Afisa kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Wilhad Tairo, akifafanua jambo kwa mfanyabiashara wa duka la Filamu wakati wa Operesheni ya kukagua Bidhaa zisizo na stika za TRA |
Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Tanzania, Sylvester Sengerema |
HALI ya Sekta ya Filamu ya
Tanzania kwa sasa ni mbaya sana. Ninathubutu kusema kwamba sekta hii ipo ukingoni mwa kifo,
kilichobaki ni ung’ang’anizi tu. Ikumbukwe kuwa mzunguko wa
maisha hufuata hatua nne: kuzaliwa, kukua, kukomaa na kuzeeka kabla ya kifo, ambapo
kama hakuna matatizo, tunategemea mwanadamu kufa baada ya hatua hizo.
Kwa hali ya sekta ya filamu ilivyo sasa, wasanii na wadau
wa filamu nchini wanapaswa kukaa chini na kutafakari kuhusu hali hii jinsi
ilivyofika hapa, kwani hali ni mbaya sana, na baada ya utambuzi wanaweza
kufanya kitu fulani na ikazaliwa upya na kufuata tena ngazi hizo. Vinginevyo
itabaki historia.
Lakini hata
wakati sekta hii ilipokuwa ikikua kwa kasi, thamani ya kazi zetu (filamu) ilikuwa
inashuka siku hadi siku na kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizokuwa na
ubora. Soko la filamu limejengwa
katika mazingira ambapo linabana sana uwezekano wa kuibuka kwa wasanii,
watayarishaji au waongozaji wapya.
Pamoja na kasoro
hiyo, bado soko hili lilifikia hatua ya sinema zetu kuuzwa sana mitaani na
kuzipiga kumbo sinema kutoka Nigeria na kwingineko, huku wanawake na vijana ndiyo
wakiwa wateja wakubwa wa sinema hizi. Kwa sisi tuliokuwa tukibahatika kutembelea
nchi za jirani kama Kenya, Congo DRC, Rwanda, Burundi nk. ni mashahidi wakubwa
wa jinsi sinema zetu zilivyoteka soko la filamu katika nchi hizo.
Ilifika mahali
ukitembelea nchi hizo na wakagundua kuwa wewe ni Mtanzania basi utakuwa katika
wakati mgumu sana kwani utaulizwa maswali mengi kuhusu filamu na wasanii wa
Kitanzania na wengi wao wakitaka uwape maelezo mengi kuhusu hizo filamu na
wasanii. Watazamaji wetu katika nchi za Afrika
Mashariki, hasa wazungumza Kiswahili, wakaonekana kuzipenda sana sinema hizi
pamoja na kuwepo kasoro nyingi, lakini walikuwa na hamasa kubwa.
Kama zilivyo sinema za Nigeria ambazo alama yake kubwa ya
kibiashara ni Kiingereza chao aina ya ‘Pidgin’,
Kiswahili cha kisasa cha Tanzania kilikuwa kinazipa utambulisho wa kitaifa
filamu hizi.
Pamoja na
kufikia hatua hii, Serikali (kupitia idara zake) haikuwahi kufanya tafiti za
kina wala kuweka kumbukumbu (data) za kusaidia kutambua thamani halisi ya sekta
au soko la filamu nchini. Hili lilikuwa kosa namba moja! Pia kulikosekana udhibiti
wa filamu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kwa njia za kiharamia kama
inavyofanyika sasa.
Ndipo yalipoanza
malalamiko kuwa Serikali ilikuwa imelala usingizi na kutoitilia maanani sekta hii
ambayo ingeweza kuwa suluhisho kubwa la ajira kwa vijana wengi, chanzo cha
mapato ya nchi na ingesaidia kutangaza vivutio vya nchi na hivyo kuvutia
watalii wengi na kuliingizia taifa pesa nyingi kupitia utalii.
Na serikali
ilipokuja kuzinduka usingizini ikakurupuka kufanya marekebisho katika Sheria ya
Ushuru wa Bidhaa, Sura 147, kwa madai ya kutambua uwepo kwa kilio cha muda
mrefu cha wasanii na wadau. Ikaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kazi ya kuweka
stempu kwenye DVD za filamu na muziki (pasipo kujua nguvu ya soko) ili uuzaji
wa kazi hizo uwe rasmi, wakidhani kuwa huko ndiko kuirasimisha sekta ya filamu
na kuwa wanawawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao.
Lakini pia tayari
kulikuwa kumeshaibuka ubinafsi mkubwa kwenye biashara ya filamu uliokuwa chanzo
cha kushuka kwa thamani ya filamu zetu. Ubinafsi wa wasambazaji wa filamu, ambapo
waliwagawa wasanii kwenye matabaka ya ‘masupastaa’ na ‘andagraundi’, kisha kuingia
mikataba ya kusambaza kazi za wasanii ‘masupastaa’ wale walio kwenye mikataba
yao tu na kuwakataa wale wasio kwenye mikataba nao ‘andagraundi’.
Kama hiyo
haitoshi, wasambazaji wa filamu wakaanza kuwalazimisha watayarishaji
wa filamu kutengeneza sinema zenye sehemu mbili au zaidi hata kama hadithi
hairuhusu! Kitendo hiki kilimlazimisha msanii kuigiza awamu ya pili ya filamu
(kwa pesa ileile) hata kama hakuwa na lengo la kuigiza sehemu hiyo, jambo
lililotafsiriwa kama kuendelea kuwanyonya wasanii kupitia kazi zao kwa malipo
kiduchu wanayowalipa.
Baadaye ikazuka
tabia ya wasambazaji wakubwa, wenye mtandao mpana kukataa kuuza sinema za
wasambazaji wengine wadogo (wanaowatumia wasanii wanaochipukia), hata kama itatokea
wasambazaji hao wadogo wataomba wafanyiwe hivyo kwa makubaliano maalum. Hali
hii ikasababisha wasambazaji wengine kukosa fursa ya kazi zao kuwafikia watu
wengi japo zilikuwa nzuri na zinahitajika mno.
Si hivyo tu,
wakashindwa hata kupeana zamu za kusambaza, soko likawa holela lisilokuwa na
muongozo huku wakishindwa kutumia soko vizuri, na matokeo yake ikalazimishwa
kuwa ili uuze ni lazima kutumia ‘masupastaa’ katika filamu, jambo lililofanya
kushindwa kutengeneza wasanii chipukizi wenye nidhamu katika kujenga sekta.
Matokeo yake sekta hii ikawa ni ya kujikimu tu, licha ya
ukuaji wa haraka uliokuwa unahubiriwa kwenye majukwaa ya siasa! Hadi leo bado hakuna
mavuno halisi katika kukuza pato la Taifa na hata watayarishaji walio wengi hawajafanikiwa
kupata matokeo mazuri kiuchumi kupitia filamu.
Sekta hii ikabaki kuwa mfano wa ‘kuganga njaa’ ili mradi mkono uende kinywani. Watayarishaji, wasanii na watendaji wengine wakabaki wakiwa wanaitumia sekta hii kujaribu kuweka mambo yao yaende sawa mezani, kwa maana ya kutafuta jinsi ya kujikimu tu!
Sekta hii ikabaki kuwa mfano wa ‘kuganga njaa’ ili mradi mkono uende kinywani. Watayarishaji, wasanii na watendaji wengine wakabaki wakiwa wanaitumia sekta hii kujaribu kuweka mambo yao yaende sawa mezani, kwa maana ya kutafuta jinsi ya kujikimu tu!
Hata hivyo, wasanii ‘masupastaa’ waliokuwa katika
mikataba na wasambazaji wakubwa wakaanza kutembelea magari, na kukatokea
matabaka huku wasanii chipukizi ‘andagraundi’ wakiwa hawathaminiwi, hapo ndiyo
ukawa mwanzo wa kujisahau na matokeo yake sekta ya filamu kukosa vitu vipya. Sanaa
ya Tanzania ikageuka kuwa ni kipaji na si taaluma. Japo ni kweli sanaa inaanzia
kwenye kipaji, lakini ni taaluma pia. Sanaa inasomewa!
Sanaa kwa Tanzania ikawa ni kati ya fani zisizo na vigezo
vya kupima utaalamu na ubora. Kukaanzishwa michakato ya kuibua vipaji vya
vijana bila kukazania kusomesha vipaji vya vijana hao. Kila mtu akijisikia
anajitangaza msanii! Tena anatengeneza pesa nyingi kuliko wasanii waliokwenda
shule. Sanaa ikawa si taaluma bali kitu kinachofanana na taaluma.
Wafanyabiashara wakaanza kuwatumia wale wanaojiita
wasanii kwa kujipatia fedha kwa kuuza kazi zao. Wasanii wakawa ni kundi
linalofikiri kuwa hawathaminiki kwa kuwa wao wenyewe wameshindwa kujithaminisha
kwa kujikomba bila kujua thamani yao.
Kukaibuka utamaduni unaoendelea hadi leo wa wasanii
kubwabwaja bila kujua wanabwabwaja nini zaidi ya ‘sanaa ni kioo cha jamii’. Ukiwauliza
dira yenu ni nini, hakuna ambaye angeweza kukuambia. Kila mmoja anasema lake. Sekta
ya filamu imekosa muongozo, mipaka, miiko na maadili katika utendaji.
Kwa kuwa sanaa ya Tanzania si taaluma bali ni kitu kinachofanana
na taaluma ikasababisha kushuka kwa ubunifu miongoni mwa wasanii nchini ambako
kumesababisha uwepo wa sinema hafifu isiyoweza kustahimili ushindani wa soko la
filamu duniani.
Hata vyama vya wasanii vilivyoanzishwa ambavyo
vilitegemewa kujikita katika kuhakikisha ubora wa utendaji wa wanachama
unazingatiwa, pamoja na kuwaadhibu wale ambao watabainika kuwa hawakutenda kazi
zao kwa mujibu wa sheria vikageuka kuwa vichekesho! Vyama hivi vilitegemewa kuwa
nguzo ya kufungua mijadala ya kuleta maendeleo endelevu huku vikifuata na
kusimamamia sheria za nchi na hata kudai mabadiliko pale inapobidi.
Lakini vyama hivi vikawa mwanzo wa makundi ya fitina,
ugomvi, chuki na hata ukiukaji wa sheria na taratibu za utendaji kazi. Vikabakia
kuwa taasisi za kubembeleza wafadhili (mapedejee) watoe hela na kulaumu
kutothaminiwa na serikali. Vikajaa unafiki na kuogopana kuambiana ukweli!
Kiukweli sekta ya filamu ya Tanzania
imesafiri njia ndefu sana hasa tunapoangalia katika suala la muda, lakini
linapokuja suala la ukuaji ili kujilinganisha na maendeleo ya haraka katika
sekta za filamu za nchi zilizoendelea duniani, inaonekana wazi kuwa hata yale
tuliyokuwa tunadai ni mafanikio tuliyoyapata ni sawa na fizikia ya muda wa
safari… Hakuna uhalisia kabisa!
Hebu tujiulize; tumekwenda umbali upi? Ukweli tunaonekana
kusimama palepale katika jiwe lilelile lisilotembea (unmovable stone).
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment