IMEANDIKWA, “Kila siri iliyo moyoni kwa mwandishi, kila
aina ya maisha aliyoyapitia, au kipimo cha akili ya mwandishi vimeainishwa kwa
kiasi kikubwa katika maandishi yake...” hii inamaanisha kuwa kazi za kimaandishi
za waandishi huwaonesha wao ni kina nani, wametokea mazingira gani, wana uwezo
gani wa kufikiri na wanataka kuwa nani.
Kupitia kujielewa wenyewe na kuridhika katika uasili
wetu, mchakato wa kuandika huwa unakuwa wa hiari zaidi na hauzuiliki.
Tunapoelewa kuwa tuna talanta (kipaji) ya kipekee ya uandishi tuliyotunukiwa na
Mungu, inatusaidia zaidi katika kuandaa makala au hadithi nzuri.
Tunakuwa na ujasiri zaidi pale tunapojikubali na kujijua
tulivyo. Tunapojiweka katika mahitaji na tamaa zetu, tunajiweka huru zaidi
kutumia vitu kutoka katika maisha yetu wenyewe na maisha ya wale ambao
wametuimarisha. Husika zetu zinakuwa imara zaidi tunapojibainisha kwa wote
ambao tunawajua katika hali ya kibinadamu.
Hivyo, mwandishi huanzaje? Anza kwa kuangalia kwanza
kinachokusukuma kama mwandishi. Ni kipi kinakusukuma zaidi? Baadhi ya waandishi
husukumwa zaidi na shauku ya kuandika, wengine husukumwa zaidi na hofu, na hata
wengine husukumwa na vyote viwili. Kile tunachokitamani sana mara nyingi pia
ndicho tunachokiogopa. Hii hutokea pasipo kufahamu kwa watu wakati wote.
Waandishi wa filamu, kwa mfano, hutamani sana kuuza kazi
zao, hutaka kuona kazi zao zikifanikiwa kwa kuoneshwa kwenye “screen” kubwa
ndani ya majumba ya sinema na hata kuwa na mapato makubwa kupitia Box Office,
lakini wanaweza kuhofia changamoto zinazoambatana na mafanikio ambayo huja kwa
kazi hiyo. Ni suala la asili tu kuhofu kile tunachokijua kwa kiasi kidogo. Sisi
ni viumbe wenye tabia fulani. Elewa mabadiliko hayaji kirahisi na hii
haijalishi hata kama matokeo yake yatakuwa ni ya kuvutia.
Hatari ambayo waandishi wengi wanaikabili ni kule
kujiweka kwenye kutarajia matokeo makubwa wakati wakiwa hawajajua ni kwa nini
wamechagua kazi ya kuandika.
Yapo maswali kadhaa ambayo kama mwandishi unayopaswa
kujiuliza:
- Je, ni lini ulijigundua kwa mara ya kwanza kwamba
unataka kuwa mwandishi?
- Ulikuwa wapi?
- Ni nini kilikuongoza kufanya uamuzi wa kuandika?
Tunapojibu maswali haya na kujiweka zaidi katika mahitaji
yetu, tunaweza kuanza kutafakari juu ya kile kinachotujenga na kulisha nafsi za
uandishi wetu.
Ieleweke. kila mwandishi ana njia yake ya kuandika. Kwa
baadhi, ni suala tu la kuendeleza utamaduni wa kuandika, ni kama vile kusugua
meno yao kila asubuhi au kula chakula kwa wakati maalum. Kwa wengine, ni suala
la umuhimu wa kuumba dunia mpya na kuwa pamoja kama waandishi wengine,
haijalishi iwapo ni waandishi marafiki wachache, kikundi au kwenye semina.
Ufunguo muhimu wa kutufanya kuandika vizuri ni kujielewa zaidi, nini
kinachotusukuma na kipi kinachochochea uandishi wetu.
Uandishi hutegemea sana Ubunifu (Creativity). Ubunifu wa
mtu hufanyika kutoka kwenye sehemu mbili. Kwanza kuna Ubunifu wa Awali (Primary
Creativity) ambao hutokea kwenye sehemu ya ubongo wa kulia, eneo ambalo ndiyo
chanzo cha mawazo/mipango na utambuzi. Ni eneo ambalo msukumo wa mwandishi
hutokea na kuchangia asilimia 10 tu ya mchakato mzima wa ubunifu.
Kisha, kuna Ubunifu wa Pili (Secondary Creativity), ambao
hutokea kwenye sehemu ya kushoto ya ubongo na huchangia asilimia 90, sehemu
ambayo hujumuisha uhariri, nidhamu, mantiki, muundo, mazoea ya kuandika, taratibu
na mpangilio.
Ili kuwa mwandishi mbunifu ni kuwa na ujasiri wa kuweza kurudia
kumbukumbu zako za utotoni, ambapo ulikuwa huru na hukuwa na msongo wa mawazo
au kufikiria sana maisha kama ulivyo sasa. Unapoanza kuandika, ruhusu upande
huo wa ubunifu wa asili kujitokeza kupitia maneno yako bila kuyakosoa au
kuyachambua maandiko yako.
Kabla hujaanza kupata taswira kichwani mwako
(visualization), kwanza tulia, fumba macho yako na jilegeze huku ukivuta pumzi
ndefu. Ukipenda unaweza kusikiliza muziki wenye kukubembeleza. Endelea kuvuta
pumzi hadi unapohisi misuli ya mwili wako inalegea. Baada ya kulegeza kabisa
viungo, pata taswira yako ukiwa mtoto mdogo. Jenga picha yako ukiwa kwenye eneo
lenye uoto asili kama vile konde lenye kijani kibichi, kwenye kiwanja cha
michezo, porini, au ufukweni mwa bahari.
Unapopata picha, jaribu kuwa sehemu ya tukio ukijumuisha
fahamu zako zote. Vuta hewa ya bahari, sikiliza sauti za ndege wakiimba, sikia
sauti ya upepo ukivuma kwenye majani, angalia rangi ya maji ya bahari na onja
radha ya chumvi ya maji hayo. Endelea kuzama kwenye tukio na jifikirie kuhusu
uwepo wako hapo ukijumuisha fahamu zako zote. Je, umevaa nini? Nywele zako
zikoje? Uko katika hali gani? Uko peke yako au na rafiki? Chukua muda kidogo na
pata picha ya unachokifikiria katika sehemu hii nzuri ya utotoni. Je, una
furaha? Huzuni? Mpweke? Unacheza? Uko huru?
Sasa chukua kalamu yako na anza kuandika kuhusu
ulichokiona. Tumia nafsi ya kwanza — wakati uliopo. Andika ukijumuisha fahamu
zako zote, ielezee picha yote uliyoiona. Usiache kuandika hadi utakapokuwa
umeandika kwa dakika ishirini. Usiiondoe kalamu yako kwenye karatasi wakati
ukiandika na usisome chochote unachokiandika hadi ukiwa umemaliza. Ni muhimu
kwako kuwa huru unapoandika na wala usihofu kuhusu matumizi ya sarufi, herufi
au alama za vituo.
Ukikwama au kama huwezi kufikiri chochote kingine cha
kuandika, basi andika kuhusu hisia za kukwama na kushindwa kuandika. Haijalishi
— usiache kuandika hadi ingalau dakika ishirini zipite. Ukipenda, unaweza
kutegesha saa na usiache kuandika hadi utakaposikia mlio. Mtindo huu wa
kuandika kuhusu jambo hili bila kufuata muundo wowote au sheria, utakusaidia
kutengeneza hadithi nzuri yenye kuleta msisimko zaidi na kumbukumbu zako za
nyuma.
Tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment