Katibu Mtendaji wa Bodi, Joyce Fisso
Msanii Elizabeth Michael, maaruf kwa jina la Lulu
SIKU ya Jumanne ya wiki hii kulikuwa na mjadala kuhusu maadili katika filamu za Tanzania uliorushwa na kituo cha redio (Radio One), mjadala ambao uliwahusisha, Rais wa shirikisho la filamu nchini, Simon Mwakifwamba, mwakilishi kutoka Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na mwananchi mmoja aliyewakilisha watazamaji wa filamu. Wadau hawa walipata nafasi ya kuchangia maoni yao kulingana na mitazamo yao . Kwa kweli sikupata kabisa bahati ya kusikia hoja zao kwa kuwa sikuwa na taarifa kama kungekuwa na kipindi kama hicho, nilipata taarifa wakati kipindi kikiwa kimekwisha na sikuweza kujua waliongea nini.
Lakini pamoja na hayo, bado hainizuii kutoa maoni yangu kuhusiana na jambo hili la maadili kwa kuwa naamini kuwa bado ipo haja kwa wadau wote kutafuta njia bora ya kutatua matatizo yaliyopo katika tasnia na soko la filamu nchini.
Sekta ya filamu ni moja ya sekta ambazo zimezongwa na matatizo mengi. Tathmini kadhaa zilizofanyika zimebaini kuwa chanzo kikuu cha matatizo haya ni kutoeleweka kwa dhana ya utamaduni, kutothaminiwa kwa shughuli za utamaduni, kupotea kwa maadili ya kitaifa na serikali kutoipa kipaumbele sana tasnia ya sanaa katika mipango yake ya maendeleo ya nchi yetu ingawa inatajwa kuwa chanzo kikubwa cha ajira na mapato ya nchi.
Nimejaribu kufuatilia kwa makini hoja za wadau mbalimbali na hata baadhi ya makala kwenye vyombo vya habari na majukwaa ya sanaa, nikagundua kuwa lawama zote kuhusiana na ukosefu wa maadili kwenye filamu zetu wanatupiwa wasanii, utadhani wao ndiyo kila kitu au ndiyo wanaobeba mustakabali wa sanaa/ filamu nchini. Ingawa hili la kutumia majina ya Kiingereza (kwa kisingizio cha filamu ikiwa na jina la Kiswahili haipati soko) huku filamu zenyewe zinazochezwa zikitumia lugha ya Kiswahili mwanzo mwisho ni kosa lao na wanastahili kubeba lawama, kwani ni kasumba mbaya sana .
Naamini kuwa tatizo tulilonalo hapa si wasanii wala kazi zao, kwani wao ni sehemu tu ya jamii hii, tatizo lililopo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii nzima. Hata haya majina ya Kiingereza pia yanatokana na jamii, kuanzia kwa viongozi wetu ambao hawaoneshi kukithamini Kiswahili. Ni lini tutaacha unafiki wa kukataa yale tunayotenda na kuhubiri tusiyotenda?
Sipendi kuwa mnafiki, lawama kubwa naitupia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ambayo sielewi imekuwa inafanya nini ili kuinusuru tasnia ya filamu. Sijui huwa wanakagua nini? Ninachokishuhudia sasa kupitia kanuni walizozindua ni wao kutengeneza miradi ili kujiongezea kipato. Kuwalaumu wasanii kwa kisingizio cha filamu wanazotengeneza 'si utamaduni wetu' wakati huohuo Bodi ya Filamu yenye dhamana ya kuhakikisha maadili hayapotoshwi inaruhusu vituo vyetu vya televisheni vioneshe tamthilia na filamu zenye maadili ya Kimagharibi saa 24, maana yake nini?
Maadili hayawahusu wasanii peke yao , yanaihusu jamii yote ambayo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, kazi ya wasanii inakuwa kielelezo cha tunu bora zinazofumbatwa katika maisha yetu: kiroho na kimwili; kimaadili na utu wema. Lakini inaonekana kuwa jamii na viongozi tuliowapa dhamana kuongoza taasisi zinazosimamia maadili katika filamu wanajitoa kwenye jukumu hili na kutupa lawama kwa wasanii!
Hebu tuache lawama na badala yake tuelekeze nguvu kwenye kukuza vipaji vya wasanii ambavyo vinahitajika sana katika kuelimisha jamii, kutoa tahadhari na kuhakikisha kuwa kile wanachokiwakilisha katika jamii kiwe msingi na changamoto ya maisha yao katika jamii.
Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya utamaduni hukua na pia huweza kufa. Je, kutokana na hali ilivyo sasa kwenye filamu zetu na soko la filamu, sanaa zetu zinakua au zinakufa?
Tatizo la maadili katika sanaa na uthibiti wa kazi chafu limekuwa gumzo na wengi wanajiuliza kwa nini tunakosa alama ya mfano ya filamu zetu? Nini chanzo cha wasanii wetu kuigiza na kuiga filamu chafu? Kwa kweli idadi kubwa ya filamu zinazotoka kila siku, pamoja na zile zilizokaguliwa na taasisi husika, bado huwezi kuziangalia ukiwa pamoja na watoto.
Utafiti na makala mengi ya waandishi huelezea kuwa fani ya filamu ipo katika hatari kubwa ya kuporomoka kwani wasanii na watayarishaji wa filamu wamepotea njia kwa kutofuata miiko, kukosa taaluma, maudhui yasiyolingana na uasili, jamii nzima kukosa maadili na mapokeo mabaya ya kazi ya sanaa. Hivyo haya yote yanaashiria hatari ya kuporomoka kwa fani hii. Je kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili?
Mapokeo ya kazi ya sanaa katika jamii yoyote ile hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika. Mapokeo mabaya husababisha kuwa na idadi lukuki ya watendaji, wadau na wasanii bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya filamu na kufanya kazi zao kuisha thamani katika muda mfupi.
Tusipokuwa makini tutazidi kuwa wasindikizaji na watu wa kupokea sanaa toka nje na kunakili, kwani asilimia kubwa ya Watanzania ni wavivu kufanya utafiti wa asili ya tulikotoka. Tusipofanya juhudi na kuacha kutupiana lawama itakuwa ni ndoto kupata alama ya Filamu za Tanzania ambayo itatambulika duniani kama ilivyo kwa tasnia zilizoendelea. Kwa sasa tunajidanganya kuwa alama ya filamu zetu ni Kiswahili, lakini tunasahau kuwa kuna nchi kama Kenya , Rwanda au Kongo, na nyinginezo pia zinatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano.
Pia tuache kujidanganya kwa fikra potofu kwamba si rahisi kupata alama ya filamu za Tanzania kama tutaamua kwa dhati kupigania maadili kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, na kuacha kurushgia mpira wa lawama.
Pamoja na yote haya, naamini kabisa kuwa serikali haiwezi kukwepa lawama hizi. Nimekuwa nikijiuliza kila mara; kwa nini serikali imeamua kuachia sanaa na utamaduni wetu uendeshwe na wafanyabiashara wachache? Kwa nini imeshindwa hata kuwekeza katika sekta hii ili kufufua na kukuza maadili na utamaduni wa Watanzania ambao unakoelekea kwa sasa tunauona kupitia wasanii na kazi zao (filamu na miziki) tunazozilalamikia?
Utamaduni na maadili ni speed governor (kidhibiti mwendo) zinazoongoza mwenendo na tabia za watu katika jamii, ni misingi wa maisha ya mtu binafsi, humuwezesha mtu kujitambua na kuwa na mwelekeo sahihi ya maisha yake.
Kinachotakiwa sasa kwa wadau wote wa tasnia hii ni kutafakari kabla ya kutenda na tuache unafiki. Katika hali hii ya tafakari matokeo ya kila tunachokusudia kutenda yako wazi kabisa mbele yetu.
Alamsiki…
No comments:
Post a Comment