Desmond Elliot, muigizaji wa Nollywood ambaye alikuwa
akiigwa na Steven Kanumba katika uigizaji wake
Marehemu Steven Kanumba
SEKTA ya filamu Tanzania kwa sasa inajulikana duniani licha ya matatizo yake, licha ya mtayarishaji wa filamu wa Tanzania kuendelea kuishi maisha ya chini yasiyo tofauti na mtu mwingine wa kawaida! Sekta ya filamu Tanzania inakua, lakini hali halisi ya soko la filamu nchini inabana sana uwezekano wa kuibuka kwa wasanii, watayarishaji au waongozaji wapya...
Sidhani kama kuna mtu atakayebisha kuwa filamu za kibongo ‘hazitesi’ katika ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo ya Maziwa Makuu. Filamu hizi zimesaidia kwa kiwango fulani kuitangaza nchi hii, kuwatangaza wasanii wa nchi hii, lakini vipi kuhusu maisha ya wasanii hawa? Je, wanapata stahili yao na wanaishi kwa kutegemea filamu pekee?
Kinadharia sekta ya filamu hapa nchini imekuwa ikikua, kwa kigezo cha sinema zetu kuonekana zikiuzwa kwa wingi mitaani, huku watu wakizichangamkia; wanawake na vijana ndio wakiwa wateja wakubwa wa sinema hizi. Pia kwa waliopata bahati ya kutembelea nchi jirani za Kenya , Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , Rwanda , Burundi na kadhalika, watakubaliana nami kuwa filamu zetu zinatesa sana maeneo hayo.
Na ikitokea ukatembelea huko halafu watazamaji wa filamu zetu katika nchi uliyotembelea wakagundua kuwa wewe ni Mtanzania, kwa kweli utakuwa katika wakati mgumu sana kwani utaulizwa maswali mengi kuhusu filamu na wasanii wa Kitanzania, na wengi wao wakitaka uwape maelezo mengi kuhusu filamu hizo na wasanii.
Lakini bado sekta ya filamu nchini haioneshi tija kwa watayarishaji, wasanii wala watendaji wengine kutokana na changamoto kadhaa. Ingawa kuna hizo changamoto, lakini hatuwezi kubisha kuwa sekta hii imeanza kuonesha matokeo/athari katika utamaduni wa Tanzania , kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Licha ya changamoto ambazo sekta hii imekuwa ikikumbana nazo ikiwa ni pamoja na ubora hafifu wa filamu zinazozalishwa na uharamia wa kazi za filamu, sekta ya filamu yenyewe bado ina nafasi nzuri ya kuwajulisha watazamaji wake, matokeo ya sekta hii Tanzania na kwingineko.
Pia uchumi wa soko huria la filamu za Bongo umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sinema za Kiswahili. Ukipita mitaa ya jijini la Dar es Salaam au katika miji yote mikubwa (Mwanza, Arusha, Mbeya na kadhalika) utaona mabanda ya kuoneshea video yakiwa yametapakaa kila kona. Pia utakutana na wauzaji wa filamu wakitembeza barabarani, si kama miaka ile ambapo watu walikuwa wakitazama sinema za kutoka nje, hususan Marekani na India … enzi ambazo watu wakizililia sinema za Tanzania pasipo kuziona.
Kuna mwanaharakati mmoja aliwahi kusema kuwa utoaji wa hizi filamu zetu kwa sasa imekuwa kama mchezo wa soka bila refa, sawa na mkutano bila mwenyekiti, darasa bila mwalimu, au nyumba (familia) bila mzazi…
Wafanyabiashara wanaahidi milioni kumi hadi ishirini kwa sinema; watoaji sinema wanalipua kazi; waigizaji hawalipwi vizuri; utengenezaji sinema unafanywa haraka haraka. Sinema zinatengenezwa kwa wiki moja hadi mbili na zinatolewa ndani ya mwezi mmoja tu. Haraka haraka…
Wasanii wa filamu wanaigiza bila script wala mazoezi, baadhi ya watengenezaji filamu wanatumia mwanya huo kula uroda na wasichana wazuri wazuri (ndiyo maana siku hizi kuwa miss ni kigezo kikubwa cha kupata nafasi ya kucheza filamu, haijalishi kama una kipaji cha kuigiza au la), sinema zinazotolewa nchini eti zinalinganishwa na za Wanaijeria! Tangu lini sinema za Wanaijeria zikawa kipimo cha filamu?
Sikatai na wala hakuna atakayebisha kuwa sinema za Nollywood zilitingisha nchi yetu wakati fulani, Nollywood pia imeshaleta athari kubwa na kusababisha kubadilisha tamaduni za Nigeria na Afrika. Japo kuna baadhi ya hoja kuhusu madai ya kuvuruga tamaduni kunakohusishwa na Nollywood, sekta hiyo imekuwa chombo kikubwa kinachotumika kuleta mageuzi na kuhifadhi utamaduni wa Kiafrika pamoja na kuwepo nguvu za utandawazi.
Sikatai na wala hakuna atakayebisha kuwa Nollywood inatumia lugha za asili za Nigeria kusimulia habari za Afrika. Ni kweli kuwa lugha na utamaduni wa watu ni muhimu katika utambulisho wao na matarajio yao kwa ajili ya kujitawala. Aidha, sikatai na wala hakuna atakayebisha kuwa Nollywood wanaelezea maisha ya jadi, mchanganyiko na ya kisasa ya watu wa Nigeria .
Lakini kwa nini sinema zao zitumike kama kipimo chetu cha filamu? Kwa nini tufuate nyayo za Nollywood katika kuzalisha sinema zetu? Kwa kipi hasa? Hii inatufanya kusimulia hadithi zao; angalia sinema zetu zinavyosimulia uchawi, zinavyosimulia mapenzi au mikasa ya kijamii utagundua hilo . Tunaiga hadithi zao, namna yao ya uchezaji, sinema zao ambazo nyingi zimekuwa zikiigwa kutoka mataifa ya Magharibi na India .
Hata hivyo, Nollywood ndiyo sekta ya pili kwa ukubwa kwa kutoa ajira katika nchi ya Nigeria baada ya sekta ya kilimo, kwani inachangia mauzo ya kati ya dola za Marekani milioni 200 na 300 kwa mwaka. Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya filamu inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo ya kukubalika kwa sinema pia huwafanya watayarishaji wa sinema, waigizaji na watendaji wengine kuwa na heshima kwenye jamii na hata kisiasa.
Mfano, wakati wa kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta nchini Nigeria , iliripotiwa kwamba Rais Goodluck Jonathan aliamua kumtuma mwakilishi wake kujadili suala hilo na wadau wa Nollywood katika mkutano wao “Nollywood Roundtable uliohusu kupunguza udhibiti wa kibiashara”. Mkutano huu uliandaliwa na kikundi cha Segun Arinze wa Chama Waigizaji wa Nigeria (AGN).
Hata hivyo, kundi jingine la Nollywood, Chama cha Watayarishaji cha Nollywood (ANCOP), wakiongozwa na Alex Eyengho, walikosoa mkutano huo. Walisema kuwa kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta hakukupaswa kuungwa mkono na kundi la Segun Arinze wa AGN. Bila kujali, suala kubwa hapa najaribu kuonesha umuhimu wa sekta ya filamu katika kubadilisha sera za kiuchumi katika uhusiano na siasa nchini Nigeria .
Serikali ya Nigeria inaichukulia sekta ya filamu kwa umakini mkubwa. Vipi kuhusu serikali yetu? Vipi kuhusu Watanzania kwa ujumla? Imekuwa ikisemwa kuwa Watanzania hatupendi au hatununui sinema zinazotolewa na Watanzania wenzetu. Kisa? Hazituvutii.
Moja ya sababu ni kwamba zinatengenezwa vibaya kwa kulipuliwa. Lakini kwa nini hata sinema zinazotengenezwa vizuri bado hatuzinunui? Kwa nini hatuzifurahii? Kwa nini hatuzitolei maoni na kuzitangaza? Tunachokiweza ni kuziponda tu! Hivi hatudhani kuwa hiyo ndiyo njia kuu itakayotufanya tuendelee kama wenzetu, tunaowaona Miungu kutuzidi?
Kwa upande wa waandaaji wa filamu tukumbushane kwamba sinema ni sanaa inayochukua muda. Hatuwezi kutengeneza sinema ikakamilika ndani ya mwezi mmoja tu. Tujipe muda katika kuifanya kazi kwa ufanisi zaidi. Ingawa wapo wanaosema kuwa sababu ya kufanya kazi haraka haraka ni kutokana na matatizo ya pesa ambapo mtu huhitaji kupata pesa haraka ili atatue matatizo yake. Lakini tunasahau kuwa ukitoa kazi nzuri yenye ubora hukaa na huuzika miaka nenda miaka rudi, tofauti na kazi zetu ambazo baada ya wiki mbili zinakuwa hazina tena soko.
Tukumbushane kujipa muda katika uandaaji wa filamu zetu: Mwezi mmoja wa mikutano kupanga mambo (wapi itapigwa picha, nani atafanya nini, waigizaji watatoka wapi, watafanya nini), mwezi mwingine kupanga usanii (mazoezi ya waigizaji, mazingira yao ), mwezi mwingine wa kupiga picha. Baada ya miezi mitatu, mingine miwili ya kuhariri na kusahihisha makosa.
Ndipo sasa kifuate kipindi cha kuitangaza kusudi iuzwe. Ukichunguza sana utagundua kuwa sinema haiwezi kumalizika chini ya miezi sita kwa mazingira ya Tanzania . Ndiyo maana wenzetu wanatoa sinema moja tu kwa mwaka lakini pesa wanazopata wanakula kwa miaka kibao. Sisi tunatoa sinema kila mwezi lakini pesa yake ni ya kujikimu tu.
Mtenegeza sinema maarufu wa Marekani, Spike Lee, anasema kuwa huwa anakuwa na kundi kuubwa la watu anaoshirikiana nao katika utengenezaji wa filamu. Ukitaka kufanya kazi nzuri yenye ubora huwezi kufanya sinema peke yako.
Ni wakati sasa tuwe kwenye makundi, tushirikiane, tuzichangamkie na tuangalie sinema zetu, tuzifurahie na tupeane moyo.
Alamsiki…
No comments:
Post a Comment