Oct 10, 2013

UTEKETEZAJI WA KAZI FEKI ZA SANAA: Ni kweli tunasaidia kumpoza msanii aliyeibiwa?



·        Tuzipitie upya sheria zetu za Hakimiliki

Maofisa wa Cosoza wakiteketeza CD na Mikanda ya wizi katika uwanda wa Kikungwi, Wilaya ya Kusini Unguja

“MWANAHARAKATI, kwanza kabisa nakushukuru sana kwa makala yako wiki hii, pili nakubaliana kabisa na wewe kuhusu ulichoandika kuhusu ‘matumizi ya muziki ni muhimu sana kwenye filamu zetu’. Ukweli ni kwamba suala la wasanii wetu kupenda kutumia nyimbo ambazo wala hawajaomba ruhusa kuzitumia ni jambo baya sana. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za Hakimiliki, haina tofauti na ambavyo wao wamekuwa wakilalamika kuibiwa kazi zao, kwani hata wao ni wezi wa kazi za wengine.

Hebu fikiria, msanii wa Tanzania ametengeneza filamu ya Kitanzania kwa ajili ya Watanzania lakini anatumia nyimbo za West Life, P square, Music Scrol ya Jumong na nyingine kibao za kudownload ili kunogesha filamu yake, halafu kesho anakuwa wa kwanza kulalamika eti anaibiwa kazi yake! Ukimgusa kutaka kumweleza ukweli utashushuliwa na kuambiwa unajifanya mjuaji sana. Nakushukuru wewe uliyejitoa kimasomaso kuwaeleza ukweli wasanii, maana sisi wengine imebidi tukae kimya tu”.

Huu ujumbe ni moja ya nyingine nyingi kutoka kwa wasomaji wa makala zangu, walizoandika ama kunipongeza au kuongezea katika kile nilichoandika kuhusiana na makala ya wiki iliyopita. Baadhi ya wasomaji kama huyu hawakusita kunikumbusha kuhusu suala la ukiukwaji wa sheria za Hakimiliki kwa wasanii wetu.

Msomaji mmoja aliniambia kuwa ni vema nikaandika kuwakumbusha wasanii wote kuwa wanatakiwa kujua haki zao zilizoorodheshwa na Sheria ya Hakimiliki na kwamba pale wanaposhindwa kuzitambua kwa sababu za utaalam wa kisheria, ni bora wakatafuta wataalam katika eneo hilo wakawasaidia.

Nakubaliana kabisa na msomaji huyu, ingawa nadhani suala hili linapaswa kwenda mbali zaidi na si kuishia kwa wasanii tu, bali lifike hadi upande wa jamii. Ni vizuri tukaelewa nini thamani ya kazi za wasanii wetu ili siku moja tusiingie matatani kwa kughushi au kukutwa na kazi ambazo zinavunja hakimilki na hakishiriki za wasanii wetu na watunzi kutoka pande yoyote ile katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.

Kuwepo kwa sheria za Hakimiliki kuna madhumuni mengi, moja kubwa ni kuhakikisha kulinda ubunifu wa mtu ili wengine wapate hamasa ya kutunga/kuandaa kazi mpya badala ya kuendelea kuibiana au kunakiliana, na hivyo ubunifu kutokusonga mbele. Siku zote penye wizi wa kazi za ubunifu hakuna ubunifu wala kusonga mbele. Sheria za Hakimiliki humsukuma mtu kukwepa kunakili au kutumia kazi ya mtu na kutumia ubongo wake kuandaa kazi mpya au kuboresha ya mwingine kiasi cha kupata kazi bora zaidi.

Lakini katika nchi yetu, wasanii wetu wengi wamekuwa maarufu kutokana na filamu zisizo na hadithi zao, za wizi na kunakili kutoka kwa wenzao nje ya nchi, hasa Nigeria, Ghana na India. Na kwa kuwa wameanza kazi kwa misingi ya wizi huwa hawawezi kufika mbali kwani pale wanapotakiwa kufanya muendelezo wa kazi zao hushindwa kwa kuwa si wabunifu. Na hata walio wabunifu wa kweli, watakuwa wamekatishwa tamaa na kuacha kubuni vitu vipya baada ya kugundua kuwa kazi zao zinaibiwa kirahisi bila kuweko na hatua zozote za maana zinazoweza kuchukuliwa.

Asilimia kubwa ya filamu zetu zimekuwa zikilalamikiwa kuwa ni za kukopi na kupesti (copy and paste) kutoka nje, ingawa hata wasanii wetu pia wanalalamika kuwa kazi zao zinaibiwa. Bahati mbaya sana jamii yetu imekuwa na tabia ya kukumbatia wahalifu na hata kuwapa sifa na heshima kwa uhalifu wao, mifano ipo, ambapo wahalifu wanatokea kuwa watu maarufu katika magazeti na mitandao ya jamii, jambo linalokatisha tamaa sana wale ambao wanataka kufanya kazi halali.

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa sheria namba saba ya mwaka 1999, kuna makundi makubwa mawili ya Haki za Wasanii zinazolindwa na sheria hii, ambazo ni Haki ya Kiuchumi na Haki za Kitamaduni ambazo mtunzi wa kazi zinazolindwa na sheria hii ana haki nazo. Lakini pia kuna sehemu inayolinda sheria za Haki za Maadili. Wakati tukivunja sheria za Haki za Kiuchumi, pia tumekuwa tukivunja Haki za Maadili za mtunzi mwingine kwa kuiba kisa/hadithi na kutumia kwenye filamu zetu na kujifanya ni cha kwetu, au kupachika sehemu ya nyimbo kwenye filamu bila idhini ya mhusika, jambo ambalo ni kosa kubwa kisheria.

Hata hivyo, haki za kiuchumi na haki za kitamaduni za mtunzi au mmiliki wa kazi ya sanaa zina mipaka yake kwa mujibu wa sheria hii chini ya kifungu cha 9 na 11 cha sheria imetoa wakati ambapo mtunzi wa kazi ya sanaa inayolindwa na sheria hii hatakuwa na mamlaka ya kukataza matumizi ya kazi yake pale itakapotumiwa na mtu mwingine. Hali hii kisheria inaitwa matumizi yasio ya kibiashara, ikiwa mtu mwingine zaidi ya mmiliki akiitumia kazi kwa ajili ya kielimu/kitaaluma, kufanya marejeo, hatahitaji kupata idhini ya mmiliki ili kufanya hivyo.

Lakini pia tumekuwa na changamoto kubwa kwenye sekta ya filamu nchini kuhusu umiliki wa filamu kutokana na mazingira ya soko letu yalivyo, ambapo wasanii hulazimika kuuza haki zao zote, kisha wakajisahau kama wao si wamiliki tena wa kazi hizo, jambo ambalo limekuwa linaleta kilio kwa wasanii wetu wengi.

Sasa nirudi kwenye mada, wiki hii nimekusudia kuliangazia jambo la Mamlaka zinazohusika kusimamia kazi zetu zinapokamata kazi za wizi na kuziteketeza. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki Zanzibar (Cosoza), ilikamata na kuteketeza CD na Mikanda ya Video, ambazo ni kazi za sanaa. Kazi ya uchomaji wa kazi hizo za kiharamia (piracy) ilitekelezwa huku Maofisa wa Idara ya Mazingira na Misitu wakifuatilia uchomaji huo wa Mikanda ya filamu iliyokamatwa na Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki Zanzibar kutoka kwa wafanyabiashara kadhaa wanaorudufu kazi hizo bila idhini, hivyo, kuiba umiliki wa miziki na filamu hizo kwa kuuza nakala za wizi (pirated copies) bila ya ruhusa ya wamiliki wa kazi hizo.

Zoezi hilo la uchomaji wa kazi hizo limefanyika katika uwanda wa Kikungwi, Wilaya ya Kasuni Unguja mnamo Jumamosi asubuhi, chini ya uangalizi wa Maofisa wa Cosoza na jeshi la Polisi Zanzibar.

Kuteketezwa kwa kazi za wizi za sanaa ni jambo zuri, lakini tunapaswa kuangalia pia na upande wa pili wa shilingi ili kuona mapungufu makubwa yaliyopo na kuyafanyia kazi, kwani pamoja na kuteketeza kazi hizo lakini msanii aliyeibiwa kazi yake amekuwa anasahaulika kwa kuwa mara zote hafidiwi, na hivyo kumkatisha tamaa na kusababisha asiweze kuzidisha ubunifu zaidi.

Kama nilivyotangulia kuandika kuwa kuna Haki za Kiuchumi, tabia za uhalifu kama wizi wa kazi za sanaa husababisha kupotea kwa haki za kiuchumi na nyinginezo, na jamii inapaswa kukemea kwa nguvu zote bila kujali sifa binafsi za mhalifu.

Pia bado sheria zetu za Hakimiliki zimekuwa zinatoa mwanya mkubwa kwa wahalifu kukiuka sheria na kuwa na jeuri ya kuchukua kazi ya msanii yeyote na kuirudufu, kisha kuiuza mtaani bila woga wowote. Hapa Tanzania, baada ya Sheria ya Hakimiliki ya mwaka 1966 kuthibitika kuwa ina mapungufu mengi, ndipo mwaka 1999 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipotunga Sheria Mpya ya Hakimiliki na Hakishiriki, namba saba ya mwaka 1999, ambayo ni sura ya 218 ya Sheria za Tanzania (kama zilivyorekebishwa mwaka 2002). Lengo la Sheria hii ni kutengeneza na kutoa manufaa zaidi na ulinzi zaidi wa kazi za wasanii wa kazi zinazolindwa na hakimiliki na hakishiriki na zingine zote zinazoendana na hizo.

Haki hizi zina msingi katika mkataba wa kimataifa wa Benne wa mwaka 1883 ambao uliridhiwa na Tanzania tarehe 25 Julai 1994, na hivyo kwa mujibu wa kanuni za sheria za kimataifa, Tanzania ina wajibu wa kutimiza yaliyomo katika mkataba huu iliyouridhia.

Uvunjaji wa hakimiliki umegawanywa katika makundi makuu mawili: kundi ambalo uvunjaji wake ni wa msingi (primary), yaani mtu anayevunja hakimiliki au hakimiliki ya mtunzi kwa kunakili, kutengeneza upya au kuionesha kazi hiyo katika hadhara bila idhini ya mmiliki halali.

Kundi la pili la uvunjaji wa kiwango cha pili (secondary), ikiwa kama mtu anayevunja hakimiliki kwa kuitumia kibiashara kazi ya mmiliki halali bila idhini yake. Hii ni pamoja na kurudufu kazi hiyo bila idhini, kuisamba au kuuza, ama kutatoa njia za kusaidia hakimiliki kuvunjwa kwa mfano kutoa vifaa vya kurudufia kazi za sanaa bila idhini ya mmiliki halali.

Tunapaswa tuzitazame upya sheria zetu za hakimiliki ili zilete ufanisi kwa pande zote, kwani sekta ya burudani ni chanzo kikubwa cha ajira na inaweza kuchangia pato kubwa kwenye pato la Taifa, na pengine inaweza kufanya vizuri zaidi endapo itapewa kipaumbele, kwa kuwa sekta ya tatu kwa ukubwa, baada ya ile ya utalii na madini.

Alamsiki.

No comments: