Oct 27, 2010

FILAMU ZA KITANZANIA: Ni kweli tuna wakosoaji wa filamu? (4)

Mwandishi wa makala haya, Bishop J. Hiluka

SIKU nilipopigiwa simu na mhariri wa gazeti hili akinitaka tuonane sikufikiria kabisa kama angenikabidhi jukumu la kuandika makala kwenye gazeti lake. Sikufikiria kwa sababu sikudhani kama angeweza kunifikiria mimi niandike badala ya wachambuzi wengi maarufu na wa muda mrefu waliopo ambao tayari wameshajijengea heshima kubwa katika uandishi.

Nilisita sana kukubali kwa kuwa sikudhani kama ningeweza kukidhi kiu ya wasomaji, lakini nilipokumbuka uzalendo wangu na kiu yangu ya kutaka tasnia ya filamu hapa Tanzania ikue nikakubali mara moja.



Vyovyote vile iwavyo, tayari mimi ni mwandishi wa “Mbiu ya Ijumaa”, naandika makala ambazo zimeniongezea marafiki wengi na hata maadui. Hii inadhihirishwa na simu nyingi ninazopigiwa na hata meseji ninazopokea kila siku, hasa kwa kuwa namba yangu ya simu imewekwa mwisho wa makala.
Niliamua kuweka namba ya simu ili nipate maoni na mitazamo ya wasomaji, lakini badala yake baadhi ya wasomaji wameamua kufanya kile ambacho kimegeuka kuwa ni adhabu na usumbufu mkubwa kwangu.

Sidhani kama binadamu mwenye akili timamu angeweza kufanya hiki kinachofanywa na wasomaji hawa ambao kazi yao ni kubip ovyo mithili ya wendawazimu! Sijajua wana nia gani kwangu kwa sababu baadhi yao unapoamua kuwapigia simu huwa hawapokei. Namba zinazoongoza kwa usumbufu wa kubip ni hizi zifuatazo; 0686 474246, 0756 337944, 0764 339213, 0766212886, 0752 729655, 0755 543380, 0759 452364 na 0659 241086.

Unaweza kuonekana mstaarabu lakini jambo dogo sana likakuharibia sifa yako. Hivi unapobip unakusudia nini? Anyway, nadhani mwenye akili timamu atakuwa kanielewa, sasa wacha nirejee kwenye mada yangu niliyoianza wiki tatu zilizopita “Ni kweli tuna wakosoaji wa filamu?”.

Sisiti kusema kuwa bado nina mashaka sana na uwezo ama mbinu wanazozitumia hawa wanaojiita wakosoaji (sidhani kama wanastahili kuitwa wakosoaji bali wapondaji), nina shaka kama kweli wanafanya tafiti za kutosha kuhusu sekta hii, na kama wanafanya basi zitakuwa ni za juujuu tu. Kama kweli wana nia ya kutaka kazi za Kitazania ziboreke basi wanapaswa kwanza kufanya tafiti za kina kabla hawajakimbilia kuziponda filamu za Kitanzania kwenye vyombo vya habari. Baada yakujiridhisha na tafiti zao ndipo waanze kutafuta njia sahihi za kuwasaidia watengeneza sinema.

Ni kweli kuna makosa katika filamu za Kitanzania, kati ya hayo yapo ambayo hayahitaji uwe na bajeti kubwa bali ni ufahamu na ujuzi, na kuna makosa yanayosababishwa na ufinyu wa bajeti na mfumo mbovu uliopo nchini (hili ni somo maalum linalohitaji siku maalum kulizungumzia).

Kila fani ina elimu yake, sio mtu unakurupuka asubuhi na kujiona wewe ni mkosoaji wa filamu. Elimu ya filamu umeipata wapi? Au na wewe uko kwenye ule mkumbo walioingia wasanii wengi kwamba; “usanii upo kwenye damu!” Sijui ukosoaji nao ni kipaji? Au kwa lugha nyingine “ukosoaji upo kwenye damu zao!”

Nimeshawahi kuandika siku moja kuwa; kuwa na "Final Cut Pro"au “AdobePremiere Pro” hakumfanyi mtu kuwa mhariri wa filamu (film editor), kuwa na "Adobe Photoshop" hakumfanyi mtu awe graphic designer, au "Microsoft Word" bado haitoshi kumfanya mtu ajiite Scriptwriter kama hana mafunzo ya weledi.

Katika elimu ya filamu (film studies) tumefundishwa nidhamu (academic discipline) inayohusu mambo mbalimbali ya kinadharia (theoretical), historia (historical), na njia bora za uhakiki makini wa sinema (critical approaches to the cinema).

Sekta ya filamu ni sekta pana sana inayojitegemea kwa kila idara, huwezi kuifananisha na soka au sanaa nyingine. Sekta ya filamu hapa Tanzania imeachwa tu kama mtoto yatima asiye na mlezi na anayejitafutia chakula chake mwenyewe huku akibezwa, kuchekwa na kusimangwa na jamii inayomzunguka ambayo ilipaswa kumsaidia ili aondokane na hali duni. Wote sisi ni mashahidi jinsi mabenki yetu, wawekezaji na makampuni makubwa hapa nchini yanavyokimbilia kuwekeza kwenye soka (ambalo hata hivyo bado halina mwelekeo), kwenye mashindano ya urembo (yanayoendeleza tamaduni za Kizungu) na kukumbatia tamthilia za nje.

Katika mambo yanayochangia kudorora kwa tasnia hii hapa nchini, vituo vya televisheni vinachangia kuididimiza tasnia hii kwa zaidi ya 50%. Hilo wala halina ubishi. Vituo vya televisheni vinazikwepa kazi za Kitanzania eti kwa sababu ya kiwango duni wakati hata wao wanatoa malipo kiduchu kwa kazi hizo hizo huku wakiwekeza pesa nyingi kwenye kazi za nje ambazo zimetengenezewa mazingira mazuri na nchi zao. Nyingi ya tamthilia hizo ama zimetengenezwa na makampuni makubwa au vituo vya televisheni vya nchi hizo vimewekeza pesa nyingi sana katika maandalizi yake.

Pia nchi hizo zimeweka viwango maalum vya uoneshaji wa kazi zinazotoka nje kwenye vituo vyao vya televisheni ili kulinda kazi za ndani tofauti kabisa na hapa kwetu ambapo utakuta michezo na filamu za nje huchukua zaidi ya 80%. Nchi kama Malaysia kwa mfano, wamefikia 80% ya kurusha vipindi vya ndani (local content) kwenye televisheni zao. Singapore 65%, na China ni 90%. Hii ni mifano michache tu.

Najua kwa kuandika haya nitakumbana na changamoto kubwa lakini nia yangu ni kuleta mjadala wa kina ili tutafute njia sahihi ya kuiokoa sekta hii isiende kombo badala ya kuacha mambo yaende ovyo ovyo tu kama ilivyo sasa. Tunapaswa kuwa na mjadala mpana kwa wadau wote kama ambavyo Shirikisho la Filamu Tanzania limeanza kuonesha kuhusu masuala muhimu yanayoihusu sekta hii, vinginevyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi.

Wakati sasa umefika kwa serikali na wadau wote (wakiwemo wanaoziponda filamu za Kitanzania) kuwekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha elimu kwa waandaaji wa filamu inatolewa. 


Wakati sasa umefika kwa serikali, wadau (wakiwemo wawakilishi wa sanaa ya filamu, Chama cha kusimamia Hakimiliki Tanzania “Cosota”, Mamlaka ya Mapato Tanzania “TRA”, Baraza la Sanaa la Taifa “Basata”, Tume ya Ushindani, “Fair Competition Commission”;) na wenye taaluma ya fani hii kufanya kwa vitendo kile wanachokiongea kila siku katika kuhakikisha kuwa sekta hii inakua na kutengeneza sinema na michezo ya kuigiza iliyo bora na siyo kusubiri vijana wasio na taaluma, mitaji na wala hawajawezeshwa wanapojitoa mhanga kutengeneza filamu na kukosea ili nyinyi muwe wa kwanza kuwatupia mawe.

Hata hivyo, juhudi na nguvu zaidi zinahitajika katika kufanikisha mapambano ya kuwakomboa wasanii, watengenezaji sinema na wasambazaji wa kazi za sanaa hapa nchini ili wapate malipo/mapato stahiki kutokana na kazi zao kitu kitakachopelekea kuboreka kwa tasnia hii hapa nchini.

Kwa kufanya hivyo na kuwawezesha wasanii na watengeneza filamu, sekta hii itakua mara dufu na kufikia kiwango kinachokubalika.

Vijana wa taifa hili tutajisikia fahari kuitwa Watanzania na hatimaye kuwa taifa ambalo vijana wake ndoto zao si kuzamia “Majuu” kama ilivyo sasa bali kuutangaza utamaduni, utalii, na historia za mashujaa wetu kupitia filamu.

Kama nilivyodokeza kwenye makala zangu zilizopita; Serikali kupitia Sera yake ya Habari na Utangazaji, inabainisha kuwa itahamasisha utengenezaji wa filamu, video na vielelezo vyenye maudhui ya Kitanzania, itakuza vipaji vya wananchi katika fani za filamu, video na vielelezo, itahamasisha uwekezaji katika tasnia ya filamu, video na vielelezo, na kwamba sanaa na taaluma ya filamu, video na vielelezo zitaendelezwa ipasavyo… sasa ni wakati muafaka wa kulionesha hilo kwa vitendo.

Tukiwa kwenye karne ya 21 ya sayansi na teknolojia, Tanzania imeonesha kuwa na utajiri mkubwa wa historia za mababu na maeneo mazuri ya kihistoria yanayofaa kutengenezea sinema, vitu ambavyo havijawekwa bado katika makabrasha ya kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kama mambo yataachwa yaende ovyo ovyo tu kama yalivyo sasa, wapondaji wa filamu wakaachwa kuendeleza chuki zao binafsi kwa wasanii na watengeneza filamu, na watengeneza filamu kuachwa wajifanyie wanavyoona inafaa tutakuja kujikuta tukiwa ni taifa lisilo na historia wala tamaduni.

Sekta ya filamu ni njia nzuri sana ambayo Serikali inapaswa kuitumia kama chanzo kipya cha mapato na chenye uhakika wa ajira kwa vijana ili ahadi aliyowahi kuitoa rais Kikwete ya kuzalisha ajira milioni moja itimie (hili nitalijadili siku nyingine).

Kama nchi, tutaweza kutangaza vivutio na utalii wa nchi hii kupitia filamu na kupelekea kuliingizia taifa mapato mengi. Kwa kweli tuna changamoto kubwa; hebu fikiria kwa nchi ambayo ina maeneo ya kuvutia, chakula, mavazi, na malazi ila hakuna hadithi, visa vya kusisimua, fasihi, n.k. Inakuwa ni nchi ya ovyo sana.

Je, ni makampuni au matajiri wangapi walio tayari kuwekeza katika kutoa mafunzo ya fani husika au kugharamia workshop kwa watengeneza sinema wa Kitanzania? Hivi ni wadau wangapi wanaoijua idadi halisi ya waandishi wa miongozo ya filamu (script) wanaoweza kuandika mwongozo wa sinema kwa ufasaha? Je, ni nini kifanyike ili kuwafanya waandishi hawa waweze kuandika scripts zinazokubalika kitaaluma? Hilo si suala la watengeneza sinema pekee bali ni jukumu la kila mdau wa sekta ya hii, wakiwemo wanaojiita wakosoaji wa filamu.

Naomba kutoa hoja.

No comments: