Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, akiwa katika Operesheni ya kuwasaka waharamia wanaodurufu kazi za wasanii |
SERIKALI ya Awamu ya Tano imeanza kuonesha juhudi katika
kuisaidia sekta ya sanaa nchini baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye, kuingia mtaani na kukamata DVDs zisizo na stika ya TRA
zinazoingia nchini kinyume na sheria pamoja na zile zinazokwepa kulipa kodi ili
kuinua uchumi wa nchi na wasanii.
Waziri Nape Nnauye ameahidi kuwa zoezi hilo litakuwa
endelevu nchi nzima akisisitiza kuwa hatua hii ni ya mwanzo kwa kuwaonesha kuwa
agizo la Rais John Pombe Magufuli, la kulipa kodi na kununua bidhaa halisi kwa
kutoa risiti linasimamiwa ipasavyo.
Aidha Waziri Nnauye aliongeza kuwa wauzaji wengi wa
bidhaa feki za filamu wamekiuka sheria zinazosimamiwa na Sekta ya Filamu na muziki,
ikiwemo sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya Na. 4 ya mwaka 1976
inayosimamiwa na Bodi ya Filamu Tanzania, sheria ya Baraza la Sanaa Tanzania
(BASATA) Na. 23 ya mwaka 1984, Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya
mwaka 1999 inayosimamiwa na Chama cha Hakimiliki na hakishirikiya (COSOTA),
pamoja na sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 chini ya kanuni za stampu kwa
bidhaa za Filamu na Muziki ya mwaka 2013 inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
Zoezi hili limelenga kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi na
wasanii ambao umekuwa unahujumiwa sana kwa kuwepo bidhaa feki za filamu
zinazoingizwa nchini na kuuzwa kwa bei nafuu na kuua soko la bidhaa za ndani na
kuingiza tamaduni zisizofaa katika jamii yetu unaimarika.
Naungana na Waziri Nnauye katika zoezi hili na namtakia
Baraka na mafanikio, lakini namkumbusha kuwa serikali yake inapaswa kwenda
mbali zaidi ya hili, vinginevyo hatutaona tija katika juhudi hizi za serikali. Serikali
itafute njia ya kuwafanya wasanii kuachana na ile dhana iliyojengeka kwamba
Sanaa ni kipaji. Sikatai, kwamba si kipaji, lakini Sanaa ni taaluma pia. Kwa
maana kuwa Sanaa inasomewa!
Ni vigumu kwa fani yoyote ile kubakia katika kundi
lisilokuwa na vigezo vya upimaji wa ubora. Kusipokuwepo vigezo vya kupima
utaalamu wa fani hii, sinema zetu zitaendelea kuwa duni, zisizothaminika na
hata kubakia kuwa sekta isiyo rasmi (japo tunaaminishwa kuwa imerasimishwa) ambayo
haiwezi kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa uwezo mkubwa kama inavyotakiwa.
Sekta ya filamu hasa ya Tanzania imekuwa ni kati ya sekta
zisizo na vigezo vya kupima utaalamu na ubora. Ndiyo maana haishangazi kuona
makampuni mbalimbali na hata watu binafsi wakikazania kuibua vipaji vya vijana
bila kukazania kusomesha vipaji vya vyao. Kila mtu akijisikia anajitangaza
msanii! Tena anatengeneza pesa nyingi kuliko wasanii waliokwenda shule.
Ni wakati sasa Serikali pia ilikazie jambo hili ili Sanaa
ya Tanzania iwe ni taaluma na si kitu kinachofanana na taaluma, ili iweze
kufikia mafanikio kama ambayo sekta nyingine zimeyapata, kwani ukichunguza utagundua
kuwa wamepitia mabadiliko mbalimbali ambayo yanawawezesha kuthaminika na
kutambulika kitaifa na kimataifa.
Serikali iangalie namna bora ya kuhakikisha wasanii
wanapata elimu (japo kwa kuwaandalia warsha na makongamano mbalimbali kwa wale
wasio na vigezo vya kuingia vyuo). Pia serikali inapaswa kuongeza idadi ya vyuo
kwani kwa sasa tuna taasisi kuu tatu tu zinazotoa mafunzo ya sanaa ya maigizo
kwa ngazi ya cheti, stashahada na shahada. Taasisi hizo ni; Chuo cha Sanaa
Bagamoyo (TaSUBa), Chuo Kikuu cha D’Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Chuo cha Ualimu Butimba kimesitisha kozi ya masomo ya
sanaa. Tokea mwaka 1975 UDSM walifundisha sanaa, wakati Bagamoyo walianza mwaka
1981 na UDOM, chuo kipya walianza mwaka 2008, na walianza vizuri sana.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na maswali hasa toka kwa
Watanzania bila kupatiwa majibu juu ya sekta ya filamu. Wasanii “masupastaa”
katika sekta ya filamu ni watu ambao watu hujiuliza kama taaluma hiyo
wameisomea au ni kwa jinsi gani ilitokea wao wakawa ndiyo watu wanaoshughulika
nayo. Maswali haya ymekuja baada ya kazi wanazozalisha kuzua maswali mengi juu
ya uwezo au kipaji cha waigizaji, pia aina ya migogoro inayowasilishwa katika
hadithi zao.
Sanaa (ikiwemo filamu) kutokuwa taaluma kunawafanya wafanyabiashara
kuwatumia wale wanaojiita “wasanii” kujipatia fedha kwa kuuza kazi zao. Na kwa
sababu wasanii ni kundi linalofikiri kuwa hawathaminiki, ni wazi wameweza
kutokujithaminisha kwa kujikomba kuambatanishwa na fani nyingine kama maendeleo,
sayansi n.k bila kutambua kuwa sanaa kama sanaa ni maendeleo, sayansi nk.
Lakini pia inashangaza kuona hata wasomi katika fani hii
wamekuwa wakiimbia sekta ya sanaa na kwenda kufanya kazi zingine na kuliacha soko
la filamu kwa wasanii wasio na taaluma wala weledi. Waigizaji wa “bongo muvi”
ni vigumu kuwachambua na kuwaelewa kwa misingi ya taaluma ya uigizaji kwani
wanapingana na mengi sana katika fani hiyo! Ukiacha kazi mbalimbali ambazo zipo
sokoni na pia zinaweza kupendwa sana na wananchi (japo zinaweza zisiwe ubora kitaaluma).
Wasomi hawa ama hawajiamini au aina ya mafunzo wanayopata
katika taasisi husika yanawafanya kuwa wakosoaji wazuri kuliko kuwa wabunifu
wazuri! Lakini pia inawezekana wameandaliwa kufanya kazi zao kwa utaalamu na
kuzingatia kanuni lakini kwa kuwa serikali imeshindwa kuweka misingi mizuri ya
soko yenye kuzingatia weledi, wamejikuta wakishndwa.
Naishauri Serikali ikijite katika kuhakikisha wasanii
wanapata taaluma kwani hakuna taaluma isiyo na muongozo, mipaka, miiko na maadili
katika utendaji. Hata sanaa ni moja ya taaluma. Tusifikiri kwamba, kwa vile ni
saana, kila mmoja anaweza kuwa sawa – aliyesomea na mwenye kipaji cha kuzaliwa.
Lazima tutofautishe vitu hivi.
Tukubali au tusikubali, pamoja na juhudi za waziri lakini
ukweli ni kwamba sekta hii inaelekea mochwari kwani ubunifu unaenda ukishuka
kila kukicha. Kutokubali uwepo wa wataalamu wa sanaa ndiyo kumesababisha dharau
katika sanaa. Kutothamini umuhimu wa ngazi za viwango ndiyo unaoleta picha kuwa
sanaa ni kazi ya kila mtu.
Suala hili kuliacha kwa wasanii na vyama vyao pekee
hakuwezi kutusaidia, kwani, vyama hivi badala ya kuwa nguzo ya kufungua
mijadala ya kuleta maendeleo endelevu huku vikifuata na kusimamamia sheria za
nchi na hata kudai mabadiliko pale inapobidi, vimebakia kuwa mwanzo wa makundi
ya chuki, fitina, ugomvi, chuki n.k.
Ikumbukwe kuwa maigizo na filamu ni sanaa za kigeni toka
ulaya na huja na kanuni zake. Taaluma ya sanaa ya uigizaji ni pana sana, siyo
rahisi kama wengi wanavyoichukulia kwa ‘uzoefu’ wa kuangalia yanayooneshwa na
wasanii wetu katika luninga zetu!
Najua kuna sehemu tulijikwaa tangu mwanzo, maana televisheni zetu zilipoanza kuonesha maigizo na filamu za wasanii wa Kitanzania zilianza kwa kuwalipa wasanii nafasi ya kupata umaarufu, siyo malipo ya pesa baada ya kufanya kazi. Tunaweza kuania hapo.
Hili ni uthibitisho tosha wa wasanii kutoichukulia fani
hii kama taaluma, na hata hali duni za wasanii wa maigizo wengi wa TV ‘waliostaafu’
au kufa masikini lakini wakiwa na majina makubwa kuliko wao wenyewe walivyo.
Kwa kawaida sanaa huwa inakusudiwa kuelimisha, kukosoa,
kuburudisha na kukumbusha jamii yale yote yanayostahili kuenziwa au kuachwa.
Lakini kwa kusahau kuwa sanaa ni taaluma kumekuwa hakuna fikra za kina katika
hadithi za filamu zetu nyingi, hatufanyi tafiti ili kuzalisha hadithi bora na
za kusisimua, pia hatuwekezi vya kutosha katika uzalishaji wenye tija kwa mlaji
au msambazaji.
Matumizi ya mchanganyiko wa lugha kama yale ya hadithi za
Kiswahili lakini jina ni la Kiingereza, inaashiria kuwepo ukosefu wa utaalamu,
kukosa uzalendo na uelewa mdogo wa misingi ya fani husika katika utamaduni wetu.
Mwisho ni kwa watazamaji wa sinema zetu, wanapaswa kuacha
uvivu wa kusema ukweli, kwani naamini kuwa wao ni watazamaji wazuri wa sinema,
siyo tu za kwetu bali hata zinazotoka nje. Hivi hadithi zote wanazozijua, au
filamu zote za Kizungu na Kihindi walizoziona hazijawawezesha kutambua tofauti
ya nini bora na nini kibovu?
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment