Jul 29, 2015

TAMASHA LA 18 LA ZIFF: Tutumie fursa kama hizi kwa ajili ya kujitangaza na kujifunza zaidi

Mkongwe, Dorothy Masuka, akiwa jukwaani katika shoo yake usiku wa Julai 19, katika tamasha la 18, la ZIFF 2015,Ngome Kongwe upande wa Mambo Club

MATAMASHA ya filamu duniani ni sehemu nzuri zaidi kwa ajili ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji wa filamu au msanii kujulikana si tu katika kanda husika bali kimataifa.

Mkurugenzi wa ZIFF, Prof. Martin Mhando
Ukibahatika kuwa mmoja wa washindi wa tuzo, unakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujitangaza na hata kupata msaada wa kipesa (funds) kwa ajili ya kutengeneza sinema bora zaidi unayohitaji siku zote kwa kuwa utaingia kwenye orodha ya watu wanaoaminiwa, na hapo ndo’ washindi hujua kuwa wapo katika mstari sahihi.



Hivi karibuni Tamasha la 18 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) limemalizika katika uwanja wa Mji Mkongwe Zanzibar. Wasanii kutoka ndani na nje ya Tanzania na pamoja na watalii wamejumuika kwa ajili ya tamasha hilo.

Tamasha hilo lenye kaulimbiu "Mawimbi na Matumaini" limefanyika kwa siku tisa, ambapo filamu 99 zilizotengenezwa na waandaaji 65 kutoka nchi 35 zimeoneshwa. Hatimaye, makundi matano ya waamuzi yakatoa tuzo 22 kwa filamu bora.

Tamasha hilo lilifunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

Kwenye ufunguzi huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilibainisha kuwa itaendelea kuunga mkono  juhudi zinazochukuliwa na Uongozi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi  Zanzibar (ZIFF) katika azma yake ya kuijengea nguvu tasnia ya Filamu Nchini inayoonekana kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya Utalii.

Hayo yalikuwemo katika Hotuba ya Dk. Ali Mohammed Shein iliyosomwa kwa niaba yake na Balozi Seif Ali Iddi, wakati akilizindua Tamasha la 18 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar.

Dk. Shein  alisema kwamba Tamasha la Nchi za jahazi limekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza Zanzibar Kimataifa hali ambayo imetoa ushawishi kwa wageni na watalii wengi kuamua kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar kujionea mazingira na rasilmali zilizopo.

Alisema kupitia Tasnia ya filamu zinazotayarishwa na wasanii mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa Fani hiyo chini ya Wataalam wa Ziff wageni na watalii mbalimbali Duniani wamekuwa wakivutiwa na fukwe pamoja na Utamaduni uliojaa ukarimu wa Watu wa Visiwa vya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa ZIFF kuendelea kufanya juhudi zaidi za kuwashawishi wasanii wa Kimataifa kuzitumia Fukwe na Tamaduni za Zanzibar katika kutengeneza Filamu mbalimbali kwa lengo la kuitangaza zaidi Zanzibar Kimataifa.

“Zanzibar ni Visiwa vya maumbile ya Utamaduni ya Ukarimu pamoja na fukwe za kuvutia mambo ambayo yakitangazwa vyema wasanii wa Kimataifa wanaweza kushawishika kuyatumia katika kutengeneza Filamu zao”. Alifafanua Dk. Shein.

Alifahamisha kwamba Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi, Tamasha la Iddi, Tamasha la Mzanzibari pamoja na Sherehe za Mwaka Kogwa zinazofanyika Makunduchi ni Mambo muhimu yanayopaswa kuimarishwa katika kukuza na kusimamia Utamaduni na Historia ya Zanzibar na Watu wake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewapongeza Wasanii wa Maigizo pamoja na Filamu Nchini kutokana na kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuelimisha Jamii sambamba na kuwapatia Burudani.

Alisema mbali ya Tasnia hiyo kutoa ajira pana kwa kundi kubwa hasa Vijana Nchini lakini pia imepanua soko la filam za nyumbani na kuleta unafuu kwa kila mtu kumudu kununua na kuangalia kazi za wasanii wa hapa Nchini hali iliyopelekea kufikia asilimia 80 ya filamu za Kiswahili zinazoangaliwa tofauti na miaka iliyopita nyuma.

Mratibu wa tamasha hilo, Prof. Martin Mhando, amesema ameitumia fursa iliyopo kuhimiza maendeleo ya tamasha hilo.

“Tamasha la filamu la Kimataifa la Zanzibar ni shughuli muhimu katika historia ya Zanzibar, ambayo haiwezi kusahauliwa. Kaulimbiu ya mwaka huu ni Mawimbi na Matumaini. Kama tunavyojua, tunaishi kisiwani Zanzibar, tunakabiliana na mawimbi yanayotoka kwa pande mbalimbali.

“Natumai kuhimiza maendeleo ya tamasha ya filamu na nchi yetu kupitia mawimbi ya tamasha la ZIFF. Leo sote tunavaa mavazi meupe, ambayo yanamaanisha nchi yetu ni nchi yenye amani na utulivu zaidi barani Afrika na kote duniani. Karibuni ZIFF, karibuni Zanzibar, asanteni.”

Mwaka huu siku ya ufunguzi wa tamasha la ZIFF iligongana na sikukuu ya IDD, kwenye hotuba yake, mwenyekiti wa tamasha la ZIFF, Mahmoud Kombo alisema, kukutana kwa shughuli hizo mbili kunawavutia watalii wengi zaidi, ambako kuna maana kubwa kwa ustawi wa utamaduni na uchumi wa Tanzania.

“Leo ni Julai 18, na ZIFF imetimiza miaka kumi na nane. Na leo pia tunasherehekea sikukuu ya Idd hapa Zanzibar. Tamasha la ZIFF kila mwaka linawavutia watalii zaidi ya elfu nne kutoka nchi mbalimbali duniani, leo pia ni sikukuu ya Idd hapa Zanzibar, nina imani kuwa mwaka huu watalii wengi zaidi watakuja hapa.

“Hivyo ZIFF inaweza kustawisha utamaduni na uchumi wa nchi yetu, na kuwafanya marafiki wengi zaidi kufahamu nchi na utamaduni wetu. ZIFF imepita miaka 18, ambayo inawafanya marafiki wengi kuifahamu Zanzibar yenye mandhari safi na kuipenda. Nafikiri nyote mtaona uzuri wa Zanzibar”

Baadhi ya nchi zilizowasilisha filamu kwenye mashindano ni Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Marekani, Ujerumani na Ufaransa. Mratibu wa tamasha hilo, Prof. Mhando, amesema filamu zinazohusiana na kupambana na ubaguzi wa rangi zimepewa kipaumbele katika tamasha hilo. Filamu ya Selma kutoka Marekani, Sarafina kutoka Afrika Kusini, Samaki Mchangani kutoka Tanzania na Septemba kutoka Kenya zote zinahusu mada hiyo.

Kati ya filamu zilizoshiriki kwenye tamasha hilo, 16 zimetengenezwa nchini Tanzania. Prof. Mhando amefurahia kuona tamasha hilo linastawisha soko la filamu la Tanzania, kuhimiza maendeleo ya utengenezaji wa filamu Tanzania, na kutoa fursa nyingi zaidi kwa Watanzania kutazama filamu kutoka nchi mbalimbali duniani.

Katika ufunguzi, watalii wengi kutoka nchi mbalimbali duniani walikuja hapa, Bibi Rose kutoka Uholanzi ni mmojawapo ambaye alikuwepo siku ya ufunguzi.

“Naitwa Rose, natoka Uholanzi. Leo tamasha hili linafunguliwa. Tamasha hili linavutia sana, kwa sababu linahusu utamaduni na filamu, hapa kuna filamu, muziki na sanaa kutoka sehemu mablimbali duniani. Naona kuna umuhimu mkubwa wa kufanya tamasha la filamu ambalo linawashirikisha watu wengi kutoka nchi mbalimbali, na wengi wao wamekuja kwa ajili ya tamasha hilo.

“Tamasha la filamu linaunganisha marafiki kutoka Afrika na sehemu nyingine duniani. Nilikuwa nadhani Afrika ni sehemu maskini, lakini leo mawazo yangu yamebadilika. Naona tamasha la filamu litawapatia watu wengi ufahamu mpya kuhusu Tanzania.”

Katika tamasha hilo, filamu za Tanzania zilizoshinda ni kama ifuatavyo: Mr. Kadamanja – Chaguo la Watu (People’s Choice Award); Samaki Mchangani – Sinema yenye Sauti Bora (Best Film in Sound); Daddy’s Wedding – Mpiga Picha Bora (Best Cinematography); na Kutakapokucha – Filamu Bora (Best Feature Film).

Wasanii wa Tanzania walioshinda ni Jokate Mwegelo – Muigizaji Bora wa Kike (Best Actress) kupitia filamu ya Mikono Salama; na Marehemu Adam Kuambiana – Muigizaji Bora wa Kiume (Best Actor) kupitia filamu ya Mr.Kadamanja. Pia Tuzo ya Muongozaji Bora (Best Director) imekwenda kwa Honeymoon Mohammed kupitia filamu ya Daddy’s Wedding.

No comments: