Rais Jakaya Kikwete
Kwanza napenda kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa angalau kuonesha kuutambua mchango wa sekta ya filamu Tanzania. Hii ni sekta ambayo bado imeonekana kupewa kisogo na hivyo kubaki mikononi mwa wajasiriamali wadogo wasio na mitaji. Haionekani kama nayo inatakiwa kupewa kipaumbele (politicalvaluable) kama sekta muhimu inayoweza kuchangia pato kubwa kwa maendeleo na ukuaji wa uchumi wataifa letu.
Sekta ya Filamu hapa Tanzania haifikiriwi sana kuwa ni taaluma adimu, ndio maana haipewi kipaumbele katika kamati za mipango serikalini. Pia sekta hii yaweza kuwa mwangamizaji na mchochezi mkubwa katika jamii ya kidemokrasia na pengine kuwa mwasilisha taarifa potofu.
Inasemekanakwamba, Rais Kikwete anapenda kuona wasanii waTanzania (wakiwemo waigizaji wa filamu na michezo ya runinga) wakifaidika kupitia vipaji na kazi zao, wawekezaji wakifaidika kutokana na uwekezaji wao, na sekta nzima ya filamu ikichangia katika pato la taifa.
Wasanii nyota wa filamu Tanzania,
Steven Kanumba na Vincent Kigosi (Ray)
Ikumbukwekuwa sekta ya filamu duniani imekua sana hasa kutokana na matatizo na ukosefu wa ajira, ndiyo hasa yaliyochangia kwa vijana wengi kujitumbukiza kwenye sekta ya filamu na kujikuta wakipata mkombozi wa ajira kupitia filamu. Kuna uwezekano mkubwa kwa sekta ya filamu nchini kuwa mkombozi wa vijana na wajasiriamali wadogo katika kukuza pato na kuongeza ajira kama ilivyo kwa mataifa yaliyofanikiwa kwenye sekta hii, endapo viongozi wa serikali wataacha hotuba na propaganda na kuiangalia sekta hii kwa mapana zaidi.
Hapa naomba nieleweke vizuri kuwa; sektaya filamu (filmmaking) haiwezi kuendeshwa na Serikali au kuwa mradi wa Serikali (government activity). Mambo yakiubunifu (creativity) hayawezi kustawi katika mazingira na huduma za umma/kiserikali (civil service environment).Serikali haipaswi kutengeneza sinema, lakini inapaswa kuweka mazingira mazuri ya utengenezwaji wa sinema, mazingira mazuri yaongezeko la mapato, na mazingira mazuri ya uwezeshaji katika ukuaji wa soko la filamu kwa watengenezaji wa filamu na wadau.
Uongozi wa nchi unapaswa kutubadilishia hiki kielelezo (paradigm) kuanzia kwenye utungaji sheria (legislating) hadi kwenye kuisaidia, kuisimamia na kuitangaza (promoting) sekta hii ya filamu. Kwa kufanya hivyo, serikali inahitaji kwanza kukijua kipimo halisi cha sekta hii na makadirio yenye umakini mkubwa (sober assessment) ya soko la filamu la Tanzania kama lilivyo.
Sekta ya filamu Tanzania kwa sasa inajulikana sana katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika kwa kutoa sinema nyingi (quantity) lakini zisizo na ubora (quality). Ukweli ni kwamba, ili sekta hii iweze kuwa mhimili imara katika kujipatia mapato (economic reward) katika soko la kimataifa; serikali na wadau kwa pamoja tunalazimika kuelekeza macho yetu katika uboreshaji ili tuingie kwene soko la kimataifa na kuudhihirisha ukweli kwamba tuna vijana wengi wenye vipaji (talented), wenye kujitosheleza (viable) na wenye mtazamo wa kiubunifu zaidi (creative vision) katika tasnia ya filamu, kitu ambacho kipo nchini kwetu.
Serikali inapaswa kupiga marufuku uingizwaji holela wa sinema zote za kiharamia/wizi (pirated films) za Hollywood, Bollywood na kwingineko zinazoingizwa nchini kutokea China ilikusaidia kukuza soko la kazi za wasanii wa ndani. Hatuwezi kujifanya tunaboresha soko la kazi zetu huku tukiruhusu uharamia wa wazi kwenye kazi za wengine ndani ya ardhi yetu. Kumekuwepo na ongezeko kubwa mno la sinema ‘feki’ zitokazo China zinazoingia Tanzania na kuuzwa kiholela tena bila kificho huku zikitishia uhai wa soko la filamu za Kitanzania mfano wa silaha za maangamizi alizodaiwa kuwa nazo Saddam Hussein wa Iraki.
Serikali inapaswa kuelekeza nguvu nyingi katika suala la utoaji wa mafunzo kwa wahusika. Kutafuta gharama za mafunzo kwa watengeneza filamu linapaswa kuwa jambo la kwanza kwa serikali katika kuutambua mchango wa sekta ya filamu. Rais Kikwete anaonekana kuwa mpenda michezo (zikiwemo sinema zetu), amelidhihirisha hilo alipoamua kuelekeza nguvu nyingi kwenye soka (ambalo hata hivyo bado lipo chumba cha wagonjwa mahututi) na hata alipotembelea Marekani alijitahidi sana kukutana na waigizaji nguli wa Hollywood na kuongea nao. Ningependa kumshauri Kikwete kuliangalia kwa mapana suala la uanzishwaji wa chombo kitakachosimamia utoaji wa mafunzo stadi hasa kwa watengenezaji filamu ambao hawakubahatika kupitia kwenye vyuo vya sanaa lakini wameonesha kuwa na vipaji, na uwezeshaji.
Sekta hii inatatizwa sana na uhaba wa mitaji. Utengenezaji sinema (moviemaking) si lelemama kama wengi wanavyodhani bali ni suala linalohitaji mtaji. Zinahitajika pesa nyingi kuweza kuandaa na kutoa filamu nzuri yenye ubora, bila kujali uzuri wa wazo (idea) ulilonalo, katika utengenezaji sinema, mwisho wa siku pesa inaongea. Ndiyo maana wanaoshikilia soko la filamu (Watanzania wenye asili ya Kiasia) ambao pia ndio wamegeuka kuwa wawezeshaji wa filamu zetu (Executive Producers) wamekuwa wakilimiliki (control) soko la filamu Tanzania watakavyo.
Binafsi sina tatizo kabisa na hawa “Marketers” wanaosimama kama wawezeshaji wakuu katika soko letu. Ukweli nikwamba, tunapaswa kuwashukuru kwa kuwa wao ndiyo watu pekee waliojitosa kuwekeza (invest) pesa zao kwenye soko letu hili la mashaka (uncertain terrain) la biashara ya filamu. Mabenki yetu hayathubutu. Serikali haijathubutu. Hata hivyo, wao wamethubutu.
Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba biashara yao imeelekezwa zaidi katika ukiritimba na kutothamini kazi kutoka kwa watengenezaji na wasanii wanaochipukia (emergent) bila kujali ubora wa kazi zao na uzuri wa hadithi zao. Kuingilia kwao kati (intervention) kwenye soko hili kunachochewa zaidi na kiu yao ya kutaka kupata faida kubwa kwa kuelekeza nguvu nyingi kwenye kutafuta hadithi zitakazowawezesha kuuza nakala nyingi zaidi, lakini pia wakishinikiza katika kuwataka watengenezaji wa filamu hizi kuwatumia wasanii fulani fulani na waongozaji fulani fulani ambao wao wanawataka.
No comments:
Post a Comment