Oct 27, 2010

FILAMU ZA KITANZANIA: Ni kweli tuna wakosoaji wa filamu?

 Florian Lawrence Mtaremwa, mmoja wa watengeneza filamu wa Kitanzania

TASNIA ya filamu ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya taifa lolote. Ni muhimu kwa sababu kubwa tatu; filamu na maigizo hutumika kama mwasilisha taarifa mkubwa katika kuifundisha ama kuionya jamii.

Kisiasa, sekta hii hutumika kama baraza la midahalo na majadiliano kwenye jamii. Na kiuchumi, sekta hii huchangia pato kubwa la mabilioni ya pesa na pia ni chanzo cha mamilioni ya ajira duniani.


 
Kabla sijaeleza nilichokusudia ningependa niwashukuru wadau walioonesha uchungu mkubwa kwa tasnia hii na wameomba tuwe na mjadala mpana kuhusu tasnia ya filamu. Nami nadhani kuwa ipo haja ya kuyazungumzahaya ili tuwekane sawa. Nimepokea ujumbe kutoka kwa mdau muhimu sana wa tasnia hii, Betty, wa Dar es Salaam aliyeniandikia; 

“Ndugu Hiluka, Mimi ni mmoja wa wapenzi wa nchi yangu katika nyanja zote, sinema zikiwemo. Kwa kweli nahisi aibu sana kwa jinsi ambavyo filamu zetu bado si halisi kwa kuwa nyingi zake zinaigwa na hasa kutoka Nigeria. Kuiga si vibaya hata kidogo kama unaiga ubora wa mambo, lakini si kuiga mpaka wazo kwa kujidai ni lako halafu unajifanya mjanja kwa kutafsiri wazo kisha ukajidai lako. Kibaya zaidi ni jinsi ambavyo tafsiri ya Kiingereza ilivyo mbovu!!!!!!! 

Hivi kwa nini hao wasanii wasitumie wajuzi wa lugha ili kutuondolea aibu ya kitaifa jamani. Hii ni kwa sababu, naamini sinema hizo hufika nje ya mipaka ya nchi yetu.Sasa kwa viwango hivyo vibovu, ikiwemo ubora wa chini wa picha na uchaguzi wa mandhari ili kuendana na maudhui ya sinema husika, kweli Tanzania inajiweka katika nafasi ipi ndani ya ushindani huu wa mambo mbalimbali, sinema zikiwemo?...” alimalizia Betty kwa uchungu mkubwa.

Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Afrika Salim mwenye namba za simu 0714 540105, wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM);
“Habari,ahsante sana kwa makala yako iliyopita, ni nzuri na nimeifuatilia kwa kuwa mimi ni mdau wa filamu za nchi zote zilizoendelea kwa tasnia hii, hasa Bollywood, Hollywood, Nollywood na Tanzania ambayo inaonesha muelekeo wa kuiteka Afrika hapo baadaye, please elezea pia makosa na nini cha kufanya kwa film industry ya Bongo...”

Pamoja na umuhimu wa tasnia hii lakini imeonekana kupewa kisogo (kwa sababu inaongelewa tu kwenye majukwaa ya siasa bila juhudi za makusudi) hapa Tanzania ingawa bado imeendelea kuwa mwasilisha taarifa mkubwa katika jamii yetu. Bahati nzuri sekta hii haijawahi kuwa mwasilisha taarifa potofu au kuwa mwangamizaji na mchochezi wa demokrasia kama ilivyokwa nchi nyingine zilizolazimika kuingia kwenye machafuko kwa sababu ya matumizi mabaya ya sekta hii.

Nina mifano mingi kwa sekta hii kutumika kwa uchochezi au propaganda chafu. Pia kuna mifano inayoonesha kuwa wakati mwingine hutumika kufichua uovu hasa uliofanywa na tawala dhalimu. 
 
Moja ya sinema za mfano iliyowahi kutoa taarifa zilizoonekana ni propaganda chafu inaitwa “DARWIN’S NIGHTMARE (2004)”, sinema iliyoichafua Serikali ya Tanzania kimataifa. Hubert Sauper, mzaliwa wa Australia anayeishi Ufaransa ndiye mtunzi na mtoaji wa sinema tashtiti (provocation) maarufu kama sinema ya mapanki. Filamu hii ilionesha kejeli kwaTanzania kiasi cha kumfedhehesha Rais Jakaya Kikwete pamoja na ummawote wa Watanzania.

Nimewahikuandika hapo awali katika makala iliyoitwa “Mustakabali wa sektaya filamu Tanzania” kwamba, sinema ya Darwin’s Nightmare nimatokeo (the outcome) ya Serikali kuipa kisogo sekta ya filamu kulikopelekea kutowang’amua watu wenye hila na nia mbaya ambao wanaweza kuendelea kutumiwa kuichafua nchi hii. Serikali ya Tanzania ilipaswa kuwa imepata onyo kupitia filamu ya mapanki na kuwa karibu zaidi na wadau wa sekta hii.

Kama nilivyodokeza, sinema pia zimekuwa zikitumika kufichua maovu yaliyofanywa na tawala dhalimu, na mojawapo ni “BLOOD DIAMONDS (2006 )”, iliyoongozwa na Edward Zwick, mzaliwa wa Chicago, katika jimbo la Illinois, Marekani. Sinema hii ilikusudiwa kufichua maovu yaliyofanyika nchini Sierra Leone. Na “JOHNNY MAD DOG (200”, sinema iliyotengenezwa kuelezea yaliyofanyika nyuma ya pazia nchini Liberia, iliongozwa na Jean-Stéphane Sauvaire.
Walioziona sinema hizi watakubaliana nami kwamba ni sinema zilizotumika kufichua siri nzito zilizozigubika tawala za nchi hizo
.
Blood Diamonds (almasi zilizotokana na umwagaji damu), ni sinema iliyofichua siri nzito iliyoyagubika machimbo ya almasi nchini Sierra Leone na kupelekea uporaji mkubwa na mauaji yaliyofanywa na wachache walio tayari kumwaga damu za wengine kwa uchu wa kujilimbikizia mali. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Sierra Leone vinahusishwa kwa kiasi kikubwa na sakata hili la madini. Baada ya filamu hii kutoka inasemekana kuwa ilisababisha biashara ya vito kudorola kwa kiwango kikubwa barani Ulaya na Marekani baada ya watumiaji kususia.

Inasemwa kuwa Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor anayekabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita kwenye Mahakama ya Kimataifa, TheHague,Uholanzi ni mojawapo ya matokeo ya sakata hilo. Sakata lililomlazimisha mwanamitindo maarufu duniani na raia wa Uingereza, Naomi Campbell, kupanda kizimbani ili kutoa maelezo kwenye mahakama hiyo kwani ilidaiwa kuwa aliwahi kupewa zawadi ya almasi zilizotokanana sakata hilo (blood diamonds) na Charles Taylor walipokutana nchini Afrika Kusini kwenye 'birthday'ya MzeeMandela.

Tangu kuanza kwa karne ya 21 nchi yetu imeshuhudia ongezeko kubwa sana la utengenezaji na utoaji wa sinema kila kukicha, hali inayoambatana na malalamiko kutoka kwa wadau, wasomi na wakosoaji kuwa sinema zetu zinakosa kabisa ubora na hazikidhi matakwa ya jamii. Kama nilivyomnukuu Bi. Betty hapo juu.

Pia hii ilipelekea kwa Mwalimu wa sanaa kutoka Chuo Kikuu Huria chaTanzania (OUT), Prof. Emmanuel Mbogo kutoa wito kwa watunzi wa filamu nchini wahakikishe kuwa wanapata mafunzo maalum ya uandishi wa miongozo ya filamu na michezo ya kuigiza (Script). Mhadhiri huyo aliyebobea kwenye sanaa aliyasema hayo mwaka jana alipofanya mahojiano na gazeti moja la burudani.

 
Katika wito wake, Prof. Mbogo alisema kuwa tatizo kubwa lililopo kwenye filamu (nyingi) za Kitanzania ni uwezo mdogo wa uandishi wa miongozo, kitu ambacho kinasababisha filamu na michezo mingi ya kuigiza kuonekana kuwa haina muelekeo. Aliongeza kuwa waigizaji wa Kitanzania wengi ni wazuri katika uigizaji lakini si katika kuandaa miongozo ya filamu, na kwa kuwa lengo ni kuzifanya filamu za Kitanzania kuwa na ubora, waandaaji wanastahili kupata mafunzo ya sanaa na uandishi wa miongozo.

"Tunaona wengi wao wanaandaa filamu nzuri na wana vipaji vya uigizaji, ila kinachoharibu ni jinsi gani wanatengeneza mwongozo wa filamu hiyo," alinukuliwa Profesa Mbogo na gazeti hilo.
Pia kuna mkosoaji anayeitwa Geoffrey Barnabas, huyu aliandika makala takribani miaka miwili iliyopita iliyonivutia na ndio maana bado naikumbuka hadi leo; “Vihiyo wameingilia sanaa ya uigizaji Tanzania”.

“Kwa kweli unapozungumzia dhana ya uigizaji nchini Tanzania ni kama unaongelea kitu kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Hapa Tanzania tuna watu wanalipua mambo na wanafanya mambo bila kuzingatia utaalamu. Wanafanya mambo ili mradi wanajua kuna kitu kinaitwa uigizaji. Kwanza, mathalani ukijaribu kuchunguza kwa makini vigezo ‘muhimu’ vinavyotumika kuwapata waigizaji wa Tanzania, utasikitika. Kuna vigezo vikubwa vitatu, vinavyotumika kuwatafuta waigizaji wa Tanzania; navyo ni umaarufu wa mtu, uzuri wa sura na kujuana. Kama huna moja ya vigezo hivyo, basi huna nafasi. Utaalamu alionao mtu hauzingatiwi kabisa.”

Aliandika Geoffrey na kuongeza, “…ni jambo lililo wazi kuwa uwanja wa filamu wa Tanzania ni sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Utakuta mtu ni mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, halafu mtu huyohuyo ndiye muongozaji mkuu. Pia mtu huyo anaweza kuwa ndiye muigizaji mkuu… Hali ni mbaya zaidi kwenye michezo ya kuigiza, kwani kuna watu wanaotengeneza ili mradi wauze sura kwenye runinga. Ukiangalia michezo yenyewe, utaona kuwa haina vigezo, yaani ni sawa na mtu achukue kamera aingie mtaani na kuanza kurekodi chochote anachokiona. Udhaifu mkubwa uko hasa kwenye jinsi ya kuendeleza hadithi. Hadithi inapoanza ikifika sehemu fulani, stori nyingine zaidi ya tano au sita zinajitokeza mpaka mtu anasahau wazo kuu la mchezo husika…”

Huo ulikuwa mtazamo wa Geoffrey. Lakini hakuishia hapo, alitaja mambo mengi ambayo kwa kiasi nilikubaliana naye, na alinifurahisha alipomalizia makala kwa kusema; “Labda nisiwalaumu sana watengeneza filamu wa Tanzania. Natambua hakuna teknolojia kubwa kama ya mataifa tajiri, lakini nafasi adimu wanayoipata kwenye vituo mbalimbali vya televisheni, waitumie ipasavyo.”
 
Nilifurahi kwa kuwa hapo ndipo hasa mada yangu ilipo. Pia nakubaliana na kauli za Prof. Mbogo na Betty, kwa kuwa wote wamegusa yalipo mapungufu, hasa eneo muhimu sana; uandishi wa miongozo (script).

Sinia yangu kurudia yaliyotamkwa au kuandikwa na wengine, bali nilitaka nioneshe ninavyokubaliana na hoja zilizo makini zenye kujenga, lakini pia nikionesha mtazamo tofauti kwa wachambuzi/wakosoaji walio wengi ambao wanatumia nafasi walizopata kwenye vyombo vya habari (magazeti, redio, televisheni na blogu) kwa ajili ya kuponda, nadhani ni kutokana na chuki tu.

No comments: