Mmoja wa waongozaji filamu nchini, Issa Mussa maaruf kama Cloud 112
SINEMA za mwanzo zilijielekeza kama vile sehemu ya jukwaa
mbele ya pazia. Kamera iliwekwa katika sehemu moja na matendo yote katika tukio
zima yalifanyika ndani ya fremu hiyo ya kamera kwa pigo moja (one shot).
Mtazamo wa watazamaji enzi hizo haukutofautiana na watazamaji ambao leo wanakaa
mbele ya jukwaa wakiangalia mchezo wa kuigiza wa jukwaani.
Muongozaji wa Kimarekani, D. W. Griffith, ndiye alikuwa
wa kwanza kuwahamishia watazamaji katika ulingo wa sinema kwa kazi zake kama
“For Love of Gold (1908)”, “The Lonely Villa (1909)”, “The Lonedale Operator
(1911)”, na ile iliyovutia zaidi, “Birth of a Nation (1915)”. Grifftith alikuja
na mbinu kabambe za kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi zake.
Sababu ya kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi ni
kuifanya hadithi yako ivutie zaidi – isisimue zaidi. Lakini hii hufanywa kwa
kuwaingiza watazamaji katika matukio, na kulenga zaidi kwenye usikivu wao hapa,
na pale.
Muongozaji anaweza kuwachanganya na kuwakanganya
watazamaji kiurahisi. Jiografia ya eneo au mwili wote wa mhusika hugawanyika.
Hivyo, yasiwepo maswali, ule mkono wa nani? Mhusika A anahusiana vipi na
Mhusika B? Mara nyingi muongozaji mzuri hapendi kusababisha mtanziko kwa
waatazamaji wake. Hupenda kuwafanya watazamaji wake wajisikie furaha katika
ulimwengu wa filamu – kuwa sehemu ya hadithi – ili kwamba hadithi yake iweze
kueleweka vizuri.
Siku zote, muongozaji hutaka watazamaji wake wajue kuwa,
“Huo wanaouona ni mkono wa Daud, na Daud ameketi kushoto kwa Jesca” (hata kama
hawajamuona Jesca kwa kipindi kirefu). Kuna wakati, hata hivyo, kama waongozaji
tunapaswa kutumia uwezekano huu wa kuwachanganya na kuwakanganya watazamaji
kama njia bora ya kutengeneza mazingira yenye kuleta msisimko au taharuki.
Sinema nyingi zilizofanikiwa huwa zina mhusika mkuu
(protagonist) aliye wazi, na swali la kwanza katika kazi yetu ya ufuatiliaji
kwenye mwongozo wa filamu ni: Nani ni mhusika mkuu kwenye filamu yetu?
Njia nyingine ya kuuliza swali hilohilo, ninayoamini
inaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa muongozaji, ni: Filamu ya nani (mhusika)?
Ni mhusika gani tunayemfuatilia kwenye filamu? Ni mhusika gani tunayemtumainia
au kumhofia – tukitumaini kuwa atapata anachohitaji, au tuna hofu kuwa
hatafanikiwa?
Kama muongozaji, ili ufanikiwe kuwateka watazamaji wako
unatakiwa kwanza kuijua “genre”. Genre ni aina ya hadithi inayosimuliwa, mfano,
hadithi ya upelelezi, ya uchawi, ucheshi, ya kutisha, ya mapenzi, na kadhalika.
Tunapoangalia filamu, tunakumbuka na kuwa na matarajio
fulani kuhusu mhusika, mandhali na matukio: ni vitu hivi ambavyo hutusaidia
kufurahia na kubashiri kile kitakachotokea baadaye na kufanyia kazi matukio
yanakoelekea.
Genre humruhusu muongozaji kubuni kitu kitakachobeba
uhalisia kwa sababu tunashindwa kuona kuwa tunachokiangalia si kitu halisi bali
kimetengenezwa. Kwa hiyo… kwenye aina ya hadithi ya kijambazi, kwa mfano,
hatutajali kama mmiliki wa jengo la wacheza kamali (casino) atauawa kwa sababu
tunamuona ndani ya genre, akiwa upande wa uadui (villain).
Makampuni ya filamu hupenda kutumia genre kwenye mambo
yote kwa ajili ya kufanya vizuri sokoni na kusaidia kutengeneza filamu yenye
mafanikio: genre maarufu huleta nafasi nzuri ya kufanikiwa sokoni, hivyo, genre
ni njia nzuri ya kupanga filamu, hurahisisha sana katika uandikaji wa hadithi
mpya.
Hata hivyo, muongozaji anapaswa kujua kuwa filamu ni
taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi, hivyo, haihitaji
mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe
unaowasilishwa na kazi husika ya filamu, ndiyo maana kuna watu wanaangalia
picha za Kihindi au Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea hata kama
hawaifahamu lugha husika.
Kuna dhana sababishi nyingi ambazo ni za lazima sana kwa
muongozaji mzuri: ubunifu, msimamo, elimu/ufahamu kuhusu sanaa, elimu/ufahamu
kuhusu watu, uwezo wa kufanya kazi na watu wengine, utayari katika kukubali
majukumu, ujasiri, ustahimilivu, na nyingine nyingi. Lakini dhana sababishi
iliyo kuu kabisa ambayo inapaswa kueleweka kwa waongozaji, ambayo ikikosekana
itatangua mengine yote, ni ubayana (clarity) — ubayana kuhusu hadithi na jinsi
kila kipengele ndani yake kinavyoweza kuchangia kwenye hadithi nzima, na pia
ubayana kuhusu kile kinachowasilishwa kwa watazamaji.
Nilipokuwa mdogo, kila nilipokuwa nikiangalia sinema
nilikuwa nikidhani kuwa sinema hutengenezwa kwa saa moja na nusu au mbili kama
ambavyo inaweza kuonekana kwa watazamaji.
Sikuwa na uhakika sana kama kulikuwa na kifaa kinachoitwa
kamera kikitumika katika utengenezaji wa sinema, na nilifikiria kuwa mazingira
kwenye sinema yalikuwa yakibadilika yenyewe (kwamba, hawakuwa wakifanya
uhariri)… Ilinichukua muda mrefu kutambua kuwa sinema zilikuwa zikitengenezwa
kwa vifaa maalum, tena kwa kipindi kirefu kuliko inavyoonekana, na kwamba
zilitengenezwa kwa kutumia mapigo maalum ya picha (shots).
Msingi mkuu wa hadithi katika sinema ni kuwa, filamu ni
zaidi ya kiwanda (sekta), ni zaidi ya onesho linalowakutanisha nyota. Filamu ni
lugha. Utengenezaji wa filamu una lugha yake. Kwa hiyo, filamu ni lugha
inayotumika kusimulia hadithi, na sauti inayotumika kusimulia hadithi hiyo ni
kamera.
Ndiyo, kama filamu ni lugha na kamera ni sauti, basi
muongozaji wa filamu ndiye msimuliaji wa hadithi hiyo, lakini “sauti”
anayoitumia kusimulia ni kamera. Katika usimuliaji wa hadithi hii, kuna mambo
sita yanayobadilika ambayo muongozaji wa filamu anaweza kuyatawala kwa kutumia
kamera. Katika mambo yote sita, kitu kinachoitwa composition (mpangilio wa
mambo yote yanayochangia kwenye muonekano wa picha kwenye fremu) ndiyo huwa
msingi mkuu.
Mambo hayo sita ni: camera angle (muonekano wa picha
kutoka kwenye kamera), image size (ukubwa wa picha – ambao unaweza kuathiri
kipimo na muonekano wa picha), motion (uhamaji – kutoka juu, chini, na kufuata
kitu), depth of field (kina cha eneo – je, ni la kawaida, limebanwa au
limeathiriwa na umbali wa fokasi kutoka kwenye lenzi), focus (lengo – kitu
kilichokusudiwa kwenye fremu ya picha), na speed (kasi –kawaida, haraka, au
taratibu).
Muongozaji wa filamu huandaa na kuunganisha wezekano
(possibilities) hizi ili kutengeneza sentensi zinazotumika kusimulia hadithi
kupitia filamu, na kisha hupanga sentensi katika “aya” – masimulizi
yaliyokamilika au matukio ya kusisimua ambayo yatategemea zaidi katika
mgandamizo, ufafanuzi, na nguvu kuu ya tatu ya vipengele vya masimulizi.
Kwa hiyo, picha unazoziona kwenye filamu zinaweza
“kusomeka” kama maandishi mengine. Pia tambua kuwa kazi yoyote ya sanaa iliyo
kwenye mpangilio mzuri wa mambo yote yanayochangia muonekano wa picha
(composition) ikiwa katika mapigo maalum ya picha (shots) yatokanayo na umbali
maalum wa kamera, kutoka kwenye muonekano/pembe ya kamera (angle), ikihusisha
mwanga (lighting), na sehemu ambapo mapigo ya picha yanawekwa katika mfuatano
maalum (sequence), vyote huvutia au kuathiri jinsi mtu anavyoweza kuitafsiri
picha hiyo.
Watengenezaji wa filamu hutumia sana umbali wa kamera na
muonekano wa picha kutoka kwenye kamera kuvuta hisia za watazamaji, ili
kukitazama kile kilichokusudiwa kikiwa katika muundo maalum wa picha au pigo la
picha na kukipa maana iliyokusudiwa.
Pamoja na hayo, pia zipo sheria mbalimbali zinazoongoza
katika uongozaji ambazo pia zimo kwenye somo muhimu la lugha ya filamu, ambazo
waongozaji wote wanapaswa kujifunza na kuzijua kabla hawajaamua kuzivunja.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment