Rais Mteule Dk. John Pombe Magufuli, akijiachia jukwaani pamoja na wasanii wa kundi la Yamoto Band kwenye uwanja wa Mashujaa mkoani Mtwara, wakati wa kampeni |
KWANZA kabisa napenda nikupongeze kwa kuchaguliwa kuwa Rais
wa Tanzania katika Awamu ya Tano, nikitumaini kuwa wananchi wamekupa ridhaa kwa
kuwa wamekuona unafaa zaidi kuiongoza nchi hii baada ya Rais Jakaya Kikwete,
ambaye uongozi wake unahitimishwa kesho Alhamisi.
Ingawa kuna minong’ono na wasiwasi mwingi kuwa huenda
wewe huna ‘interest’ kabisa na masuala ya sanaa, na uongozi wako utajikita
zaidi kwenye kujenga barabara, reli, uwekezaji, kilimo, mifugo, uchimbaji
madini nk, lakini nina imani kuwa uongozi wako utawapa wasanii tumaini jipya.
Naamini utatimiza ahadi zako kwa wasanii kwa kuwa wao pia
wamekusaidia sana na walikuwa karibu na wewe wakati wote wa kampeni zako za
urais. Ila kinachonisikitisha ni kwamba tangu nchi yetu ipate uhuru takriban miaka
54 iliyopita, hakuna kiongozi aliyesimamia kwa dhati (kivitendo) maendeleo ya
wasanii na ustawi wa sekta nzima ya sanaa, ingawa hata viongozi waliopita
walifanyiwa kampeni na wasanii.
Japo kiongozi aliyekutangulia (Jakaya Kikwete) alijaribu
kuwa karibu sana na wasanii lakini hatukuona dhamira ya dhati kutoka kwenye serikali
yake katika kuwasaidia wasanii. Wapo watakaonishangaa kusema haya, lakini ukweli
utabaki kuwa ukweli. Serikali ya Awamu ya Nne imekuwa ikijinadi kuwajali
wasanii na imeonesha kwa vitendo kuwa karibu nao pindi kunapotokea misiba ya wasanii
maarufu, na pengine kuwaalika kula futari ikulu na kupiga picha na rais!
Kama huku ndiko kuwajali wasanii, sawa. Lakini sidhani
kama hili ndilo hitaji kubwa la wasanii kwa ustawi wao na wa sekta ya sanaa.
Serikali iliyopita ilikuwa inafanya maigizo tu, kwani hakuna urasimishaji
wowote uliofanyika wenye tija zaidi ya kuwaingiza wasanii na kazi zao kwenye
mfumo wa stempu za TRA.
Rais Magufuli, kwenye sekta ya sanaa, Idara ya Maendeleo
ya Utamaduni ndiyo uti wa mgongo wa sanaa nchini, lakini idara hii imekuwa ni tatizo
kubwa sana kwa mustakabali wa maendeleo ya sanaa nchini. Sijui utafanyaje,
lakini nakushauri, kama ikikupendeza, uihamishie Idara hii kwenye Wizara ya
Maliasili na Utalii, ili kazi za sanaa ziweze kuchangia kwa kiwango kikubwa
uchumi wa Taifa hili. Sekta ya Filamu nchini ikiendelezwa vizuri ni chanzo
kikubwa cha ajira kwa vijana, njia madhubuti ya kukuza utalii na uchumi wa
Taifa na wa wananchi kwa ujumla.
Nakuhakikishia kuwa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni
imesheheni utajiri mkubwa sana wa utamaduni na uchumi kupitia sanaa, nyimbo na filamu
zetu. Tatizo ni kwamba hadi sasa sekta hii bado haijawa rasmi (ukiachia kiinimacho
cha stempu za TRA).
Idara ya
Maendeleo ya Utamaduni imekuwa haichukuliwa kwa umuhimu wake, na imehama Wizara
zaidi ya kumi toka nchi hii ilipopata Uhuru wake mwaka 1961. Kwanini? Sidhani
kama hali hii inatokea tu kwa bahati mbaya. Mwaka 1995 na pia mwaka 2010, Idara
hii ilisahauliwa kutajwa wakati wa kutangaza Baraza la Mawaziri baada ya
Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010 tulipewa taarifa kuwa jambo hilo lilitokea kwa bahati
mbaya ingawa mwaka 1995 hapakutolewa maelezo yoyote, ila kimya kimya ikaelezwa kuwa
Utamaduni utaendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu.
Pia
uliangalie hili la Maafisa Utamaduni tulionao leo hii, wa Wilaya na Manispaa, ambao
wamekuwa hawawajibiki katika Wizara inayohusika inayobeba Idara ya Maendeleo ya
Utamaduni, bali wako chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo ni wizara tofauti kabisa na ile inayohusika
na Utamaduni.
Kwa hali
hiyo, shughuli za pamoja za Kitaifa zinazohusu Utamaduni ni ngumu kuzifanya katika
mazingira ya sasa, ndiyo maana hata Mashindano ya Kitaifa ya kazi za sanaa
hayasikiki tena, hata shughuli zinazohusika na maslahi ya pamoja ya wasanii
kama vile ulinzi wa haki za wasanii (Hakimiliki) umekuwa wa shaghalabaghala,
maana hakuna ajenda ya pamoja kwa viongozi hawa wanaotegemewa kuwa karibu
kabisa na wasanii.
Nakumbuka miaka
ya nyuma sana, wakati huo nikiwa mdogo, Maafisa Utamaduni walikuwa kimbilio la
wasanii, waliweza kutafuta vifaa vya muziki kwa wanamuziki, kutafuta maeneo ya
kufanyia mazoezi kwa wasanii wasio na nafasi. Hata yale majumba yaliyojengwa
karibu kila wilaya maarufu kama ‘Community Centres’ yalikuwa chini ya Maafisa
Utamaduni na kuwa mahala ambapo serikali ilipajenga maalum kwa ajili ya shughuli
za sanaa.
Community Centres
hazipo tena baada ya kugeuzwa aidha kuwa ofisi za Manisipaa au kukodishwa kwa
watu binafsi kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali vijana waliomo
katika Manispaa wanapewa sehemu maalum kufanya shuguli zao za sanaa.
Kwa kukosa
sera nzuri za sanaa, kukosekana kwa Community Centres na mkanganyiko katika
Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ni mambo ambayo, tupende tusipende,
yanadidimiza sanaa nchini japo serikali iliyopita ilijidai kuwathamini wasanii.
Pia ukiangalia Bajeti ya Tamisemi unajiuliza ni asilimia ngapi ya bajeti
hiyo huenda katika shughuli za Utamaduni?
Tunasahau
kuwa Utamaduni ukilelewa vizuri ni chombo chenye nafasi nyingi sana za ajira,
huweza kuongeza pato la eneo husika kwa kuhamasisha maendeleo, huleta uzalendo,
ubunifu wa mambo mbalimbali ya Utamaduni, huweza kuhamasisha Utalii katika
Utamaduni, na huwa ni sehemu ya Utalii ambayo kwa bahati mbaya sana haijatumika
kikamilifu katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.
Mkanganyiko huu umeifanya sekta ya sanaa kuyumba kwa kuwa
inashughulikiwa na wizara tatu tofauti; Wizara ya Viwanda na Masoko, Wizara ya
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, hali ambayo imekuwa ikisababisha
migongano ya kiutendaji na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja wa sekta hii
katika wizara moja.
Sekta ya filamu na sanaa kwa ujumla ilikuwa inakua kwa
kasi lakini sasa tunashuhudia ikiporomoka kwa kasi ya ajabu, hivyo, nguvu kubwa
lazima iwekezwe ili kuhakikisha kuwa sekta hii inaendelea kukua na kuwa chanzo
kikubwa cha ajira na mapato miongoni mwa Watanzania ikiwa ni pamoja na
kulitambulisha taifa katika ngazi mbalimbali za kimataifa.
Rais, sina hakika kama unaielewa nguvu ya soko la sanaa
na umuhimu wa utamaduni na uchumi, na iwapo utasimamia vyema basi sekta hii
itasaidia kupanuka kwa ajira hapa nchini.
Labda tu nikudokeze kuwa sekta ya sanaa hapa nchini ni sawa
‘shamba la bibi’, kila anayejisikia anaingia, anavuna tani yake na kufaidi
mazao pasipo kulima, huku serikali ikiwa haipati kitu!
Kwa leo naomba niishie hapa, sitaki nikuchoshe kwa kuwa
ndiyo kwanza umeingia ofisini, una jukumu kubwa la kuangalia ukubwa na
mpangilio wa serikali yako (ambayo uliahidi itafanya kazi kwa ufanisi). Panapo
majaaliwa nitaelezea jinsi sekta hii ilivyouawa na nani walioiua.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment