NIKIWA sijui hili wala lile hivi karibuni nilijikuta natumiwa
ujumbe wa WhatsApp kwenye simu yangu kutoka kwa mdau mmoja wa filamu. Ujumbe ambao
nilipoutazama kwa makini nikagundua kuwa haukuwa umeandikwa na mdau aliyenitumia
bali ama alitumiwa au aliukopi kutoka kwa mdau mwingine.
Ujumbe huu uliandikwa hivi: “Habari? Mungu hulipa hapa
hapa, tulimpakazia Bishop kila aina ya hila kulinda mambo yetu lakini tukajiona
washindi bila kujua dhambi kubwa tuitendayo itatuhukumu tulipo. Kwa tatizo hili
la Tanzanite film festival, Katibu tena atang’oka? Nasubiri muujiza. Hongera sana
ndugu yangu Bishop, dhuluma uliyofanyiwa inawahukumu.”
Ujumbe huu ukanifanya kutafakari sana nini maana yake kwa
kuwa sikuwa najua kile kilichokuwa kinaendelea kwenye sekta ya filamu, hasa baada
ya mimi kuamua kukaa kando na kutokujishughulisha tena na masuala ya wasanii
wala harakati za vyama vyao.
Katika kufuatilia kwangu nikaambiwa kuwa kuna mtafaruku
mkubwa umeibuka ndani ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), baada ya Bodi ya
shirikisho hilo kumtuhumu kiongozi wake mkuu, Simon Mwakifwamba, kuwa na tabia
ya kufanya maamuzi pasipo kufuata katiba wala kuishirikisha bodi yake. mtafaruku
huu umechangiwa na uzinduzi wa tamasha la filamu la Tanzanite uliofanyika
jijini Arusha, ambapo Bodi ya TAFF imedai kuwa kiongozi wao anatumia mwamvuli
wa shirikisho kujinufaisha binafsi.
Siku chache baadaye nikatumiwa jumbe nyingine mbili-tatu za
WhatsApp kutoka kwa wadau tofauti, kati yao mmoja akinukuu makala moja yenye
kichwa cha habari “Waliokimbia harakati za TAFF kwa mwenendo mbovu na fitina za
rais.”
Katika makala hayo mambo mengi na ya kushangaza yalitajwa
kuhusiana na tuhuma za kiongozi wa TAFF, Simon Mwakifwamba, na namna ambavyo
amekuwa akifanya njama za kuhakikisha wale wanaoonekana kuwa tishio kwake
wanang’olewa ili afanye mambo yake kwa uhuru. Ikatajwa orodha ndefu ya viongozi
walioondoka au kuondolewa katika nafasi zao ndani ya shirikisho, wakiwemo makatibu
wakuu wawili, makamu wa rais na wajumbe wa bodi kadhaa.
Makala hayo yanaendelea kupasha kuwa ndani ya harakati za
wasanii kuna unafiki mkubwa kwani lile kundi la watu waliokuwa wakimuunga mkono
kiongozi huyo mkuu wa TAFF, sasa wamegeuka na kuanza kumshambulia wakitaja
tuhuma zake nyingi alizozifanya miaka ya nyuma, eti hana msaada katika sekta ya
filamu! Kama hiyo haitoshi, nikapigiwa simu na wadau kadhaa wakitaka kujua msimamo
wangu kuhusu sakata hili.
Jibu langu lilikuwa rahisi tu, sijui chochote na sitaki
kujua kichoendelea kwa kuwa sina maslahi yoyote kutoka upande wowote wa mgogoro
huo. Nilisema hivyo nikijaribu kupima faida na hasara za malumbano haya, maana
huko nyuma kumekuwepo malumbano ya muda mrefu kati ya Mwakifwamba na lililokuwa
kundi la Bongo Movies Unit, ambayo hayakuwa na tija zaidi ya kuchafuana. Nikakumbuka
ule usemi wa “vita vya panzi ni furaha
ya kunguru.”
Sekta ya
filamu imesheheni utajiri mkubwa sana lakini inaongoza kwa wadau wake kuwa
fukara (kwani imefukarishwa makusudi na watu wachache) na inazongwa na matatizo
makubwa. Ni sekta inayoshika namba moja kwa migogoro. Tathmini nyingi
zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika zinabainisha kuwa chanzo kikuu cha
matatizo haya ni kukosa dira, unafiki mkubwa miongoni mwa wasanii na wadau wa
filamu na mgawanyiko miongoni mwao.
Siku zote
nimekuwa naamini kabisa kuwa misuguano baina ya wasanii nchini imekuwa inawafanya
wawekezaji waliokuwa tayari kuwekeza katika sekta ya filamu kusita kuingia kwa
sababu kukosekana kwa umoja (maelewano), hili ni tatizo kubwa linaloathiri
sekta nzima ya filamu kwa ujumla na kufanya utendaji kazi kuwa mbovu.
Utengano ni tatizo
ambalo hata aliyekuwa Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk.
Emmanuel Nchimbi, aliwahi kuthibitisha kulijua. Hili tatizo mara nyingi huchangiwa
kwa kiasi kikubwa na kukosa uelewa, kukosa dira, kutokuwewepo malengo, kuwa na mipango
mibovu na uchoyo usiokuwa wa lazima.
Pia husababishwa
na kutokujiamini kwa baadhi ya wasanii, watayarishaji na hata viongozi ndani ya
harakati za filamu nchini. Ukweli ni kwamba wapo watu wachache wanaofaidika kutokana
na mgawanyiko huu, na kusababisha soko la filamu kuparanganyika na watu walioko
sokoni kujaribu tu kupata faida iliyo kubwa zaidi bila kuangalia upande wa pili
unafaidikaje. Kwa maana hiyo, mgawanyiko unachochewa zaidi na uchoyo na
ubinafsi.
Pamoja na kuwepo malumbano kwa kipindi kirefu, lakini hali
ya malumbano ya sasa imechukua sura mpya baada ya kujitokeza makundi mawili,
moja ni la wanaotaka kumng’oa kiongozi wa TAFF, ambao wamefikia hatua ya kudai
haki yao kwa kuupeleka mgogoro huu kwenye ngazi za juu serikalini, na kundi la
pili linaona kuwa kuna chuki binafsi na kwamba kiongozi huyu anaonewa.
Ilinishtua sana juzi (Jumatano) baada ya kupokea simu
kutoka kwa mtendaji mmoja serikalini akiniuliza kuhusu mgogoro huu ambao kwa
maelezo niliyopewa ni kwamba kwa sasa umetua katika Ofisi ya Makamu wa Rais!
Baada ya kutafakari sana kuhusu malumbano haya na hatua
zinazochukuliwa nikajikuta najiuliza maswali mengi ambayo sikuwa na majibu,
ingawa pia nilijaribu kuwauliza baadhi ya wadau wa kundi linalotaka kiongozi
wao ang’oke.
Nilijiuliza kuwa kama tuhuma za kiongozi huyu wa TAFF
zimekuwa zinafahamika kwa kipindi kirefu (si za jana wala leo), na huko nyuma ziliwahi
kufanyika juhudi za kutaka kumuondoa madarakani, na badala yake katibu wake
akatolewa kafara. Je, kwanini hawa wanaotaka kumng’oa waliamua kumchagua kwa
kura za kishindo (asilimia 97) katika uchaguzi wa hivi karibuni kama walijua
kuwa si muadilifu?
Katika kipindi kisichozidi mwezi tangu kiongozi huyu
achaguliwe, zikaanza juhudi za kutaka kumng’oa (tena kutoka kwa walewale
waliompigia kura)! Je, hawaoni kama tuhuma wanazozielekeza kwa kiongozi wao
zitatafsiriwa kama ni chuki binafsi? Inawezekanaje mtu awe na tuhuma mbaya kwa
miaka minne, kisha ndani ya kipindi kifupi cha uchaguzi tuhuma zifutike na mara
tu baada ya uchaguzi kupita tuhuma ziibuke upya (tena kutoka kwa walewale
waliompa sifa kemkem na kumchagua kwa kishindo)?
Kwa maswali haya na mengine nikaukumbuka wimbo wa msanii
mmoja wa Bongo Fleva, 20 Percent wa “Ya Nini Malumbano”. Nilidhani baada ya
kambi mbili zilizokuwa hasimu (za TAFF na Bongo Movies) kuungana na kufanya
uchaguzi basi wangefungua ukurasa mpya, hasa baada ya sisi wengine kuonekana huenda
tulikuwa kikwazo, kumbe ni mwanzo wa mgogoro mpya!
Hivi migogoro hii itaisha lini? Ingawa mimi si mtabiri
lakini nauona mwisho wa mgogoro huu kuwa mbaya zaidi ya ilivyowahi kutokea
kabla. Mgogoro na malumbano yaliyopo sasa hayaishii kuwachafua wale wanaolengwa
tu, bali yanaichafua sekta nzima ya filamu, na hivyo wote waliomo ndani ya
sekta ya filamu kuonekana hawajitambui.
Kwa mtazamo wangu, nadhani walikuwa bado wana nafasi ya
wao wenyewe kukaa na kuzungumza mambo yao kwenye vikao vyao vya ndani na
kufikia muafaka, badala ya njia hii ya kuanika matatizo na tuhuma zao kwenye mitandao
na hata kuandika barua kwenye wizara na idara za serikali kuelezea matatizo
yaliyomo ndani ya chombo chao.
Hebu tujiulize; nani mfaidika wa mgogoro huu? Kwa vyovyote
si kundi la kiongozi anayetakiwa kung’oka wala kundi la wale wanaokusudia kumng’oa
madarakani. Kinachokwenda kufanyika sasa kwa makundi yote mawili ni “bora
tukose wote”. Ninashuhudia mikakati mizito na muda si mrefu tutashuhudia watu
wakianza kugawana mbao!
Ni bora kuangalia mustakabali wa sekta ya filamu kwa
maendeleo ya filamu badala ya kuongozwa na maslahi binafsi, maana yeyote
atakayeshinda katika mgogoro huu asifikiri atadumu milele. Huo utakuwa ni
mwanzo wa vita mpya!
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment