Nov 7, 2014

TAFA AWARDS: TUZO KUBWA ZA FILAMU TANZANIA



Logo ya Tuzo za Filamu Tanzania (TAFA)
Shirikisho la Filamu Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Binary & Pixels wameanzisha Tuzo za Filamu nchini Tanzania zinazotazamiwa kuwa Tuzo kubwa zaidi kuwahi kutolewa. Kuanzia 1 Novemba hadi 30 Novemba 2014 ni kipindi cha watayarishaji na wasanii kutuma/kupeleka kazi zao kwa ajili ya kuwania Tuzo hizi. Fomu zinapatikana kwenye ofisi za TAFF au kwenye website ya Shirikisho hili: GONGA HAPA

Hizi ndo Kanuni na Masharti ya kushiriki kwenye Tuzo za TAFA:


1. Kila anayekubali kushiriki kwa kuingiza filamu yake TAFA anahesabika kuwa amekubaliana na Sheria na Kanuni hizi. Tuzo hizi hazina ada ya kushiriki. Filamu lazima ziingizwe na mtu mwenye umiliki wa haki za filamu husika. Ni wajibu wa mtu anayetaka kuingiza filamu kushiriki TAFA kupata ridhaa ya hakimiliki kutoka kwa mmiliki/wamiliki
wa hakimiliki ya/za maudhui yote yaliyomo kwenye filamu itakayoingigwa kushiriki TAFA.

2. TAFF au wanachama wake wowote HAWATAHUSIKA na uingizwaji wa filamu usiokuwa na ridhaa ya hakimiliki zitakazohusika na filamu hizo.

3. Uingizaji wa filamu ni uthibitisho wa kuipa ridhaa TAFA kuonesha filamu hiyo wakati wa Msimu huu. Kila filamu inaweza kuoneshwa zaidi ya mara moja kutokana na maamuzi ya waandaaji wa TAFA. Wakati wa Msimu, hakuna filamu iliyoingizwa kushiriki TAFA itakayooneshwa kwenye sehemu ambazo hazijateuliwa kwa madhumuni
hayo, kabla ya kuoneshwa rasmi wakati wa Dhima ya TAFA.

4. Uingizaji wa filamu kushiriki TAFA unaipa TAFA ridhaa ya kutumia picha jongefu na picha mnato zitokanazo na filamu kwa ajili ya maonesho ya uhamasishaji wa TAFA.
5. Fomu za kushiriki zinapatikana kwenye wavuti wa TAFF, ambapo zinapaswa kupakuliwa (download), kuchapishwa, kujazwa na kuwekewa sahihi, kisha kupelekwa kwenye ofisi za Shirikisho, pamoja na nakala mbili za DVD au Blu-Ray za filamu, pamoja na maelezo kamili kwa uenezi wa habari za filamu. Ingizo la filamu litakuwa limekamilika baada ya Shirikisho kupokea fomu iliyotimiza masharti ya ushiriki.

6. Filamu zitakazochaguliwa kushindanishwa hazitaondolewa kwenye mpango wa tuzo baada ya kuingizwa rasmi pamoja na fomu ya ushiriki.

7. Taarifa za kuchaguliwa kwa filamu zitaoneshwa kwenye TAFA na Shirikisho kwa muda maalum ili kuwawezesha wahusika kufanya maandalizi ya kushiriki kwenye Dhima ya TAFA.

8. Maandalizi ya TAFA ni wajibu wa waandaaji wake pekee, na maamuzi yao ni ya mwisho na yasiyopingika.

9. Rais wa Shirikisho ndiye peke mwenye haki ya kutoa maamuzi juu ya jambo lolote ambalo halijahusishwa na Kanuni na Masharti haya, iwapo litatokea.

10. Kila filamu itakayoingizwa kushiriki TAFA lazima iambatane na Cheti cha Uhakiki kutoka kwa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania (TFCB).

11. Kila filamu itakayoingizwa kushiriki TAFA lazima iambatane na Cheti cha Usajili wa Hakimiliki kutoka kwa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA).

Ø  Kazi zinazotakiwa ni zile zilizotengenezwa kuanzia 1 Januari 2014 hadi 31 Oktoba 2014, zilizotengenezwa kwa lugha yoyote ila ziwe na subtitle (tafsiri ya maandishi) kama tu lugha iliyotumika si Kiingereza.
Ø  Kazi za urefu wowote; filamu ndefu “feature length” (dakika 50 na kuendelea), filamu fupi “short film” (si zaidi ya dakika 30).
Ø  Majaji watakaozipitia kazi hizi ni watu makini na watatoka katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania), hivyo msiwe na wasiwasi kuwa kunaweza kutokea upendeleo
Ø  Kazi itakayotumwa au kuwasilishwa kwenye ofisi za TAFF iwe katika mfumo wa Blu-ray au DVD PAL

Aina za Tuzo zitakazotolewa ni kama ifuatavyo:

1.    Best Feature Film – Tuzo itatolewa kwa Filamu Bora ndefu bila kujali kama ni kazi ya kwanza ya muongozaji anayeanza, na Tuzo itakabidhiwa kwa Mtayarishaji tu wa filamu hiyo
2.    Best First Feature Film – Tuzo hii kwa Filamu Bora ndefu iliyoongozwa na Muongozaji anayeanza ambaye hii ni filamu yake ya kwanza, na itakabidhiwa kwa wote, Muongozaji na Mtayarishaji
3.    Best First Screenplay – Tuzo hii itatolewa kwa Mwandishi Bora wa Script wa Tanzania ambaye hii ndiyo script yake ya kwanza
4.    Best Screenplay – Tuzo hii itatolewa kwa Mwandishi Bora wa Script wa Tanzania bila kujali kama ni script ya kwanza ya Mwandishi mchanga
5.    Leader’s or President’s Awards – Tuzo hii itatolewa kwa Filamu Bora ya Tanzania iliyotengenezwa kwa bajeti chini ya Dola 3000. Tuzo hii itatolewa kwa mshindi; Mwandishi wa Script, Mtayarishaji na Muongozaji (KWA FILAMU ZOTE ZINAZOANGUKIA HAPA UTATAKIWA KUWASILISHA BAJETI YA MWISHO YA UTENGENEZAJI WA KAZI YAKO)
6.    Best Director – Tuzo hii itatolewa kwa Muongozaji Bora wa Filamu wa Tanzania bila kujali kama ni Muongozaji ambaye hii ni kazi yake ya kwanza
7.    Best Cinematography – Tuzo hii itatolewa kwa Mpigapicha Bora wa Filamu wa Tanzania
8.    Best Editing – Tuzo hii itatolewa kwa Mhariri Bora wa Filamu wa Tanzania
9.    Best Documentary – Tuzo hii itatolewa kwa Filamu Bora ya Makala kutoka Afrika Mashariki, na itakabidhiwa kwa Aliyeingiza Sauti (Narrator), Muongozaji na Mtayarishaji
10. Best African Film – Tuzo hii itatolewa kwa Filamu Bora ya Kiafrika
11. Best Female Lead – Tuzo hii itatolewa kwa Muigizaji Mkuu wa Kike wa Tanzania
12. Best Supporting Female – Tuzo hii itatolewa kwa Muigizaji Msaidizi wa Kike wa Tanzania
13. Best Male Lead – Tuzo hii itatolewa kwa Muigizaji Mkuu wa Kiume wa Tanzania
14. Best Supporting Male – Tuzo hii itatolewa kwa Muigizaji Msaidizi wa Kiume wa Tanzania
15. Best Comedian Male and Female – Tuzo hii itatolewa kwa Wachekeshaji Bora Wakiume na Wakike wa Tanzania
16. Lifetime Achievement – Tuzo hii itatolewa kwa Msanii Mkongwe ambaye maisha yake yote amejitolea kwa ajili ya sanaa
17. Tribute Awards – Tuzo hii itatolewa kwa Msanii na Mtayarishaji ambaye amesaidia sana kuijenga tasnia ya filamu. Tuzo hii itatolewa kwa familia au mshindi
18. Best Composer (Soundtrack) – Tuzo hii itatolewa kwa mtayarishaji wa muziki au soundtrack ya sinema
19. Best International Film – Tuzo hii itatolewa kwa filamu iliyopo kwenye soko la kimataifa, na itatolewa kwa Mwandishi, Muongozaji, Mtayarishaji na Muigizaji
20. Best Subtitle – Tuzo hii itatolewa kwa Mtafasiri wa Kiingereza au lugha nyingine yoyote ya kigeni
21. Best TV/Radio Show – Tuzo hii itatolewa kwa Mtangazaji wa kipindi cha televisheni au redio kinacholenga masuala ya filamu
22. Best Film Critic: Tuzo inatolewa kwa mchambuzi bora wa filamu anayehamasisha ubora wa filamu kwenye tasnia.
23. Best Animated Film: Tuzo inatolewa kwa Mwongozaji wa filamu bora ya michoro, iliyo kamili au iliyo fupi.
24. Best Selling Film: Tuzo inatolewa kwa Watayarishaji wa filamu kamili yenye mauzo bora.

Kazi zote zitumwe kabla ya 30 Novemba 2014 zikiambatana na Fomu Rasmi na uthibitisho kutoka Bodi ya Filamu na Cosota. Zitumwe kwa:

Bishop Hiluka | Katibu Mkuu
Shirikisho la Filamu Tanzania
P.O. Box 90248, Dar es Salaam
Simu: +255 755666964 | 255 715666964 | +255 767230974
Website: www.taff.or.tz

No comments: