Jul 14, 2015

Benson Wanjau Karira (Mzee Ojwang Hatari) afariki dunia

Benson Wanjau Karira maarufu kama Mzee Ojwang Hatari

Muigizaji mkongwe wa vichekesho nchini Kenya, Benson Wanjau Karira maarufu kama Mzee Ojwang Hatari, amefariki dunia siku ya Jumapili usiku katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta alipokuwa amelazwa.

Mzee Ojwang wakati akichukuliwa vipimo vya macho

Mzee Ojwang alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu (Pneumonia). Muigizaji huyo ambaye alikuwa kinara katika vipindi vya Vitimbi, Vioja Mahakamanii, Vituko na Kinyonga, pamoja na kazi nyingine, alikuwa hajaonekana kwenye televisheni kwa muda mrefu.


Gwiji huyo wa vichekesho ambaye alikuwa mmoja wa wachekeshaji maarufu sana wa Kenya, awali alilazwa katika hospitali ya Loresho katikati ya mwezi Machi wakati akitibiwa tatizo la kupoteza uwezo wa kuona. 

Machi 10 mwaka huu, Kikundi cha Vitimbi kikiongozwa na Mary Khavere maarufu kama Mama Kayai, kilimtembelea Meya wa Nairobi, Mike Sonko, ofisini kwake kuomba msaada katika kumhudumia Mzee Ojwang hospitalini.

Ugonjwa wake uliifanya serikali kujitokeza kulipa gharama zake za matibabu huku Waziri wa Habari, Fred Matiagi, akisema serikali itaangalia maslahi ya Kikundi cha Vitimbi.

Mzee Ojwang alisoma katika Shule ya Misheni ya Kanisa la Pumwani ambapo alifanya mtihani wake mwaka 1952. Baadaye alijiunga na masomo ya juu katika Shule ya Kagumo.

Kwa miaka 35, Mzee Ojwang Hatari alikuwa akiigiza vichekesho katika televisheni yaa Kenya, KBC.  

Kwa mara ya kwanza alijiunga na sekta ya filamu alipokuwa na miaka 34. Ilikuwa katika miaka ya 1970 na alikuwa ndo kwanza amemaliza shule na kuanza kazi katika duka. Aliacha kazi na kujiunga na Hospitali ya Mater kama fundi msanifu (technician) lakini baada ya miaka minne alijikuta akijiingiza kwenye masuala ya burudani, hivyo kuutumia muda wake wa mapumziko kufanya maigizo.

Mwaka 2009, wasanii wa Vitimbi walipewa tuzo wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Kalasha. Mwaka uliotangulia, Mzee Ojwang alikuwa ametambuliwa na Wakenya kama mchekeshaji aliyeaminika zaidi miongoni mwa wachekeshaji nchini Kenya.


Mzee Ojwang aliwahi kubainisha kuwa anapenda fani ya uigizaji, na ataendelea kuigiza katika maisha yake yote. Alioa na alikuwa na watoto wawili.

No comments: