Apr 12, 2018

Sanaa ina nafasi kubwa katika jamii

Wasanii wa kizazi kipya wanaounda kundi la Tanzania All Stars wakiwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara

UHAKIKA wa sanaa – iwe sanaa yoyote ile – ni kipaji kutoka kwa Mungu, ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji.

Ijapokuwa kudhihiri kwa sanaa kunatokana na jinsi sanaa yenyewe itakavyobainishwa, lakini huo si uhakika wote wa sanaa. Kabla ya kubainishwa, kuna hisia na utambuzi na udiriki wa sanaa yenyewe na kwamba mambo yote yanachimbukia hapo.

Baada ya kuonekana, kutambuliwa na kubainishwa uzuri, unyofu na uhakika wa sanaa, hapo ndipo zinapoweza kuzuka maelfu na nukta ndogondogo na nyembamba sana ambazo baadhi ya wakati hawawezi kuziona nukta hizo isipokuwa wasanii wenyewe.

Mtu asiye msanii anaweza kushindwa kuona hata nukta moja kati ya hizo na sababu yake ni kuwa msanii ana kurunzi na kipaji cha kipekee cha kuweza kupenya ndani kabisa na kuona nukta hizo nyembamba, ndogondogo na uhakika halisi.

Hiyo ndiyo huitwa sanaa ya kweli na ya uhakika kutokana na kuwa imechimbuka kutoka katika udiriki, ubainifu na utambuzi wa kweli.

Kabla ya mtu yeyote mwingine, thamani za sanaa na nafasi yake ya kweli katika jamii inabidi wasanii wenyewe waitambue na kuipa heshima yake.

Wasanii wanapaswa kujua thamani ya shehena yenye thamani kubwa iliyomo ndani ya dhati zao. Namna ya kuheshimu na kujua thamani ya kipaji hicho nayo ni kule kuupa usanii hadhi yake na kuuweka katika nafasi unayostahiki.

Sanaa ni miongoni mwa nukta za fahari na zenye thamani kubwa katika moyo wa mwanaadamu.

Sanaa ina lugha pana ambayo hakuna lugha yoyote nyingine yenye upana kama huo. Si lugha ya sayansi, wala lugha ya kawaida, wala lugha ya mawaidha yenye upana kama wa lugha ya sanaa.

Inabidi sanaa ipewe umuhimu na kila leo inabidi ipanuliwe na inabidi pafanyike juhudi za kuhakikisha muundo wa kujivunia wa sanaa ndiyo unaotumiwa.

Bila ya kuwepo sanaa, matamshi ya kawaida hayawezi kupata nafasi yake katika akili ya mtu yeyote yule, hasa wakati sanaa inapokuwa na mvuto na athari za kudumu.

Sanaa ni ala na nyenzo nzuri sana ya kufikisha na kupanua fikra sahihi. Sanaa ni ala, ni zana ni chombo; naam chombo muhimu mno.

Si sahihi kuipuuza sanaa na kudharau wajibu wa kuiendeleza, kuikuza na kuipanua sanaa, na si sahihi kudhani kwamba sanaa ni dhambi au kufikiri ni makosa kuwa msanii na vitu kama hivyo.

Sanaa ni uhakika wenye fahari kubwa na kwa kawaida mtu anayepewa kipaji hicho na Mungu huwa ni kama ambavyo watu wengine walivyopewa utajiri, hivyo, anapaswa kujua uzito wa jukumu alilopewa, yaani ajue thamani ya neema alizopewa na Mungu na atekeleze jukumu lake kwa mujibu wa neema hizo.

Majukumu hayo si lazima yote yawe ni ya wajibu wa kijamii, kidini au kisheria, hapana, kwani kuna majukumu mengi ambayo mtu anatekeleza kwa kusukumwa tu na nafsi yake.
Wakati mwanaadamu ana macho, hiyo ni neema ambayo baadhi ya watu hawanayo. 

Lakini pamoja na kwamba macho hayo yanampa mambo mazuri na yana ladha hizi na zile kwa mwanaadamu, lakini pia mwanaadamu ana majukumu ambayo anapaswa kuyatekeleza kutokana na kuwa na neema hiyo ya macho.


Hata hivyo, wakati mwingine sanaa inatumiwa vibaya kisiasa. Siasa katika dunia ya leo inafanya ushakii wa kutumia vibaya sanaa. Kama tutasema wanasiasa hawafanyi hivyo tutaonekana hatujui yanayoendelea.

Si kuwa wanasiasa wa leo tu ndio wanaotumia vibaya sanaa, bali wanasiasa wa huko nyuma pia walikuwa wakifanya vivyo hivyo.

Kwa mfano, sekta ya filamu duniani inadhibitiwa na mabeberu, sinema ni moja ya sanaa za kisasa zilizopiga hatua kubwa kabisa.

Taasisi kubwa kabisa na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza sinema duniani leo hii ni ile ya Kimarekani ya Hollywood.

Mtu anapojiuliza, Hollywood inawatumikia akina nani, majibu yake huwa rahisi kuyapata. Ni rahisi kujua Hollywood inatumikia fikra gani na iko mrengo gani.

Taasisi hiyo kubwa ya sinema na utengenezaji filamu ambayo ina makumi ya mashirika na makampuni makubwa makubwa ya kutengeneza filamu, imeajiri wacheza filamu, wasanii, wasimamiaji wa sinema, waandishi na watungaji mbalimbali na kuwekeza fedha nyingi sana katika upande huo kwa shabaha ya kutumikia lengo maalumu.

Lengo hilo ni la kufanikisha mambo ya kisiasa za kibeberu za Magharibi.

Hata hapa nchini, wasanii wamekuwa wakitumika kisiasa huku hali zao wenyewe katika upande wa maisha yao zikiwa si nzuri sana, ndiyo maana haishangazi kuona wakijiingiza kwenye biashara haramu kama dawa za kulevya.

Hata watu ambao wanawekeza katika masuala ya sanaa huwa mara nyingi wanapokuwa wameshikamana na vitu maalumu wanashindwa hata kurudisha fedha walizowekeza.

Kwa kweli inabidi kuwasaidia watu hao na kama hawakusaidiwa huamua kufanya jambo lolote lile litakaloweza kuwadhaminia fedha za kuweza kuendelezea kazi zao.

Lililo muhimu kwao wakati huo ni kupata watazamaji wengi zaidi na jambo hilo si kwamba ni zuri wakati wote.

Kukimbilia kwenye mambo ya kifuska, kueneza fikra za maingiliano haramu ya kijinsia na mambo kama hayo katika utengenezaji filamu ni jambo ambalo kwa kiasi fulani linafanyika kwa lengo la kufanikisha fikra hiyo ya kuvutia watazamaji wengi zaidi.

Lakini msanii hapaswi kumpa kijana kitu ambacho kitamsukuma kwenye ufuska na ufisadi. Kufanya hivyo kunakwenda kinyume kabisa na fikra ya kumfanya mtu awe huru kuamua na kuchagua anachotaka.

Masuala ya kuchochea fikra za watu hayampi mtu uhuru wala fursa ya kufikiri na kuchukua maamuzi anayopenda. Bali humsukuma mtu moja kwa moja upande maalumu bila ya kuwa na nguvu zozote za kuamua.

Inabidi kazi za kisanii zifanyike kwa sura ambayo msanii ataweza kuwaonesha watu kazi zake za kisanii bila ya kuchochea hisia wala kufanya jambo ambalo mtazamaji atalazimika kuvutika upande wake bila ya kuwa na uhuru wa kuamua.

Kama kazi ya kisanii itamvutia mtu bila ya kutumia vitu kama hivyo, hapo ndipo mtu atakapoweza kujua kuwa kazi hiyo ya kisanii imefikia kwenye kiwango bora.

No comments: