Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya
TAKRIBAN miezi miwili iliyopita nilibahatika kukutana na kiongozi mmoja mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika kikao kisicho rasmi wakati akijaribu kuangalia uwezekano wa kukusanya mapato kupitia tasnia ya burudani, hasa muziki na filamu.
Japo mimi si kiongozi wa taasisi yoyote lakini nilipata heshima ya kukutanishwa naye kwa kuwa wanathamini mchango wangu katika kuikuza na kuiendeleza tasnia hii. Katika makala hii sitaelezea tulichozungumza, nitajaribu kuongelea jambo moja ambalo nadhani ni kikwazo kinachoikabili Mamlaka ya Mapato katika kukusanya mapato kupitia tasnia ya burudani.
Siyo siri kwamba sekta ya burudani imesheheni utajiri mkubwa sana wa utamaduni na uchumi kupitia filamu za Kibongo, na sina shaka kwa hili kwani nina data. Tatizo ni kwamba hadi sasa tasnia ya filamu bado haijawa rasmi na imepelekea wadau wake waendelee kuwa masikini wa kutupwa.
Kumekuwepo nadharia kwamba Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za wanyonge nchini (Mkurabita) inataka kuirasimisha tasnia hii ili kuwafanya wasanii wafanye kazi kwenye mazingira yaliyo rasmi kwa kuwa hali ilivyo sasa inawafanya wakose fursa nyingi za kukuza kazi zao na kuongeza vipato.
Bahati mbaya katika nchi hii tumekuwa tukiishi katika nadharia zaidi, kwani matamko yoyote yanayotolewa na viongozi huwa hayafanyiwi kazi, hata kama kinachoongelewa kina tija. Nakubaliana kabisa na malalamiko ya wasanii kukosa fursa za kupata mikopo kwenye asasi za kifedha, mianya ya kufanya kazi mbalimbali za serikali, na hata kama kazi zao za sanaa zinakua lakini hazithaminiwi ipasavyo kutokana na wao kutokuwa rasmi.
Pengine walioanzilisha Mkurabita walikuwa na lengo zuri wakitaraji mafanikio mbalimbali yatokane na mpango huo, lakini bado kuna changamoto nyingi katika kufanikiwa kwake. Changamoto hizo ni pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya watendaji serikalini unaopelekea wananchi kukosa uelewa pia, urasimu uliopo kwenye wizara na Idara mbalimbali serikalini, uwepo wa sheria zenye mkanganyiko kama ile ya manunuzi (Procurement Act) na kadhalika.
Urasimishaji wa Biashara yoyote ni jambo lisiloepukika kama tunataka kuendelea, ili wasanii waweze kuwa na maendeleo na kukua kiuchumi hawana budi kurasimishwa ikiwa ni pamoja na kazi wanazozifanya.
Sifa za kuwa rasmi ni kusajiliwa kwa kazi zao, kuwa na jina la biashara, zenye ubia, zikifanywa kikampuni, zenye leseni ya biashara, zenye eneo/mahali maalum pa kufanyia kazi, zilizo kwenye kumbukumbu inayoeleweka, zinazotofautisha mali ya biashara na binafsi.
Hakuna 'excuse' yoyote ambapo wasanii wanaweza kukuza pato lao, kuondokana na umaskini na hata kushindana kimataifa kama hawataingizwa kwenye mfumo rasmi ambao utawafanya watambulike ndani na nje ya nchi ili kujenga mazingira ya wao kuweza kukopesheka, kupata fursa za kikazi na kukuza kazi wanazozifanya. Katika mataifa mengine wasanii wako rasmi na wameweza kuvuma na kupaa kiuchumi.
Nadhani sasa ni wakati muafaka Serikali ione umuhimu wa kuwashirikisha wasanii katika masuala yote na nyakati zote na si kusubiri wakati wa kampeni za uchaguzi tu. Hapa serikali itakuwa haiwatendei haki wasanii.
Katika kuirasimisha tasnia hii tutahitaji chombo cha kusaidia maendeleo ya miradi kama sehemu muhimu ya kuifanya sekta hii ifikie tunapopataka, na ni msingi muhimu ambapo mkakati wowote wa utengenezaji wa filamu unapaswa kujengwa.
Tunahitaji chombo kitakachozingatia kuchangia fedha kwa miradi ya maendeleo katika makundi kama; sinema ndefu na fupi, Makala (Documentaries) na Uhuishaji (Animation).
Misaada ya maendeleo itakayotolewa ichukuliwe kama uwekezaji na kuweka mifumo ya kufidia matumizi yote ya maendeleo na riba kwa kazi wakati mradi unaingia katika awamu ya uzalishaji (production phase). Endapo mradi utashindwa kueleweka, chombo kilichoundwa kiwe na haki ya kurejesha gharama.
Chombo kizingatie kusaidia katika uzalishaji wa filamu na makala ama kwa njia ya mikopo au ruzuku. Kizingatie katika kutoa fedha za uzalishaji hasa kama uwekezaji na mrejesho wa gharama za matumizi wakati wa utoaji wa usambazaji na maonesho. Pamoja na yote chombo kihakikishe kuwa usambazaji na maonesho ya filamu za ndani na makala zinalifikia soko la uhakika.
Naamini kuwa mafanikio ya filamu yoyote iliyokamilika au uzalishaji wa video hutegemea masoko na promosheni. Chombo hiki kitapaswa kutoa mikopo kwa ajili ya masoko na matangazo ili kuhakikisha filamu na video zinaonwa na watazamaji wa ndani na kimataifa.
Chombo pia kiunge mkono juhudi za masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu ambazo zina maslahi kwa watazamaji wa Tanzania.
Ili kuongeza vyanzo vya mapato Serikali itapaswa kuzindua Mpango Kasi wa Kukuza Uchumi wa Tanzania kupitia filamu na muziki. Mkakati huo utoe vipaumbele vyake katika ukuaji kwa sekta, ambapo tasnia ya filamu, TV na kadhalika virasimishwe.
Kuifikiria tasnia ya filamu na burudani kama kipaumbele muhimu cha ukuaji wa uchumi itaonesha kukiri kuwa uchumi wa dunia ya sasa unahama kutoka zama za viwanda kwenda zama za habari. Ieleweke kuwa tasnia ya filamu Marekani (Hollywood) inashika nafasi ya pili nchini humo na ya tatu duniani katika ukusanyaji mapato.
Tutake tusitake uchumi wa dunia sasa unahama kuelekea zama za habari na usimamizi wa elimu na biashara; hii inathibitishwa na mkazo ulioongezeka katika utafiti na maendeleo na kuongezeka kwa teknolojia.
Tuwe na sera na idara ya Utafiti chini ya nguzo ya zama za habari katika kukuza utafiti sahihi na sera za kutoa taarifa ambayo itaongeza taarifa ya ndani ya usimamizi wa uwezo wa soko katika tasnia ya video, na kutoa taarifa zitakazofikiwa kwa urahisi na vyombo vyote binafsi na vya umma kwa anayetaka kujua zaidi kuhusu sekta hiyo.
Sera zitakazosimama katika misingi ya utendaji ya idara kama:
-Kutoa michango ya mara kwa mara kukuza sera na mchakato wa sheria katika sekta. Kwa kuchangia katika mifumo hii, tutakuwa tukihakikisha kuwa sera zinaendelezwa na hatua inayofuata ni kwa manufaa na faida ya walaji/ watazamaji, serikali na sekta;
-Kuendeleza sera na miongozo kwa ajili ya sekta katika baadhi ya maeneo;
-Kufanya utafiti katika jambo lolote kwenye tasnia ili kuishauri serikali kuhusiana na maendeleo muhimu katika sekta na kama chombo cha kuweka taarifa ya sekta ya maendeleo yaliyopo;
-Kuanzisha na kutekeleza usimamizi wa mfumo wa habari (Mfumo wa Habari wa Kisekta) ambao utatumika kama mfumo wa takwimu za kina wa sekta ili kujenga mizani yenye ufanisi katika utoaji taarifa na kutunza takwimu za kuaminika. Hii itasaidia kufikiwa kwa ushirikiano wa sekta, na taasisi husika za kiserikali ambazo zinahusika na sekta hii;
-Kutoa huduma mbalimbali kwa wadau wote husika na wananchi, hii itaweza kusaidia katika taarifa zinazohusiana na ushirikiano wa watengeneza filamu, takwimu za makampuni, takwimu za filamu za ndani na kadhalika. Wigo wa huduma ya idara iwe kupelekea kukua kwa kasi na kwa msaada wa tasnia na takwimu sahihi za kibenki, huduma hizi zitaweza kuongezeka katika mambo mengine ya kusisimua;
-Yawepo mazungumzo na kuanzisha mikataba ya ushirikiano kati ya chombo husika na watu wowote, mashirika na taasisi.
Naamini malengo ya serikali yanaelekezwa katika maendeleo ya vijijini, kuongeza ajira na maendeleo ya biashara. Ni muhimu sasa kuanzisha chombo hiki pamoja na kuirasimisha sekta hii katika kuonesha jinsi gani ya shughuli za tasnia zinachangia Pato la Taifa, ongezeko la ajira sambamba na mchango wake kwa maendeleo ya vijijini na mshikamano wa jamii.
Jambo muhimu katika kutoa ushahidi wa hili ni kusambaza taarifa za mara kwa mara kuhusu sekta. Ni muhimu katika kukusanya takwimu zitakazotoa taarifa ya viashiria vya utendaji muhimu kwa ajili ya sekta ya filamu, ambayo itapatikana mara kwa mara.
Ushiriki wa jamii na kushauriana ni muhimu katika mchakato wa maendeleo ya sera. Ili kuwa na ushiriki wa pamoja kati ya wadau wote (serikali, tasnia na vyama vya kiraia), chombo kitakachoundwa lazima kiwe na uwezo wa kutoa na kusimamia majukwaa ya uwasilishi ili kuwezesha mazungumzo. Aidha, lazima kiwe na uwezo wa kukutana na wadau mbalimbali.
Ushiriki wa umma pia ni sehemu muhimu ya mkakati wa chombo kufikia malengo ya milenia (Vision 2025). Mkakati kwa malengo hayo iwe ni kuhusu Kuipeleka Tasnia kwa Wananchi, ambapo wananchi watahusishwa moja kwa moja na wadau wote wa tasnia hii. Katika hali hii, sera zinatakiwa kuwa muhimu na zenye lengo la kushughulikia mahitaji ya wadau na kuthamini michango na huduma zitakazotolewa na chombo hiki.
Tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment