Bayport

Bayport

fofam

fofam

imetosha

imetosha

Ads

Ads

Oct 18, 2014

Uongozaji si kujua ‘action’ na ‘cut’ tu, unatakiwa pia kuijua lugha ya filamuMmoja wa waongozaji filamu nchini, Issa Mussa maaruf kama Cloud 112

SINEMA za mwanzo zilijielekeza kama vile sehemu ya jukwaa mbele ya pazia. Kamera iliwekwa katika sehemu moja na matendo yote katika tukio zima yalifanyika ndani ya fremu hiyo ya kamera kwa pigo moja (one shot). Mtazamo wa watazamaji enzi hizo haukutofautiana na watazamaji ambao leo wanakaa mbele ya jukwaa wakiangalia mchezo wa kuigiza wa jukwaani.

Muongozaji wa Kimarekani, D. W. Griffith, ndiye alikuwa wa kwanza kuwahamishia watazamaji katika ulingo wa sinema kwa kazi zake kama “For Love of Gold (1908)”, “The Lonely Villa (1909)”, “The Lonedale Operator (1911)”, na ile iliyovutia zaidi, “Birth of a Nation (1915)”. Grifftith alikuja na mbinu kabambe za kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi zake.

Sababu ya kuwafanya watazamaji kuwa sehemu ya hadithi ni kuifanya hadithi yako ivutie zaidi – isisimue zaidi. Lakini hii hufanywa kwa kuwaingiza watazamaji katika matukio, na kulenga zaidi kwenye usikivu wao hapa, na pale. 

Muongozaji anaweza kuwachanganya na kuwakanganya watazamaji kiurahisi. Jiografia ya eneo au mwili wote wa mhusika hugawanyika. Hivyo, yasiwepo maswali, ule mkono wa nani? Mhusika A anahusiana vipi na Mhusika B? Mara nyingi muongozaji mzuri hapendi kusababisha mtanziko kwa waatazamaji wake. Hupenda kuwafanya watazamaji wake wajisikie furaha katika ulimwengu wa filamu – kuwa sehemu ya hadithi – ili kwamba hadithi yake iweze kueleweka vizuri.

Siku zote, muongozaji hutaka watazamaji wake wajue kuwa, “Huo wanaouona ni mkono wa Daud, na Daud ameketi kushoto kwa Jesca” (hata kama hawajamuona Jesca kwa kipindi kirefu). Kuna wakati, hata hivyo, kama waongozaji tunapaswa kutumia uwezekano huu wa kuwachanganya na kuwakanganya watazamaji kama njia bora ya kutengeneza mazingira yenye kuleta msisimko au taharuki.

Sinema nyingi zilizofanikiwa huwa zina mhusika mkuu (protagonist) aliye wazi, na swali la kwanza katika kazi yetu ya ufuatiliaji kwenye mwongozo wa filamu ni: Nani ni mhusika mkuu kwenye filamu yetu?

Njia nyingine ya kuuliza swali hilohilo, ninayoamini inaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa muongozaji, ni: Filamu ya nani (mhusika)? Ni mhusika gani tunayemfuatilia kwenye filamu? Ni mhusika gani tunayemtumainia au kumhofia – tukitumaini kuwa atapata anachohitaji, au tuna hofu kuwa hatafanikiwa?

Kama muongozaji, ili ufanikiwe kuwateka watazamaji wako unatakiwa kwanza kuijua “genre”. Genre ni aina ya hadithi inayosimuliwa, mfano, hadithi ya upelelezi, ya uchawi, ucheshi, ya kutisha, ya mapenzi, na kadhalika.

Tunapoangalia filamu, tunakumbuka na kuwa na matarajio fulani kuhusu mhusika, mandhali na matukio: ni vitu hivi ambavyo hutusaidia kufurahia na kubashiri kile kitakachotokea baadaye na kufanyia kazi matukio yanakoelekea.

Genre humruhusu muongozaji kubuni kitu kitakachobeba uhalisia kwa sababu tunashindwa kuona kuwa tunachokiangalia si kitu halisi bali kimetengenezwa. Kwa hiyo… kwenye aina ya hadithi ya kijambazi, kwa mfano, hatutajali kama mmiliki wa jengo la wacheza kamali (casino) atauawa kwa sababu tunamuona ndani ya genre, akiwa upande wa uadui (villain).

Makampuni ya filamu hupenda kutumia genre kwenye mambo yote kwa ajili ya kufanya vizuri sokoni na kusaidia kutengeneza filamu yenye mafanikio: genre maarufu huleta nafasi nzuri ya kufanikiwa sokoni, hivyo, genre ni njia nzuri ya kupanga filamu, hurahisisha sana katika uandikaji wa hadithi mpya.

Hata hivyo, muongozaji anapaswa kujua kuwa filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi, hivyo, haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za Kihindi au Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea hata kama hawaifahamu lugha husika.

Kuna dhana sababishi nyingi ambazo ni za lazima sana kwa muongozaji mzuri: ubunifu, msimamo, elimu/ufahamu kuhusu sanaa, elimu/ufahamu kuhusu watu, uwezo wa kufanya kazi na watu wengine, utayari katika kukubali majukumu, ujasiri, ustahimilivu, na nyingine nyingi. Lakini dhana sababishi iliyo kuu kabisa ambayo inapaswa kueleweka kwa waongozaji, ambayo ikikosekana itatangua mengine yote, ni ubayana (clarity) — ubayana kuhusu hadithi na jinsi kila kipengele ndani yake kinavyoweza kuchangia kwenye hadithi nzima, na pia ubayana kuhusu kile kinachowasilishwa kwa watazamaji.

Nilipokuwa mdogo, kila nilipokuwa nikiangalia sinema nilikuwa nikidhani kuwa sinema hutengenezwa kwa saa moja na nusu au mbili kama ambavyo inaweza kuonekana kwa watazamaji.

Sikuwa na uhakika sana kama kulikuwa na kifaa kinachoitwa kamera kikitumika katika utengenezaji wa sinema, na nilifikiria kuwa mazingira kwenye sinema yalikuwa yakibadilika yenyewe (kwamba, hawakuwa wakifanya uhariri)… Ilinichukua muda mrefu kutambua kuwa sinema zilikuwa zikitengenezwa kwa vifaa maalum, tena kwa kipindi kirefu kuliko inavyoonekana, na kwamba zilitengenezwa kwa kutumia mapigo maalum ya picha (shots).

Msingi mkuu wa hadithi katika sinema ni kuwa, filamu ni zaidi ya kiwanda (sekta), ni zaidi ya onesho linalowakutanisha nyota. Filamu ni lugha. Utengenezaji wa filamu una lugha yake. Kwa hiyo, filamu ni lugha inayotumika kusimulia hadithi, na sauti inayotumika kusimulia hadithi hiyo ni kamera.

Ndiyo, kama filamu ni lugha na kamera ni sauti, basi muongozaji wa filamu ndiye msimuliaji wa hadithi hiyo, lakini “sauti” anayoitumia kusimulia ni kamera. Katika usimuliaji wa hadithi hii, kuna mambo sita yanayobadilika ambayo muongozaji wa filamu anaweza kuyatawala kwa kutumia kamera. Katika mambo yote sita, kitu kinachoitwa composition (mpangilio wa mambo yote yanayochangia kwenye muonekano wa picha kwenye fremu) ndiyo huwa msingi mkuu.

Mambo hayo sita ni: camera angle (muonekano wa picha kutoka kwenye kamera), image size (ukubwa wa picha – ambao unaweza kuathiri kipimo na muonekano wa picha), motion (uhamaji – kutoka juu, chini, na kufuata kitu), depth of field (kina cha eneo – je, ni la kawaida, limebanwa au limeathiriwa na umbali wa fokasi kutoka kwenye lenzi), focus (lengo – kitu kilichokusudiwa kwenye fremu ya picha), na speed (kasi –kawaida, haraka, au taratibu).

Muongozaji wa filamu huandaa na kuunganisha wezekano (possibilities) hizi ili kutengeneza sentensi zinazotumika kusimulia hadithi kupitia filamu, na kisha hupanga sentensi katika “aya” – masimulizi yaliyokamilika au matukio ya kusisimua ambayo yatategemea zaidi katika mgandamizo, ufafanuzi, na nguvu kuu ya tatu ya vipengele vya masimulizi.

Kwa hiyo, picha unazoziona kwenye filamu zinaweza “kusomeka” kama maandishi mengine. Pia tambua kuwa kazi yoyote ya sanaa iliyo kwenye mpangilio mzuri wa mambo yote yanayochangia muonekano wa picha (composition) ikiwa katika mapigo maalum ya picha (shots) yatokanayo na umbali maalum wa kamera, kutoka kwenye muonekano/pembe ya kamera (angle), ikihusisha mwanga (lighting), na sehemu ambapo mapigo ya picha yanawekwa katika mfuatano maalum (sequence), vyote huvutia au kuathiri jinsi mtu anavyoweza kuitafsiri picha hiyo.

Watengenezaji wa filamu hutumia sana umbali wa kamera na muonekano wa picha kutoka kwenye kamera kuvuta hisia za watazamaji, ili kukitazama kile kilichokusudiwa kikiwa katika muundo maalum wa picha au pigo la picha na kukipa maana iliyokusudiwa.

Pamoja na hayo, pia zipo sheria mbalimbali zinazoongoza katika uongozaji ambazo pia zimo kwenye somo muhimu la lugha ya filamu, ambazo waongozaji wote wanapaswa kujifunza na kuzijua kabla hawajaamua kuzivunja.

Alamsiki.

No comments: