Muigizaji wa filamu ya Yesu, Brian Deacon |
TAKRIBAN baada ya miaka 35 tokea sinema ya Yesu
iliyoigizwa na Brian Deacon, muigizaji ambaye watu wengi wa kizazi cha siku
hizi huamini kuwa ndiye Yesu, imerudiwa tena katika mfumo wa hali ya juu,
kuanzia picha na hata uchanganyaji wa sauti.
Jesus, filamu ambayo ndiyo imevunja rekodi na inaongoza
duniani kwa kutafsiriwa kwenda lugha nyingi, kwani kwa mujibu wa kitabu cha
kumbukumbu cha Guiness, (Guiness World
Record) filamu hiyo imetafsiriwa kwenda lugha 1,197 tofauti duniani kote,
na kutazamwa na zaidi ya mara bilioni moja, huku watu zaidi ya milioni mbili
wakiokoka kutokana na kutazama sinema hiyo.
Utengenezaji upya wa filamu hiyo umehusisha kupitia
'frame' moja baada ya nyingine. Sekunde moja ina takriban fremu 24, yaani kwa
lugha rahisi, picha 24 ndani ya sekunde moja ambazo zinatengeneza mtiririko wa
muondoko, na hivyo kufanya jumla ya fremu 173,000 kupitiwa moja baada ya
nyingine na kisha kuihariri upya na kusawazisha rangi ili iendane na mfumo wa
kisasa.
Kwa upande wa sauti, mfumo wa 5.1 Surround system ndiyo
ambao umetumika, huku maeneo mengine yakiongezewa sauti kulingana na
utayarishaji wa kisasa ulivyo kwa kizazi cha sasa.
Filamu hiyo ambayo imepewa jina la 'The Jesus Film',
inakuwa ya kipekee kama ambavyo wakati inatengenezwa miaka 36 iliyopita,
ilikuwa na mashiko kwa ulimwengu, kutokana na namna ilivyoandaliwa,
kutayarishwa na kuongozwa.
Filamu hii ilipotoka miaka 36 iliyopita, kwa kweli ilikuwa mbele, yaani imeendelea kuliko sisi. Mkurugenzi mtendaji wa Jesus Film Project ameeleza, akisifia namna ilivyosukwa ikasukika, ambapo kila kilichoigizwa, kimetoka kwenye Biblia, na kupitia na wachungaji na wanazuoni zaidi ya 450 ili kujiridhisha dhidi ya upotoshaji.
Brian Deacon, muigizaji
ambaye katu hatosahaulika kwa wasifu aliouonesha, mara nyingi alikuwa
akichanganywa na Yesu, hasa kwa watu ambao wanatazama filamu hiyo bila kuwa na
rejea ya mafundisho.
Na licha ya kwamba
filamu hii imetazamwa na wengi ulimwenguni, ni watu wachache tu nchini Marekani
ambao wameiona, ila kwa kuwa imetengenezwa upya kwa namna ya kisasa zaidi
katika kuadhimisha miaka 35 tokea kupikwa mnamo mwaka 1979, inaaminiwa kuwa
watu wengi zaidi wameiona, ikizingatiwa kuwa nakala moja ya DVD itajumuisha
lugha za Kiingereza, Kispanish, Kikorea, Kiarabu, Kifaransa, Kijerumani,
Kivietnam, na Kimandarin.
Machi 2014 ndiyo mwezi
ambao filamu hiyo ilianza kutazamwa kwenye majumba ya sinema ulimwenguni,
ambapo kufikia mwezi Aprili, filamu hiyo ilikuwa imewekwa pia kwenye mfumo wa
DVD na Blu-Ray.
No comments:
Post a Comment