Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo
Dk. Emmanuel John Nchimbi
TUKIWA tunaelekea kutimiza miaka 50 tangu tuwe huru, jamii ya Kitanzania imeendelea kupoteza mila na tamaduni zake kila kukicha. Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana iliundwa mwaka 1962, rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, alitamka wazi kuwa Utamaduni ndiyo kiini na roho ya Taifa, na nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.
Nalazimika kusema kuwa miaka hii hamsini ya uhuru nchi yetu inashuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii huku tasnia ya sanaa/utamaduni ikionekana kutelekezwa kabisa na serikali yetu bila kujali kuwa tasnia hii imesheheni utajiri mkubwa ambao kama ungetiliwa maanani ungeliingizia taifa hili pato kubwa.
Ingawa sekta ya sanaa na utamaduni imekuwa katika mfumo wa serikali tangu 1962 nafasi yake katika maendeleo ya taifa bado haijatambuliwa kikamilifu. Cha kushangaza pamoja na umuhimu uliopo katika suala la sanaa na utamaduni kwa maisha ya watu, bado sera ya utamaduni imepewa nafasi finyu sana katika serikali yetu tangu ilipoanzishwa wizara ya kushughulikia masuala ya sanaa na utamaduni.
Sera ya utamaduni ilizinduliwa Agosti 23, 1997 mjini Dodoma, hii ilikuwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.
Lakini pamoja na yote hayo, mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, ambapo utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inadhaniwa kuwa 'eti maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili' pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.
Lakini pamoja na yote hayo, mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, ambapo utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inadhaniwa kuwa 'eti maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili' pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.
Serikali kutoipa umuhimu tasnia ya sanaa/utamaduni ndiyo sababu ya uchafu na tatizo la maadili tunalolishuhudia sasa katika filamu zetu, kwani kumekosekana udhibiti wa kazi chafu. Wengi wamekuwa wanajiuliza kwa nini tunakosa alama ya mfano wa filamu zetu? Nini chanzo cha wasanii wetu kuigiza na kuiga filamu chafu (zisizo na maadili)?
Nimewahi kusoma mahala fulani kuwa mapokeo ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika. Hivyo kama sanaa zetu haziakisi tamaduni zetu, tujue kuwa vizazi vijavyo vitarithi mambo yasiyokuwa yetu.
Nimewahi kusoma mahala fulani kuwa mapokeo ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika. Hivyo kama sanaa zetu haziakisi tamaduni zetu, tujue kuwa vizazi vijavyo vitarithi mambo yasiyokuwa yetu.
Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya Utamaduni hukua na pia hufa. Hebu sasa tujiulize maswali haya; je, sanaa zetu zinakua au zinakufa au zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi? Je, filamu zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo? Au kizazi chetu kinaweka kumbukumbu potofu ya filamu zetu na utamaduni kwa vizazi vijavyo?
Kwa nini kila kukicha ni filamu za mapenzi peke yake zinazotawala kwenye tasnia yetu au hadithi zisizo na asili yetu tulizonakili kwa wenzetu zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje? Kwa nini hatutaki kutumia visa vyetu wenyewe hadi tuige kutoka kwa wenzetu?
Kwa kweli haya ni maswali muhimu na inabidi kila mdau aliye kwenye tasnia ya filamu na sanaa kwa ujumla anapaswa ajiulize katika kazi zake za sanaa za kila siku. Tusipokuwa makini tutajikuta tukipita njia potofu na kukipoteza kizazi chetu kwa kuwa njia tunayoenda nayo sasa katika filamu zetu ni ile iliyojengwa juu ya msingi wa wimbi la utandawazi unaoakisi utamaduni wa Kimagharibi.
Tutake tusitake, ukweli ni kwamba fani yetu ya filamu kwa sasa ipo katika hatari kubwa ya kuporomosha mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu kwani watayarishaji na wasanii walio wengi katika tasnia hii wameshapotea njia kwa kutofuata au kutoijua miiko na maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya hadithi yanaonekana dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.
