Apr 18, 2018

Kusambaza video chafu, wasanii wanaelekea kubaya

Wasanii Nandy na Bill Nass katika clip ya video chafu iliyoenea mtandaoni


Hamisa Mobeto
INASHANGAZA sana! Katika kipindi ambacho Sheria za mitandaoni zimetungwa ili kudhibiti matumizi ya mitandao hiyo, ndipo mdudu mbaya sana wa video chafu kaingia katika tasnia nzima ya burudani.

Kabla ya huu mtindo mpya wa video zinazodhalilisha utu tumekuwa tukishuhudia jinsi wasanii wa kike wanavyokuwa nusu watupu kitu kinachosemwa eti ndiyo maendeleo (kupiga hatua), na pengine inabainishwa kuwa hiyo ndiyo dalili ya kuwepo kwa mafanikio katika tasnia hii.

Wachambuzi wengi wa burudani wamekuwa wakiandika makala/uchambuzi kuwaponda wasanii wenye tabia za kupiga picha chafu, lakini wakasahau kuwa hata vyombo vya habari (wakiwemo wao wenyewe) haviwezi kukwepa kuwa ni sehemu ya kashfa hizi.

Vyombo vya habari (hasa magazeti pendwa) ndivyo vimekuwa mstari wa mbele kusambaza, japo vyombo hivyo hivyo kwa njia ya ajabu sana vimekuwa pia mstari wa mbele kulaani.

Haiwezekani nguvu ya kupita tu ikatusababishia mabadiliko tunayoyashuhudia sasa kwa kisingizio cha utandawazi au maendeleo.
Kabla ya awamu hii ya Rais John Magufuli nilikuwa nashuhudia tukiwekea picha za wasanii walio nusu utupu kwenye kurasa za mbele za magazeti yetu, mtindo ulioanza polepole ukiwa umepambwa na maelezo kuwa hiyo ilikuwa njia ya kurekibisha tabia, au mara nyingine ulifanywa kwa kisingizio cha kuonesha jinsi wasanii wetu walivyochanganyikiwa kwa kuiga tamaduni za Magharibi.

Ilishangaza sana kuona magazeti yanashupalia kutafuta picha mbalimbali zilizowaonesha wasanii wa kike wakiwa watupu, na wasanii wengi walijipeleka wenyewe kwenye vyombo vya habari, na kupiga picha chafu ili kujitengenezea skendo mbaya kwa dhumuni la 'kutoka kisanii'.

Ndiyo maana ilikuwa haishangazi kuona wasanii walioandikwa vibaya kutolalamika au kuchukua hatua zozote za kisheria. Si hivyo tu, hata pale wasanii walipohisi umaarufu wao unachuja waliwatafuta waandishi na kutengeneza skendo kwa kile walichodai ‘kuosha nyota!’

Sasa imeonekana magazeti hayana dili tena, mambo yote ni mtandao, kwa kuwa tunakwenda na wakati! Au siyo? Hivyo kwa sasa video ndizo zimekuwa zikitafutwa kwa udi na uvumba na hata wengine kuahidiwa fedha nyingi kama watafanikiwa kuvujisha video za wenzao.

Hali hii ya kuvujisha video chafu za wasanii wetu kwenye mitandao na kupatiwa promo kubwa zinawafanya mpaka watoto wadogo kupata taarifa hizo bila hata kuhangaika.

Kwa sasa imekuwa ni fasheni kwa wasanii wengi wa nchi hii, maarufu na hata wasiokuwa maarufu, kujitafutia kiki kwa njia ya skendo ya picha na video chafu kwa kisingizio cha kutafuta ‘promo’.

Mwanzoni mdudu wa skendo na picha chafu alikuwa ameweka kambi kwenye tasnia ya filamu (Bongo Movie) lakini kwa sasa ameenea kwenye sekta nzima ya burudani, hii inatokana na dhana mbaya ya ‘biashara ni matangazo’.

Huu msemo wa ‘biashara ni matangazo’ umekuwa ukichukuliwa vibaya na ni hatari sana si tu kwa uhai wa maadili katika sanaa, lakini pia kwa uhai wa maadili katika vyombo vya habari.

Dhana hii imekuwa chachu ya kuchochea sanaa chafu na inakinzana na tamaduni zetu kwa kisingizio cha utandawazi. Hata hivyo ieleweke kuwa dhana ya biashara ni matangazo inakubalika katika biashara zisizohusiana na sanaa, burudani au utamaduni kwa kuwa inapotumika kuhusisha kazi za sanaa husababisha uchafu huu tunaouona.

Wengi wa wanaojiita mastaa, iwe wa filamu au muziki waliopata umaarufu kupitia skendo za magazetini au wanaokubali picha zao za utupu zitumike kwenye mitandao hawaijui thamani ya ustaa wao.

Hata skendo zao za ngono mfululizo tunazoziona kwenye vyombo vya habari ni ujinga mtupu!

Inashangaza kuona mtu akiimba wimbo mmoja tu au kutokea kwenye filamu moja au mbili, tena kwa kushirikishwa kwenye sehemu ndogo sana, ataanza kujiita staa na kujitafutia skendo kwenye magazeti na mitandao ya kijamii ili asomwe. Ndiyo maana sishangai kuona zinaibuka skendo za aibu kibao!

Sitaki kumumunya maneno, vyombo vya habari (magazeti, redio na televisheni) na mamlaka zinazosimamia maadili katika vyombo vya utangazaji kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hawawezi kukwepa lawama hizi.

Hivi inakuwaje vyombo vya habari kuruhusu video za wasanii maarufu duniani kurushwa bila hata kuangalia maadili yaliyomo humo yanaendana vipi na hadhi ya nchi yetu huku tukiwafungia wasanii wa ndani?

Tunawaandaaje watoto wetu kwa kuruhusu kurusha sanaa chafu za aina hii kwenye vyombo vyetu vinavyoangaliwa na kila rika?

Hali hii kwa sasa inakuwa ngumu hata kwa watoto kukwepa kupata picha, video na taarifa hizo hata kama tukiamua kuwafungia ndani, TV itawaletea au mazungumzo mazito ya vipindi vinavyoendelea katika radio zetu mida ya kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana. Bila hata kuwepo na chembe ya staha hali hii imekuwa kubwa kwa kisingizio kikubwa cha uhuru wa kutoa habari.

Imefika wakati, tena nadhani tumechelewa kulisema hili; ni lazima sasa tufungue mdomo na kusema kuwa inatosha. Mamlaka zinazohusika na udhibiti zisisubiri shinikizo bali wawe macho saa ishirini na nne kufanya kazi zao kwa weledi.

Watambue kuwa hata nchi ambazo wasanii wetu waiga, huwa zina staha zake kutokana na mila za huko. Picha hizi za utupu zisiwe zinapatikana kiholela hivi, kama ni vipindi vya TV basi zichambuliwe na zihamishiwe vipindi vya usiku wakati watoto wamelala, magazeti yenye picha za aina hii yatafutiwe njia za kuratibu, ikiwezekana picha hizo zisiwekwe kabisa ukurasa wa mbele ambapo hata watoto wanaona mara moja.

Pia tuache unafiki wa kuhubiri tusichotenda na kutenda tusichohubiri, hasa kwa vyombo vya habari ambavyo kila siku ‘vinashadadia’ skendo za wasanii na kutuonesha picha za utupu kwa kisingizio cha kurekebisha tabia.

Ni mambo ya ajabu: unapigaje picha ya binti akiwa mtupu usiku wa manane akiwa klabu kisha unaweka katika ukurasa wa mbele wa gazeti lako asubuhi na kudai eti unamrekebisha mtu tabia? Hapa sioni kama kuna kurekebishana, bali kiukweli tunasambaza tu yale yaliyokuwa siri usiku na kuyaweka hadharani hata kwa watoto.

No comments: