Dec 23, 2015

Ni vema kufanya utafiti kabla hujawadharau Wasanii

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye

WIKI iliyopita kwenye gazeti la Raia Mwema kulikuwa na makala yenye kichwa: “Baraza jipya la mawaziri, mkorogo usio hamasa kwa mabadiliko”, kutoka kwa mwandishi ninayemheshimu, Joseph Mihangwa. Nimekuwa msomaji mkubwa wa Mzee Mihangwa (kwangu ni sawa na baba’angu), kwa miaka mingi, nimekuwa msomaji wake na sijawahi kufikiria kumkosoa. Lakini nadhani ameteleza kidogo kwa kubeza juhudi za wasanii wa nchi hii.

Nov 4, 2015

DK. JOHN MAGUFULI: Wasanii wanasubiri utekelezaji wa ahadi zako

Rais Mteule Dk. John Pombe Magufuli, akijiachia jukwaani pamoja na wasanii wa kundi la Yamoto Band kwenye uwanja wa Mashujaa mkoani Mtwara, wakati wa kampeni

KWANZA kabisa napenda nikupongeze kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania katika Awamu ya Tano, nikitumaini kuwa wananchi wamekupa ridhaa kwa kuwa wamekuona unafaa zaidi kuiongoza nchi hii baada ya Rais Jakaya Kikwete, ambaye uongozi wake unahitimishwa kesho Alhamisi.

Ingawa kuna minong’ono na wasiwasi mwingi kuwa huenda wewe huna ‘interest’ kabisa na masuala ya sanaa, na uongozi wako utajikita zaidi kwenye kujenga barabara, reli, uwekezaji, kilimo, mifugo, uchimbaji madini nk, lakini nina imani kuwa uongozi wako utawapa wasanii tumaini jipya.

Oct 21, 2015

WITO KWA WASANII: Kuna maisha hata baada ya uchaguzi

Baadhi ya wasanii wa Filamu wakiwa kwenye uzinduzi wa Kampeni za mgombea Urais wa Chadema anayeungwa mkono na UKAWA, Edward Lowassa
MWAKA HUU ninashuhudia mihemko ya ajabu ya kisiasa kwa wasanii kushabikia siasa na wanasiasa! Kwa mara nyingine tena nashuhudia namna wasanii wa fani mbalimbali wanavyodhihirisha umuhimu wao katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, wakihusika katika kampeni za vyama, na kwa wagombea wa ngazi tofauti.

Nilipoona mihemko hii nilijiuliza kama kuna manufaa yoyote wanayopata kwa kushiriki kampeni hizi? Jibu likawa, yapo, kwani hiki ni kipindi cha mavuno kwa wasanii.

Je, unajua kuwa Filamu ya Yesu imerudiwa upya?

Muigizaji wa filamu ya Yesu, Brian Deacon

TAKRIBAN baada ya miaka 35 tokea sinema ya Yesu iliyoigizwa na Brian Deacon, muigizaji ambaye watu wengi wa kizazi cha siku hizi huamini kuwa ndiye Yesu, imerudiwa tena katika mfumo wa hali ya juu, kuanzia picha na hata uchanganyaji wa sauti.

Jesus, filamu ambayo ndiyo imevunja rekodi na inaongoza duniani kwa kutafsiriwa kwenda lugha nyingi, kwani kwa mujibu wa kitabu cha kumbukumbu cha Guiness, (Guiness World Record) filamu hiyo imetafsiriwa kwenda lugha 1,197 tofauti duniani kote, na kutazamwa na zaidi ya mara bilioni moja, huku watu zaidi ya milioni mbili wakiokoka kutokana na kutazama sinema hiyo.

Oct 7, 2015

KAMPENI 2015: U wapi uchumi na utajiri wa wasanii? - 2

Wasanii wa filamu, Anti Ezekiel na Jackline Wolper,
wakiunga mkono siasa za Chadema
Msanii wa vichekesho, Steven Mengere (Steve Nyerere),
katika mikutano ya CCM
WIKI HII nimelazimika kuendeleza mjadala wa ‘uchumi na utajiri wa wasanii’, hasa baada ya baadhi ya wasomaji wangu kunitumia ujumbe kutaka ufafanuzi katika mambo fulanifulani. Hata hivyo, wengi wao wanakubaliana na hoja yangu kwamba sanaa siyo sekta ya kuchezewachezewa, wala haipaswi kupuuzwa hata kidogo na wanasiasa wetu.

Sep 30, 2015

KAMPENI 2015: U wapi uchumi na utajiri wa wasanii?

Wasanii waliopo katika kampeni ya Mama Ongea na Mwanao mpigie kura Dk. Magufuli
KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zimepambwa zaidi na wasanii mbalimbali. Kumekuwepo na mhemuko wa ajabu wa wasanii kujitokeza kwenye majukwaa ya siasa, wengi wao wakijipambanua kuwa wafuasi au mashabiki wa vyama na wanasiasa fulani. Zikiwa zimesalia siku 22 tu kabla ya kupiga kura kuichagua serikali ijayo (Rais, Wabunge na Madiwani), hali bado ni ya mashaka kwa sekta ya sanaa.

Wasanii wanatumika kwa kiasi kikubwa kwenye majukwaa ya siasa, kiasi cha mikutano kugeuka kuwa matamasha ya burudani, huku wakiwa hawajui majaliwa yao kuhusu ustawi wa sekta ya sanaa, zaidi ya kupigwa porojo na ahadi zisizotekelezeka.

Sep 16, 2015

Sekta ya filamu Tanzania imekosa uhalisia


KATIKA wasanii mastaa ambao wangepaswa kuishi maisha mazuri hapa Tanzania, wasanii wa filamu ndiyo wangepaswa kuwa wanashikilia chati za juu kutokana na jinsi kazi zao zinavyotengeneza fedha nyingi. Kwa mujibu wa takwimu, kazi za wasanii hao zimekuwa zikiingiza fedha nyingi tofauti na ilivyokuwa awali, lakini maslahi hayo hutofautiana kwani wapo baadhi ambao hawashikiki.

Sep 9, 2015

Tuache utengenezaji sinema wa kulipuwa


SEKTA YA FILAMU nchini imekuwa inakua kwa kasi na kuwa kimbilio la vijana wengi, hata wale walioshindwa (failures) katika sekta zingine. Ukuaji wake umeambatana na changamoto nyingi katika kufikia ubora unaokubalika kimataifa kwenye filamu zetu.

Filamu ni nguzo muhimu sana ya Utamaduni wa nchi. Filamu zimeibuka kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali katika karne ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa mengi kama hii.

Aug 26, 2015

Je, tunaweka mipaka kwa watoto kutazama televisheni/filamu?

Watoto wanaangalia televisheni

MAJUZI jirani yangu mmoja (ambaye amenunua kisimbuzi hivi karibuni) aliniita nyumbani kwake na kuniomba nimsaidie kuweka namba za siri (password) kwenye baadhi ya chaneli za televisheni yake ili kuwadhibiti watoto wake wasiweze kuangalia sinema na vipindi visivyo na maadili. Aliamua kufanya hivyo baada ya kugundua uwepo wa chaneli zinazoonesha mambo yenye ukakasi.

Kwa sasa ni jambo la kawaida sana kwa watoto wengi kutazama filamu, televisheni, video, kucheza michezo (games) ya kompyuta, na kutumia Intaneti. Kulingana na makadirio fulani, watoto na vijana hutazama na kuvitumia vyombo vya habari kati ya mara 20 au 30 zaidi ya wakati wanaotumia kufanya mambo na familia zao. Jambo hilo huwafanya watoto wapate habari nyingi zenye kudhuru.

Aug 12, 2015

Uchaguzi 2015: Hivi Wasanii wamebeba ajenda gani?

* Waepuke kuendelea kutumiwa kisiasa
Msanii maaruf wa filamu, Jacob Steven (JB) akiwa kaongozana na
Rais Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Abrahman Kinana,
mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli na viongozi wengine,
siku wasanii walipofanya sherehe kumuaga Rais Kikwete katika
Ukumbi wa Mlimani City

“TUMEPATA mafanikio ya kuridhisha kwa upande wa sanaa za filamu na muziki. Vijana wetu wa tasnia hizi wamekuwa wanafanya vizuri kiasi kwamba leo hii Bongo Flavor na Bongo Movie zimevuka mipaka ya Tanzania. Zinaitangaza sanaa ya Tanzania, lugha ya Kiswahili pamoja na nchi yetu. Vijana hawa wameitoa kimasomaso Tanzania na kutufutia unyonge tunaopata kwenye michezo. Tasnia hizi zimeajiri vijana wengi, wanalipa kodi na wanasaidia sana katika kuhamasisha na kufikisha ujumbe kwa mambo muhimu katika jamii.”

Jul 29, 2015

TAMASHA LA 18 LA ZIFF: Tutumie fursa kama hizi kwa ajili ya kujitangaza na kujifunza zaidi

Mkongwe, Dorothy Masuka, akiwa jukwaani katika shoo yake usiku wa Julai 19, katika tamasha la 18, la ZIFF 2015,Ngome Kongwe upande wa Mambo Club

MATAMASHA ya filamu duniani ni sehemu nzuri zaidi kwa ajili ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji wa filamu au msanii kujulikana si tu katika kanda husika bali kimataifa.

Mkurugenzi wa ZIFF, Prof. Martin Mhando
Ukibahatika kuwa mmoja wa washindi wa tuzo, unakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujitangaza na hata kupata msaada wa kipesa (funds) kwa ajili ya kutengeneza sinema bora zaidi unayohitaji siku zote kwa kuwa utaingia kwenye orodha ya watu wanaoaminiwa, na hapo ndo’ washindi hujua kuwa wapo katika mstari sahihi.

Jul 22, 2015

Kukua kwa sekta ya filamu Tanzania kutakuza utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwa na muigizaji
Anti Ezekiel, siku walipotembelea Marekani kutangaza utalii

SEKTA ya Filamu nchini ikiendelezwa vizuri ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana, njia madhubuti ya kukuza utalii na uchumi wa Taifa na wa wananchi kwa ujumla. Sekta ya Filamu (kwa kuzingatia kuwa ni sehemu ya habari “media”) inapotumika vizuri, hufanya kazi kama mhimili huru unaosimamia dola.

Katika nchi ambayo Bunge linakosa meno dhidi ya udhaifu wa serikali, vyombo vya habari navyo vikawa kimya, sekta hii inaweza kuwa nyenzo imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na kuieleza jinsi mambo yasivyo sawa. Lakini pia sekta hii ina nguvu kubwa kiutamaduni, na chanzo kizuri cha kupashana taarifa.

Jul 20, 2015

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuiunga mkono ZIFF

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono  juhudi zinazochukuliwa na Uongozi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi  Zanzibar (ZIFF) katika azma yake ya kuijengea nguvu tasnia ya Filamu Nchini inayoonekana kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya Utalii.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wakati  akilizindua Tamasha la 18 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar.

Jul 18, 2015

Buhari kuipiga jeki sekta ya filamu NIgeria

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari

Rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari, ameendeleza kile kilichoanzishwa na mtangulizi wake, Goodluck Jonathan, katika kusaidia sekta ya filamu kwa kuapa kuhakikisha anasaidia sekta ya filamu nchini humo kutoanguka kutokana na uharamia wa kazi.

Alisema kuwa sekta ya filamu ya Nollywood inafanya vizuri ila inaweza kuathiriwa na uharamia. Sekta hii ina thamani ya dola bilioni 5 (sawa na paundi bilioni 3), lakini watengeneza filamu bado wanasota kutengeneza faida  kwa sababu ya uharamia.

Jul 14, 2015

Benson Wanjau Karira (Mzee Ojwang Hatari) afariki dunia

Benson Wanjau Karira maarufu kama Mzee Ojwang Hatari

Muigizaji mkongwe wa vichekesho nchini Kenya, Benson Wanjau Karira maarufu kama Mzee Ojwang Hatari, amefariki dunia siku ya Jumapili usiku katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta alipokuwa amelazwa.

Mzee Ojwang wakati akichukuliwa vipimo vya macho

Mzee Ojwang alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu (Pneumonia). Muigizaji huyo ambaye alikuwa kinara katika vipindi vya Vitimbi, Vioja Mahakamanii, Vituko na Kinyonga, pamoja na kazi nyingine, alikuwa hajaonekana kwenye televisheni kwa muda mrefu.

Jul 7, 2015

Mabanda ya Video: Tutazame upande wa pili wa shilingi

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo

Mjumbe wa Bodi ya Filamu, Dk. Vicensia Shule (kushoto), akizungumza katika kikao na wafanyakazi wa kampuni ya usambazaji ya Proin Promotion. Katikati ni Bishop Hiluka na kulia ni Mzee Silvester Sengerema (Kaimu Mwenyekiti Bodi ya Filamu)

INGAWA nchini Tanzania televisheni imekuwapo tangu mwaka 1973 (Zanzibar), Tanzania Bara televisheni imeanza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Hadi 1996 kulikuwa na vituo vitatu tu vya televisheni: CTN, DTV na ITV. Kupingwa kwa televisheni Tanzania Bara na kuwapo kwa Radio moja (RTD) tokea miaka ya baada ya uhuru ulikuwa mkakati wa serikali kujenga utamaduni wa Umoja, Udugu na Utanzania.

Enzi hizo (nilikuwa bado mdogo) watu walikuwa wanakwenda kwenye majumba maalum ya sinema kuangalia sinema kwa wakati maalum na masharti maalum. Majumba haya yalikuwepo katika kila mji-makao makuu ya mkoa na baadaye katika wilaya, na idadi yake ilitegemea ukubwa wa mji.

Jul 1, 2015

Filamu zinaweza kutumika kama tiba

·         Lakini pia zinaweza kuacha athari ya kisaikolojia

Wapenzi wa sinema wakisubiri kuangalia sinema katika moja ya
maonesho ya sinema kwenye viwanja vya Tangamano, jijini Tanga
TUPENDE tusipende, nyakati hizi za karne ya 21 tunalazimika kutumia vyombo mbalimbali vya mawasiliano, kama magazeti, simu, redio, vinasa sauti, televisheni, filamu, mtandao, n.k. Vyombo hivi vimechangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuifanya dunia yetu kuwa ndogo sana. Tunaweza kuvitumia vyombo hivi kwa ajili ya kujielimisha na kujiburudisha ingawa kwa walio wengi, maendeleo ya vyombo hivi ni kama kitendawili. Kila wakati vyombo hivi vinakuwa vya teknolojia mpya na vya rahisi kutumia.

Jun 29, 2015

“Spec Scriptwriting”, uandishi wa filamu wenye changamoto nyingi

Waandishi mahiri wa script Tanzania, Dk.Vicensia Shule na
Bishop Hiluka, katika moja ya mikutano ya Bodi ya Filamu
Ikiwa una matumaini kuwa siku moja utakuja kufanya kazi ya uandishi wa script kwa ajili ya filamu au televisheni, basi unahitaji kuwa na ufahamu wa jinsi ya kuandika “spec” script. Spec Script ni kifupi cha Speculative script, huu ni uandishi wa filamu wa kubahatisha (speculation), ambao kama mwandishi unaandika script yako ukiwa hujui nani atakuja kutumia script hiyo – hii humaanisha kuwa unaandika script bure (pasipo kulipwa au kuajiriwa na mtu). Kwa maana nyingine ni kwamba hakuna mtu aliyekuajiri au anayekulipa kuandika script hiyo. 

Unaandika ukiwa na matumaini ya kuja kuuza kwa mnunuzi yeyote atakayevutiwa na kisa chako au kuajiriwa kwa ajili ya kuandika script kwa sababu ya hiyo, lakini ili kuwa na nafasi au uwezekano, huna uchaguzi bali kuandika spec script.

Jun 22, 2015

Sekta ya televisheni na mchango wa utamaduni

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel, akikata utepe kuzindua Tamthilia ya 'Doudou na Wakwe Zake' katika Viwanja vya TBC mwaka 2014
SEKTA ya Televisheni nchini kwa sasa imekuwa ni sehemu muhimu sana ambayo haiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya mwananchi, iwe mwananchi huyo anamiliki seti ya televisheni au la. Kwa kutazama vipindi mbalimbali vya televisheni mtu huweza kufahamu mambo mengi makubwa yanayoendelea nchini na hata nchi za nje, na kwa kutazama televisheni unapata burudani za kila aina.

Japo sekta ya televisheni nchini inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo kutokana na dunia kuingia zama za dijitali lakini pia ina changamoto kubwa. Kwa upande mmoja, maendeleo ya haraka ya dijitali yameiletea sekta hiyo fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina za uenezi wa habari zimekuwa nyingi, kwa mfano, televisheni kwenye mtandao wa internet, simu za mkononi zinaendelea haraka na makundi mengi ya televisheni ya nchi za nje yameingia kwenye soko la televisheni nchini, hali kama hiyo imekuwa shinikizo kubwa kwa sekta ya televisheni na filamu nchini.

Jun 17, 2015

Sekta ya Filamu duniani inahodhiwa na Wayahudi

Mtengeneza filamu wa Hollywood, Steven Spielberg
KATIKA zama zetu hizi, sinema ni chombo muhimu sana kinachotumiwa kueneza utambulisho, utamaduni na fikra. Mfano maalumu wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya sinema duniani ni uwekezaji wa Wamarekani na Waisrael (Wayahudi) katika sekta ya filamu. Wakati wengine wamelala, Wayahudi walifahamu mapema sana taathira ya sekta ya sinema na umuhimu wake katika propaganda na ili kuidhibiti sekta hii walitumia uwezo wao wote.

Katika miaka ya karibuni Serikali ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran wameonekana kuanza kuzinduka katika usingizi na kuanza kujipenyeza kwenye sekta ya filamu duniani ili kueneza utambulisho na tamaduni za Kiislamu dhidi ya tamaduni za Kimagharibi, lakini bado wana kazi ngumu sana kufuta alama zilizoachwa na sinema za Hollywood, chini ya udhibiti wa Israel na Marekani.

Waraka wa Bond Bin Sinnan, kwa Wasanii wa filamu Tanzania

Abdulrazaq Sinnan, maarufu kama Bond Bin Sinnan
Wasanii wa Bongo Movie wakiwasalimia wananchi waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, wakati wa kutangaza nia ya kugombea Urais kupitia CCM
Jina langu naitwa Abdulrazaq S.H. Sinnan ingawa asilimia kubwa ya Watanzania wananifahamu kwa jina la Bond Bin Sinnan kwa takribani miaka 15 sasa najishughulisha na masuala ya tasnia ya filamu nikiwa kama mtunzi, muigizaji, mzalishaji na muongozaji wa filamu. Hivyo nina upeo na uzoefu mkubwa wa tasnia ya filamu Tanzania. Naijua faida yake, matatizo yake na mengine mengi yanayoihusu tasnia hii.

Kwanza nianze kwa kuwapongeza sana wasanii wenzangu wa filamu nchini kutokana na kujituma kwetu mpaka tumefanya tasnia hii kuwa ajira kubwa kwa watanzania wengi sana. Vilevile tasnia hii imekuwa ni burudani kubwa kwa wana Afrika Mashariki na Kati kwani zaidi ya watu milioni kumi wanaangalia filamu za Kitanzania.

Jun 12, 2015

Sekta ya filamu inaendeleza ubaguzi dhidi ya wanawake


Mmoja wa waigizaji maaruf wa sinema za Hollywood, Angelina Jolie
Ripoti moja ya utafiti wa kwanza kufanyika duniani kuhusu wahusika wa kike katika filamu, umebainisha kuwa ubaguzi wa wanawake na wasichana umeenea mno katika sekta hiyo ya filamu. Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi Septemba mwaka jana imetokana na utafiti ulioidhinishwa na taasisi ya Geena Davis kuhusu Jinsia katika vyombo vya habari, ikisaidiwa na Shirika linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, pamoja na Wakfu wa Rockefeller.

Sir Christopher Lee, nyota wa filamu ya Dracula afariki

Moja ya scene alizocheza hayati Christopher Lee
Sir Christopher Lee
Mwigizaji wa siku nyingi na nyota wa filamu zilizopendwa na wengi, Sir Christopher Lee, amefariki akiwa na umri wa miaka 93. Msanii huyo ambaye jina lake kamili ni Christopher Frank Caradini Lee alizaliwa mnamo mwaka 1922, alikuwa mwigizaji wa filamu na mchekeshaji mzaliwa wa Uingereza aliyejenga jina lake kwa kuigiza katika filamu ya Dracula na Frankenstein katika filamu ya kutisha aligiza katika zaidi ya filamu 250.

Jun 10, 2015

Hadhi ya Sekta ya Filamu Tanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na marehemu Steven Kanumba
KUMEKUWEPO mjadala kama hali ya sasa katika soko la filamu linaweza kuitwa ‘sekta rasmi’ ambapo mitaji, mitambo na rasilimali zipo kila mahali. Hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana pasipo uwepo wa Sera ya Filamu. Sera ya Filamu ni hati nzuri inayoandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu na masoko.

Ni hati kuhusu hadhi na thamani ya sekta inayoonesha kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni, inayotambua kuwa Filamu ni njia ya kipekee ya mawasiliano, ni njia ya kuelimisha na kuburudisha, inayotuweka pamoja, kupashana habari na kuhamasishana.

Jun 6, 2015

Makundi mapya ya sanaa za maigizo yajirekebishe

Wasanii wa Kundi la Sanaa la ABY, Malapa Buguruni
Jacob Steven maaruf kwa jina la JB
Ni wazi kwamba huwezi kuzungumzia maendeleo yaliyopatikana kwenye tasnia ya filamu nchini bila kutaja Nyota Academia, Kaole Sanaa Group, Kidedea, Kidedea Original, Mambo Hayo na makundi mengine ya sanaa za maigizo.

Kimsingi makundi haya ndiyo yaliwaibua wasanii wakubwa nchini kama marehemu Steven Kanumba, Vicent Kigosi (Ray), Jacob Stephen (JB), Yvonne Cherry (Monalisa), Blandina Chagula (Johari), Jengua na wengine wengi ambao wanaendelea kuipeperusha vyema bendera ya filamu za Bongo ndani na nje ya Tanzania.

Jun 5, 2015

Hiroshi Koizumi, mwigizaji wa filamu za Godzilla afariki dunia akisumbuliwa na homa ya mapafu

Hiroshi Koizumi, enzi za uhai wake
Moja ya sinema za Godzilla
Hiroshi Koizumi, msanii wa Japan ambaye aliigiza katika filamu nyingi za Godzilla amefariki akiwa na umri wa miaka 88. Kulingana na ripoti, alifariki mjini Tokyo tarehe 31 Mei 2015, kutokana na homa ya mapafu (Pneumonia) katika hospitali ya Tokyo.

Koizumi aliigiza kama Godzilla katika filamu ya ‘Godzilla Raids Again’ ikiwa ni filamu ya kwanza ya Godzilla. Baadaye aliigiza katika filamu kadhaa za kutisha ikiwemo ‘Mothra’, ‘Godzilla vs The Thing’ na ‘Ghindorah and the Three headed Monster’.

Jun 3, 2015

Mitandao ya kijamii inaweza kuwa darasa muhimu sana kwa wanataaluma

Baadhi ya waandishi wa Skripti wanaounda "Scriptwriters Club", 
walipokutana kujadili changamoto zinazowakabili. Mwandishi wa 
makala haya, Bishop Hiluka (nyuma ya mwenye shati nyekundu) 
ni mmoja wao
MIMI ni shabiki mkubwa wa mitandao ya kijamii, hususan Facebook, Twitter, YouTube nk. napenda kutumia mitandao hii ili kutafuta taarifa mpya na ku-share uelewa wangu (knowledge). Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu ya kutuunganisha na watu – aidha kusikia au kutaka kusikika. Natambua nguvu ya mitandao ya kijamii katika kufikisha ujumbe, na huwa nafanya kila niwezalo kuitumia ili kufikisha sauti yangu isikike na hatimaye kuleta tofauti inayokusudiwa. 

Lakini tofauti na hivi, wengi hawaitumii mitandao hii ipasavyo, ndiyo maana mimi si shabiki wa makundi (groups) yaliyopo kwenye mtandao wa WhatsApp, si shabiki kwa kuwa makundi mengi ya WhatsApp ni kama vijiwe vya porojo, hayana dira wala malengo, mara nyingi kinachofanyika ni kupiga porojo zisizo na maana.

May 27, 2015

Wasanii wanapokubali kutumika kisiasa!

Bishop Hiluka, Simon Mwakifwamba na Michael Sangu
wakati wa harakati za kupigania ukombozi wa msanii
HISTORIA huwa haina haja na wale wote wenye kushindwa, labda tu kunukuu tarehe walizokutwa na umauti wao... Sekta ya filamu Tanzania ambayo ilionekana kupiga hatua siku hadi siku, siku za karibuni imeonekana kuanza kudorora. Ipo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Ni ukweli usiopingika, sekta ya filamu ipo chumba cha wagonjwa mahututi ikisubiri kupelekwa mochwari, hasa kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kunusuru hali hii, hali ambayo kwangu ni kama mazingaombwe.

May 13, 2015

Kuna nini Sekta ya Utamaduni?

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, 
Dk. Fenella Mukangara
MUUNDO wa uendeshaji wa sekta au shughuli yoyote hutokana na azma ya kushughulikia matatizo yaliyopo. Muundo huo huwa ni nyenzo ya awali kabisa ya kutatua matatizo hayo. Kwa hiyo idara na sehemu zinazoundwa katika asasi na aina ya wataalamu wanaoajiriwa huzingatia majukumu na kazi za asasi ile katika muhula husika.

Ingawa Sekta ya Utamaduni imekuwa katika mfumo wa serikali tangu 1962, nafasi yake katika maendeleo ya taifa bado haijatambuliwa kikamilifu. Mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inaaminika kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

May 6, 2015

SEKTA YA FILAMU: Kenya inapiga hatua wakati sisi tunasinzia

Gavana wa Kaunti ya Machakosi, Alfred Mutua
SEKTA ya Filamu nchini Kenya imetajwa kama sekta muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa nchi hiyo, hasa katika kuvutia watalii na kutoa nafasi za ajira kwa vijana wa Kenya. Lakini sekta hiyo kwa muda mrefu imekosa wafadhili wa kuiwezesha kufikia kiwango hicho na kuendelea kubaki nyuma huku sekta zingine kama utalii zikinawiri.

Sasa sekta hii imeanza kupiga hatua kubwa baada ya kupigwa jeki na hazina ya vijana nchini humo, ambayo ilitenga kiasi cha shilingi milioni 300, ili zitumiwe na vijana kwa njia ya mikopo katika kuijenga sekta hiyo na kuiimarisha nchini kote. Kwa miaka sasa sekta hii ya filamu nchini Kenya imekuwa iking'ang'ana kujikita, lakini isiwezekane.

Apr 22, 2015

Tunahitaji mapinduzi ya kweli ya sekta ya filamu Tanzania

Simon Mwakifwamba, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania
Dilesh Solanki, Mkurugenzi wa Kampuni ya Steps Entertainment
HALI ya tasnia ya filamu nchini kwa sasa inakatisha tamaa, wasanii na viongozi wao wengi wamefikia ukomo wa kufikiri, wanaonekana kuridhika na hali ilivyo au pengine wamekata tamaa, ingawa bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi. Vyombo vya kuwasimamia, likiwemo Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), vimekosa dira.

Ni wasanii wenyewe kupitia chombo chao, ndiyo wamesababisha sekta hii ishuke kutokana na tabia zao, hii inawagusa wasanii wote, wanawake na wanaume. Wamechukulia kada hii kama sehemu ya kujitangaza zaidi kuliko kazi, viongozi wao wanachukulia nafasi zao kama fursa ya kuwakutanisha na wakubwa au matajiri ili wapige vibomu, ilimradi siku ziende.

Feb 4, 2015

Dunia na historia ya filamu

D. W. Griffith

Muongozaji wa filamu Tanzania, John Lister Manyara
SINEMA za mwanzo zilijielekeza kama vile sehemu ya jukwaa mbele ya pazia. Kamera iliwekwa katika sehemu moja na matendo yote katika tukio zima yalifanyika ndani ya fremu moja ya kamera na kwa pigo moja (one shot). Mtazamo wa watazamaji kipindi hicho haukutofautiana na watazamaji ambao leo wanakaa mbele ya jukwaa wakiangalia maigizo ya jukwaani. Ni D. W. Griffith, aliyekuwa wa kwanza kuwahamishia watazamaji katika ulingo wa sinema kwa kazi zake za “For Love of Gold (1908)”; “The Lonely Villa (1909)”; “The Lonedale Operator (1911)”; na iliyovutia zaidi, “Birth of a Nation (1915)”.

Jan 1, 2015

Mwaka 2014 umeshuhudia vifo mfululizo vya wasanii

* Wapo waliohusisha vifo hivi na kafara

Marehemu George Otieno Okumu "Tyson"

Marehemu Adam Phillip Kuambiana
 TUMEINGIA mwaka mpya 2015 tukitaraji mafanikio makubwa zaidi na tukiuaga mwaka 2014 uliokuwa wa simanzi kwa tasnia ya filamu tulipokumbwa na taharuki kufuatia vifo vilivyotokea mfululizo vya wasanii wa filamu vilivyotokea katika muda mfupi mfupi. Kufuatia vifo hivyo tetesi zilienea mitaani kwamba vifo hivyo vilitokana na kutoana kafara!