DVD feki zikiwa tayari kwa kuuzwa
Hakuna ubishi kuwa nguvu zaidi zinahitajika katika kufanikisha mapambano ya kuwakomboa wasanii, watengenezaji na wasambazaji wa kazi za sanaa ili wapate malipo/mapato stahiki kutokana na kazi zao. Nashangaa kuwa Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (Cosota) kimeonekana kulala usingizi, badala ya kuchukua hatua.
Sehemu kubwa ya umma – wakiwemo wasanii wenyewe - haijui chochote kuhusu Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, hata Cosota bado haichukui hatua madhubuti za kuendesha kampeni kamambe nchi nzima ili kuuelimisha umma pamoja na wasanii kuhusu Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Najua baadhi ya wasomaji watanishangaa ninaposema kuwa Cosota iendeshe kampeni nchi nzima, hasa kwa kuzingatia kuwa chama hiki kina watendaji wachache na hakijasambaa nchi nzima, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa Cosota ingeweza kushirikiana na vyombo vya habari, kama vituo vya televisheni, redio na hata magazeti kufanya kazi hiyo kama mojawapo ya majukumu ya vyombo hivyo katika kuuelimisha umma.
Nakumbuka mwaka juzi ilifanyia semina ya wadau katika ukumbi wa Alliance francaise ambapo haya ninayoyaandika yalizungumzwa, na hata Cosota walikuwepo lakini sioni juhudi zozote za makusudi zikichukuliwa ili kunusuru jambo hili. Elimu ambayo inapaswa kutolewa na Cosota kwa kuvishirikisha vyombo vya habari ilenge kueleza madhara ya kununua kazi feki za wasanii – muziki, filamu na machapisho mbalimbali ambayo, mbali na kutokuwa na ubora wa viwango, lakini pia husabisha kukosekana kwa mapato stahiki (kodi) kwa upande wa serikali na (mrahaba) kwa upande wa wasanii.
Moja ya maazimio kwenye semina ile ilikuwa ni kwa Cosota kushirikishwa katika vituo vya forodha (bandarini na mipakani) katika uingizaji bidhaa za kazi za sanaa nchini kama vile zinavyoshirikishwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (Tanzania Food and Drug Authority) kwa bidhaa za chakula na dawa; Shirika la Viwango Tanzania (Tanzania Bureau of Standards) kwa bidhaa zenye viwango vinavyotambulika kimataifa; pamoja na Tume ya Ushindani wa Biashara (Fair Competition Commission – FCC) kwa bidhaa bandia.
Cosota pia walitakiwa wasajili na kutoa leseni kwa maduka/maktaba yanayouza/kukodisha CD/DVD za muziki/filamu, vibanda vya “video” vinavyoonesha sinema na majumba ya starehe/kumbi zinazopiga muziki. Badala yake tunajionea kazi hii kuanza kufanywa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.
Pia imesemwa kuwa kwa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority) imepata mafanikio makubwa katika kukusanya kodi kwa upande wa sigara na pombe kali kutokana na kuamuru matumizi ya ukanda wa lakiri (Bandroll/hologram) kwa watengenezaji/waagizaji wa bidhaa hizo, vivyo hivyo, TRA au Cosota waanzishe utaratibu huo huo kwa kazi za sanaa. Hii itasaidia kupambanua kati ya bidhaa (CD/DVD) halisi na zile feki.
Hii itawezesha TRA kupata thamani halisi ya kazi hizo kwa ajili ya kutoza kodi na pia kutoa adhabu kwa wale wanaoiba kazi za wasanii. Inasahngaza sana kuwa hadi sasa hakuna anayefahamu tasnia ya filamu nchini ina thamani ya kiasi gani? Pia hata mapato ambayo serikali inayapata kutokana na kazi hizi za sanaa ni “kiduchu” mno kwa kuwa hakuna kumbukumbu (Data) zozote zilizotunzwa kuhusiana na tasnia hii.
Watendaji wote katika tasnia hii wanapaswa wasajili kampuni au taasisi zao kisheria kwa msajiri wa makampuni (Brela) ili iwe rahisi kutambuliwa na serikali pamoja na taasisi zake.
Serikali inatakiwa kutunga sheria kali za Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki na adhabu kali zitolewe kwa wezi wa kazi za sanaa kwani kwa sheria ilivyo sasa, adhabu zinazotolewa ni ndogo sana kiasi kwamba maharamia wanaoiba kazi hizo hawashindwi kumudu kuzilipa. Hapa nina mifano michache kuhusiana na adhabu zilizowahi kutolewa: Mkoani Kagera mhalifu alikutwa na kanda 500 feki, akahukumiwa faini ya shilingi 45,000/- na akarudishiwa kanda zake.
Mhalifu mwingine aliwahi kukutwa na FUSO nzima ya mikanda ya video, akapigwa faini ya shilingi 200,000/- na mzigo akarudishiwa, siku hizi ni msambazaji maarufu wa filamu za Kibongo! Kwa hukumu kama hizi, tunategemea nini? Ni kweli tuna nia ya dhati kukomesha uharamia wa kazi za sanaa?
Pia Serikali ihakikishe kwamba Jeshi la Polisi na Mahakama wanasimamia sheria hizo kwa ukamilifu. Lakini kuna jambo moja linalofanyika ambalo sikubaliani nalo, ni hili la kupunguza gharama za uzalishaji bidhaa hizo ili bei nayo ipunguwe kwa mlaji wa mwisho katika kukabiliana na ushindani wa bidhaa feki, ambapo wasambazaji wa filamu wameamua kulifanya kwa kuwa naamini kuwa halitusaidii kukabiliana na bidhaa feki.
Ni kweli bidhaa feki pia husababisha wasanii kukata tamaa kwani huona jasho lao halilipi na hivyo huacha shughuli hizo na kuua vipaji vyao, lakini tungeangalia kwa makini nini kinachosababisha kuwepo bidhaa feki, na wala si kupunguza bei ya bidhaa. Naamini yapo mambo ambayo yanachangia uwepo wa bidhaa feki, ikiwa ni pamoja na sheria dhaifu, watuhumiwa kulindwa na viongozi n.k.
Jeshi la Polisi lisiwe linawakamata watengenezaji na wasambazaji wa kazi feki tu, bali pia liwakamate watumiaji (walaji) wa kazi hizo pale wanaponunua bidhaa hizo, ili kupunguza, kama siyo kuondoa kabisa mahitaji (market demand) ya bidhaa feki.
Kama Tume ya Ushindani wa Biashara (Fair Competition Commission – FCC) inaweza kukamata makontena kwa makontena ya bidhaa bandia wakati yakiingizwa nchini kupitia vituo vya forodha ( bandarini na mipakani), kwenye maghala ya kuhifadhia mizigo na mpaka madukani na kuziteketeza bidhaa hizo, kwa nini wasifanye hivyo kwa bidhaa za kazi za sanaa ( DVD na CD) za filamu na muziki?
Suala la bidhaa feki limesambaa sana katika kazi za sanaa – kwa mfano: DVD na CD za filamu na muziki zinazoingizwa nchini kutoka nchi za Mashariki ya mbali. Cosota inapaswa kuwaelimisha wasanii, watengenezaji na wasambazaji wa kazi za sanaa na kuwahimizwa kushirikiana kwa karibu sana nayo ili kukabiliana na wizi wa kazi hizo.
Kwa kuwapa elimu, wasanii, watengenezaji na wasambazaji watapata elimu ya kutosha kuhusu tasnia yao – filamu; Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki na wataweza kufuata maadili ya taaluma yao ili kazi wanazotengeneza ziwe za viwango vya juu, na hivyo basi kuvutia katika soko, siyo la ndani tu, bali hata ziweze kuuzwa katika soko la nje ya nchi.
Kwa kuwa suala hili la wizi wa kazi za sanaa limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu sasa; na kwa kuwa hakuna mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na juhudi hizo, nadhani wadau wote tunapaswa kutafakari namna nzuri ya kufanya ili tuondokane na kilio hiki cha kila siku juu ya wizi wa kazi za sanaa.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment