Nov 26, 2014

Uandishi bora wa Filamu: Tuanze kuwafundisha watoto jinsi ya kuandika script

Magdalena Hiluka, akiwa na miaka 4 wakati huo. Inashauriwa 
kumpa hamasa mtoto katika umri mdogo ili kujenga kipaji chake 


Tangazo (poster) la filamu ya Mke Mchafu.

NIANZE makala yangu kwa kumpongeza Mtayarishaji na Muongozaji wa filamu nchini, John Lister Manyara, kwa sinema yake “MKE MCHAFU” ambayo ni sinema pekee ya Tanzania iliyokubalika kuoneshwa kwenye ndege za Shirika la Ndege la Emirates. Haya ni mafanikio makubwa. Sinema hii imewashirikisha waigizaji maaruf wa Tanzania; Zuberi Mohammed (Niva), Hisan Muya (Tino) na Blandina Chagula (Johari) na wengineo, imeongozwa na John Lister na mimi (Bishop Hiluka) ndiye niliyeiandika. Mafanikio ya sinema hii yananihusu kwa kiasi kikubwa.

Nov 7, 2014

TAFA AWARDS: TUZO KUBWA ZA FILAMU TANZANIALogo ya Tuzo za Filamu Tanzania (TAFA)
Shirikisho la Filamu Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Binary & Pixels wameanzisha Tuzo za Filamu nchini Tanzania zinazotazamiwa kuwa Tuzo kubwa zaidi kuwahi kutolewa. Kuanzia 1 Novemba hadi 30 Novemba 2014 ni kipindi cha watayarishaji na wasanii kutuma/kupeleka kazi zao kwa ajili ya kuwania Tuzo hizi. Fomu zinapatikana kwenye ofisi za TAFF au kwenye website ya Shirikisho hili: GONGA HAPA

Oct 18, 2014

Uongozaji si kujua ‘action’ na ‘cut’ tu, unatakiwa pia kuijua lugha ya filamuMmoja wa waongozaji filamu nchini, Issa Mussa maaruf kama Cloud 112

SINEMA za mwanzo zilijielekeza kama vile sehemu ya jukwaa mbele ya pazia. Kamera iliwekwa katika sehemu moja na matendo yote katika tukio zima yalifanyika ndani ya fremu hiyo ya kamera kwa pigo moja (one shot). Mtazamo wa watazamaji enzi hizo haukutofautiana na watazamaji ambao leo wanakaa mbele ya jukwaa wakiangalia mchezo wa kuigiza wa jukwaani.

Muongozaji wa Kimarekani, D. W. Griffith, ndiye alikuwa wa kwanza kuwahamishia watazamaji katika ulingo wa sinema kwa kazi zake kama “For Love of Gold (1908)”, “The Lonely Villa (1909)”, “The Lonedale Operator (1911)”, na ile iliyovutia zaidi, “Birth of a Nation (1915)”. Grifftith alikuja na mbinu kabambe za kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi zake.

Siku hizi tuna vichekesho au mizaha?


Wachekesha maaruf nchini, marehemu Hussein Mkiety (Sharomilionea) na Amri Athuman maaruf KIng MajutoNILISHANGAA binti yangu, Magdalena, 10, aliposema siku hizi hapendi kuangalia comedy za Tanzania akidai hazichekeshi. Comedy ni neno la Kiingereza lenye asili ya Ugiriki likimaanisha futuhi au ucheshi kwa Kiswahili. Ni vichekesho vyenye lengo la kufurahisha, kufundisha na kuburudisha watazamaji, katika televisheni, filamu, na kwenye majukwaa. Unapocheka ndivyo maisha yanavyokua bora zaidi!

Ucheshi ni mwanga unaouangazia moyo, ni igizo lililobuniwa kuchekesha, kuburudisha, na kumfanya mtu astarehe. Muundo wa ucheshi ni kuzidisha hali ya mambo ili kuleta uchekeshaji, kwa kutumia lugha, matendo, na hata wahusika wenyewe. Ucheshi huhoji na kufuatilia yalipo mapungufu, makosa au hitilafu, na vitu vinavyokatisha tamaa ya maisha, na kuleta uchangamfu na wasaa wa kufurahia maisha.

Sep 13, 2014

Unachokiandika kinakutafsiri ulivyo


 
IMEANDIKWA, “Kila siri iliyo moyoni kwa mwandishi, kila aina ya maisha aliyoyapitia, au kipimo cha akili ya mwandishi vimeainishwa kwa kiasi kikubwa katika maandishi yake...” hii inamaanisha kuwa kazi za kimaandishi za waandishi huwaonesha wao ni kina nani, wametokea mazingira gani, wana uwezo gani wa kufikiri na wanataka kuwa nani.

Kupitia kujielewa wenyewe na kuridhika katika uasili wetu, mchakato wa kuandika huwa unakuwa wa hiari zaidi na hauzuiliki. Tunapoelewa kuwa tuna talanta (kipaji) ya kipekee ya uandishi tuliyotunukiwa na Mungu, inatusaidia zaidi katika kuandaa makala au hadithi nzuri.

Aug 21, 2014

Filamu zetu zinaharibiwa na waongozaji


·         Wengi hawana sifa zinazohitajika na hawataki kujifunza
UKWELI tuna tatizo kubwa kwenye tasnia ya filamu Tanzania kwa waongozaji wengi kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: “standby... action... cut!” na kusahau kuwa muongozaji ndiye anayepaswa kumtengeneza muigizaji aweze kuuvaa uhusika ipasavyo kwa kutegemea script ilivyo. Kama muigizaji atashindwa kuvaa uhalisia, mara nyingi hilo siyo kosa lake bali ni kosa la muongozaji kwa kushindwa kumtengeneza, na hutafsiri uwezo wa muongozaji ulipokomea.

Mtazamo wangu, mtu yeyote anayetaka kuwa muongozaji mzuri wa filamu katika tasnia yetu anapaswa kujifunza kwa makini hatua kwa hatua kwa kusoma machapisho na kuhudhuria warsha na mafunzo ya muda mfupi — si kwa ajili ya kujifunza njia nzuri ya utengenezaji wa filamu, bali kwa ajili ya kupata msukumo wa kufuatilia masuala muhimu ya uumbaji wa kisanii kwa bidii na kwa umakini.

Jun 25, 2014

USHINDI WA SHOESHINE FESTICAB: Kwanini hatutilii maanani filamu fupi?

 Amil Shivji


TAKRIBAN wiki mbili zilizopita nilikuwa mjini Bujumbura nchini Burundi kwa mwaliko wa Shirika la Kijerumani la GIZ, ambapo Mtandao wa Wanafilamu wa Afrika Mashariki ulikuwa ukizinduliwa rasmi, sambamba na Tuzo za filamu kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu la Burundi (Festicab) 2014, linalofanyika jijini Bujumbura.Kabla ya safari yangu hii, nilipata bahati ya kupitia nchi zingine kama mbili ambapo nilipata nafasi ya kukutana na watengeneza filamu wa nchi hizo, na kwa kweli nilijifunza mengi kutoka kwao.

Jun 16, 2014

HARAKATI ZA TAFF: Serikali, sikieni kilio chetu kwa mustakabali wa TaifaKatibu Mkuu wa TAFF, Bishop Hiluka, akitoa ufafanuzi katika warsha ya wadau wa sanaa nchini, iliyofanyika kwenye hoteli ya Chichi, Kinondoni B, jijini Dar es Salaam hivi karibuni
 
HEBU jaribu kupata picha: umelima shamba lako na kupanda mahindi ambayo umeyatunza vizuri na yako tayari kuvunwa… unaamka siku moja na kukuta kuna mtu kayavuna na ameanzisha biashara inayompatia fedha nzuri wakati wewe uliyelima huna hata fedha ya kula! Au umenunua suti nzuri akaja mtu akaivaa harusini, kesho yake anakuja kukutaarifu jinsi walivyomsifia harusini kwa kupendeza na suti yako. Hiyo ndio picha ilivyo katika shughuli za sanaa Tanzania. Na haswa katika mambo ya filamu.

Katika mifano hii midogo moja kwa moja unapata picha halisi ya kile kinachoendelea kwenye tasnia ya filamu na hata sanaa zingine hapa nchini, ambayo tunaweza kuiita kuwa ni shamba la bibi, kwani kila anayejisikia anaingia, anavuna tani yake na kufaidi mazao pasipo kulima.

Jun 11, 2014

Wasanii wanajifunza nini kwenye vifo mfululizo vya wasanii wenzao?

Marehemu Said Ngamba maaruf kwa jina la Mzee SmallKWANZA naomba nianze kwa kutoa pole kwa familia nzima ya wasanii na wadau wa filamu nchini kufuatia vifo mfululizo vya wasanii wa filamu ndani ya wiki tatu; Adam Kuambiana, Rachel Haule, George Otieno “Tyson) na Said Ngamba maarufu kama Mzee Small. Mfululizo wa vifo hivi umeambatana na uvumi au dhana potofu inayosambaa kwa kasi, eti vifo mfululizo vya wasanii vinatokana na kafara inayofanywa na baadhi ya wadau (wasanii) ndani ya tasnia ya filamu kwa lengo fulani lenye maslahi kwao.

Uvumi huu umejitokeza hasa baada ya kushuhudia kundi la watu fulani likiwa ndiyo kinara wa kukumbatia misiba ya wasanii nyota, kuunda kamati mbalimbali na kuchangisha fedha nyingi ambazo baadhi yake zimekuwa zikitumika kununulia majeneza ya bei mbaya, vyakula vya gharama (utadhani kuna sherehe) na shughuli zingine ikiwemo ukodishaji wa magari ya kusindikiza msafara wakati wa mazishi. Lakini kama hiyo haitoshi, kumeripotiwa pia kufanyika kwa ubadhirifu wa pesa.

May 31, 2014

Kudumaa kwa Sekta ya Filamu Tanzania kunatokana na kukosa muongozo

Naibu Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, 
Juma NkamiaAlhamisi wiki hii, Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilisoma bajeti yake ya mwaka 2014/15 na kuweka vipaumbele vyake. Lakini pamoja na kuigusa sekta ya filamu bado imekuwa haipewi kipaumbele japo imeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajira na pato la Taifa.

Tanzania ni moja ya nchi chache zenye maeneo mazuri ya kuvutia yanayofaa kabisa kwa kutengenezea filamu, ni nchi yenye wasanii wengi wazuri wenye vipaji lakini waliokosa muongozo. Tasnia ya filamu na muziki nchini ni sekta tajiri sana lakini zisizopewa kipaumbele.

May 14, 2014

Kwa hili la kukaa mezani na kuutazama upya mfumo unaofaa, naipa tano Serikali

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akizungumza Bungeni


KATIKA jitihada za kuhakikisha kuwa wasanii hapa nchini Tanzania wanatengenezewa mazingira mazuri zaidi ya kufaidika na kazi wanazotengeneza, Serikali imetoa maagizo kwa Chama Cha Hatimiliki Tanzania, COSOTA na Mamlaka ya Mapato nchini, TRA, kukutana ndani ya siku tano za kazi kuanzia sasa. Mpango huu ni kwa ajili ya kutengeneza makubaliano juu ya mfumo utakaofaa kwa ajili ya kukusanya na kudhibiti mapato ili kuboresha faida kwa wasanii na serikali.Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, alitoa kauli hiyo bungeni ambapo alitaka waangalie namna ya kuboresha stempu/stika zinazobandikwa katika kazi za wasanii ili badala ya kutumika kukusanya ushuru peke yake zitumike pia kulinda kazi za wasanii hao.

Apr 30, 2014

Nollywood na mchango wa uchumi Nigeria, Tanzania na upuuzaji wa sekta ya hakimiliki

Desmond Eliot, msanii wa Nollywood

HIVI karibuni Nigeria imetangazwa kuwa ndilo Taifa lenye uchumi mkubwa barani Africa na kuipita Afrika Kusini. Pato Ghafi la Ndani (Gross Domestic Product ‘GDP’) la Nigeria limefikia Dola Billion 509 huku lile la Afrika ya Kusini likifikia Dola Bilioni 322.

Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Nigeria, Nigeria imekuwa Taifa lenye uchumi mkubwa Afrika baada ya wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za Mawasiliano na Filamu (Nollywood) kwenye takwimu. Ni dhahiri kuwa soko la Filamu la Nigeria linatoa mchango mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Nigeria ilionekana kama taifa linalotegemea zaidi uuzaji wa mafuta na ilikadiriwa kuwa pato la mafuta lilichangia asilimia 32 kwenye GDP lakini ripoti ya wanauchumi hivi karibuni imeonesha sasa pato la mafuta huchangia Asilimia 15 tu ya pato ghafi la ndani.

Mar 25, 2014

MATOKEO YA UBINAFSI NA UMIMI: Msanii awabeza wasanii wenzake...

*Haya ni matokeo ya kupoteza dira kama Taifa
Viongozi wa Mashirikisho la Sanaa wakiwa pamoja na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Paul Mtendah (wa pili kushoto) na Maria Sarungi (wa tatu kushoto), kwenye hoteli ya Dodoma, kabla ya vikao vya Bunge kuanza


WIKI iliyopita kwenye gazeti moja litolewalo kila siku (ambalo limetoka kifungoni hivi karibuni) kulikuwa na makala ya mwandishi mmoja ambaye pia ni msanii aliyesomea taaluma ya sanaa katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, iliyobeza juhudi zinazofanywa na wasanii hivi sasa kupigania kutajwa kama mojawapo wa kundi muhimu kwenye Katiba ya nchi. Makala hayo yaliyojikita katika kile ambacho mwandishi huyu (nitamtaja zaidi kama msanii) alidai kuwa wasanii wenzake wamekumbuka shuka wakati kumekucha, kiasi cha kuzua mjadala mkubwa kwenye mtandao wa kijamii wa facebook.

Mar 5, 2014

KATIBA MPYA: Wasanii kazeni uzi, mmeshatumiwa sana

Kikosi Kazi cha wasanii 12 kilichokwenda Bungeni Dodoma kuonana na Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa katika picha ya pamoja na Mh. Samwel Sitta

IMEKUWA ni kawaida kila wakati wa uchaguzi kuona wasanii wakitumika kuvuta watu wakati wa mikutano ya kampeni za wagombea urais, ubunge na hata udiwani. Hutumiwa kuwavuta watu ili wafike kwenye mikutano hiyo kabla ya wanasiasa kuanza kampeni zao za kutaka kuungwa mkono.

Pindi wanasiasa wanapopata madaraka wamekuwa hawawakumbuki tena wasanii hadi pale uchaguzi mwingine unapokaribia. Hili ni jambo linalokatisha tamaa, na limeendelea kujitokeza hata sasa wakati tukiwa kwenye mchakato wa kutafuta Katiba mpya itakayotuongoza kwa miaka mingine hamsini baada ya uhuru, ambapo vikao vya Bunge Maalum la Katiba vimeanza mjini Dodoma tangu Februari 18, mwaka huu.

Wanasiana wameonekana kupeleka nguvu zao kwenye masuala ya kisiasa kama muundo wa serikali na masuala yenye maslahi ya kisiasa na kusahau mambo mengine muhimu ya kijamii, ikiwemo suala la wasanii ambao hutumika kama kivutio cha kuwavuta wapigakura kuja kwenye mikutano kusikiliza sera za vyama.

Hivi karibuni timu ya wasanii kumi na mbili ilikwenda Dodoma kuongea na Wajumbe wa Bunge la Katiba ili kuwashawishi kuingiza vipengele viwili muhimu kwenye katiba ya nchi baada ya Tume ya Katiba kuyapuuza maoni yao. Wasanii kupitia Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa waliunda Baraza la Katiba ambapo Mashirikisho yalitoa mapendekezo kadhaa yaliyofikishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Pamoja na mapendekezo hayo kupokewa lakini hakukuwepo na jambo lolote lililotokana na mawazo hayo (pamoja na uzuri wake) lililochukuliwa na kuingizwa kwenye rasimu ya Katiba.

Kumekuwepo na kasumba ya kuendelea kuitambua sekta ya sanaa kama ni sehemu ya utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential).

Kwa mujibu wa utafiti wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wa mwaka 2006 unaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na wasanii milioni 6. Sasa ni miaka saba imeshapita na kwa vyovyote idadi hii itakuwa imeongezeka mara dufu hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia imekuwa sana na asilimia 60 ya Watanzania ni vijana.

Ninapozungumzia wasanii namaanisha watu wote wanaofanya kazi za sanaa na ubunifu, na si kama wengi wanavyodhani kuwa ni wale wanaoigiza au kuimba tu. Sanaa kwa sasa ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika la Hakimiliki la Kidunia (WIPO) ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato uliotokana na shughuli za Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini. Pia mchango wa ajira katika kazi zilizotokana na Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii. Pia wasanii ndiyo wamekuwa wakilipa jina na utambulisho Taifa hili.

Hivyo, inashangaza kuona kuwa Rasimu ya Katiba imetambua uwepo wa makundi mbalimbali kama wakulima, wavuvi, wafanyakazi, wafugaji nk. lakini ikashindwa kutambua uwepo wa kundi kubwa la wasanii!

Kwa takwimu hizi utagundua kuwa wasanii ni kundi kubwa sana linaloyazidi makundi mengine huku likizidiwa na kundi moja tu la wakulima, pia ni kundi linalochangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi, hivyo kutolitambua ni makosa. Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Hakimiliki la Dunia (WIPO) wa Septemba 2012, sekta ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 4.275.

Kwa kutambua jambo hilo, Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) likishirikiana na Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (TAMUNET) waliunda Kikosi Kazi cha watu 12 na kwenda Dodoma kupigania mambo makuu mawili.

Kwanza wasanii kutajwa na kutambuliwa katika Katiba mpya kuwa ni kundi rasmi kutokana na ukubwa wa kundi hili nchini, kama yalivyotajwa makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi na kadhalika, pia mchango wake katika ajira ya vijana na ukubwa wa pato linalotokana na kundi hili, ambalo kutokana na kutokutambuliwa linapotelea katika mifuko ya watu na kukosesha wasanii na Taifa pato kubwa.

Kikosi Kazi hiki pia kilitaka ubunifu ulindwe kwanza kwa ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) kutajwa rasmi katika katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi zao uweko kama ilivyo katika mali nyingine za wananchi wengine. Kwenye Rasimu ya Katiba imetajwa ulinzi wa kazi zinazohamishika na zisizohamishika lakini mali zisizoshikika (za ubunifu) hazikutajwa.

Milikibunifu ni mkusanyiko wa haki mbalimbali anazopewa mbunifu. Wasanii hulindwa na Hakimiliki ambayo ni sehemu tu ya Miliki Bunifu. Kampeni ya wasanii kuhusu hili la Intellectual Property (IP) kutajwa katika katiba ni kuwa katika Katiba kumetajwa ulinzi wa mali zinazohamishika na zisizohamishika, lakini mali zisizoshikika zinazotokana na ubunifu hazikutajwa na ndiyo maana pamoja na sheria kuweko, serikali huzilinda hizo kama fadhila.

Nchi kadhaa hutajwa kuwa zilikuwa na uchumi sawa na Tanzania wakati nchi yetu ikipata uhuru wake mwaka 1961, zikiwamo Singapore, Korea Kusini, Thailand, Malaysia na kadhalika, na kilichowafanya kutuacha kimaendeleo na kupata maendeleo ya haraka ni ulinzi na uendelezaji wa Miliki Bunifu na ndiyo maana leo kuna Samsung, Hyundai, LG, Daewoo nk. Suala hili la Miliki Bunifu ni pana zaidi ya sheria ya copyright ambayo nayo kutokana na spidi ya teknolojia hujikuta ikipitwa na wakati kila baada ya muda mfupi, ni muhimu kuwa katika sheria mama (Katiba) ambayo itaangalia hali leo na miaka 50 baadaye.

Kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa ya ubunifu katika maeneo nyeti ya kiuchumi kama vile kilimo, kwa hiyo ipo haja ya kuhakikisha uvumbuzi huo unalindwa ipasavyo. Ni muhimu pia kulinda mali asili zetu kama vile utamaduni, na maeneo ya kijiografia. Maeneo mengine yanayohitaji kulindwa ni pamoja na muziki, na sanaa.

Kuwepo kwa kwa sheria ya Miliki Bunifu kwenye Katiba ya nchi kutaleta uhakika wa ulinzi wa haki hizi na kutawezesha kutungwa kwa sheria bora zaidi za ulinzi wa haki ambao matokeo yake katika nchi zilizofuata mfumo huu ni maendeleo makubwa sana katika sanaa na teknolojia.

Wizara ya Viwanda na Biashara umeshaandaa sera ya Taifa ya Miliki Bunifu itakayokidhi mahitaji ya nchi kwa kujenga msingi wa matumizi ya Miliki Bunifu ili kuchangia kikamilifu katika kufikia lengo la Taifa la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025. Lakini sera hii bila kukaziwa kwenye sheria mama inaweza isipewe uzito unaostahili.

Ieleweke kuwa Ubunifu ni nyenzo muhimu sana ya kuongeza ubora wa bidhaa na huduma zinazozalishwa kwa gharama nafuu. Kutajwa kwenye Katiba ya nchi, Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu itasaidia kufikiwa kwa malengo ya 2025 ikiwemo kupunguza umasikini nchini. Kufanikishwa kwa lengo hili la kitaifa kutasababisha ukuaji wa uchumi wetu kwa kiwango kati ya asilimia 8 hadi 10 katika sekta ya kilimo sambamba na sekta ya viwanda inayotegemewa na karibu asilimia 70 ya Watanzania.

Kwa hiyo, hili si jambo linalohusu sanaa peke yake bali ni suala mtambuka kwa maslahi ya Taifa zima. Hii itawezekana tu iwapo itatambuliwa na kusababisha kuwepo maendeleo ya kibiashara na uhamasishaji wa matumizi ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu vya ndani katika masoko ya maeneo EAC na SADC pamoja na masoko mengine ya kimataifa ambako kuna ushindani mkubwa.

Tanzania ni mjumbe wa WTO katika kundi la nchi masikini (LDCs) ambapo inayo fursa ya kufaidika na makubaliano mbalimbali ya kimataifa ambayo hupatikana tu pale ambapo nchi husika itazingatia utekelezaji makini na wa kimkakati wa Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu. Ni wakati sasa wa kutambua uhalali wa sanaa na Miliki Bunifu kwa kuviweka kwenye Katiba mpya kwa maendeleo ya nchi.


Alamsiki.

Feb 12, 2014

BUNGE LA KATIBA: Wawakilishi wa sanaa lisimamieni suala la sanaa na utamaduni nchini

Paulynus R. Mtendah, mjumbe mteule wa Bunge la Katiba akiwakilisha wadau wa sanaa na filamu

BUNGE la katiba litaanza vikao vyake Jumanne ya wiki ijayo kwa mujibu wa taarifa rasmi. Vikao vitaanza baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa wajumbe 201 wa bunge hilo hivi karibuni, ambapo tasnia ya filamu na sanaa kwa ujumla imefanikiwa kupata wawakilishi watatu: Maria Sarungi, Asha Mtwangi na Paulynus Mtendah.

Maria Sarungi ni mdau na mtayarishaji wa filamu na masuala ya burudani kwa ujumla, Asha Mtwangi ni mdau muhimu wa tasnia ya filamu na katibu wa Bodi ya TAFF Trust Fund, iliyo chini ya Shirikisho la Filamu Tanzania, na Paulynus Mtendah ni mtayarishaji wa filamu na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania.

Ni wazi kuwa Bunge la Katiba hii litatekwa na wanasiasa na katiba itapitishwa kwa maslahi na utashi wa kisiasa zaidi huku ikipuuza mambo mengine ya msingi kwa jamii, hasa wasanii. Ukiisoma Rasimu ya Katiba tangu mwanzo hadi mwisho utagundua kwamba utamaduni hauna nafasi kabisa katika nchi hii kwa sasa licha ya kuambiwa kuwa ndiyo roho ya Taifa. Ni wakati sasa tunapaswa tuwe na na Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana kama kweli tunataka utamaduni uwe roho ya Taifa.

Kutokana na nafasi hii tuliyopata, wawakilishi wetu waitumie fursa hii kupigania masuala ya sanaa na utamaduni kwa kuwa hakuna mwanasiasa yeyote atakayeongelea masula ya sanaa wala utamaduni, kila mmoja anafikiria siasa tu. Kila kona unakopita utasikia majadiliano juu ya muundo wa muungano, tume ya uchaguzi na mengineyo.

Kwa kudharau utamaduni tunasahau kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, na hii kama tanzu muhimu ya utamaduni wala si kitu kilichoibuka tu. Sanaa ndicho chombo ambacho jamii zisizokuwa na jadi ya kusoma na kuandika inatumia katika kuhifadhi na kuwasilisha kumbukumbu za mambo muhimu katika maisha yao.

Tutambue kuwa sanaa ni kazi ya ubunifu tena yenye ufundi na mvuto kama sumaku, kazi nzuri ya sanaa ni ile iliyo na ubunifu, uasili na inayotumia mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.

Sanaa zetu za ufundi wa asili zimesahaulika na tumepokea zile za nje na hali hii imesababisha watanzania kuwa watazamaji wa vituo vya sanaa za nje  badala ya kuweka nguvu zaidi katika kubadili fikra zetu ili bidhaa zetu za ufundi ziendane na matakwa ya dunia kwa kuziboresha sanaa zetu za asili. Jambo la msingi ni kuhakikisha tunazingatia, tunazitambua na tunazilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria.

Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya Utamaduni hukua na pia hufa. Kwa kuudharau utamaduni, sanaa zetu kwa sasa zinakufa au pengine zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi, tusipochukua juhudi za ziada tutazika kabisa uasili wa sanaa zetu tulizopokezwa na wazee wetu kutoka kizazi hadi kizazi?.

Kwa kuupuuza utamaduni wetu, sanaa zetu zilivyo leo haziweki kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo, na kama kuna kumbukumbu basi ni kumbukumbu potofu. Kwa kudharau utamaduni kumesababisha leo hii tumekuwa tukisikiliza nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu bali zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje.

Idara ya Utamaduni ina dhina ya kuongoza, kusimamia, na kudhibiti shughuli za ukuzaji wa Sanaa za Filamu, Maonyesho, Ufundi na Muziki; kusimamia ukuzaji wa lugha ya Kiswahili, lugha za Asili na za Kigeni; na kusimamia shughuli za Mila na Desturi. Tuache kulalamika na tuchukue hatua sasa kuunusuru utamaduni na sanaa zetu.

Ukiangalia kwa kina kuhusu utamaduni wa nchii, utagundua kupuuzwa kwake, japo baada ya uhuru mwaka 1961, iliundwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962, Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Sera ya utamaduni ilizinduliwa Agosti 23 mwaka 1997 mjini Dodoma ikiwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.

Cha kushangaza, pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwa maisha ya watu bado sera ya utamaduni imepewa nafasi finyu mno katika serikali yetu tangu ilipoanzishwa wizara ya kushughulikia masuala ya sanaa. Na hata rasimu ya Katiba mpya imeonesha kutokuupa nafasi kabisa utamaduni.

Pamoja na kuwepo kwa sera ya utamaduni (ingawa nayo ina mapungufu mengi), inabidi wadau wote wa sekta ya utamaduni wajiulize, je umma wa Watanzania umefikishiwa machapisho ya sera hii ya utamaduni ili waisome na kuielewa?

Je umma umeelimishwa kikamilifu juu ya sera hii ili uweze kushiriki katika utekelezaji kwa upana wake? Na je ushirikishwaji wa vyombo vya habari katika kusaidia msukumo wa wananchi kuielewa sera ya utamaduni umepewa nafasi ya kutosha?

Mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inaaminika kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

Kwa kiasi fulani uhusiano kati ya utamaduni na maendeleo ulitambuliwa na Serikali ya Tanzania katika miaka ya 70. Kwa mfano, iliyokuwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana (1979) iliwateua wataalam wake kadhaa waandike kitabu kiitwacho Utamaduni Chombo cha Maendeleo. Katika dibaji ya kitabu hicho, aliyekuwa Waziri wa Wizara husika alitoa maelezo yanayojaribu kuonesha uhusiano kati ya utamaduni, uhuru na maendeleo. Nanukuu:

“Kuna sababu nyingi za kuutambua Utamaduni kuwa ni chombo ni maendeleo. Moja ni kuwa vipengele na fani mbalimbali za Utamaduni ndizo zilizoko katika kiini cha Umoja wa jamii. Utamaduni ni sehemu ya siasa ya Taifa letu lenye msingi na shabaha ya Umoja wa kweli. Uhuru wetu uliletwa na Umoja. Maendeleo hayapatikani bila ya uhuru na Umoja. Hivyo Utamaduni kama Nguzo ya Umoja, ni chombo cha maendeleo (Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, 1979, uk. vii)”.

Kama jitihada za kukuza utamaduni, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), lilianzishwa mwaka 1967, miaka sita baada ya uhuru, kwa ajili ya kukuza Kiswahili ili kiwe lugha inayoweza kutumiwa katika nyanja zote za jamii, utawala, elimu, mafunzo na biashara.

Miaka minane baadaye Serikali ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa, ambayo yaliunganishwa mwaka 1984 kuwa Baraza la Sanaa la Taifa la sasa (Basata). Madhumuni ya Basata na mabaraza yaliyolitangulia, ni kufufua, kuendeleza na kukuza sanaa za asili za Watanzania.

Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzisha masomo ya sanaa tangu mwaka 1966. Mwaka 1973, mafunzo ya sanaa kwa walimu wa shule za msingi yalianzishwa katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa katika Chuo cha Ualimu Butimba Mwanza.

Chuo cha Sanaa Bagamoyo, sasa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), kilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wasanii. Aidha mwaka 1985 serikali ilianzisha matamasha na mashindano ya fani mbalimbali za utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda hadi taifa.

Tuelewe kuwa Utamaduni huipa jamii utambulisho. Sura na haiba ya jamii huweza kueleweka na kuelezeka kutokana na utamaduni wa watu wake. Utamaduni hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kupitia lugha, sanaa na imani za kiroho. Mila na desturi wanazofuata, matamasha au sherehe wanazoendesha, mavazi yao, chakula chao na taratibu nyingine za utamaduni wanazofuata huunganisha jamii.

Utamaduni ndiyo “kidhibiti mwendo” kinachoongoza mwenendo na tabia za watu katika jamii. Ndiyo msingi wa maisha ya mtu binafsi. Humuwezesha kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake. Ndiyo msingi wa maendeleo na ubunifu katika jamii. Maendeleo ya uchumi katika maana yake pana ni matokeo na sehemu ya utamaduni wa watu. Maendeleo yasiyojengwa katika misingi ya utamaduni wa jamii ni maendeleo yasiyokuwa na maana kwa jamii hiyo.


Alamsiki.

Jan 16, 2014

Waziri ateua Bodi mpya ya Filamu na Michezo ya KuigizaWaziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amemteua Mheshimiwa Pindi Chana kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Uteuzi huu unatokana na Mamlaka aliyopewa Waziri huyo chini ya kifungu cha 13(i) cha Sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza Na.4. ya mwaka 1976.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo kwa Vyombo vya habari uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wengine wa Bodi umeanza tarehe 3 Desemba 2013.

Jan 8, 2014

Sawa tunaibiwa, je tunaibiwaje?

* Hivi tunamjua mwizi wetu?


Wasanii wa filamu wakionesha kazi bandia za filamu zinazouzwa mtaani


MWAKA uliopita 2013 kwa tasnia ya filamu nchini tuliuaga kwa pilikapilika mbalimbali, mojawapo ikiwa ni mkutano mkubwa wa wadau wa filamu na muziki uliofanyika 30 Disemba 2013 kwa kuandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Cosota, Bodi ya Filamu, Basata, Shirikisho la Filamu (TAFF) na Shirikisho la Muziki (TMF). Pia kulikuwepo maandalizi ya chinichini ya wasanii/watayarishaji kuandaa maandamano makubwa ya kuishinikiza Serikali ichukuwe hatua dhidi ya maharamia wa kazi za sanaa.

Isingekuwa busara za uongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania inawezekana hivi sasa kungekuwa na tafrani, kwani wasanii/watayarishaji hawa walikuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa msambazaji wa filamu kuwa endapo hawatafanya hivyo, yeye atajitoa kusambaza filamu, jambo lililowatia hofu wasanii hawa na aliwapa masharti kuwa ili aendelee kusambaza kazi zao ni lazima wafanye maandamano yenye kulaani na kuishinikiza serikali kabla ya tarehe 1 Januari 2014.

Jan 1, 2014

Tutafute fursa za masoko ya filamu zetu nje ya nchi


Wasanii wakifuatilia jambo kwenye moja ya vikao


MAJUZI nilijikuta nipo kwenye kikao kimoja cha wadau waliojiita wenye uchungu na tasnia ya filamu nchini, nilikuwepo hapo si kama mchangiaji bali kama msikilizaji wakati baadhi ya wadau hao walipokuwa wakijadili kuhusu mfumo unaofaa kwa ajili ya kusambaza na kuuza filamu zetu. Katika kikao hicho ambacho naamini hakikuwa rasmi bali kilichokuja baada ya mjadala mrefu ulioibuliwa kuhusu makato ya kodi ya asilimia tano wanayodai kukatwa na msambazaji wa filamu kwa kisingizio kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagiza kukwatwa kwa kodi hiyo.