Kwa hali hii ya serikali kutoizingatia sekta hii na kukosa udhibiti wa sanaa huku ikituacha tujifanyie tunavyodhani inatufaa ni ishara ya hatari (dangerous alarm) inayoashiria mporomoka kwa fani hii. Je, kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili?
Ninachoamini ni kuwa sanaa ya filamu ni zao la matokeo ya juhudi za mtayarishaji, watendaji wengine katika kazi ya filamu na wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu na hii kama tanzu muhimu ya utamaduni si kitu kilichoibuka tu. Hivyo tunapaswa kuwa makini sana na filamu tunazozalisha.
Jambo muhimu na la msingi hapa ni kwa Serikali na wadau wote kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Sanaa ya filamu ni kazi ya ubunifu yenye ufundi na mvuto, hivyo inapaswa kutopoteza ubunifu, uasili au kukosa mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.
Hadi sasa filamu nyingi za Kitanzania au michezo ya kuigiza katika Luninga ni vitu vilivyopoteza mwelekeo kwani leo hii inafuata mifumo na mtiririko wa kigeni zaidi hasa filamu za Nigeria, tamthilia za Philippine, Amerika ya Kusini na kwingineko. Yote hii inasababishwa na wavamizi kwenye fani hii waliodhani kuwa mtu akikosa kazi ya kufanya basi kimbilio lake ni kwenye sanaa hasa filamu.
Matokeo yake tumejikuta tukiwa na idadi kubwa ya watayarishaji filamu, waandishi wa miswada, waongozaji filamu na waigizaji bandia wasio na misingi wala kanuni za fani husika jambo linalosababisha kazi zetu kuwa sawa na Big G inayoisha utamu kwa muda mfupi, huku watu wenye taaluma na misingi wakitupwa nje ya soko kwa kuwa sanaa siku hizi imekuwa ni biashara isiyozingatia maadili ya Taifa.
Si vibaya kujifunza kutoka kwa wenzetu ambao wana maendeleo, lakini siyo vema kuiga tamaduni zao ambazo kwetu ni upotoshwaji wa taratibu zetu za kimaisha. Tunapaswa kuiga hekima na busara za waliondelea na kuacha yale yasiyofaa tofauti na ilivyo sasa ambapo tunaacha mazuri na kunakiri upotofu.
Hivi tunajisikiaje pale tunaposhindwa kuziangalia filamu zetu tukiwa mahala pamoja na watoto au watu tunaowaheshimu?
Tunaposherehekea miaka hamsini ya uhuru, Serikali na wadau wote katika tasnia tuna jukumu la kuhakikisha tunalinda tamaduni zetu na kuwa urithi bora kwa vizazi vijavyo ambapo nao pindi watakaposherehekea miaka mia moja ya uhuru wawe na kitu cha kujivunia kutoka kwenye jamii yao ya asili.
Tunaposherehekea miaka hamsini ya uhuru, Serikali na wadau wote katika tasnia tuna jukumu la kuhakikisha tunalinda tamaduni zetu na kuwa urithi bora kwa vizazi vijavyo ambapo nao pindi watakaposherehekea miaka mia moja ya uhuru wawe na kitu cha kujivunia kutoka kwenye jamii yao ya asili.
Tusiwe wasindikizaji kwa kila kitu au watu wa kupokea kila kitu toka nje huku tukishindana kunakili (copy and paste) kama yalivyo. Tuache uvivu au kufanya mambo kwa mazoea bali tufanye utafiti wa asili tulikotoka na hivyo kusimama kama watetezi wa kazi za sanaa za waliotutangulia.
Na mwisho ni kuhusu majina ya filamu zetu. Ingawa mimi huwa sina tatizo na majina ya Kiingereza kwenye filamu zetu lakini naamini kuwa hii ni kasumba mbaya sana. Filamu kuwa na jina la Kiingereza huku yenyewe ikitumia lugha ya Kiswahili mwanzo mwisho kwa kisingizio cha soko, siyo sawa!
Tuonane wiki ijayo…
No comments:
Post a Comment