Jan 19, 2011

Nini mustakabali wa usambazaji filamu Tanzania?



Msanii na muongozaji wa filamu, Juma Kilowoko (Sajuki)

Flora Mvungi, msanii aliyejizolea umaarufu 
kupitia Bongo Dar es Salaam

KATIKA makala ndefu “Soko la filamu Tanzania linakua?” iliyoisha wiki iliyopita nilidokeza kuhusu tafrani iliyopo kwenye biashara ya usambazaji wa filamu na hujuma zilizopo kutaka kuwaondoa wasambazaji wadogo. Wasomaji kadhaa walinitaka nieleze mtazamo wangu kuhusu mustakabali wa usambazaji filamu badala ya kueleza matatizo yaliyopo tu.

Ili kuelewa mustakabali wa usambazaji filamu, ni muhimu kwanza kuhoji kuhusu yaliyopita. Tunapaswa kuanza kujiuliza: kuna tatizo gani katika usambazaji wa filamu Tanzania?


Katika tasnia ya filamu kwa nchi zilizopiga hatua na zenye uchuni mkubwa, filamu za kibiashara kwa kawaida huanza na ‘box office’ (huu ni mfumo maalum unaoanzia kwenye uoneshaji wa sinema ndani ya majumba ya sinema 'theatres') au kutolewa katika njia ya sinema, baadaye hutolewa kwenye video, kurushwa kwenye vituo vya televisheni za kulipia, katika televisheni za umma, na hatimaye kwenye vyombo vingine vya habari saidizi (video games, katuni na kadhalika) na mwisho kutolewa kama bidhaa rasmi (DVD, VHS) kwa matumizi ya nyumbani.

Huu ni mfumo maalum wa kimasoko katika studio kubwa za filamu nchini Uingereza, Marekani, India na hata Afrika Kusini. Ni mfumo unaotumika hasa katika mkondo mkuu (main stream) ambapo huwa wanawekeza na kusambaza kazi zilizotegenezwa kwa bajeti kubwa sana.

Pamoja na kuanzishwa kwa teknolojia ya digitali katika video inayojitosheleza - kuongezeka kwa filamu kwa wingi zaidi ya mfumo wa usambazaji unavyoweza kufanya kazi, hivyo, watengenezaji filamu wameanza kutafuta fursa mpya na kusababisha mabadiliko makubwa katika mfumo wa usambazaji wa Hollywood.

Kuanzishwa kwa teknolojia ya digitali katika video na mafanikio yake na kukubalika kimataifa kumefungua fursa mpya katika ulimwengu wa utengenezaji filamu na utaalamu unaoambatana na tasnia hii. Kwa sasa, studio kubwa za Hollywood zinajaribu kurekebisha mgawanyo wao katika mfumo wa usambazaji ili kwenda na wakati wa teknolojia ya video, mwaka 2004 mapato ya studio yaliyotokana na mauzo ya DVD peke yake yalifikia Dola za Kimarekani bilioni 20.9 ikilinganishwa na dola bilioni 7.4 zilizotokana na tiketi za sinema kwa mwaka huo.

Leo hii, imekuwa ni mkakati wa kimasoko kutumia maonesho ya sinema kama njia ya uzinduzi kwa ajili ya kutoa DVD. Kwa kweli filamu zilizofanikiwa kuoneshwa zinafikia karibu asilimia 80 ya maktaba za video. Wengi wa watengenezaji filamu huukwepa mfumo wa sinema na kwenda moja kwa moja kwenye DVD, kama ilivyo kwa tasnia ya filamu hapa Tanzania.

Hapa swali ni hili: Kwa nini tasnia ya filamu Tanzania ambayo imeshamiri kwenye teknolojia ya video, bado kuna ubabaishaji katika kuhakikisha sekta hii inakua? Kwa nini?

Jibu ni kwamba hivi sasa hali halisi ya soko la kimataifa imetuthibitishia kwamba usambazaji wa filamu ni jambo la kawaida kiujumla na usimamiaji wa nyanja zote lazima ueleweke na kutumiwa ipasavyo. Watazamaji wa filamu hawanunui filamu kwa sababu tu zinapatikana au kusambazwa. Na hawanunui filamu kwa sababu tu eti fulani na fulani wamecheza.

Kutokana na utafiti wangu, kuna vigezo muhimu viwili ambavyo vinaweza kutuongoza katika dhana nzima ya mafanikio katika usambazaji filamu;
(1) Maudhui/Mahitaji ya Watazamaji (Content/AudienceConnection) na
(2) Jukwaa la Uwasilishaji (MediaDelivery Platforms).

Ningependa kukaribisha mjadala mpana kuhusu mambo haya kwa lengo la kutafuta jinsi tasnia yetu inavyopaswa kutengeneza mfumo wake wa kimasoko ilitusonge mbele.

Maudhui/Mahitajiya Watazamaji:

Kwa miaka kadhaa, sekta ya filamu Tanzania imeshuhudia utofauti mkubwa kati ya maudhui katika hadithi zetu na kile watazamaji wanachokihitaji, na matokeo yake yameendelea kuyumbisha mikakati ya soko na sera za usambazaji. Maudhui lazima yahusishwe moja kwa moja na mahitaji ya watazamaji ili kuwe na nafasi ya mafanikio kwenye soko.

Maudhui yanayofaa katika kizazi cha leo ni yale yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja. Mafanikio yanayotokana na maudhui yanategemea sana mmenyuko wa watazamaji, na kujenga maudhui yaliyo kwenye mstari na mwelekeo wa watazamaji na matarajio yao imekuwa vigumu, na sasa inahitajika kwa watayarishaji/ waandishi wa miongozo ya filamu kujihusisha moja kwa moja na mtazamo wa watazamaji katika mazingira waliyomo. Kwa matokeo haya, utafiti ni suala la kupewa umuhimu mkubwa kabla ya kuandaa kazi husika.

Kitu ambacho mtayarishaji/ mwandishi anapaswa kujua kuhusu watazamaji wake ni muhimu sana kwa mafanikio katika biashara ya usambazaji. Kujenga maudhui bila uelewa mkubwa na ufafanuzi kwa walengwa, ni kama kufunga safari ya kwenda mahali bila kufikiria jinsi ya kufika huko. Kama maudhui yako hayakushikamana na aina ya maisha au matarajio ya watazamaji wako, jua umewapoteza.

Kundi la kwanza la watazamaji wa filamu ni la akina mama wa nyumbani, wafanyakazi wa ndani, na vijana wasio na ajira. Kundi la pili ni la watazamaji linalotokana na matokeo ya moja kwa moja ya kituo cha Africa Magic kuonesha filamu kwenye familia za watu wa tabaka la kati na la juu wenye uelewa mpana kwa maana ya kwenda shule.

Na bila shaka kuna kundi la tatu linalotokana na watazamaji Watanzania walio nje ya nchi na Waafrika (hasa wanaojua au kukipenda Kiswahili) katika bara la Afrika na maeneo waliko. Ni muhimu kuelewa kwamba kila moja ya makundi haya ya watazamaji yana muundo na mawazo ambayo ni tofauti sana na kundi jingine.

Utafiti nilioufanya kwa miaka mitatu unaonesha kwamba watazamaji wa filamu za Kitanzania wamegawanyika kama ifuatavyo:
Asilimia 67 ya watazamaji wa filamu hizi wanaishi Tanzania, asilimia 25 wanatoka katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, na asilimia 8 wanatoka sehemu zilizobaki za dunia, hasa ambao wanajua Kiswahili au maeneo ambayo Kiswahili kinafundishwa.

Pia ni asilimia 30 ya wakazi wanaoishi mijini ndiyo huangalia filamu za Kitanzania. Takwimu hii inatofautishwa kulingana na umri: Asilimia 50 ya watazamaji hawa ni wenye umri kati ya miaka 10-24, asilimia 30 ni wenye umri kati ya miaka 25-34, asilimia 15 ni kati ya watu wenye umri wa miaka 35-49 na asilimia 5 tu ya watu wenye umri zaidi yamiaka 50 ndiyo huangalia filamu hizi. Dar es Salaam ndiyo mji unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watazamaji wa filamu ikichukua asilimia 31. Hata hivyo, vijana wadogo ndiyo wenye mazoea ya kwenda kwenye mabanda ya video.

Katika utazamaji filamu hizi, kuna dhana ambayo huendana na mitazamo ya watazamaji (matamanio, maadili, na mtazamo wa mtu binafsi kulingana na uzoefu wake katika kuangalia kazi mbalimbali) na vitu hivi huathiri namna watazamaji wanavyohusiana na dunia inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na maudhui.

Kabla hadithi yako haijawafikia watazamaji, tayari mtazamaji atakuwa na picha ya kipi anataka kukiamini na kama hadithi yako imeandaliwa katika mtazamo mzuri, mtu wa aina hiyo huamini na hununua kazi bila kusita. Kama hadithi itaifikia jamii ya watazamaji ambao mtazamo wao utalingana na kisa chako, wigo wake utapanuka, watu watapeana taarifa kwa njia ya neno kwa neno (ambayo ni njia ya ufanisi zaidi kwa mkakati wa soko) na hujenga nidhamu ya utazamaji wa filamu.

Hakuna hadithi inayofanikiwa kama watazamaji hawapati kitu wanachokiamini - na kwa wastani wa filamu 100 za Kitanzania, watazamaji wetu hawataweza na wala hawataona kila kitu wanachohitaji, watachukua na kuchagua kati ya filamu nyingi wanazoziona ili kuridhisha matakwa yao.

Maudhui yanayokubalika sana ni yale yanayosimulia jambo linalofahamika zaidi kwa watazamaji. Hii inaweza kupimwa kwa njia mbalimbali, wengi hasa, utafiti wa msingi unaweza kutusaidia kutambua aina ya hadithi tunazohitaji kuwaambia walengwa, aina ya wahusika tunaowahitaji kutusaidia kwenye hadithi zetu, aina ya watazamaji tunaowahitaji kuwaambia hadithi zetu, na majukwaa sahihi kwa ajili ya kusambaza hadithi zetu.

Kuwaelewa watazamaji ni hatua moja muhimu sana katika mchakato wa biashara ya filamu. Kubainisha maudhui ili yaendane na matarajio yao ni muhimu sana. Kama huwezi kuambatanisha maudhui yako yaende sambamba na mtazamo wa watazamaji, basi, hadithi itapuuzwa.

Kama mtayarishaji wa filamu, suala la kwanza unatakiwa kuwajengea msingi watazamaji katika maudhui uliyoyakusudia, ukielewa kwamba unaweza kuwa bosi kwenye kampuni yako ya production; LAKINI UNACHOKIFANYA SI KWA AJILI YAKO! NI KWA AJILI YA WATAZAMAJI NA HADITHI ZAO!

Pamoja na ukamilifu wa filamu katika usambazaji mara kwa mara, watazamaji kwa urahisi wanaweza kujiendekeza katika mitazamo yao (indulge their world views); wakapuuza kazi ambayo haiwaakisi wao moja kwa moja.

Kuandaa hadithi iendane na ladha ya watazamaji - hasa kwa kuelewa kuwa watazamaji hawataki kubadilishwa mitazamo yao, wanataka kuimarisha mitazamo yao (they want it to be reinforced) - itakusaidia kuanzisha mijadala kuhusu masuala muhimu kwa watazamaji wako.

Vizuri tu kama, utaambatanisha ubora wa kiufundi wa filamu yako uendane na ubora wa watazamaji wako waliouzoea. Hutoweza kufanya biashara - kwa mfano, kuwapa filamu yenye ubora hafifu (low quality film) watazamaji ambao wamezoea kuangalia sinema za kigeni, ambazo zimetengenezwa kwenye tasnia za filamu zilizoendelea zaidi kwa kiwango cha juu cha ubora.

Itaendelea

No comments: