Oct 30, 2013

Wasomi wetu na kisa cha ‘Heri mimi sijasema’!


Wasomi kama hawa ni tegemeo katika jamii yetu, wanapokwepa majukumu yao kama wasomi ni hasara kwa taifa

NILIPOKUWA mdogo, moja ya sababu kubwa iliyonifanya nipende sana kwenda shule ni kusoma na kusikia hadithi na visa mbalimbali, ama kwa kuvisoma kwenye vitabu (wakati huo kila shule ilikuwa na maktaba yenye vitabu vya kutosha), au masimulizi kutoka kwa walimu wenye kupenda kufundisha kwa mifano. Hadithi nilizozisikia na kuzisoma zilijaa mafunzo ya kila aina, hadithi kama zile za kina Juma na Roza, Bulicheka na mke wake Elizabeth na Wagagagigikoko, au ile hadithi maaruf ya ‘Heri mimi sijasema’.

Hii ni hadithi iliyohusu vita katika ufalme fulani, ambapo wapiganaji watatu wakiwa vitani waliamua kujificha kwa kujifunika na nyasi, bahati mbaya adui akawa anapita eneo lile na kuwakanyaga bila kujua. Mmoja wa wapiganaji hao akalalamika; “kwanini unawakanyaga wenzio kama nyasi?” Yule adui akashtuka kuwa pale kuna mtu kajificha akamchoma mkuki na kumuua.

Mpiganaji wa pili akamuonya mwenzake; “kwanini wewe unasema, je, tukigundulika?” Adui akamchoma mkuki na kumuua pia. Yule wa tatu kwa kujiamini akiamini kuwa yeye yuko salama akasema; “heri mimi sijasema”. Naye akachomwa mkuki na kufa. Huo ukawa mwisho wa wapiganaji wale watatu.

Kipindi kile cha utoto niliifurahia sana hadithi hii japo sikuwa nikielewa hasa undani wa kisa hiki na mafundisho yake kwa jamii. Baadaye nilipokuwa nikisomea utabibu, nilianza kugundua kuwepo baadhi ya mafundisho yanayotokana na visa kama hiki nilivyovisoma: hasa pale nilipozama kusoma somo la matatizo ya akili (psychiatry).

Katika psychiatry, kuna kitu kinaitwa ‘mental mechanism’, huu ni mfumo wa ulinzi wa kisaikolojia na mbinu inayotumika kujifariji ili kukidhi mahitaji ya mtu kijamii, kiutamaduni na kihisia kwa madhumuni ya kupunguza msongo wa mawazo, wasiwasi au kuchanganyikiwa. Kwa maana nyingine, mtu huutumia mfumo huu katika kujifariji kuwa matatizo anayoyaona si yake, hayakusababishwa na yeye bali ya watu wengine kabisa.

Zipo aina nyingi za mental mechanism; kama Repression, Denial, Displacement, Projection, Introjection, Conversion, Dissociation, Provocation Behaviour, Counter-Phobic Behaviour, Compensation, Overcompensation, Rationalisation, Identification, Fantasy, Regression, Suppression, Isolation na nyingine nyingi.

Nitatoa mifano michache ya hizi mental mechanisms na jinsi zinavyofanya kazi kabla sijajikita kuelezea nilichokusudia: mfano, Repression: hii ni aina ambapo mtu hujaribu/hujifanya kuuondoa kabisa ukweli mchungu ndani ya fahamu zake, ili imsaidie kusahau kabisa mambo ambayo hayamletei amani ya moyo/akili. Mfano mtu hujifanya kulisahau tukio aliloshuhudia la kumuona jirani/ ndugu yake akiliwa na mamba mbele ya macho yake.

Denial: mtu hukataa kuukubali ukweli au ukubwa wa baadhi ya mazingira, ili kupunguza au kuzuia simanzi na hisia zisizoepukika, kama vile hasira, hatia, kuchanganyikiwa, aibu, nk.

Displacement: Baadhi ya mambo ya kukera (kama mashambulizi ya kimwili au matusi) au hisia (kama vile hasira, chuki, dharau, nk) kwa mtu au kitu yanaweza kuhamishiwa kwa mtu au kitu kingine, ili kuepuka wasiwasi au hofu isiyoepukika. Kwa mfano; mwalimu wa kike aliyegombana na mumewe, huhamishia hasira zake kwa wanafunzi.

Projection: Mtu hujitahidi kuelekeza lawama au mapungufu kwa mtu mwingine ili kujaribu kuzuia hisia ya wasiwasi au hatia au upungufu uliojitokeza. Mfano rahisi ni pamoja na mwanafunzi aliyefeli mtihani kusingizia kuwa ‘mwalimu alitunga mtihani mgumu ili kumkomoa’, au hulaumu kutokana na 'muda aliopewa haukutosha'.

Rationalisation (sizitaki mbichi hizi): Hii mbinu hutumika wakati mtu anataka kufanya kitu lakini anahisi aibu au hofu kuhusu kufichua nia ya kweli, au aliyepigania jambo akashindwa, hivyo huibua sababu ya uongo. Mfano wa kijana aliyemfukuzia binti akamkosa, hutafuta sababu ili kujifariji; “kwanza mwanamke mwenyewe miguu yote ya kushoto”. 

Fantasy (Alinacha): fikra za matukio ambayo hayajawahi kutokea au hali ambayo wala haipo. Fantasies imekuwa moja ya mental mechanism pale watu wanapoitumia kama chanzo cha kuwaletea furaha na faraja, kwa ajili ya kupunguza msongo wa akili unaosababishwa na matakwa ambayo hayawezi kushughulikiwa. Ni hali ya kawaida sana kwa watoto na watu ambao bado wana akili za kitoto, au kwa mgonjwa wa schizophrenia.

Sasa nirudi kwenye mada niliyokusudia leo, nimejikuta nikiyakumbukia yote haya kutokana na hali hali halisi iliyopo sasa kwenye tasnia ya filamu nchini, hasa kutokana na ukweli kwamba sinema za Tanzania zimekuwa zikilalamikiwa kwa kutokuwa na ubora, hadithi za kuiga na kukosa mvuto.

Hivi karibuni kupitia mtandao wa kijamii wa facebook kulikuwa na mjadala mkali kuhusu tasnia hii ya filamu nchini, huku kundi moja la watu wanaojiita “wasomi” kuonekana kukosoa sana huku wakilitupia lawama kundi jingine la “wasiokwenda shule”.

Mmoja aliandika hivi kwenye mtandao: “mimi sitazami kabisa huu utumbo unaoitwa Bongo Movie, kwanza hawa jamaa hawashauriki, aidha utengenezaji filamu imekuwa sawa na ushabiki wa mpira ambao hauhitaji utalaamu. Hawa ni waongozaji (director) uchwara ambao wanafanya kazi kwa kubahatisha na kubabaisha. Tasnia imeingiliwa na wahuni.”

Baada ya kuambiwa watengeneze za kwao zitumike kama mfano ‘Msomi’ mwingine akaandika: “Binafsi nimesomea sanaa na si kwa kubahatisha lakini nimejitoa katika utendaji, nafanya criticism, natoa maelekezo na mafunzo. Juzi niliitwa na Curious Pictures Afrika Kusini, kufanya mapitio ya kazi zao zitakazoanza kutoka mwezi Januari, hapa kwetu nikishauri naambiwa ya kwangu iko wapi...”

Nilijitumbukiza kwenye mjadala huo na kuwalaumu wanaojiita wasomi kuwa wao ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa tasnia ya filamu nchini, kwa kuwa hawakusoma ili wabaki kujisifia kwenye mitandao na vijiwe vya kahawa bali kuyafanyia kazi waliyoyasomea, msomi mmoja akanijibu kama ifuatavyo:
“Bishop Hiluka, tunakuwa wakosoaji kwa sababu mnachofanya huko kwenye field ni pumba, nataka niwaeleze kinagaubaga; ninakiri na niko tayari kutukanwa kwa hilo, hakuna filamu katika bongo movie ila watu waliokaa mbele ya kamera wapo. Mtu anayeelewa ugumu wa kazi na gharama hawezi kuingia ila kama ni mwenye njaa. Ndio maana wasomi tunajitenga kuingia kwenye uwozo. Utamwambia msomi aingie kwenye movie ya gharama ya laki nane? Ndio maana tunaona madudu. lazima mfike mahali muone wasomi wanachokosoa ni cha kweli…”

Maneno haya na mengine mengi ndani ya mitandao, kwenye vyombo vya habari na hata kwenye vijiwe imekuwa ni sehemu ya kawaida kwa watu wanaojiita wasomi kuwaponda watengeneza filamu wetu, wamekuwa mafundi wa kuponda kila kukicha pasipo hata kutoa ufumbuzi wa nini kifanyike ili kuboresha kazi zetu.

Kuendelea kuponda (kukosoa) bila wao kujitoa kwa dhati katika kuonesha njia ya namna sinema zinavyopaswa kuwa ni kujaribu kukwepa majukumu kwa kutumia mental mechanism aina za ‘projection’ na ‘denial’ kwa kujaribu kuwasukumia lawama wengine. Hivi kama wewe umesoma na una elimu nzuri tu ya taaluma, unasubirije kwanza mazingira ya tasnia yaboreshwe na hao wanaotengeneza pumba ili wewe uje ufanye kazi? Sekta ya filamu itaborekaje kama ‘wasomi’ watabaki mtaani wakilalamika na kuponda?

Hivi unapoponda bila kutumia usomi wako kuboresha mazingira siku ukitoka nje ya Tanzania, utajitofautishaje na Watanzania watengeneza sinema wengine ilihali hata wewe ni Mtanzania?

Ni kweli tuna matatizo mengi kwenye sinema zetu, watunzi wa filamu hawana mafunzo ya uandishi wa miongozo ya filamu na michezo ya kuigiza (Script), ndiyo maana tatizo kubwa lililopo kwenye filamu (nyingi) za Kitanzania ni uwezo mdogo wa uandishi wa miongozo, kitu ambacho kinasababisha filamu na michezo mingi ya kuigiza kuonekana kuwa haina muelekeo.

Pia waigizaji wa Kitanzania wengi ni wazuri katika uigizaji lakini si katika kuandaa miongozo ya filamu, na kwa kuwa lengo ni kuzifanya filamu za Kitanzania kuwa na ubora, hawa wanaojiita wasomi kwa pamoja wangejikita katika kuwaelimisha waandaaji na kutengeneza mazingira bora ya kufanyia kazi yenye kuendana na soko la ushindani kimataifa. Badala yake tumekuwa na kundi kubwa la ‘wasomi mbumbumbu’ linaloishia kuponda tu na kujitoa (projection na denial) kwenye lawama za sisi hatutengenezi pumba. Hii haina tofauti na kile kisa cha ‘heri mimi sijasema’. 

Nimalizie kwa kuwapongeza baadhi ya wasomi (kwangu hawa ndiyo wasomi): Dk. Vicensia Shule, Dk. Mona Mwakalinga, Prof. Martin Mhando, Amanzi Ali Katindi, na wengineo kwa kujitoa kwa dhati kuwa karibu na wasanii hawa wanaopondwa na kuwapatia mafunzo watengeneza sinema wetu.

Alamsiki.

No comments: