Jan 13, 2012

Hatimaye gwiji wa maigizo, Mzee Kipara azikwa jijini Dar es Salaam

Picha zilizopo juu zinawaonesha baadhi ya wasanii na wananchi waliojitokeza kumzika Mzee Kipara, wengine wakiwa wamebeba jeneza wakati wa kuelekea Makaburi ya Kigogo, Jijini Dar es Salaam

Baadhi ya waumini wa Kiislam walifanya ibada ya kusalia maiti ya Marehemu Mzee Said Fundi eneo alilokuwa akiishi la Kigogo jijini Dar es Salaam

Maelfu ya wakazi wa jijini la Dar es Salaam na vitongoji vyake, jana Alhamisi walijitokeza katika mazishi ya msanii mkongwe wa sanaa ya maigizo, Fundi Said maarufu kwa jina la Mzee Kipara aliyefariki dunia katika nyumba aliyokuwa amepangishiwa na Kundi la Sanaa la Kaole iliyopo Kigogo Mbuyuni, Dar es Salaam.

Mzee Kipara, alikuwa msanii mkongwe katika tasnia ya uigizaji Bongo, aliyetumia sehemu kubwa ya maisha yake katika sanaa ambaye juzi (Jumatano), Januari 11, mwaka huu, saa 2:00 asubuhi, Mungu alimchukua baada ya maumivu ya muda mrefu.

Mzee Kipara ambaye siku za hivi karibuni alikuwa akiishi maisha ya mateso makubwa kuliko jina lake kufuatia kutelekezwa na wahusika kulinganisha na kazi aliyoifanya ya kuelimisha na kuburudisha jamii, alikuwa hawezi kugeuka kitandani zaidi ya kukoroma.

Mara kadhaa Mzee Kipara alilalamika kusumbuliwa na miguu ambayo ilikuwa ikivimba, na hii ilisababishwa na high blood pressure inayosababisha moyo kupanuka na kushindwa kufanya kazi, kitaalamu huitwa Congestive Cardiac Failure (CCF). Hali hiyo husababisha moyo kushindwa kusukuma maji kutoka chini kwenda juu, hivyo miguu kuvimba na tatizo hilo kitaalamu huitwa Oedema.

Mazishi yake yalifanyika jana saa 10 jioni katika makaburi ya Kigogo, jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na Waziri wa Afrika Mashariki, Mh. Samuel Sitta, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan na viongozi wengine akiwemo mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Henry Clemens, pamoja na wasanii mbalimbali.

HISTORIA YAKE KATIKA SANAA

Mzee Kipara alianza sanaa mwaka 1964 kwa kufanya kazi za mitaani kabla ya kujiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) sasa ikiitwa TBC Taifa na kukiendeleza kipaji chake alichokuwa amejaaliwa na Mungu ambapo aliweza kuonyesha umahiri katika uigizaji ambao ulimpatia umaarufu mkubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akiwa RTD Mzee Kipara aliigiza katika michezo mingi na kipengele kilichompatia umaarufu zaidi ni ule uigizaji wake wa kujifanya mbabe na mkorofi na kujikuta akijizolea mashabiki lukuki hasa ukizingatia wakati huo Tanzania ilikuwa na kituo kimoja cha redio na mamilioni ya wanachi walikuwa wakiitegemea kwa ajili ya kupata habari mbalimbali na burudani ikiwemo michezo mbalimbali ya uigizaji iliyokuwa ikirushwa wakati huo.

Mwaka 1999, akiwa na wasanii wenzake, akina Zena Dilip, Rasia Makuka, marehemu Mzee Pwagu na Mama Haambiliki, walijiunga na Kundi la Sanaa la Kaole ambalo lilikuwa likirusha maigizo yake katika kituo cha televisheni cha ITV.

ASILI YAKE

Mzee Kipara aliishi sehemu nyingi katika Jiji la Dar; Gerezani, Ilala na Kigamboni, lakini asili yake ni Mkoa wa Tabora. Alizaliwa mwaka 1922, Ndala – Nzega, mkoani Tabora.

No comments: