Feb 2, 2011

Pamoja na changamoto, soko la filamu litakua na kudumu

 Said wa Ngamba, mmoja wa waigizaji nguli
katika tasnia ya filamu Tanzania

 Baadhi ya waigizaji wakiwa kwenye kikao cha wadau wa filamu

* Wauzaji wa filamu wanapaswa kushirikiana na makampuni yenye mitandao nchi nzima
* Mafunzo juu ya maarifa pia yapewe kipaumbele

USIKU wa Jumatatu wiki hii sikupata usingizi kabisa, nilijiwa na mawazo yaliyoshindikana kufutika akilini mwangu, mawazo ambayo yameendelea kunitesa hadi niandikapo makala hii, kuwa kuna nguvu kubwa inayotambaa mikononi mwa wauzaji wa filamu nchini... Kubwa sana. Kitendo kinachofanywa na wauzaji kuwa na umuazi wa mwisho kama wauze kazi au la, na hakuna njia mbadala kinazidi kuwatesa watayarishaji wengi wa filamu hapa nchini.

Mwisho wa wiki iliyopita kulikuwa na kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania wakilalamikia kitendo cha msambazaji mmoja mkubwa kuwadhibiti wasambazaji wadogo kwa kujipangia bei ambayo wasambazaji wengine hawataweza kufanya biashara.

Viongozi wa shirikisho walitaka iwepo sheria ya udhibiti itakayopanga kiwango maalum kitakachotumiwa na wasambazaji wote ili kuleta uwiano mzuri na tija katika biashara, lakini walijikuta wakisalitiwa na wasanii na watengeneza filamu wenzao kudhoofisha hoja zao.

Wakati viongozi wa shirikisho wakiwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wenzao (wenye mkataba mnono na msambazaji anayelalamikiwa) waliwahi ofisini kwa Waziri wa wizara husika kulalamika kuwa kikundi cha watu wachache wenye mpango wa kuivuruga tasnia ya filamu wamepeleka madai yasiyo na maana kwa mkuu wa mkoa!

Kilichofanywa hapa kimetokana na kutumia nguvu ya pesa na hakina tofauti na hadithi ya mpini (mti) unaowekwa kwenye shoka na kutumiwa kuimaliza miti mingine.

Ndiyo maana nahisi kuwa shirikisho la filamu Tanzania lazima lisaidiwe kufanikiwa katika hili, bila kujali. Ni lazima lifanikiwe kwenye hili kwa mustakabali wa tasnia ya filamu nchini.

Tuna waongozaji filamu wenye uwezo mkubwa wa kuihabarisha jamii kupitia tasnia ya filamu katika 'angle' mbalimbali, ingawa inakuwa vigumu kwao kutengeneza sinema kwa ufanisi na kwa kiwango kizuri kutokana na mparaganyiko uliomo ndani ya tasnia hii.

Leo nitajaribu kubainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili tasnia hii, na kwa nini ni muhimu kwa wasanii kupewa muongozo (script) wiki chache kabla ya upigaji picha.

Nikiwa mmoja wa wanaharakati wa sanaa ya filamu, naziangalia changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya filamu hapa nchini wakati huu, kubwa ikiwa ni masoko ya sinema (hasa kwa wasambazaji wadogo). Hii ni kwa sababu soko letu si kubwa na halijasambaa sehemu kubwa japo kuenea Afrika Mashariki.

Wengi wa wasambazaji walio katika soko la sinema la nchi hii, hufanya biashara ama wakiwa Dar es Salaam au Mwanza, bila kupanua mtandao wa masoko yao sehemu nyingine.

Changamoto ya pili ni suala la uharamia wa kazi za sanaa ambalo ni dhahiri imekuwa tatizo, si tu kwa watengenezaji wa filamu, lakini hata kwa waandishi pia, kwa hiyo, kwa maoni yangu, ufumbuzi wa tatizo ni lazima wauzaji wa kazi za sanaa wafikirie kuanzisha ushirikiano tofauti na ilivyo sasa. Hapa nawakusudia wasambazaji wadogo.

Wasambazaji wa filamu wanatakiwa kutafuta namna ya kupata mafunzo juu ya maarifa yao kuhusu masoko. Masoko si kuuza tu bidhaa bali pia inahusu ushirikiano. Inahusu namna ya kupanua mtandao wa mtu mmoja mmoja au kundi.

Kama msambazaji ana duka Mwanza, na katika miaka miwili, msambazaji huyo hajaweza kupanuka zaidi, basi ni bora akafanya mpango wa kutafuta washirika wengine wa kibiashara au chombo/mashirika mengine kwa ajili ya usambazaji wa sinema zake.

Kuna vyombo/mashirika ambayo yamefanikiwa kuwa na mitandao karibu nchi nzima, wasambazaji/wauzaji wa filamu wanaweza tu kushirikiana na mashirika hayo kwa ajili ya usambazaji wa sinema katika maeneo mengi nchini.

Hivyo kama mtandao wa usambazaji wa filamu wa msambazaji fulani utakua na kupanuka zaidi, basi faida katika uwekezaji kwa waandaaji filamu pia itakuwa kubwa na kuwafanya kuwa na pesa zaidi zitakazowawezesha kufanya utafiti, na watakuwa na uwezo wa kuwalipa wasanii wao vizuri kuliko ilivyo hivi sasa.

Kwa sasa, asilimia ya watu wanaofaidika na uzalishaji wa filamu hapa nchini iko chini ya asilimia 15. Hawa ni muigizaji mkuu, Muongozaji mkuu, Mpigapicha, na watu wengine wachache, lakini watu wengine waliobaki katika tasnia hii hasa kwenye uzalishaji hawapati kabisa kile wanachostahili kupata. Kwa mfano, kama kuna watu 30 katika eneo la upigaji picha (location), ni watu wachache mno wasiozidi 5 ndiyo watakaopata malipo stahiki kutokana na kazi hiyo ya uzalishaji.

Hivyo, kama kutakuwepo soko pana zaidi kwa sinema, walio wengi katika eneo hili la uzalishaji wataweza kupata mishahara/posho nzuri itakayowawezesha kuishi vizuri.

Changamoto nyingine ambayo lazima tuikubali ni kuhusu lawama kwamba sinema nyingi mno zinazotengenezwa nchini zimezama zaidi kwenye mapenzi, mauaji, ukahaba na uchawi. Nimewahi kuulizwa na wasomaji kwa nini inakuwa hivyo? Au hatuna hadithi nyingine ambazo tunaweza kuzitumia?
Ikumbukwe kuwa utengenezaji wa sinema ni jambo linalohitaji sana mgawanyo wa kazi (division of labour). Kuna waongozaji, waigizaji, waandishi wa miswaada (scriptwriters) na kadhalika, lakini msingi mkuu wa sinema yoyote ni mwongozo (script). Hapa haijalishi kabisa uzuri wa kisa (plot), kama hadithi haiko katika mpangilio mzuri, basi itakuwa ni kazi bure.

Hakuna kisa kinachoweza kuifanya sinema ipendeze bila kuwepo 'storyline' nzuri. Hii inamaanisha kwamba endapo waandishi wa miongozo watalipwa vizuri, watakuwa na uwezo wa kufanya utafiti wa kina kabla hawajakimbilia kuandika muongozo.

Inaweza hata kuwachukua zaidi ya mwaka mmoja kufanya utafiti wa hadithi wanazohitaji kuziandika, kwa sababu watazama kwenye kina cha habari, kujua ni nini hasa kinachoendelea katika hali halisi ya maisha ya jamii kuhusiana na hadithi wanayohitaji kuiandika.

Wataweza kufanya mahojiano na watu wengi kuhusiana na hadithi waliyoikusudia. Utengenezaji wa sinema pia hufafanuliwa kwa lugha ya kigeni kama 'make-believe world', hii ni kwa sababu hadithi yoyote iwavyo, ni lazima iakisi maisha halisi ya jamii. Kwa hiyo, waandishi wenye ujuzi ni muhimu sana kwa ajili ya kuiokoa sekta yetu ya filamu.
Leo hii, kila mtu anaamini kuwa anaweza kuandika hadithi nzuri, na kinachoumiza zaidi ni ule ukweli kwamba waandishi hawa hawajawahi kuhudhuria japo warsha juu ya uandishi au kujiendeleza kwa kozi yoyote ya uandishi wa skripti.

Kwa maana hiyo, hii ndiyo imekuwa sababu ya haya yote kutokea katika mtizamo wa aina moja, wakati kuna mitazamo elfu moja na moja ambayo mada zinaweza kuwasilishwa. Hivyo, hadi tutakapokuwa na waandishi wazuri na waongozaji wazuri, suala la kutengeneza sinema ya mada fulani kutoka 'angle' moja tena na tena litaendelea. Hii ni changamoto nyingine ya kutothamini kujiendeleza kielimu.

Kwa nini nashauri kuwapatia wasanii skript wiki chache kabla ya upigaji picha? Kufanya hivi ni muhimu kwa sababu humpa muongozaji muda zaidi wa kuifanyia kazi hadithi.

Kile kinachowasilishwa katika hadithi kinaweza kuwa hakijawahi kutokea kabisa. Hivyo, kwa sababu ya hili, wasanii wanahitaji kupewa muda wa kuisoma hadithi, kuitafakari kwa kina ili kuielewa, na ikiwezekana, kufanya utafiti wao wenyewe juu ya nini wanataka kuwasilisha, hivyo kwa wakati wapokwenda kwenye eneo la upigaji picha (on set), watakuwa wamewiva kihisia kulingana na mahitaji ya hadithi, na kuwa na uwezo wa kutoa tafsiri halisi ya wajibu wao wanapocheza.

Hii ni muhimu kwa sababu miongoni mwa watazamaji, kuna watu ambao wamekuwa na uzoefu mkubwa kuliko kile wasanii wanachokiwasilisha, na uwasilishaji wowote usio sahihi kwa uzoefu huu, watakuwa wameiangusha sinema na kupelekea mauzo kushuka.

Kwa mfano, msanii anapowasilisha katika nafasi ya udaktari, mpelelezi au mwanasheria ni lazima apate muda wa kutosha kufanya utafiti jinsi gani hawa wataalamu wanavyofanya au kutenda katika maisha yao halisi, endapo atawasilisha kitu kingine tofauti na hali halisi itakuwa ni janga kamili.

Tusisahau kwamba kuna madaktari, wapelelezi na wanasheria ambao pia wanaangalia sinema hizi, hivyo uwasilishaji wowote usio sahihi kuhusu majukumu yanayowasilishwa na wasanii, utawafanya wataalam hawa kupoteza imani au hamu ya kufuatilia kazi hizi.

Hivyo, nashauri kuwapa wasanii skript mapema ili wawe na muda mwingi wa kufanya utafiti kuhusu majukumu yao kwenye sinema. Pia uibuaji wa vipaji utasaidia pale ambapo wasanii maaruf wanaodhani kuwa wamefika na hawana kabisa muda wa kusoma skripti.

Alamsiki

No comments: