Oct 18, 2014

Siku hizi tuna vichekesho au mizaha?


Wachekesha maaruf nchini, marehemu Hussein Mkiety (Sharomilionea) na Amri Athuman maaruf KIng Majuto



NILISHANGAA binti yangu, Magdalena, 10, aliposema siku hizi hapendi kuangalia comedy za Tanzania akidai hazichekeshi. Comedy ni neno la Kiingereza lenye asili ya Ugiriki likimaanisha futuhi au ucheshi kwa Kiswahili. Ni vichekesho vyenye lengo la kufurahisha, kufundisha na kuburudisha watazamaji, katika televisheni, filamu, na kwenye majukwaa. Unapocheka ndivyo maisha yanavyokua bora zaidi!

Ucheshi ni mwanga unaouangazia moyo, ni igizo lililobuniwa kuchekesha, kuburudisha, na kumfanya mtu astarehe. Muundo wa ucheshi ni kuzidisha hali ya mambo ili kuleta uchekeshaji, kwa kutumia lugha, matendo, na hata wahusika wenyewe. Ucheshi huhoji na kufuatilia yalipo mapungufu, makosa au hitilafu, na vitu vinavyokatisha tamaa ya maisha, na kuleta uchangamfu na wasaa wa kufurahia maisha.

Kuna wakati comedy zilijizolea umaaruf mkubwa nchini na kufanya vijana wengi kuingia kwenye sanaa ya vichekesho. Hata hivyo, ucheshi haukuanza leo, nakumbuka nikiwa mdogo tulizowea kusikiliza Mahoka, na vichekesho vya Pwagu na Pwaguzi vikirushwa Redio Tanzania, hakuna shaka kuwa hawa jamaa walikuwa vinara wa vichekesho kwa jinsi walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu.

Na waliokwenda kwenye kumbi mbalimbali hasa Dar es Salaam na miji mikubwa walishuhudia vikundi vya sanaa kama Kibisa, Muungano, Mandela, Bima, vikundi vya Jeshi nk. kwa kweli walifurahia vichekesho vya kina King Majuto, Branco Minyugu, Bartholomew Milulu na wengineo. Ukija kwenye magazeti pia ungekutana na Chakubanga na Polo, na Kingo. Pia jarida la Sani lenye vikaragosi kama Kipepe, Madenge, Pimbi, Sokomoko, Ndumilakuwili, Lodi Lofa nk.

Wachekeshaji ni wasanii wenye umuhimu wa aina yake katika jamii. Ndiyo hutufanya tusahau uchungu wa maisha kwa jinsi ambavyo wanatuvunja mbavu tukiwasikiliza redioni, kuwaona kwenye televisheni au hata kukutana nao mitaani.

Miaka ya 1990 baada ya kuanzishwa vituo vya televisheni, viliibuka vipindi vya ucheshi vya kina Mzee Small, Mzee Majuto, na Onyango na wengine, ambao nikiri kuwa walituburudisha sana. Baadaye wakaibuka Max na Zembwela na 'Mizengwe' yao na kutupa burudani kulingana na wakati. Baada ya kifo cha Max, Zembwela na Mizengwe walianza kuchuja, ndipo wakaibuka Ze Comedy (EATV) waliouteka umma wa Watanzania kwa vichekesho na staili ya aina yake.

Ndipo kukaibuka wasanii na vikundi vingi wanaoigiza kinachoitwa vichekesho kwenye TV na filamu kila kukicha. Lakini kwa sasa wachekeshaji wetu wanachoigiza sidhani kama kinapaswa kuitwa vichekesho bali mizaha.

Komedi kwa kawaida imegawanyika katika mifumo ya aina kuu mbili: comedian-led (wachekeshaji), kwa kutuletea kichekesho kilichopangiliwa vizuri, utani au michoro na situation-comedies (sit-com) ambayo huelezea kisa kilichomo ndani ya hadithi inayosimuliwa.

Sikatai, Tanzania tunao baadhi ambao ni wachekeshaji wazuri sana lakini wamekosa mwongozo.Ila nyingi ya hizi zinazoitwa komedi zipo kwenye ‘stage’ ya mwisho ya 'mzunguko wa maisha'. Mzunguko wa maisha hufuata vielelezo vinne: kuzaliwa, kukua, kukomaa na kuzeeka kabla ya kifo, mwanadamu hufa baada ya stage hizo, lakini komedi kama wachekeshaji wakitambua kwamba vichekesho vyao vinaboa wanaweza kufanya kitu fulani na ikazaliwa upya na kufuata tena ngazi hizo.
Wachekeshaji wetu wanapaswa kuongeza wigo wa ubunifu na kujifunza zaidi kama wanataka kuendelea kutusisimua, aidha wanashauriwa kufuatilia vichekesho vya wenzetu, wawashirikishe wengine, wabadili mfumo, watafute maoni, watumie lugha sanifu, wazame ndani ya akili za wateja wao kujua mahitaji yao na wasome alama za nyakati.

Kinachoua sanaa ya ucheshi ni pamoja na kukosa ubunifu, dharau, kukosa malengo, kutojua watazamaji wanataka nini, na kulewa umaarufu. Vinginevyo ni bora turudi kwenye visa na vituko vya kina Ndumilakuwili, Kipepe, Lodi Lofa, Madenge, Pimbi, Kifimbo Cheza, Sokomoko na wengineo.

Alamsiki.

No comments: