Jan 5, 2011

Soko la filamu Tanzania linakua? (4)

Moja ya kazi za Kitanzania, Pretty Girl

Fake Pregnant, kazi nyingine ya Tanzania

*Kulazimisha filamu iwe na sehemu mbili hata kama hadithi hairuhusu siyo haki 
*Kuna hujuma za kuwaondoa wasambazaji wadogo

KWA takwimu za makusanyo “kiduchu” zilizotolewa na serikali kupitia Naibu Waziri nilizozionesha wiki iliyopita, wasanii na watayarishaji wa filamu wa Kitanzania wanapolalamika kunyonywa jasho lao watu wasipende kuwabeza (kwa kisingizio eti hawakusoma na hawazijui haki zao) kwa kuwa kuna matatizo makubwa zaidi ndani ya sekta hii kuliko inavyodhaniwa.

Kwa mfano, unapoongelea suala la usambazaji wa filamu zetu ni jambo linaloumiza sana kichwa. Unapokutana na mtayarishaji wa filamu hapa nchini ukaongea naye kuhusu biashara ya uuzwaji/ usambazaji wa filamu unaweza kulia, jinsi biashara inavyojengewa mazingira ya kuwa ngumu kuliko biashara nyingine yoyote.

Hili ni suala linalopaswa kujadiliwa na wadau wote wa filamu na tunapaswa kujiuliza ni nani mwenye tatizo kati ya Wasambazaji, Wasanii, Watayarishaji, au mnunuzi wa kawaida kabla hatujakimbilia kuushutumu upande mmoja.

Historia ya usambazaji wa filamu hapa nchini imeanza miaka ya 2000 japo hadi sasa hakujawa na ushindani wenye tija katika kuiendeleza tasnia hii, usambazaji hapo awali ulijikita sana katika kusambaza kazi za muziki na si kazi za filamu.

Soko la filamu lilikuwa likikua taratibu na kuleta ufanisi, lakini hivi sasa kitendo kinachofanywa na wasambazaji wa filamu nchini, hasa msambazaji mmoja mkubwa ambaye ndiye aliyekuja na wazo la kuwalazimisha watayarishaji wa filamu kutengeneza sinema yenye sehemu mbili hata kama hadithi hairuhusu, kwa kweli siyo haki kabisa. Pia kumlazimisha msanii kuigiza awamu ya pili ya filamu (kwa pesa ileile) hata kama msanii hana malengo ya kuigiza ni kuendelea kuwanyonya kupitia kazi zao kwa malipo kiduchu wanayowalipa.

Kulazimisha sinema iwe na namba moja na mbili kunapelekea kuoneshwa kipande kimoja cha mtu kwa zaidi ya dakika tano akifanya tukio moja, jambo ambalo limekuwa likiwakera watazamaji badala ya kuwaburudisha na kuwaelimisha kama ilivyo dhana nzima ya filamu na uigizaji.

Hili ni kama jeraha kubwa ambalo linaelekea kwenye kuwa gonjwa sugu mfano wa saratani (malignant) katika tasnia ya filamu nchini ambapo tumekuwa tukishuhudia filamu zisizo na ubora zikijitokeza kila uchao huku wasanii wakiambulia patupu. Kukosekana kwa ubora wa filamu zetu kumekuwa kukichangiwa sana na wasambazaji ambao ndiyo wanaolimiliki soko zima la filamu watakavyo.

Ili kuonesha kuwa biashara ya usambazaji wa filamu ni biashara inayolipa sana na serikali inapaswa kuwa mdau katika hili ili kukusanya pato kubwa kupitia biashara hii: kumekuwepo njama za makusudi zinazofanywa na msambazaji mmoja mkubwa wa filamu hapa Tanzania ambaye nina ushahidi kwamba amekuwa akitumia mpaka Taasisi za Kiserikali katika mkakati wake wa kuhakikisha kuwa anawaondoa kabisa katika biashara hii wasambazaji wengine wadogo.

Kampuni hiyo ya usambazaji wa filamu ambayo ilianza kama miaka mitano tu iliyopita ikiwa kampuni ndogo tu, hivi sasa ni kampuni kubwa na wamiliki wake wamekuja na mkakati wa kuhakikisha kuwa wasambazaji wengine hawafanyi biashara. Kampuni hiyo imefikia hataua ya kupunguza bei ya jumla ya DVD mpaka kufikia shilingi 1600 kwa DVD moja, ikiwa na lengo la kufikia kiwango ambacho hakitaweza kufanyika kwa wasambazaji wadogo. 
 
Ieleweke kuwa kampuni hii inaagiza DVD tupu za China na ina mitambo yake ya kudurufu (dubbing), wakati wasambazaji wadogo wanategemea kununua DVD tupu kutoka kampuni hiyo na kufanyiwa dubbing kitendo kinachowafanya kutumia gharama kubwa, hivyo si rahisi kushindana na msambazaji huyo.

Miaka mitano iliyopita wakati huo pesa yetu ilikuwa na thamani kidogo (dola 1 ilikuwa haizidi shilingi 1000), DVD moja iliuzwa kwa shilingi 5000 na zaidi (zaidi ya dola 5), hivi sasa DVD inauzwa shilingi 1600 (sawa na dola 1)! Hivi kwa takwimu hizi ni kweli soko la filamu Tanzania linakua au linadorora? 
 
Pia kushusha bei si tu kunashusha thamani ya kazi lakini pia kunawaondoa wasambazaji wadogo ambao wameamua kuwekeza ili kuhakikisha tasnia hii inakua. Wasambazaji hawa ni muhimu sana katika biashara ya filamu na hapa ndiyo lile swali nililomuuliza Rais kuhusu mkondo tunaoufuata kati ya mainstream au independent film linapopata ufafanuzi, kwani kwa kuangalia tu bila hata kufanya utafiti wa kina utagundua kuwa wasambazaji wadogo wapo kundi la Independent. 
 
Aina hii ya wasambazaji wadogo huwa na faida kubwa zaidi kwa wasanii katika tasnia ya filamu popote duniani ingawa wao kwa kawaida huwa wana eneo dogo la kusambaza kazi zao lakini huwaibua wasanii wengi ambao huwa maarufu na baadaye kuangukia kwa wasambazaji wakubwa (major movie studio) kama ninavyokusudia kuelezea hapa chini.

Kwa taarifa tu, kuna kampuni moja ya kizalendo iliyojizolea umaarufu mkubwa sana siku za nyuma kwa kutengeneza kazi na kuzisambaza hadi kufikia hatua ya kuwasafirisha wasanii wake kwenda kuigiza nchini Nigeria na hata kuwaleta wasanii nguli kutoka Nigeria, kampuni hii hivi sasa inapigwa vita kubwa na msambazaji huyu mkubwa tena kwa kutumia taasisi za serikali. 
 
Hakuna asiyejua kuwa msambazaji huyu mkubwa alianza kwa kuwapora watendaji wakuu na wasanii ambao sasa ni maarufu walioibuliwa na kampuni hiyo ya kizalendo, pia ili kuidhoofisha kabisa kampuni hiyo msambazaji huyu mkubwa kaamua kuweka masharti magumu kwa mtayarishaji au msanii yeyote atakayeshirikiana na kampuni hiyo ya kizalendo kuwa hatafanya naye kazi abadan. 
 
Hivi hii maana yake nini? Kuna utamu gani kwenye biashara hii ya usambazaji wa filamu kiasi cha kutumia mamilioni ya pesa na vitisho ili kuwanyong'onyesha wasambazaji wengine?

Kukua kwa tasnia ya filamu kunatokana na kuwepo kwa kampuni zenye ushindani wenye tija na soko la uhakika linalomfanya mtayarishaji kuwa na uhakika wa kuuza kazi yake tofauti na ilivyo hapa kwetu ambapo watayarishaji wa filamu wamekumbwa na sintofahamu kutokana na ukiritimba unaofanywa na msambazaji huyu mkubwa. Mwendendo mzima wa usambazaji wa filamu hapa nchini tangu ulipoanza unaonesha kuwa soko letu halikui bali limeparaganyika (fragmented).

Watayarishaji wa filamu wengi ambao wamekuwa wakipeleka kazi zao kwa msambazaji huyu mkubwa, kazi ambazo kwa kweli ni nzuri kwa maana ya ubora wa picha na hadithi zinazozingatia mazingira, tamaduni na hali halisi hujikuta wakikwamishwa na kazi zao kukataliwa kwa sababu tu hawakuwachezesha wasanii fulani ambao ni “lebo” ya msambazaji huyu au kwa kuwa sinema zao hazina “stori” za aina fulani zinazotakiwa na msambazaji.
Pia filamu hizo hukataliwa kwa kuwa eti hazina sehemu mbili, kitu ambacho ni unyanyasaji na hujuma kwa soko la filamu.

Sikubaliani kabisa na hoja inayotolewa na msambazaji huyu kwamba eti kuna wasanii fulani ambao bila wao sinema haiwezi kufanya vizuri sokoni (haiuzi). Kama ingekuwa kweli kwa nini filamu za wasanii haohao wanaodaiwa kuuza zinafanyiwa promosheni kubwa sana? 
 
Huwezi kusema watu fulani wanauza kwa kuwalinganisha na wengine wakati uwanja wa kibiashara hauko sawa, hawa wanafanyiwa promosheni kubwa mno, kuanzia kwenye magazeti, mabango makubwa, magari ya matangazo, hadi kwenye vituo vya televisheni na wengine hawapati kabisa fursa hiyo ya kutangaziwa kazi zao.

Mbona kuna kazi nyingi tu za wasanii wanaodaiwa kuuza ambazo zimefanya vibaya sokoni, na sababu kubwa ni kwamba hazikupata promosheni ya kutosha. Kama kuna anayebisha nipo tayari kutoa ushahidi.

No comments: