Apr 25, 2018

Tuzuie teknolojia isikwapue haki za wasanii



Wakati Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) ikizidi kuimarika na kuchukua nafasi ya njia kongwe za mawasiliano, tasnia ya ubunifu nayo inajikuta kwenye changamoto ya kuakisi mabadiliko hayo ya wakati.

Tasnia ya ubunifu (Sanaa) ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji; ambapo wabunifu (wasanii) wanayo dhamana ya kueneza ujumbe na elimu kwa jamii.

Tasnia hii ni mjumuiko wa hakimiliki bunifu ambazo zinapaswa kulindwa ili jamii iendelee kunufaika na kazi hizi za ubunifu, ambazo sasa zimeenea duniani kote.

Sifa kuu maalumu ya sanaa ni kwamba inatoa athari zake kwa mbunifu na mtazamaji/msikilizaji, hata kama katika mambo mengi mbunifu hatalizingatia hilo, na ijapokuwa katika aghlabu ya wakati, mtazamaji/msikilizaji hatalihisi hilo.

Kwa mfano, athari za tungo za kishairi, filamu, michoro na aina nyingine za sanaa, sauti ya kuvutia na muziki mzuri – ambapo yote hayo ni katika sanaa – huziathiri nyoyo za wanaofuatilia au kusikiliza bila wenyewe kujua.

Sanaa si kama utajiri ambao unapatikana mara moja kwa kutoka kijasho cha uso na girisi mikononi. Madhali mtu hana kipaji cha sanaa, hata akijitahidi vipi bado ataendelea kubakia katika asili yake ile ile ya kimaumbile.

Pia kipaji cha kisanii si kitu ambacho mtu anaweza kukichuma kama utajiri bali huwa ni kipawa maalumu anachotunukiwa msanii na Mungu.

Mungu ndiye humpa mwanaadamu neema zote hata kama njia ya kumfikia neema hizo huwa ni kupitia jamii, baba, mama, mazingira anayoishi na vitu vingine kama hivyo.

Vivyo hivyo, msanii hufanya juhudi zake, lakini hiyo fursa na hima ya kufanya juhudi nayo hupewa na Mungu. Msanii anapaswa kufanya juhudi za kukuza kipaji chake cha usanii ndani ya nafsi yake.

Kila msanii peke yake ni kama dunia nzima na sifa hiyo maalumu ya msanii imo ndani ya nafsi yake. Na kama mtu angelipata fursa ya kudiriki dhati ya wasanii angeliweza kuona shani za dunia na maajabu yake.

Ndani ya dunia iliyojaa furaha na majonzi, matumaini na wasiwasi ndani yake, ni sanaa pekee yenye uwezo wa kutibu majeraha na hata kuifanya jamii iwe na furaha.

Si hivyo tu, kwa sasa tasnia ya ubunifu ina nguvu sana duniani, hasa filamu na muziki, na imeenea duniani kote na kusaidia katika ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, japo tasnia hii inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo kutokana na kuingia katika zama za dijitali (teknolojia) lakini pia imeanza kukumbana na changamoto kubwa na mkwamo.

Kwa upande mmoja, maendeleo ya haraka ya teknolojia yameiletea sekta hii fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina ya uenezi wa sanaa hizi zimekuwa nyingi, kwa mfano televisheni za kwenye mitandao ya intaneti (online tv); simu za mkononi n.k., zimeingia kwenye soko la televisheni na imekuwa shinikizo kubwa kwa sekta ya ubunifu.
Lakini hiyo ingeweza kuwa habari njema kama teknolojia hii isingekuwa inatumika vibaya kurahisisha ukwapuaji wa kazi hizo adhimu. Ukuaji wa teknolojia umefanya maharamia wa kazi za sanaa kukwapua kwa urahisi kazi za sana na hivyo kuzidi kuwafukarisha wasanii.

Utakuta watu wanapakua filamu na miziki kwenye mitandao, kurudufu na hata kutembea nazo kwenye flashi diski, huku wasanii wakibaki fukara! Kwa kweli hii si haki, hasa ikizingatiwa kuwa Mungu ametoa neema ya kipawa kwa msanii ili aweze kuishi kwa kutumia kipawa chake.

Ukitazama hali ya wasanii wenyewe katika upande wa maisha yao kwa kweli si nzuri sana (japo wanaishi maisha ya kuigiza), na mara nyingi hata huwa si nzuri kabisa.
Hata watu ambao wanawekeza katika masuala ya sanaa huwa mara nyingi wanashindwa hata kurudisha fedha walizowekeza.

Ni vyema tukatambua hali zao kuwa wanahitaji sapoti ili waendelee kueneza ujumbe na elimu kwa jamii, utakapotizama filamu au kusikiliza muziki, wakati mwingine fikiria wabunifu wote walioandaa filamu hiyo na kumbuka kuna hakimiliki inayowawezesha kupata kipato chao.

Na pili fikiria changamoto za teknolojia, kwa kuwa huu ni wajibu wa kila mtu na wala siyo wa watunga sera pekee.

Ni vipi tunaweza kutumia fursa hii ya kipekee ya intaneti ya kueneza utamaduni na wakati huo huo kuhakikisha wabunifu wanaendelea kubuni na wanapata kipato chao kwa kuandaa filamu na video zinazoboresha maisha yetu?

Kwa kweli inabidi kuwasaidia wasanii na kama hawakusaidiwa wanaweza kuamua kufanya jambo lolote lile litakaloweza kuwadhaminia fedha za kuweza kuendelezea kazi zao.

Ndiyo maana mara nyingi tumeshuhudia wakitumika katika biashara haramu kama ya dawa za kulevya. Wasiwasi wangu tu wasije wakatokea watu wasioitakia mema nchi yetu na kuwatumia kuleta machafuko, kueneza fikra za maingiliano haramu ya kijinsia na mambo kama hayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 2006, nchini Tanzania kulikuwa na wasanii milioni 6, ingawa kwa vyovyote watakuwa wameongezeka kwani imekwishapita miaka kumi na mbili na hata teknolojia imekua.

Sanaa ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika la Hakimiliki la Kidunia (WIPO) ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato uliotokana na shughuli za Hakimiliki ulikuwa zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini.

Pia mchango wa ajira katika kazi zilizotokana na Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii. Pia wasanii ndiyo wamekuwa wakilipa jina na utambulisho Taifa hili.

Pia kwa mujibu wa utafiti wa WIPO wa Septemba 2012, sekta ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa asilimia 4.275. Hivyo, ni vema tukahakikisha teknolojia haitumiki kukwapua haki za wasanii, kwa mustakabali wa taifa na jamii yetu.

No comments: