Feb 9, 2011

Kutoka Mahoka, Pwagu na Pwaguzi hadi maigizo yenye mizaha!

Marehemu Mzee Pwagu, mmoja wa wachekeshaji 
waliojizolea umaaruf mkubwa nchini

Said Ngamba (Mzee Small), mchekeshaji 
wa kwanza Tanzania kuigiza kwenye Televisheni

Charlie Chaplin, mchekeshaji maarufu wa enzi za 'silent film'

Mr Bean, mchekeshaji maaruf wa Uingereza

WIKI iliyopita nilimkuta binti yangu wa miaka 6, Magdalena, akiwa na mama yake wameketi sebuleni wakiangalia katuni za Tom & Jerry, nilichukua rimoti na kuwabadilishia nikiweka kipindi cha Komedi kinachorushwa na moja ya vituo vyetu vya televisheni, kipindi kilichokuwa gumzo sana siku za nyuma na kilipendwa na watu wa rika zote.

Niliweka kipindi hicho nikijua wao ni wafuatiliaji wakubwa, kuna wakati tulikuwa tukigombana kwa kuwa walitaka kuangalia komedi hata pale nilipokuwa nikifuatilia habari muhimu kwenye vituo vingine.

Niliweka komedi nikiamini kwamba hawakujua kama kipindi wakipendacho kilikuwa hewani, kumbe nilikosea kwani binti yangu alinijia juu akitaka niondoe kipindi hicho huku akiungwa mkono na mama yake, hapa nanukuu alichosema; “Ondoa mimi sitaki hiyo, kwanza watu wenyewe siku hizi hata siwaelewi,” mwisho wa kunukuu.

Comedy ni neno la Kiingereza lenye asili ya Ugiriki likimaanisha futuhi au ucheshi kwa Kiswahili, ni vichekesho (humorous) vyenye lengo la kufurahisha, kufundisha na kuburudisha watazamaji, hasa katika televisheni, filamu, na kwenye majukwaa ya sanaa. Inasemwa kwamba unapocheka ndivyo maisha yanavyokuwa bora zaidi!

Ucheshi ni kama mwanga unaouangazia moyo, ni igizo lililobuniwa ili kuchekesha, kuburudisha, na kumfanya mtu astarehe. Muundo wa ucheshi ni kuzidisha hali ya mambo ili kuleta uchekeshaji, kwa kutumia lugha, matendo, na hata wahusika wenyewe.

Ucheshi mara nyingi huhoji na kufuatilia kwa makini yalipo mapungufu, makosa au hitilafu, na vitu vinavyokatisha tamaa ya maisha, na kuleta uchangamfu na wasaa mdogo wa kufurahia maisha ya kila siku.

Tasnia ya filamu hasa katika ucheshi imekuwa inasonga mbele na kuzidi kujizolea umaarufu siku hizi, vijana wengi wanajitokeza kuingia kwenye sanaa ya uigizaji wa vichekesho. Navutiwa sana na ari ya sanaa ya vijana wa Kitanzania pamoja na kuwepo mapungufu.

Enzi zile nikiwa mdogo, kabla sijaanza darasa la kwanza na hata baada ya kuingia shule ya msingi tulizowea kusikiliza vipindi vya Mahoka na Pwagu na Pwaguzi, vikirushwa na Redio Tanzania, hakuna shaka hawa jamaa walikuwa vinara wa vichekesho kwa jinsi walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu bila kuwaona.

Na kwa waliokwenda kwenye kumbi mbalimbali hasa hapa Dar es Salaam na miji mikubwa walikutana na vikundi vya sanaa kama Kibisa, Muungano, Mandela, Bima nk. na hawakukosa kufurahia vichekesho vya kina King Majuto, Braco Minyugu, Bartholomeo Milulu na wengineo.
Ukija kwenye magazeti pia kulikuwa na vikaragosi maarufu vya Chakubanga na Polo, na baadaye Kingo ambaye bado yupo hadi sasa. Pia jarida la Sani na vikaragosi waliodumu hadi sasa kama Komredi Kipepe, Madenge, Dk. Love Pimbi, Sokomoko, Profesa Ndumilakuwili, Lodi Lofa nk.

Kwa kawaida wachekeshaji (Comedians) ni wasanii ambao wana umuhimu wa aina yake katika jamii. Hawa ndio hufanya wakati mwingi watu tusahau uchungu wa maisha kwa jinsi ambavyo wanatuvunja mbavu tukiwasikiliza redioni, kuwaona kwenye televisheni au hata kukutana nao mitaani. Isitoshe wasanii hawa, kwa kupitia michezo au vichekesho vyao, hutoa mafunzo mazuri sana kwa kijamii.

Kwa bahati mbaya sana, nchini Tanzania bado hakuna mifumo mizuri kwa ajili ya wasanii kama hawa kufaidi vizuri jasho litokanalo na kazi zao. Wengi wao wanakuwa na hali ya kimaisha isiyolingana na vipaji walivyonavyo.

Baada ya kuanzishwa vituo vya televisheni hapa nchini mwaka 1994, aliibuka Mzee Small, baadaye Mzee Majuto na wenzake na hata Onyango na wenzake, ambao nakiri kuwa walituburudisha sana.

Kisha wakaja Max na Zembwela na 'Mizengwe' yao na kutoa burudani kulingana na wakati. Baada ya kifo cha Max, Zembwela na Mizengwe walianza kuchuja taratibu, ndipo wakaibuka Ze Comedy (EATV) ambao waliuteka umma wa Watanzania kwa vichekesho na staili ya taarifa ya habari.

Hivi sasa kumeibuka wasanii na vikundi vingi wanaoigiza kile kinachoitwa vichekesho (comedy) kwenye televisheni na filamu ambazo zinatoka kila kukicha. Lakini, ukweli ni kwamba wanachoigiza sidhani kama kinapaswa kuitwa vichekesho bali maigizo yenye mizaha. 
 
Msomaji mmoja alinitumia ujumbe wiki chache zilizopita akiniuliza kama maigizo ya mizaha siku hizi ni comedy? Na kama ni hivyo na ucheshi utaitwaje?

Komedi kwa kawaida imegawanyika katika mifumo ya aina kuu mbili: comedian-led (wachekeshaji), kwa kutuletea kichekesho kilichopangiliwa vizuri, utani au michoro, na situation-comedies au kwa kifupi “sit-com” ambayo huelezea stori/ kisa kilichomo ndani ya hadithi inayosimuliwa.

Situational comedy ni aina ambayo kisa husimuliwa na kinachekesha wakati mwingine bila kuanza na stori fulani kuhusu tukio au jambo.

Vipengele vyote vya ucheshi vinaweza kuonekana kwa pamoja na/ au kuingiliana. Pia kuna mfumo wa ucheshi unaojulikana kama 'Comedy hybrids' ambapo huenda pamoja na aina nyingine: musical-comedy (ucheshi kwa njia ya muziki), horror-comedy (ya kutisha), na comedy-thriller (ya kusisimua).

Pia kuna ucheshi wa papo kwa papo jukwaani (stand-up comedy), aina hii ya ucheshi ambayo Wakenya wamefanikiwa sana, mfano kundi la Ridiculous lililojulikana zaidi kama “Red Corna ambalo Ze Comedy waliiga ucheshi wa papo kwa papo lakini wakashindwa kabla hawajarukia kuigiza taarifa ya habari ambayo pia wameiga kutoka Red Corna ya Kenya.

Niliwahi kushuhudia jinsi Ze Comedy walivyokuwa wanahangaika kuchekesha papo kwa papo pale kwenye ukumbi wa Starlight! Aina hii ya ucheshi wa papo kwa papo inahitaji uelewa mkubwa sana wa jambo unalotaka kuliigiza ili lichekeshe, kwani kichekesho kinategemeana sana na tukio la papo kwa papo au lililotokea!

Hii ni kwa sababu sisi Waaafrika kwa sehemu kubwa hutumia ishara, mifano katika hadithi na matukio ya kuchekesha. Ucheshi kwa kawaida huwa na mwisho wenye kufurahisha, ingawa wakati mwingine unaweza kuegemea mambo yanayosisimua au mabaya.

Sikatai, hapa Tanzania wapo baadhi ya wachekeshaji wazuri sana lakini wamekosa mwongozo mzuri wa kuwafanikishia kazi zao. 

Wachekeshaji wetu wanapaswa kuongeza wigo wa ubunifu na kujifunza zaidi kama wanataka kuendelea kutusisimua, aidha wanapaswa kufuatilia vichekesho vya wenzetu ikiwa ni pamoja na kununua kazi hizo, wawashirikishe wengine, wabadili mfumo, watafute maoni, watumie lugha sanifu, wazame ndani ya akili za wateja wao kujua mahitaji yao na wasome alama za nyakati.

Kutokana na haya nakubaliana na binti yangu aliyesema kuwa siku hizi hawaeleweki, kwani sioni kama kuna ubunifu wa kuchekesha zaidi ya kufanya mizaha na kuwakashifu watu wengine. Ni vichekesho gani hivi hata kufikia hatua ya kumkejeli mgonjwa au mtu aliyeishiwa eti kafulia!
Ieleweke kuwa kinachoua sanaa ya ucheshi ni pamoja na kukosa ubunifu, dharau (mfano unaposema sisi tunalipwa nyinyi mnacheka), uongozi usio na malengo, kutokujua watazamaji wanataka nini, na kulewa umaarufu.

Baadhi ya wasomaji wamewahi kunipigia simu na wengine kuniandikia ujumbe mfupi kunitaka nizungumzie suala la hizi zinazoitwa komedi, vimbwanga, futuhi na mengine mengi, na wengine wakashauri kuwa ni bora turudi kwenye visa na vituko vya kina Ndumilakuwili, Kipepe, Lodi Lofa, Madenge, Pimbi, Kifimbo cheza, Sokomoko na wengineo.

Kila jamii ina utamaduni wa kipekee sana wa kuchekesha. Bahati mbaya Watanzania tumeathiriwa na mifano ya nje. Vijana wa Tanzania wameshindwa kuelewa kwamba tunatazama filamu za nje kwa ajili ya kuangalia wenzetu wanafanyaje kazi zao lakini si kuiga kwani si mwalimu mzuri kwetu.

No comments: