauri Serikali ihakikishe taarifa muhimu kuhusu soko la filamu zinapatikana. Ili masoko yaweze kuwa katika ushindani mzuri, wadau wote sokoni wanapaswa kuwa wamepata taarifa sahihi kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba kutokana na matendo yao. Ikiwa baadhi watakuwa na taarifa sahihi zaidi kuliko wengine, hizo tofauti zitapelekea kuwepo na matokeo mabaya. Serikali lazima iingilie kati kwa kutoa taarifa ambazo masoko yanapaswa kuwa nazo, na kuweka mazingira bora zaidi yenye mafanikio na haki.
Taarifa, kama kilivyo kitu kingine chochote cha thamani tukitafutacho ni gharama kukipata, lazima tutoe kitu cha thamani ili tupate taarifa iliyo sahihi na kwa wingi zaidi. Taarifa yenyewe kama ilivyo ni bidhaa inayopitia mchakato wa ubadilishanaji kuhusu masoko; kwa mfano, tunanunua vitabu ambavyo vina taarifa kwa sababu tunathamini taarifa iliyoko kitabuni kuliko tunavyothamini kile tunachokitoa badala yake.
Serikali inapaswa kuwa wakala wa kusaidia masoko yaweze kufikia kwenye “ubora” unaotakiwa na tumekuwa tukitegemea kuona serikali ikianzisha sera “bora” na makini kwa kutuanzishia chombo maalum kitakachokuwa na uwezo wa kuzitangaza kazi zetu ambacho kitakuwa na vitengo vitano:
-Kitengo kinachohusika na utoaji wa taarifa za upatikanaji wa pesa (funding information) na kutoa fursa kwa watengenezaji wa sinema.
-Kitengo kinachoandaa takwimu za kina na kutoa fursa ya kuzitangaza kazi zetu katika masoko mengine duniani hivyo kuongeza uwezekano wa kuuza kazi zetu kimataifa na kuigiza pesa za kigeni.
-Kitengo kinachowalazimisha wasanii na watengeneza filamu kupata mafunzo ya weledi (professionalism).
-Kitengo kinachosimamia mapato (revenue generation) yatokanayo na filamu. Serikali yoyote iliyofanikiwa katika sekta ya filamu ina kitengo cha aina hii.
-Kitengo kinachosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia/wizi (piracy) wa kazi za sanaa na kuwafanya watengenezaji kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato (economic reward) yatokanayo na kazi zao.
-Kitengo kinachosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia/wizi (piracy) wa kazi za sanaa na kuwafanya watengenezaji kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato (economic reward) yatokanayo na kazi zao.
Nimekuwa nikiandika mara nyingi kuishauri serikali kuirasimisha sekta hii ili kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato kupitia tasnia ya filamu, hata hivyo, bahati mbaya sana hali halisi katika nchi yetu sivyo ilivyo. Katika nchi hii, siasa imepewa kipaumbele kiasi cha kuathiri mfumo mzima wa maisha yetu bila kujali ni nini tunapoteza.
Ikiwa tunataka kuelewa mahusiano kati ya sera na matokeo ni vizuri akilini mwetu ikaeleweka kwamba suala la mali ni dhana ya kisheria wakati ambapo utajiri ni dhana ya kiuchumi. Haya mawili huwa yana kawaida ya kuchanganywa, lakini yanapaswa kutofautishwa.
Michakato ya masoko mara nyingi hugawanya tena utajiri kwa wingi mno. Kinyume chake, ugawanyaji tena wa rasilimali usiofuata matakwa ya wengi (unapofanywa na wachache, hujulikana kama “wizi”) unapaswa kukatazwa chini ya kanuni inayoendesha soko huria, ambayo inahitaji kwamba mali lazima ieleweke vizuri na iwe imewekewa ulinzi wa kisheria.
Soko la filamu hapa nchini limejikita katika kanuni ya mwenye nguvu ndiye anayefaidi (Darwinism) kitu ambacho ni hatari kwa taifa, kwa sababu pia muundo wa soko letu umekuwa ukishusha hadhi ya utamaduni na sanaa zetu.
Ni bora tukatahadharisha kuwa sanaa na utamaduni ndivyo vitu vyenye mwitiko mkubwa kwa vipengele vya nafsi ya mwanadamu, na kwa maana hiyo, haviwezi kuachwa mikononi mwa wachache kuamua hatma yake ama kuuzwa na kununuliwa kama vile nyanya. Kuiachia sanaa mikononi mwa wenye pesa wachache ni sawa na kuusaliti utu tuliourithi wa sanaa.
Ili masoko yaweze kutoa mwongozo kwa ajili ya kuratibu jamii, mali na mikataba lazima iweze kuwekewa misingi mizuri ya kisheria. Serikali inayoshindwa kutoa hizo huduma zenye manufaa kwa jamii huzuia masoko yasishamiri. Serikali inaweza kutimiza matakwa ya umma kwa kutumaini mamlaka yake kuunda mfumo bora wa sheria na haki, siyo kwa ulegevu, ila ni kwa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na wakati huo ijue kuheshimu mipaka katika kutumia madaraka yake.
Serikali dhaifu si sawa na serikali inayoheshimu mipaka ya madaraka yake. Serikali dhaifu ambayo pia haiheshimu mipaka ya madaraka yake inaweza kuwa hatari sana kwa sababu itafanya mambo ambayo haipaswi kufanya, na hii ni hatari kubwa sana kwa taifa.
Masoko huria hufanya kazi vizuri zaidi kwa kule kuwepo kwa serikali inayoongozwa kwa misingi ya utawala bora na inayosimamia na kutekeleza utawala wa sheria bila upendeleo katika uendeshaji wake.
Ni vizuri ikakumbukwa pia kwamba yapo matatizo mengi ambayo yanapaswa kutatuliwa kwa harakati za makusudi; haitoshi tu kusisitiza kwamba michakato ya masoko huria itatatua matatizo yote.
Alamsiki
No comments:
Post a Comment